Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini Iran inahusika katika migogoro mingi?
- Author, Luis Barrucho
- Nafasi, BBC World Service
Wakati vita huko Gaza vikiendelea, jukumu la Iran katika Mashariki ya Kati linavutia hisia za ulimwengu.
Iran inaunga mkono Hamas katika mzozo wa Israel na Gaza, na imeanzisha mashambulizi dhidi ya Iraq, Syria na Pakistan, na silaha zake zimetumiwa na Urusi dhidi ya Ukraine.Ingawa Iran inakanusha kuhusika moja kwa moja katika baadhi ya mashambulizi katika Mashariki ya Kati - kama vile mashambulizi dhidi ya Israel kutoka Lebanon, mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya wanajeshi wa Marekani nchini Jordan, na mashambulizi yaliyolenga meli za Magharibi katika Bahari ya Shamu kutoka kambi za Yemen - makundi yanayoungwa mkono na Iran yakiri kuhusika.
Lakini makundi haya ni kina nani na ni nini ushiriki wa Iran katika migogoro hii?
Je, Iran inaunga mkono makundi gani?
Kuna wingi wa makundi yenye silaha kote Mashariki ya Kati yenye uhusiano na Iran, ikiwa ni pamoja na Hamas huko Gaza, Hezbollah nchini Lebanon, Houthis nchini Yemen, na wengine walioko Iraq, Syria na Bahrain.
Kinachojulikana kama "axis of resistance", mengi ya makundi hayo yametengwa kuwa makundi ya kigaidi na nchi za Magharibi, na kwa mujibu wa Ali Vaez, mtaalamu wa Iran katika Taasisi ya Kundi la Mgogoro, wana lengo moja: "Kulinda eneo dhidi ya Vitisho vya Marekani na Israel.
"Mtazamo mkubwa ambao ni tishio la Iran ni kuhusiana na Marekani, na baada ya hapo tu ni Israel, ambayo Iran inaiona kama kibaraka wa Marekani katika eneo," anasema na kuongeza: "Mchezo mrefu wa Iran umeunda mtandao huu wa ajabu unaoiruhusu kuwa na nguvu."
Iran ilikanusha kuwa ilihusika moja kwa moja na shambulio la ndege zisizo na rubani huko Jordan tarehe 28 Januari, ambalo liliua wanajeshi watatu wa Marekani, lakini kundi la Islamic Resistance la Iraq, ambalo linaundwa na makundi mengi yakiwemo baadhi ya wanaoungwa mkono na Iran, lilidai kuhusika na shambulizi hilo.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa wanajeshi wa Marekani kuuawa na mashambulizi katika eneo hilo tangu shambulio baya la Hamas la Oktoba 7 dhidi ya Israel, ambalo lilizusha vita huko Gaza, hivyo shinikizo lilikuwa kwa Rais wa Marekani Joe Biden kulipiza kisasi.
Kujibu shambulizi hilo, Marekani ilishambulia Jeshi la Walinzi wa Iran (IRGC) vikosi vya Kikurdi na wanamgambo washirika huko Iraq na Syria wiki moja baadaye, na mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Uingereza juu ya shabaha ya Houthi inayoungwa mkono na Iran nchini Yemen ikafuata.
Iran mara nyingi hujikuta kwenye ukingo wa migogoro, ingawa imepita zaidi ya miongo mitatu tangu nchi hiyo ilipokuwa rasmi katika vita mara ya mwisho.
Ingawa Iran mara kwa mara inakanusha kuhusika moja kwa moja na washirika wale, Tehran imeunga mkono makundi ya wanamgambo tangu mapinduzi ya nchi hiyo, miaka 45 iliyopita, na wakawa sehemu mashuhuri ya mkakati wa usalama wa taifa wa utawala huo mwanzoni mwa miaka ya 1980.
Historia ya Iran na uhusiano wake na Marekani
Matukio mawili katika historia ya kisasa ya Iran yanasaidia kueleza nafasi ya nchi katika eneo hili na uhusiano wake mbaya na Marekani.
Mapinduzi ya Irani ya 1979 yalishuhudia Iran ikitengwa na Magharibi.
Huko Marekani, utawala wa Jimmy Carter ulikuwa na hamu kubwa ya kuwaachilia wanadiplomasia 52 wa Marekani waliokuwa wakishikiliwa mateka katika mji mkuu wa Iran wa Tehran kwa takriban mwaka mmoja, na kulikuwa na hisia kwamba Iran ilistahili kuadhibiwa na kutengwa katika jukwaa la kimataifa.
Hii ilipelekea Marekani na washirika wa Magharibi kupendelea Iraq, ambayo ilitawaliwa na Saddam Hussein kutoka 1979 hadi 2003, dhidi ya Iran.
Vita vya Iran na Iraq vilizuka na kudumu kuanzia mwaka 1980 hadi 1988.
Mzozo huo uliisha kwa Iran na Iraq zote kukubaliana kusitisha mapigano, lakini kwa gharama kubwa, watu milioni moja waliuawa au kujeruhiwa pande zote mbili, na uchumi wa Iran kuharibiwa.
Hili lilizua fikra miongoni mwa maafisa wakuu wa Iran kwamba Tehran ilihitaji kuwa na uwezo wa kuzuia uvamizi wowote katika siku zijazo kupitia njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuendeleza mpango wa makombora ya balistiki na mtandao wa washirika.
Baadaye, uvamizi ulioongozwa na Marekani dhidi ya Afghanistan (2001) na Iraq (2003), pamoja na maasi mbalimbali katika ulimwengu wa Kiarabu kuanzia 2011 na kuendelea yaliimarisha mtazamo huo.
Iran inataka nini na kwanini?
Upande wa kijeshi, Iran inachukuliwa kuwa dhaifu zaidi kuliko Marekani, kwa hivyo wataalam wengi wanaamini kuwa mkakati huu unaoitwa wa kuzuia ni muhimu katika kuendelea kwa utawala wa Irani.
"Vita na Marekani ni jambo la mwisho ambalo Iran na ‘axis of resistance’ wanataka," anasema Alex Vatanka, ambaye ni mkurugenzi mwanzilishi wa mpango wa Iran katika Taasisi ya Mashariki ya Kati (MEI).
"Iran inataka kuishinikiza Marekani kutoka Mashariki ya Kati. Huu ni mkakati wa muda mrefu wa kuchosha upande mwingine," Vatanka anasema.
Kamran Martin kutoka Chuo Kikuu cha Sussex nchini Uingereza anakubali, na anahoji kuwa Iran inataka kuwa mchezaji mwenye nguvu katika jukwaa la dunia.
"Iran ya kale, ambayo kihistoria inajulikana kama Uajemi, ina historia hii na ilikuwa taifa kubwa la Asia ya Magharibi kwa zaidi ya karne 12," mhadhiri mkuu wa uhusiano wa kimataifa anaeleza.
"Iran inaamini kuwa inastahiki nafasi kubwa katika masuala ya kieneo na kimataifa, pamoja na utamaduni wake tajiri wa sanaa na fasihi ya Kiajemi unaozingatia mtazamo huu wa Iran kama dola na nguvu kubwa."
Iran ina udhibiti kiasi gani?
Mwanaharakati wa kisiasa na mwanazuoni wa Kiirani Yassamine Mather, kutoka Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, anahoji kuwa Iran haina udhibiti mkubwa hivyo kwa washirika wake.
Akiwatumia Wahouthi wa Yemen wanaoshambulia meli katika Bahari ya Shamu kwa mfano, Mather anasema: "Hawafuati tu amri za Iran. Wana ajenda yao ya kuonekana kama jeshi lenye nguvu ndani ya eneo, na sio tu washirika wa Iran."
Ali Vaez, kutoka Crisis Group, anakubaliana na hilo. "Tatizo kwa taifa kama Iran, kutoa sera yake ya kikanda kwa watendaji wasio wa serikali, ni kwamba haina udhibiti kamili wa mtandao."
Hata hivyo, Iran ina mpango wa nyuklia, ambao Vaez anasema "sasa umeendelea zaidi kuliko wakati wowote katika miaka 20 iliyopita" na anadhani hii inaweza kusababisha "tatizo kubwa zaidi kwa Israeli na Magharibi, kuliko kile Iran inachofanya kupitia mtandao wa washirika na vibaraka wake".
'Vita vya Tatu vya Dunia?'
Mashambulizi yanapoongezeka katika eneo lote, ndivyo pia utafutaji wa mtandaoni unapozunguka maneno "Vita vya Tatu vya Dunia".
Vatanka kutoka MEI anasema Iran lazima iwe na uangalifu kwa sababu inakabiliwa na shinikizo kutoka ndani ya mipaka yake, kufuatia maandamano ambayo hayajawahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni, yakiongozwa na wanawake dhidi ya serikali.
"Kuna idadi ya watu wa Iran waliokasirika sana ambao hawaoni mantiki katika kile ambacho utawala wa Tehran unafanya katika eneo hilo."
Kadhalika, nchi za Magharibi hazitaki vita na Iran aidha anasema Ellie Geranmayeh, ambaye ni naibu mkuu wa mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni.
"Rais wa Marekani hawezi kumudu hili wakati wa maandalizi ya uchaguzi. Israel haiwezi kumudu hili wakati inajua kwamba iko katika mazingira magumu sana kwa sasa kimataifa, kutokana na operesheni zake huko Gaza," anasema.
Pia, Geranmayeh, kama wataalam wengi wanavyokubali kwamba vita kamili haiko katika ajenda ya upande wowote.
Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi