Kwa nini kuwakopesha pesa marafiki na jamaa kunatuingiza kwenye matatizo?

fc

Chanzo cha picha, AFP

    • Author, Brian Lufkin
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Wengi wetu tuna uzoefu wa kukopesha fedha ndugu wa karibu; iwe jamaa ambaye hajalipa kodi ya nyumba, au pesa taslimu kwa rafiki.

Ingawa tatizo hutokea pale mtu huyo anapochelewesha malipo ya mkopo huo kwa miezi kadhaa, au anapoonekana hana nia ya kulipa mkopo huo.

Hakuna shaka kwamba pesa na uhusiano vinaweza kuleta shida kidogo. Kwa kawaida tunawakopesha watu wa karibu, lakini wataalam wanasema kukopesha pesa kunaweza kuvuruga uhusiano huu wa karibu.

Na hilo linaweza kuunda hisia mchanganyiko kwa pande zote mbili, kama vile aibu, haya, au hasira.

Watalaamu wanasema nini?

C

Chanzo cha picha, TBW

Maggie Bigger, mwanasaikolojia na mtaalamu wa masuala ya fedha anayeishi Pennsylvania, Marekani anasema watu huzungumza sana kuhusu pesa, lakini hawaulizani kwa undani kuhusu hali zao ya kifedha.

"Kuna aina fulani ya mashaka kuhusu pesa, kuhusu ulicho nacho na usichokuwa nacho," anaongeza.

G. Michael Collins, mkurugenzi wa kitivo cha Usalama wa Fedha katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, Marekani, anasema pesa ni mada ambayo hakuna mtu anayeweza kuinyamazia, na husababisha utata na mashaka katika mahusiano.

Anafafanua: "Ukienda benki na kuchukua mkopo, mwenye benki anajua ikiwa unaweza kulipa mkopo huo au la, na unasaini mkataba. Usipolipa, kutakuwa na madhara, kama vile kukunyima mshahara au kuchukua gari lako. Lakini tunapomkopesha pesa jamaa au marafiki, hatuna mkataba wa aina hiyo."

Ukopeshaji huo usio na maandishi na "ukosefu wa uangalizi na uwajibikaji" ndio hutia watu wasiwasi.

Pia, kutoa pesa hubadilisha muundo mzima wa uhusiano. "Ukimpa mtu pesa, anakuwa ni mdaiwa, iwe atakulipa au la - basi ghafla unakuwa mtu mwenye nguvu zaidi katika uhusiano huo kuliko yeye," anasema Bigger.

Pesa hubadilisha muundo wa uhusiano. "Hawi tu rafiki au mwanafamilia, anakuwa ni mdaiwa," anasema Brad Klontz, mwanasaikolojia wa fedha na profesa katika Chuo Kikuu cha Nebraska-Creighton.

Pia, mkopeshwaji anakabiliwa na mashaka mengi na kujishuku, kwa sababu yuko karibu na mtu mkopeshaji wake. Wataalamu wanasema mikopo mingi hairejeshwi. "Mara tisa kati ya kumi, mtu aliyekopa pesa kwa rafiki halipa!" Anasema Bigger.

Klontz anakubali, akisema, "Lazima uwe tayari kwa 100% kutoka siku ya kwanza kwamba huenda hutorudishiwa pesa ulizokopesha."

Tabia za wenye madeni

fd

Chanzo cha picha, Getty Images

Mara nyingi, mtu anayeomba mkopo kwanza atalipa bili zake zote kabla ya kufikiria kulipa mkopo, na wengine huwa na mawazo kwamba mkopeshaji pesa anazo za kutosha kwa hiyo hajali pesa alizotoa kama mkopo!

"Kwa ujumla, mtu anayekukopa anajitenga na wewe, halafu unahisi unyonge. Unahisi kama unatumiwa vibaya na unahisi kama mtu haheshimu mipaka yako au haheshimu pesa zako," anasema Klontz.

"Hizi ni nyakati nyeti sana, kwa sababu ukikopesha inaweza kuharibu uhusiano, na usipokopesha inaweza pia kuharibu uhusiano, kwa sababu wanaweza kuhisi kama hukuwasaidia katika nyakati ngumu walipokuhitaji," anaongeza.

Bila shaka, kumlipia rafiki chakula au kinywaji ni tofauti sana na kumkopesha mtu kiasi fulani cha pesa. Watafiti wanasema kukopesha marafiki pesa huleta shida pale inapotokea zaidi ya mara moja na rafiki yako halipi deni lake.

Lipi la kufanya?

SD

Chanzo cha picha, BIA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ikiwa mtu atakuomba umkopeshe kiasi kikubwa cha pesa, "kanuni ya kwanza ni kujipa wakati wa kufikiria," kama Baker anavyosema, na unapaswa kushauriana na mwenzi wako, familia, au mtu yeyote anayehusika katika maamuzi yako ya kifedha.

Collins anasema hata kama hakuna mkataba ulioandikwa, bado unapaswa kuwa na mpango wenye tarehe mahususi wa kupokea deni hilo.

Ikiwa unamlipia mtu nusu ya kodi yake - mwambie, ‘najua unalipwa tarehe 15 ya mwezi, basi vipi kuhusu uirudishe dola 500 tarehe 17? Ikiwa unataka kuilipa mara mbili kwa mwezi, nipe dola 250 tarehe 15 na dola 250 tarehe 30."

"Kuwa muwazi sana juu ya muda wa mkopo kurudi," anasema Collins.

Lakini Begar anasema, “hili linaweza kuonekana ni gumu kwa wengine, lakini litamlazimisha yeyote atakayeniazima pesa kusaini mkataba wa maandishi”.

Begar anasisitiza kwamba mkopeshaji anapaswa kuwa muwazi kadiri iwezekanavyo.

"Mpe mtu nafasi ya kufikiria masharti yako ya mkopo na kuamua ikiwa kweli anataka mkopo kutoka kwako au ikiwa itakuwa bora kwenda benki. Hapaswi kuudhika wala hilo halipaswi kuharibu uhusiano wenu," anaongeza.

Na bila kujali jinsi mkopo unavyosaidia mtu, unapaswa kukaa mbali na kukopesha pesa rafiki ambaye anajulikana kuwa kwa masuala ya kifedha halipi madeni.