Mauaji ya Haniyeh ni kikwazo kwa usitishaji mapigano

    • Author, Jeremy Bowen
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Israel imefanya mapigo mawili makubwa kwa maadui zake.

Haijathibitisha kwamba ilimuua kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh huko Tehran, lakini ni vigumu kuamini ni nani mwingine angetaka auawe zaidi ya Israel. Kuhusu kamanda wa Hezbollah Fuad Shukr, Israel inasema imemuua huko Beirut.

Kwa Israel, kila kiongozi mkuu wa Hamas ni halali kumlenga baada ya mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023, ilikuwa ni siku moja mbaya zaidi ya umwagaji damu kwa Israeli tangu kuundwa taifa hilo 1948.

Fuad Shukr, Israel inasema, aliuawa kwa sababu alihusika na shambulio la roketi lililoua watoto na vijana 12 katika Milima ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel.

Hezbollah imethibitisha kuwa aliuawa katika sambulizi la Beirut. Lakini inakanusha kutekeleza shambulio katika milima ya Golan.

Kwa mara nyingine tena, Mashariki ya Kati imejaa hofu kwamba vita vya pande zote vinavyohofiwa tangu tarehe 7 Oktoba vinakaribia. Licha ya kuwa hakuna upande unaotaka vita kutanuka.

Israel imekuwa ikishinikizwa na washirika wao Marekani, kutoa jibu kwa kundi la Hezbollah litakalowaumiza bila kuangamiza na kuzua vita vikubwa zaidi.

Lakini mauaji ya viongozi wawili wakubwa ni sawa na kucheza na shilingi karibu na shimo la choo.

Kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah, anaweza kuamua kwamba shambulio dhidi ya ngome yao kusini mwa Beirut itajibiwa kwa shambulio la kuilenga Tel Aviv.

Israeli pia inaweza kuwa na mahesabu kwamba Iran haitaingia vitani juu ya kiongozi wa Palestina aliyeuawa, ingawa kifo chake katika mji mkuu wao, chini ya ulinzi wao, ni fedheha.

Kumuua Haniyeh, baada tu ya kukutana na rais mpya wa Irani, ni maonyesho makubwa ya nguvu za Israel.

Hatari ya mzozo mkubwa

Jamhuri ya Kiislamu ilifikiri kuwa iliweka kizuizi iliporusha mamia ya makombora na ndege zisizo na rubani kwenda Israel mwezi Aprili – fikra hizo kumbe sio za kweli.

Shambulizi la Aprili pia lilikuwa ni kulipiza kisasi, kwa shambulio la anga la Israel lililoua majenerali wawili wa Iran katika ubalozi wa Iran mjini Damascus.

Wanamgambo wanaoiunga mkono Iran nchini Iraq wameweka wazi kuwa wanailaumu Marekani kwa kile kilichotokea. Na katika Bahari ya Shamu, Houthis wanaweza kuongeza mashambulizi yao kutoka Yemen.

Ni muhimu kutambua kwamba Mashariki ya Kati tayari iko katika vita vya kikanda, lakini pia ni muhimu kujua kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

Katika eneo lenye misukosuko zaidi duniani, mauaji na kulipiza kisasi inafanya kuwa vigumu kujenga njia ya kidiplomasia ili kusiwe na tishio la migogoro ya pande zote.

Njia pekee ya kuepuka vita kuenea

Hatua pekee ya kuaminika ya kupunguza mvutano Mashariki ya Kati ni kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.

Wiki chache nyuma, Marekani ilisema usitishwaji wa mapigano ulikuwa unakaribia. Hilo lilikuwa gumu kufikiria, kwani pande hizo mbili za mzozo zina maana isiyolingana ya usitishaji mapigano.

Kwa Hamas, usitishaji mapigano unamaanisha kujiondoa kwa Israel huko Gaza na mwisho wa uhasama. Kwa Israel, inamaanisha kusitisha kwa muda ili iliruhusu kuachiliwa baadhi au mateka wote waliosalia, na kuanzisha tena vita baadaye.

Sasa usitishaji mapigano huko Gaza unaonekana kuwa mbali kama zamani, ingawa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema bado ni kipaumbele cha kidiplomasia ya Marekani.

Ismail Haniyeh alikuwa kiongozi wa upande wa Hamas katika mazungumzo ya kusitisha mapigano. Akiwa na wenzake, akiwasiliana na Marekani na Israel kupitia mkuu wa usalama wa taifa wa Misri na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohamed bin Jassim al Thani.

Waziri Mkuu alichapisha majibu yake kwa mauaji ya Haniyeh kwenye X, akiandika: "Mauaji ya kisiasa na kuendelea kuwalenga raia huko Gaza wakati mazungumzo yanaendelea, inatufanya kuuliza namna upatanishi huu unavyoweza kufanikiwa wakati upande mmoja unaua mpatanishi wa upande mwingine."

Mauaji hayo yanalingana na dhana ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ya "ushindi kamili" dhidi ya Hamas, kuliko wazo la Marekani kwamba usitishaji mapigano ni muhimu ili kuepuka janga kubwa zaidi la kikanda.

Pia itaimarisha imani ya wakosoaji wa Netanyahu ndani na nje ya Israel kwamba anataka kurefusha vita, ili kuepusha wakati wa kutazama makosa aliyoyafanya ambayo yaliwapa nafasi Hamas kushambulia na matokeo mabaya Oktoba 7.

Marekani na Ufaransa pia zimejitahidi sana kutafuta njia ya kidiplomasia ya kukomesha vita kati ya Israel na Hezbollah. Lakini hatua muhimu ya kwanza itakuwa usitishaji mapigano huko Gaza, hatua ambayo ambayo tayari imepata pigo jingine.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla