Rais wa Kenya apata pigo mara mbili katika mipango yake ya kodi
Basillioh Rukanga na Jewel Kiriungi
BBC News, Nairobi

Chanzo cha picha, Reuters
Bila shaka Rais wa Kenya William Ruto anajihisi kukwama - baada ya kupata pigo jingine kwa mipango yake ya kuongeza ushuru kwa serikali yake yenye ukosefu wa fedha na inayolemewa na madeni.
Baada ya maandamano ya hivi majuzi ya kupinga ushuru - ambayo yalishuhudia bunge likichomwa moto - alikubali shinikizo la umma na kuondoa mswada wake wa fedha wa kipindi kipya cha fedha .
Lakini wiki iliyopita mahakama ya rufaa ilivunja mipango yake ya kodi ya mwaka jana .
Majaji watatu kwa kauli moja waliamua kwamba sheria ya 2023 iliyopandisha ushuru kwenye mishahara, mafuta na miamala ya pesa kwa njia ya simu "ilikuwa na dosari kubwa" na "kinyume cha katiba" kwa kuwa haikufuata taratibu zilizowekwa.
Hatua zote mbili zinaleta changamoto kwa uwezo wa serikali kukusanya fedha za ziada kufadhili bajeti ya taifa na kulipa deni lake la umma la $78bn (£61.4bn).
Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya bajeti, Ndindi Nyoro, aliiambia BBC kuwa uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama unaweza kusababisha upungufu mkubwa katika bajeti ya mwaka huu na kuifanya serikali isiweze kuendesha shughuli zake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Ukiangalia hatua zote mbili za kifedha ambazo sasa zimezuiwa , kwa jumla, tunazungumzia zaidi ya shilingi trilioni nusu [$3.8bn] kama mapato yaliyopotea," Bw Nyoro alisema.
Serikali inawasilisha mswada wa sheria ya fedha bungeni kabla ya mwanzo wa kila mwaka wa fedha mwezi Julai, ikiwasilisha kodi mpya au kubadilisha zilizopo, ili kupata pesa zaidi.
Wakati huo huo serikali pia inawasilisha kile kinachojulikana kama mswada wa matumizi - hii inaonyesha jinsi mapato yatakavyogawanywa na kutumika katika idara zote za serikali.
Mkwamo katika fedha za serikali umedhihirika wakati mswada wa matumizi ya mwaka huu ulipotiwa saini kuwa sheria huku wakati huo huo mswada unaolingana wa fedha wa kufadhili mpango wa matumizi ukiondolewa.
Huku mipango ya serikali ya kodi kwa miaka miwili mfululizo ikivurugika, wachambuzi wanasema huenda matumizi yakalazimika kuwiana na sheria ya fedha kuanzia 2022.
Mwanauchumi Odhiambo Ramogi anasema uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama pia unaleta shaka kwa walipa kodi, ingawa mahakama iliamua kwamba ushuru ambao tayari umekusanywa hauwezi kurejeshwa.
Serikali imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo katika Mahakama ya Juu, mahakama kuu nchini humo - na kuomba uamuzi wa mahakama ya mwanzo usitishwe hadi rufaa yake isikizwe.
Ilisema kuwa haikuwezekana kusanidi upya mifumo mara moja kwa sheria ya 2022, na hali hiyo inaweza kusababisha kukwama kwa baadhi ya huduma za serikali.
Mahakama ya Juu ilikataa lakini ikakubali kuwa ni suala la dharura na kwamba kesi hiyo itasikilizwa mwezi huu - ingawa kwa kawaida mwezi Agosti huwa ni kipindi cha mapumziko kwa mahakama.

Chanzo cha picha, AFP
Shinikizo la mara moja huenda likatoka kwa Wakenya wanaotatizika kifedha ambao wanataka kuona bei za bidhaa zikishuka, anasema mwanauchumi Ken Gichinga.
Mfano mzuri utakuwa ni kushuka kwa bei ya petroli.
"Watu watataka ufafanuzi kuhusu bei ya mafuta," aliambia BBC.
Bw Ramogi anasema chaguo bora kwa serikali ni "kutayarisha upya mswada mwingine wa fedha".
Lakini ikizingatiwa kwamba Wakenya wanapinga vikali ushuru mpya, jambo la mbadala litakuwa ni kukopa zaidi, anasema.
Hata hivyo hilo pia linaweza kuwa gumu, kutokana na viwango vya deni la nchi vay makadirio ya mashirika ya kimataifa ya viwango vya mikopo ya Moody's na Fitch.
Wengine wanapendekeza kuwa suluhisho linaweza kuwa kuongeza kodi ambazo ni za kibunifu na zisizowaumiza kupita kiasi raia - ingawa haijulikani wazi ni jinsi gani hilo linawezekana.
Wataalamu wote wanasema kwamba kwa sheria yoyote ya ushuru ya siku zijazo, wabunge watahitaji kujumuisha maoni ya umma.
"Ushirikiano wetu wa kitaifa na mazungumzo kuhusu masuala ya umma vinabadilika," mtaalamu wa sera na utawala Vincent Kimosop aliiambia BBC, akieleza kuwa Wakenya sasa wanashiriki kikamilifu katika jinsi nchi yao inavyoendeshwa.
Kupunguzwa kwa matumizi pia kunapaswa kuendelea.
Bw Nyoro anasema serikali tayari imepunguza kwa kiasi kikubwa na bado inaweza kulazimika kuondoa bajeti yake yote ya maendeleo na mishahara ya wafanyikazi wa serikali.
"Nisingependa kufikiria kuwa bajeti ya elimu inapunguzwa, usumbufu wa ufadhili wa elimu ya juu, kupunguzwa jwa watumishi wa umma, na kuzorota kwa huduma za afya ," alisema.
Tatizo kubwa kwa uchumi wa Kenya lilikuwa mzigo wa madeni ambao nchi hiyo imejitwika kwa miaka 12 iliyopita, aliongeza.

Chanzo cha picha, AFP
Katika kujibu hatua ya kuondolewa kwa mwada wa fedha , Bw Ruto alitia saini mswada wa sheria wa matumizi ya ziada ili kuendana na kupunguzwa kwa mapato kunakotarajiwa Jumatatu.
Inapunguza matumizi ya serikali kwa takriban $1.2bn, na kupunguzwa kwa matumizi katika ofisi ya rais, wizara na ufadhili wa uchukuzi na miradi mingine ya maendeleo.
Hatua hiyo imepigiwa debe na kamati ya bajeti ya bunge kuwa "inapunguza matumizi, na kuleta uwiano kati ya hatua za kubana matumizi na kuboresha maisha ya watu na uchumi".
Lakini serikali pia inakabiliwa na changamoto zaidi ya kisheria, na vikundi viwili vya haki vinapinga mamlaka ya serikali kutumia bila kuzalisha mapato sawa na matumizi.
Wanahoji kuwa mchakato wa nyongeza wa bajeti bungeni haukufuata sheria - na wameomba mahakama kuingilia kati "kukomesha kuhujumiwa mara kwa mara wa katiba yetu".
Serikali italazimika kushughulikia hilo mahakamani inaposubiri matokeo ya rufaa yake katika Mahakama ya Juu.
Bw Nyoro anasema "hakuna hakikisho la kufaulu" kwa serikali katika vita vyake mahakamani - na maamuzi yote ambayo Bw Ruto anayakabili ni magumu.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla












