Kiongozi mkuu wa Hamas Ismail Haniyeh ameuawa nchini Iran - kundi hilo lasema

Muda wa kusoma: Dakika 2

Na Thomas Mackintosh

BBC News

Kiongozi mkuu wa Hamas Ismail Haniyeh ameuawa nchini Iran, kundi hilo limesema.

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano, Hamas ilisema Haniyeh aliuawa katika uvamizi wa Israel kwenye makazi yake mjini Tehran.

Kwa mujibu wa kundi hilo, Haniyeh alifariki baada ya kushiriki sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Iran Masoud Pezeshkian aliyeapishwa siku ya Jumanne.

Hakuna aliyekiri kuwajibika na mauaji hayo

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Irani (The Iranian Revolutionary Guard Corps) lilisema chanzo cha "tukio" hakijafahamika mara moja lakini "kinachunguzwa", shirika la habari la AFP liliripoti.

Kundi la Wapalestina linalodhibiti Gaza lilisema Haniyeh "aliuawa katika uvamizi wa kihaini wa Wazayuni".

Israel bado haijajibu au kutoa taarifa.

Ismail Haniyeh ni nani?

Haniyeh, mwenye umri wa miaka 62, alikuwa mwanachama mashuhuri wa vuguvugu la Hamas mwishoni mwa miaka ya 1980.

Israel ilimfunga Haniyeh kwa miaka mitatu mwaka 1989 huku ikikabiliana na uasi wa kwanza wa Wapalestina.

Kisha alihamishwa mwaka 1992 hadi ardhi isiyomilikiwa na nchi yoyote kati ya Israel na Lebanon, pamoja na baadhi ya viongozi wa Hamas.

Haniyeh aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa Palestina mwaka 2006 na Rais Mahmoud Abbas baada ya Hamas kushinda viti vingi zaidi katika uchaguzi wa kitaifa, lakini alifutwa mwaka mmoja baadaye baada ya kundi hilo kukiondoa chama cha Fatah cha Bw Abbas kutoka Ukanda wa Gaza katika wiki moja ya ghasia .

Haniyeh alikataa kuondolewa kwake kama "kinyume cha katiba", akisisitiza kwamba serikali yake "haitaacha majukumu yake ya kitaifa kwa watu wa Palestina", na kuendelea kutawala huko Gaza.

Alichaguliwa kuwa mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas mnamo 2017.

Mnamo 2018, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilimtaja Haniyeh kuwa gaidi . Amekuwa akiishi Qatar kwa miaka kadhaa iliyopita.

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah