Je 'vita kati ya Israel na Iran vitakuwaje?' - Sunday Times

Muda wa kusoma: Dakika 5

Vita vingine vinakaribia kuzuka wakati wowote kati ya Iran na Israel baada ya kuuawa kwa kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran. Vita vimekuwa vikipamba moto kwa miezi 10 kati ya Israel na Hamas, ambayo Israel inaweza kuizuia. Lakini hali itakuwaje baada ya mauaji ya Haniyeh?

Hivi ni vichwa vya habari miongoni mwa mada kadhaa zilizojadiliwa na magazeti maarufu ya kimataifa.

Tukianza na Sunday Times na makala ya Michael Clarke yenye kichwa cha habari "Vita kati ya Israeli na Iran vinaweza kuwa na muonekano upi?"

Mwandishi huyo ambaye alihusisha mauaji hayo na Israel, ambayo haijatoa tamko lolote kuhusu operesheni hiyo, anasema kuwa mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh Jumatano asubuhi, saa chache baada ya kuuawa kwa kiongozi wa Hezbollah Fouad Shukr, huenda yakaanzisha mzozo mpya katika njia ya vita vya moja kwa moja kati ya Israel na Iran.

Anaongeza kuwa Waisraeli wamewapa changamoto Wairan kuanzisha vita kuhusu Haniyeh wakati Tehran itakapojibu - ambayo bila shaka itafanya hivyo - ndani ya siku chache zijazo.

Serikali za Magharibi, kwa mujibu wa mwandishi huyo, zinasema Israel na Iran zote hazitaki vita kamili.

Inaaminika kuwa Iran itawahimiza washirika wake wengine (Hamas na Wahouthi nchini Yemen) kuiunga mkono Hezbollah katika mapigano, lakini hatimaye itatoa kafara moja kati ya makundi hayo ili kuepuka kuwa upande mbaya wa vita vya moja kwa moja na Israeli.

Unaweza pia kusoma:

Pia kuna wasiwasi unaoongezeka, hasa mjini Washington, kwamba katika kutafuta kujilinda kisiasa Netanyahu na Wayahudi wenye msimamo mkali wanaoiunga mkono serikali yake huenda wanajiandaa kukabiliana na Hezbollah nchini Lebanon mapema zaidi, mwandishi anabainisha.

Iwapo serikali ya Israel itakuwa tayari kuanzisha vita vipya na Lebanon, vita hivyo vitakuwaje? Kwa hakika havitakuwa kama vita vya awali vya mwaka 1978, 1982, au 2006, ambavyo vililipa jeshi la Israeli ushindi ambao ulitatua matatizo kidogo ya usalama wa nchi.

Licha ya Hezbollah kutopendwa miongoni mwa Walebanon, kwa mtazamo wa mwandishi, imekuwa na nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa miaka ishirini iliyopita, na ina maelfu ya makombora, ikiwa ni pamoja na ndege zisizo na rubani na silaha za roketi, ambazo zinaiwezesha kuishambulia Israel.

Mwandishi anasema kwamba vita vya awali vya Israeli nchini Lebanon kwa ujumla vimekuwa vikilenga kusafisha eneo la Lebanon la maadui zake na kuunda eneo llisilo la mapigano, lakini kazi hii itakuwa ngumu zaidi wakati huu. Ikiwa Hezbollah watarusha makombora yake yote, watazidi mara moja uwezo wa ulinzi wa anga wa Israeli.

Iwapo Waisraeli hawawezi kuishi na tisho hilo, anasema, watalazimika kuanzisha mfululizo wa mashambulizi ya haraka ndani ya Lebanon ili kukamata maeneo ya kurusha makombora. Ikiwa hawawezi kufanya hivyo, basi wanaweza kujaribu mashambulizi makubwa ya anga ili kupunguza tisho la makombora, ambayo yanaweza kuilazimisha Hezbollah kutumia nusu nyingine ya silaha zake za nyuklia.

Ikiwa Israel itajikwaa katika eneo la milima ya Lebanon, au ijikute ikishambulia maeneo ya kaskazini zaidi ambayo yatakuwa na athari ndogo za kimkakati, operesheni hiyo itakuwa ngumu, na mashambulizi mapya kutoka Hamas mjini Gaza na Ukingo wa Magharibi, na kutoka kwa Wahouthi nchini Yemen yataikumba Israel , mwandishi anahitimisha.

"Hakuna kitu kilicho wazi"

Na kwa upande wake gazeti la Kiebrania la Haaretz na makala ya uchambuzi iliyoandikwa na Jack Khoury yenye kichwa cha habari "Netanyahu ana uwezo wa kuzuia vita vya kikanda – anachotakiwa kufanya tu ni kuweka makubaliano na Hamas."

Mwandishi anasema kwamba mvutano juu ya tisho la kuongezeka kwa hali ya vita vya kikanda katika siku zijazo unaweza kuonekana katika kila kona ya Mashariki ya Kati. Lakini zaidi ya swali la "kiufundi" la iwapo Iran itaishambulia Israel, swali muhimu ni : Je, vita vya kikanda vitazuka?

Anaongeza kuwa hofu ni kubwa, na inaweza kusababisha matukio ya kutisha. Hakuna kitu kilicho wazi, na hakuna mtu aliye na majibu ya uhakika.

Lakini pamoja na yote haya, mwandishi anaelezea, kuwa kuna mtu mmoja ambaye ana uwezo wa kumaliza mapigano, au angalau kutuliza mgogoro unaokaribia: Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu.

Iwapo atatangaza kwamba anataka kufikia makubaliano na Hamas ambayo yanahakikisha usitishaji mapigano katika Ukanda wa Gaza na kurejea kwa mateka walioshikiliwa huko, na kisha kuitisha mkutano wa baraza la mawaziri na mjadala wa Bunge la wawakilishi la Israel kuhusu suala hilo, ingawa liko mapumzikoni, hii itapunguza mara moja mvutano.

Makala hiyo inasema kuwa tangazo kama hilo halitakuwa ni kujisalimisha kwa Iran na Hezbollah, na bila shaka sio kwa Hamas. Ukweli ni kwamba maafisa wote waandamizi wa kijeshi nchini Israel, pamoja na Marekani na nchi nyingine zote katika eneo hilo, wanaunga mkono kufikiwa kwa makubaliano ya pande hasimu.

Idadi kubwa ya wananchi wa Israel pia wanaunga mkono kufikiwa kwa makubaliano, kutoka kwa familia za mateka na wafuasi wao kwa vyama vya upinzani, ambavyo vilimuahidi Netanyahu usalama wa kuwazuia mawaziri wa siasa kali za mrengo wa kulia kuiangusha serikali yake.

Mwandishi anahitimisha kuwa hii haijumuishi kujadili kuondolewa kwa makazi, kukombolewa kwa eneo, au kuanzishwa kwa taifa la Palestina. Inahusisha tu kuwarudisha mateka katika nyumbani, kumaliza vita ambavyo vimedumu kwa karibu miezi kumi, na kutoa nafasi nzuri ya kuzuia vita.

"Netanyahu alijifunza mengi kutokana na mawazo ya Trump"

Tunahitimisha taarifa za magazeti na gazeti la Asharq Al-Awsat kwa makala ya maoni iliyoandikwa na Tariq Al-Hamid, yenye kichwa "Baada ya Haniyeh."

Mwandishi anasema kwamba kinachokuja baada ya mauaji ya Haniyeh ni kitu kimoja, na kilichokuja kabla yake ni kingine. Iwapo Iran itajibu mauaji ya Haniyeh yenyewe, au kupitia washirika wake, ukweli sasa unabadilika, na kwa kile Netanyahu anachokitaka.

Anaongeza kuwa licha ya Marekani kuwa na nguvu kubwa, imeshindwa kwa miezi tisa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas. Sasa, kwa mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh Jumatano, mzozo wa umwagaji damu kati ya wawili hao unaonekana kuongezeka, wakati walinda amani wa Marekani wakisimama kando.

Mwandishi anathibitisha kwamba, baada ya ziara yake ya hivi karibuni Washington na Biden kujiondoa katika kinyang'anyiro cha urais, Netanyahu hajali tena mtu yeyote, hata utawala wa Marekani, na atafanya kama anavyotaka

Akifafanua kwamba Netanyahu alitambua kuwa hatua ya Biden kujiondoa imevuruga utaratibu wa mambo , na sasa alikuwa na malengo kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuthibitisha uongozi wake wa ndani au hata kuweka ramani mpya ya jinsi mambo yatakavyofanyika kwa rais wa Marekani ajaye. Kama ni Kamala Harris, hii inamaanisha kuwa atapata ukweli ambao lazima aushughulikie.

Ikiwa rais ni Trump, Netanyahu ameandaa mpango wa hatua za kutekeleza kwa ajili yake. Netanyahu alijifunza mengi kutokana na namna Trump alivyofikiria, hususan mauaji ya Qassem Soleimani, na kufuata nyayo zake katika kuwaua watu ambao hawakutarajiwa anaodhani walikuwa hatari kama vile Haniyeh, na nchini Iran.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla