Bomu lililotegwa Tehran miezi miwili iliyopita” lilimuua Haniyeh - New York Times

Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika mkusanyiko wa magazeti leo tumesoma ripoti inayozungumzia habari mpya inayohusiana na mbinu ya kumuuwa kiongozi wa Palestina Ismail Haniyeh na makala inayozungumzia athari za mauaji ya viongozi waliokuwa na uadui na Israel katika suala la mateka..

Tunaanza ziara yetu na gazeti la Marekani, The New York Times, ambalo waandishi wa habari walihitimisha kwamba mauaji ya Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Hamas, yalitekelezwa na kilipuzi ambacho kilisafirishwa kwa siri hadi kwenye nyumba ya wageni ya Walinzi wa Mapinduzi ya Iran mjini Tehran yapata miezi miwili iliyopita.

Gazeti hilo la Marekani linasema kuwa lilitegemea maafisa saba kutoka Mashariki ya Kati wakiwemo Wairani wawili pamoja na afisa wa Marekani.

Watano kati yao walithibitisha kuwa bomu hilo lililipuliwa kwa mbali, baada ya kuthibitisha kuwa Haniyeh alikuwa chumbani mwake.

Maafisa wa Mashariki ya kati walisema Haniyeh alikaa katika nyumba hiyo ya wageni mara kadhaa wakati wa ziara yake mjini Tehran, na kwamba ingawa Israel haijakiri kuhusika na mauaji yake, mashirika yake ya kijasusi yaliifahamisha Marekani na serikali nyingine za Magharibi juu ya undani wa operesheni hiyo katika matokeo ya hivi karibuni, ilisema ripoti hiyo.

Uvumi uliokuwepo ulidai kuhusu uwezekano kwamba Israel ilimuua Haniyeh kwa shambulio la kombora kutoka kwa ndege isiyo na rubani, sawa na kombora lililorushwa kwenye kambi ya kijeshi huko Isfahan mwezi Aprili, ambalo lilizua utata wakati huo kuhusu pengo katika ulinzi wa anga wa Iran.

Gazeti hilo linasema katika makala yake - iliyoandikwa na wanahabari wake watatu - kwamba safari hii operesheni hiyo ilitumia mwanya tofauti wa usalama katika jengo la makazi ambalo lilipaswa kulindwa vikali, lakini liliruhusu bomu kufichwa kwa wiki kadhaa kabla ya kulipuliwa.

Gazeti la Marekani halikujua jinsi bomu hilo lilifichwa katika nyumba hiyo ya wageni, lakini maafisa wa Mashariki ya Kati waliozungumza na gazeti la New York Times walisema kwamba mauaji hayo yalichukua miezi kadhaa kupangwa na kuhitaji ufuatiliaji wa kina wa boma hilo.

Gazeti la Marekani halikujua jinsi bomu hilo lilifichwa katika nyumba hiyo ya wageni, lakini maafisa wa Mashariki ya Kati waliozungumza na gazeti la New York Times walisema kwamba mauaji hayo yalichukua miezi kadhaa kupangwa na kuhitaji ufuatiliaji wa kina wa boma hilo.

Maafisa hao wawili wa Iran walisema hawakujua jinsi au lini vilipuzi hivyo vilitegwa kwenye chumba hicho.

Gazeti la New York Times liliwanukuu maafisa wa Mashariki ya Kati liliozungumza nao wakisema kuwa mlipuko huo ulitokea saa 2 asubuhi kwa saa za huko, na kwamba wafanyakazi wa jengo hilo walikimbia kutafuta chanzo cha kelele hiyo kubwa, hadi walipofika kwenye chumba cha Haniyeh.

Timu ya madaktari katika jengo hilo ilikimbilia chumbani mara baada ya mlipuko, na kutangaza kwamba Haniyeh alikufa mara moja. Walijaribu pia kumfufua mlinzi, lakini pia alikufa.

Maafisa hao wawili wa Iran walisema kuwa kiongozi wa harakati ya Jihad ya Kiislamu ya Palestina, Ziad al-Nakhalah, alikuwa anakaa karibu, lakini chumba chake hakikuharibiwa sana, ikionyesha mipango makini katika kumlenga Haniyeh haswa, kwa mujibu wa makala hiyo.

Gazeti hilo la Marekani pia limesema, likiwanukuu maafisa wa Iran, kwamba usahihi na ustadi wa shambulio hilo ni sawa na mbinu ya silaha ya roboti yenye udhibiti wa mbali ambayo Israel ilitumia kumuua mwanasayansi mkuu wa nyuklia wa Iran, Mohsen Fakhrizadeh, mwaka 2020.

"Kuwaua maadui wa Israeli hakutarudisha mateka"

Tunaendelea na uhariri wa gazeti la Israel la Haaretz, ambalo linasema kuwa shinikizo la kijeshi halielekezi kuachiliwa kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa Gaza.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mauaji ya kiongozi wa Hezbollah Fouad Shukr huko Beirut, na kiongozi wa kisiasa wa vuguvugu la Hamas la Palestina Ismail Haniyeh mjini Tehran, "yanarudisha kwa Israel heshima iliyopoteza" tarehe 7 Oktoba.

Hata hivyo, gazeti hilo linaendelea, "mauaji ya watu mashuhuri yangechelewesha kurejea kwa mateka na kukwamisha mpango ambao ungesababisha kuachiliwa kwao."

Gazeti hilo la Israel lilitumia taarifa ya binti wa mmoja wa mateka hao, ambapo inamtuhumu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa kujaribu kuzuia kutekelezwa kwa mapatano hayo.

Ripoti hiyo inasisitiza kwamba kuna "njia moja ya kuondokana na mgogoro huu," ambayo ni kusitisha mapigano na kufikia makubaliano kwa ushirikiano na Marekani, ndani ya mpango wa kina wa Rais wa Marekani Joe Biden, ambao unajumuisha "mpango wa mateka, kumaliza vita , makubaliano ya ulinzi pamoja na kufanya upya mazungumzo ya kutatua migogoro ya Israel na Palestina.

Gazeti hilo lilihitimisha makala yake kwa kubainisha alichosema Waziri wa Ulinzi Yoav Galant kuhusu Israel kutotaka vita, na kuhusu dhamira yake ya kuwarejesha mateka na kuunga mkono mpango huo.

Imatafsiriwa na kuchapishwa na Seif Abdalla