Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Israel Gaza: Idadi ya vifo vya Gaza inasema nini kuhusu vita
Na Merlyn Thomas
BBC Verify
Takriban Wapalestina 20,000 huko Gaza wameripotiwa kuuawa tangu Israel ilipoanza kulipua eneo hilo kutokana na mashambulizi ya Hamas ya tarehe 7 Oktoba. BBC Verify inachunguza kile idadi ya waliofariki Gaza inafichua kuhusu mzozo huo.
Kwa wastani, karibu watu 300 wameuawa kila siku tangu kuanza kwa mzozo huo, ukiondoa usitishaji vita wa siku saba, data kutoka kwa wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas zinaonyesha. Mkurugenzi wa dharura wa Shirika la Afya Ulimwenguni wa kanda hiyo Richard Brennan anasema anachukulia takwimu hizi za majeruhi kuwa za kuaminika.
Kuhesabu waliofariki ni changamoto katika eneo lolote la vita , na madaktari huko Gaza wanasema huenda idadi ya waliofariki itakuwa kubwa zaidi kwani haijumuishi miili iliyozikwa chini ya vifusi vya majengo yaliyoharibiwa au ile isiyopelekwa hospitalini.
BBC Verify imeangalia kwa kina takwimu hizo, jinsi zinavyolinganishwa na migogoro mingine na athari kwa idadi watu wachanga wa Gaza.
Idadi kubwa ya vifo
Kasi ya mauaji katika vita hivi imekuwa "ya juu sana", anasema Prof Michael Spagat, ambaye ni mtaalamu wa kuchunguza idadi ya vifo katika migogoro duniani kote, kama vile vita vya Iraq 2003, vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Colombia, vita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na vita vya awali kati ya Israel na Gaza.
"Katika mfululizo wa vita vya Gaza vinavyoanzia 2008, vita vya sasa hivi havijawahi kutokea kwa idadi ya watu waliouawa na kutobagua kwa mauaji," anaongeza.
Idadi hiyo 20,000 inawakilisha karibu 1% ya wakazi milioni 2.2 wa Gaza.
BBC imezungumza na wataalamu wa kijeshi ambao wameelezea aina mbalimbali za mabomu yaliyotumiwa na Israel - baadhi ya takriban 100lb na mengine makubwa kama 2000lb - kuwa yamechangia moja kwa moja ukubwa wa vifo katika mzozo huu.
Kuwa karibu na athari za mabomu makubwa zaidi ni kama "kuteleza kwenye Dunia huku wimbi la mshtuko likiifanya ardhi kuwa miyeyusho kwa muda," anasema Marc Garlasco, mchambuzi mkuu wa zamani wa kijasusi katika Pentagon na mpelelezi wa zamani wa uhalifu wa kivita wa Umoja wa Mataifa, ambaye alizungumza na waathiriwa na mashahidi wa mabomu haya.
Kinachowaumiza zaidi ni kwamba Gaza ina msongamano mkubwa wa watu. Ni 41km tu (maili 25) kwa urefu na 10km (maili sita) upana. Kwa wastani, kabla ya mzozo huo, kulikuwa na zaidi ya watu 5,700 kwa kila kilomita ya mraba huko Gaza - sawa na msongamano wa wastani wa London.
Israel ilianza kampeni yake ya kijeshi huko Gaza kufuatia mashambulizi ya Hamas, ambapo watu 1,200 waliuawa, wengi wao wakiwa raia. Miezi mitatu baadaye, inakabiliwa na shinikizo kubwa juu ya idadi ya majeruhi wa raia.
Katika mizozo ya duniani kote kati ya 2011 na 2021, kwa wastani 90% ya waliouawa walikuwa raia wakati silaha za milipuko zilitumiwa kwenye maeneo yenye watu wengi, kulingana na kikundi cha utafiti na utetezi cha Action on Armed Violence.
Kwa mujibu wa tathmini za kijasusi za Marekani zilizoonwa na CNN, katika vita hivi, Israel ilikuwa imedondosha zaidi ya mabomu 29,000 kwenye Gaza tangu vita vilipoanza na katikati ya mwezi wa Disemba, huku 40-45% ya mabomu haya yakiwa bila kuongozwa.
Mabomu haya "yanaweza kukosa shabaha yao kwa hadi mita 30, ambayo ni tofauti kati ya kupiga Makao Makuu ya Hamas na ghorofa iliyojaa raia", anasema Bw Garlasco, ambaye amefanya kazi katika vita vitatu vya awali huko Gaza na sasa ni mshauri wa kijeshi wa shirika la amani la Uholanzi PAX.
Kikosi cha Ulinzi cha Israel (IDF) kimesema kinachukua hatua za tahadhari ili kuepusha uharibifu kwa raia.
Inasema hatua hizi ni pamoja na maonyo kabla ya mgomo katika hali ambapo inawezekana kufanya hivyo. Israel pia imesisitiza kuwa rekodi yake ya kuua raia imekuwa bora zaidi kuliko katika mizozo mingine ya kimataifa.
IDF inasema "itakomesha mashambulizi tunapoona kuwepo kwa raia bila kutarajiwa. Tunachagua silaha zinazofaa kwa kila lengo - ili zisilete uharibifu usio wa lazima."
Israel pia inasema kuwa Hamas inatumia raia wa Gaza kama ngao za binadamu.
Je, ni raia wangapi wameuawa?
Wanawake na watoto ni takriban 70% ya wale ambao wameuawa huko Gaza wakati wa mzozo wa sasa, inasema wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas.
Hata hivyo, takwimu za Hamas hazitofautishi kati ya raia wanaume na wapiganaji.
Uchambuzi rasmi wa hapo awali wa vifo kutoka Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Hamas tarehe 19 Disemba, ambayo ilifikia 19,667, ulisema kuwa zaidi ya watoto 8,000 na wanawake 6,200 wameuawa. Pia ilisema kuwa wafanyikazi wa matibabu 310, wafanyikazi wa ulinzi wa raia 35 na waandishi wa habari 97 wameuawa - wote wakiwa raia.
Vita hivyo vina athari mbaya sana kwa watoto wa Gaza. Takriban nusu ya wakazi wa eneo hilo ni chini ya miaka 18, kulingana na data iliyotolewa mwaka wa 2022 na wizara ya afya.
Kumekuwa na zaidi ya watu 52,000 waliojeruhiwa katika mzozo huo hadi sasa, wizara ya afya inasema. Ingawa hakuna takwimu za hivi punde za idadi ya watoto waliojeruhiwa, tarehe 3 Novemba waliripotiwa kujeruhiwa 24,173 - ikiwa ni pamoja na watoto 8,067, wanawake 5,960 na wanaume 10,146.Gaza sasa ni "mahali hatari zaidi duniani kuwa mtoto", kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la watoto, Unicef.
"Vitongoji vizima, ambapo watoto walikuwa wakicheza na kwenda shule, vimegeuzwa kuwa rundo la vifusi , bila maisha ndani yake," Adele Khodr, mkurugenzi wa Unicef kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
Je, hii inalinganishwaje na vita vingine?
Kila mzozo ni wa kipekee kwa jinsi unavyopiganwa, lakini wataalamu hao ambao BBC imezungumza nao wanakubalianakwamba kiwango cha mauaji huko Gaza ni kikubwa zaidi kuliko katika maeneo mengine yaliyopiganwa hivi karibuni.
"Tunachokiona kuhusiana na vifo vya raia tayari kimepita viwango vya madhara kutokana na migogoro yoyote tuliyoandika," alisema Emily Tripp, mkurugenzi wa Airwars, shirika ambalo limefuatilia vifo vya raia katika vita na migogoro tangu 2014.
Mchambuzi wa zamani wa kijasusi wa Pentagon Marc Garlasco alisema: "Ili kupata kiasi sawa wa vilipuzi vikubwa vinavyotumika katika eneo dogo lenye watu wengi, tunaweza kulazimika kurudi kwenye vita vya Vietnam kwa mfano - kama vile mlipuko wa mabomu ya Krismasi ya 1972, wakati takriban tani 20,000nya mabomu yaliangushwa Hanoi wakati wa Operesheni Linebacker II." Takriban raia 1,600 wa Vietnam waliuawa katika milipuko ya mabomu ya Krismasi.
Kinyume chake, mashambulizi ya anga na mizinga ya muungano unaoongozwa na Marekani yaliua chini ya raia 20 kwa siku, kwa wastani, wakati wa mashambulizi ya miezi minne ya kuwafukuza IS katika mji wa Raqqa nchini Syria mwaka 2017, kulingana na Amnesty International. Haijulikani ni raia wangapi waliishi hapo wakati huo, lakini maafisa wa Umoja wa Mataifa walikadiria kuwa kulikuwa na kati ya 50,000 na 100,000. Zaidi ya hayo, zaidi ya raia 160,000 waliripotiwa kukimbia makazi yao na kuwa wakimbizi wa ndani wakati huo.
Na uchunguzi wa Associated Press ulionyesha kuwa kati ya raia 9,000 na 11,000 waliuawa katika vita vya miezi tisa kati ya vikosi vya Iraq vilivyoungwa mkono na Marekani na IS kwa mji wa Mosul nchini Iraq vilivyomalizika mwaka 2017.
Hii ni sawa na wastani wa vifo vya raia chini ya 40 kwa siku, kwa wastani. Mosul ilikuwa na idadi ya watu wanaokadiriwa kuwa chini ya milioni mbili wakati IS ilipouteka mji huo mnamo 2014.
Wakati wa takriban miaka miwili ya vita vya Ukraine, Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takriban raia 10,000 wameuawa.
Hata hivyo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa ufuatiliaji wa haki za binadamu pia umetahadharisha kuwa takwimu halisi inaweza kuwa kubwa zaidi kutokana na changamoto na muda unaohitajika kuhakikiwa.
Na kulinganisha viwango vya vifo katika migogoro tofauti ni vigumu, kwa sehemu kwa sababu mbinu tofauti hutumiwa kukadiria vifo.
Wapiganaji wangapi wa Hamas wameuawa?
Israel imesema lengo lake ni kuiangamiza Hamas lakini haijabainika ni wanachama wangapi waliouwa. Maafisa hapo awali walitaja "maelfu" na mahali pengine "7,000".
Hamas imepigwa marufuku kama shirika la kigaidi na serikali za Israeli na Uingereza na nchi nyingine za magharibi ..
Lakini ilipoulizwa moja kwa moja, IDF ilisema "haina idadi kamili ya magaidi wa Hamas waliouawa".
Shirika la habari la AFP liliripoti kuwa maafisa wakuu wa Israel walipendekeza kuwa Israel imewaua raia wawili wa Palestina kwa kila mpiganaji mmoja wa Hamas. Uwiano huo ulielezewa na msemaji wa IDF Jonathan Conricus kama "chanya kabisa", kwa CNN.
BBC haijaweza kuweka mbinu wazi ya kuthibitisha idadi ya wapiganaji waliouawa.
Prof Michael Spagat, alisema "hatashangaa hata kidogo" ikiwa karibu 80% ya waliouawa walikuwa raia.
Nambari za IDF za wapiganaji waliouawa "zimekuwa kila mahali, bila maelezo au ufafanuzi", aliongeza.
Hakuna "takwimu za kuaminika" za uwiano wa raia na wapiganaji waliouawa huko Gaza, wanasema Hamit Dardagan na John Sloboda wa Iraq Body Count, shirika linalochunguza idadi ya vifo katika vita vya Iraq.
End of Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel-Gaza
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi