Jinsi Marekani 'ilivyoishangaza' Israel katika baraza la Usalama la UN

Tunaanza ziara ya waandishi wa habari na magazeti ya Israel, ambayo yalijaribu katika baadhi ya makala zao kueleza umuhimu wa kutopiga kura kwa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu rasimu ya azimio la kusitisha mapigano huko Gaza wakati wa mwezi wa Ramadhani.

Katika gazeti la "Israel Hayom" chini ya kichwa "Marekani iliishangaza vipi Israel?" Mwandishi na mchambuzi Sherit Avitan Cohen anaelezea kilichokuwa kikitokea saa za mwisho kabla ya upigaji kura katika Baraza la Usalama.

Anasema, "Mazungumzo ya siri, shinikizo la kidiplomasia, na mvutano unaoongezeka. Haya ndiyo masaa yaliyotangulia mzozo unaoongezeka kati ya Israel na Marekani kuhusu kuandaa maandishi ya azimio la Baraza la Usalama, na ulijumuisha viwango vyote kati ya mataifa hayo mawili.

“Awali Israel ilijaribu kushirikiana na Marekani kulainisha sehemu ya azimio hilo, lakini hilo liliposhindikana, Israel ilijaribu kuishawishi Ikulu ya White House kutumia mamlaka yake ya kura ya turufu, na hilo liliposhindikana, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitoa kauli kali dhidi yake ya Marekani, na kuuweka hadharani mgogoro huo.” Kulingana na Cohen.

Cohen ananukuu uvujaji uliopatikana na gazeti la Israel Hayom kabla ya upigaji kura, unaoeleza kuwa "mazungumzo yalifanyika usiku kati ya Waziri Ron Dermer na maafisa wakuu katika Ikulu ya White House, na kati ya Balozi wa Umoja wa Mataifa Gilad Erdan na mwenzake, Balozi Linda Thomas. -Greenfield.

Licha ya mafanikio ya Marekani katika Mazungumzo haya ya kufifisha rasimu ya awali ya azimio hilo, mwishowe kuachiliwa kwa mateka na usitishaji vita viliunganishwa na kuwa kifungu kimoja, na azimio hilo pia halikulaani harakati ya Hamas baada ya mashambulizi ya Oktoba. 7.”

"Mambo haya yaliifanya Israel kumtaka katika masaa ya mwisho rafiki yake mkubwa kutumia kura yake ya turufu dhidi ya pendekezo hilo, akimaanisha Marekani," kwa mujibu wa mwandishi huyo.

"Lakini basi maafisa wakuu wa Israeli walisikia kwa mara ya kwanza kwamba ngazi za juu katika Ikulu ya White House zinasisitiza wakati huu kutotumia kura ya turufu, jambo ambalo liliishangaza Israeli, ambayo iliona uamuzi huo kuwa hatari kubwa, kwa sababu tafsiri zake zilikuwa pana na zinaweza kusababisha tatizo kubwa kwa Israeli,” kulingana na kile ambacho Mwandishi Cohen alitaja.

Katika gazeti la Jerusalem Post, mtafiti na msomi Susan Hatice-Rolfe, aliyekuwa mshiriki wa Baraza la Knesset la Israel, alichapisha makala yenye kichwa “Kujitenga kwa Israeli kunaongezeka, na masuluhisho ni ya kipuuzi chini ya serikali ya sasa.”

Mwandishi anaanza makala yake kwa kurejelea yale ambayo gazeti The Economist lilichapisha Jumamosi iliyopita, ambapo lilisema katika kichwa chake cha habari “Israeli peke yake.” Rolfe anasema kwamba wiki zilizofuata shambulio la Oktoba 7 zilileta uungwaji mkono wa ajabu kutoka kwa viongozi wa dunia kwa Israeli, na "walihalalisha jibu lake kali la kijeshi, ambalo lilijumuisha kuelekeza mashambulizi mabaya ya kijeshi na kiutawala dhidi ya Hamas, wakati utawala wa Marekani ulikwenda mbali zaidi ya hapo, na kuahidi kuipatia Israeli silaha na risasi zote inazohitaji, pamoja na kusafirisha shehena ya ndege na majeshhi ya Marekani katika eneo hilo.

Israeli inaweza kufanya nini ili kujilinda?

“Je, kuna njia ya kuwashinda Hamas kwa idadi ndogo zaidi ya vifo vya raia? Je, kuna njia ya kupigana vita ambayo haviwaachi Israeli pekee?” Swali lililoulizwa na mwandishi wa New York Times David Brooks, katika makala aliyochapisha ambayo anazungumzia maoni yanayoielezea Israel kuwa imetengwa katika vita vyake, haswa kutokana na kuzorota kwa uhusiano wake na Marekani.

Mwandishi anakiri kwamba mkakati wa Israeli unakabiliwa na matatizo halisi. Maoni ya umma ya ulimwengu yanasonga mbele dhidi ya Israeli, na mabadiliko makubwa katika uhusiano yamekuwa na Washington, ambapo wafuasi wakubwa wa kihistoria wa Israeli wameanza kukosoa.

Mwandishi anauliza: "Ikiwa mbinu ya sasa ya kijeshi ya Israeli sio ya kibinadamu, ni nini mbadala?"

Kulingana na ukweli kwamba Israel ina haki ya kujilinda na kupigana na Hamas baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, anasema, "Ukweli mwiba unaojitokeza ni kwamba vita hivi ni kidogo sana kama vita vingine, kwa sababu ukumbi wa michezo wa maamuzi uko chini ya ardhi," akimaanisha mtandao mkubwa wa vichuguu ambavyo Hamas ilijenga, na Israeli inashutumu kwamba Hamas hutumia vichuguu hivi kuhifadhi silaha, kutengeneza makombora, kushikilia mateka, na zaidi.

Waisraeli hawapati njia rahisi ya kuharibu vichuguu isipokuwa kwa kusafisha ardhi, lakini hii ina madhara ya hatari na ya uharibifu, kwa sababu majengo machache yanaweza kustahimili milipuko mikubwa, ambayo husababisha uchafu mwingi na uharibifu, kulingana na makala, ambayo inasema kwamba uharibifu uliosababishwa na Israeli huko Gaza ni mkubwa zaidi kuliko yale ambayo Syria ilifanya huko Aleppo na zaidi ya yale ambayo Urusi ilifanya huko Mariupol, kulingana na uchambuzi uliochapishwa na Associated Press.

Wakati huohuo Brooks anabainisha kuwa Israel ilichukua hatua na majaribio mengi ya kuwalinda raia wakati wa vita, kwa kuwaonya juu ya kuwashambulia kwa mabomu na kuwaelekeza katika maeneo salama, lakini kulikuwa na vikwazo vinavyohusiana na kutokuwepo kwa mitandao ya mawasiliano na kukatika kwa umeme, jambo ambalo limesababisha vifo vya watu wengi..

Brooks anaamini kwamba mkakati uliopitishwa na Hamas ni "uovu mtupu." Lakini msingi wake ni kuelewa jinsi matukio ya ardhini yanavyoweza kustawi katika ulimwengu wa kisiasa, wakati udhaifu mkuu wa mkakati wa Israel siku zote umekuwa kwamba inalenga kuwashinda Hamas kijeshi bila ya kushughulikia malalamiko ya Wapalestina na bila ya kuzingatia vya kutosha matokeo mapana zaidi.

Aliongeza, "Viongozi wa Hamas wanapotazama Washington ikiongeza ukosoaji wake kwa Israel, wana uhakika kwamba mkakati wao umefanikiwa."

Mkakati mmoja mbadala ni Israel kufanya kampeni ndogo sana dhidi ya Hamas na kwa nguvu ndogo. Israel lazima pia iwasilishe kwa ulimwengu maono ya kuijenga Gaza, kulingana na mwandishi.

Lakini kutokana na "hali ya uhasama mkali sasa inayolikumba eneo hilo," kama mwandishi anavyoeleza, haiwezekani kwa Waisraeli na Wapalestina kuchukuwa maono mapya ya siku zijazo hadi Hamas itakaposhindwa kabisa kama jeshi tawala.

Ujasiri wa kidiplomasia wa Kiarabu unahitajika

Mzozo wa Marekani na Israel unazidi kutokota katika Ikulu ya White House, na mzozo huo unaanza kufichuka wazi, kwa mujibu wa makala ya mwandishi wa habari wa Lebanon Sam Mansi katika gazeti la Asharq Al-Awsat, ambapo anawataka Waarabu kuchukua hatua za ujasiri za kidiplomasia kutumia mzozo kati ya washirika wawili wa kihistoria, Marekani na Israel.

Anasema: “Wakati ambapo uhusiano wa Marekani na Israel umefikia kiwango hiki cha mvutano, sauti za Wapalestina na Waarabu zinaongezeka kutoka upande zaidi ya mmoja, kuanzia kuhoji na kukataa misimamo ya Washington, hadi kuituhumu kuwa inapanga kubaki Gaza, ikizingatiwa kuwasili kwa majeshi wa Marekani kwenye ardhi ya Gaza ikiwa ni mwanzo wa uwepo wa Mmarekani wa muda mrefu katika sekta hiyo...

Uwasilishaji huu wa hali ya mahusiano kati ya utawala wa Marekani na Netanyahu uko mikononi mwa Wapalestina hasa Waarabu kwa ujumla, kwa sababu ni ujinga kupuuza mabadiliko haya katika sera ya Washington katika hatua hii, na ni muhimu kushika fursa hii ambayo inaweza kuwa na mipaka kwa wakati na mahali kabla ya kuzama katikati ya uchaguzi wa rais na kile ambacho wanaweza kusababisha, haswa ikiwa Donald Trump atafika Ikulu ya White House.

Mansi anasisitiza kuwa mzozo huo ni kati ya utawala wa Joe Biden na serikali ya Benjamin Netanyahu na washirika wake kutoka kwenye haki ya itikadi kali, na si na Israel, au taifa hilo.

Hata hivyo, "Washirika wa Marekani wa Kiarabu lazima wafanye kazi kwa bidii ili kuoanisha misimamo ya Marekani kwa ajili ya lengo la Palestina, na kujenga juu yao ili kuiendeleza, na sio Kutoa visingizio vya Waisraeli kuungana tena na Washington," kulingana na mwandishi.

Al-Mansi anafafanua hatua zinazohitajika katika hatua inayofuata, ambazo ni: "Kwanza, uwazi juu ya chaguo la amani na tofauti kati ya adui, rafiki, mpenzi na mshirika, pili, uhalisia na tofauti kati ya iwezekanavyo, magumu na yasiyowezekana. , tatu mageuzi ya Wapalestina, na hatimaye kufaidika na mafunzo ya vita hivi, kuanzia na makumi ya maelfu ya waathiriwa wasio na hatia na hasara mbaya ya nyenzo..

Pamoja na hayo kuna mabadiliko ya kimataifa ambayo yanawahurumia Wapalestina na si lazima kwa Hamas, ambayo ni huruma ya kimataifa isiyo na kifani.”

Mwishoni mwa makala yake, mwandishi huyo anasema: “Kukutana na Marekani katikati ni hitaji la dharura la kimkakati la Waarabu na Wapalestina, kibinadamu na kisiasa, kujinasua kutoka katika mduara uliofungiwa ambapo mzozo wa Israel na Palestina unafanyika na athari zake kwa usalama wa kikanda, haswa baada ya matokeo ya vita huko Gaza na athari zake katika siku zijazo.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla