Yevgeny Prigozhin:Je,Putin atatekeleza ahadi yake kumsamehe?

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Mkuu wa kundi la mamluki la Wagner bado anachunguzwa na mamlaka ya Urusi licha ya Kremlin kuahidi kufuta mashtaka yote dhidi yake, kwa mujibu wa mashirika matatu makuu ya habari ya Urusi na gazeti jingine.

Shirika la kijasusi la ndani la Urusi, FSB, bado lina kesi iliyofunguliwa dhidi ya Yevgeny Prigozhin, kulingana na vyanzo ambavyo havikutajwa vinazungumza na vyombo vya habari.

Chini ya makubaliano yaliyopatanishwa na kiongozi wa Belarus Alexander Lukahsenko kutatua mgogoro huo mwishoni mwa Jumamosi, Kremlin ilisema kesi ya jinai dhidi ya Prigozhin itafutwa na wapiganaji wake hawatachukuliwa hatua za kisheria.

Lakini tovuti ya Kommersant, ikinukuu chanzo kisichojulikana, ilisema uamuzi wa kuanzisha kesi ya jinai bado haujafutwa, na uchunguzi wa uasi huo unaendelea. Kiliendelea kunukuu chanzo hicho kikisema muda hautoshi wa kufunga kesi hiyo.

Ili kuwa wazi, maelezo haya yanatoka kwa vyombo vya habari vya Urusi, na bado hatujaweza kuyathibitisha kwa njia huru.

Bado haijulikani ni nini hasa maana ya mpango huo, na bado hatujasikia kutoka kwa Prigozhin au kiongozi wa Urusi Vladimir Putin.

Kiongozi wa Wagner bado hajaonekana popote.

Kremlin alisema wikendi hii kwamba alikuwa akienda Belarusi.

Prigozhin - ambaye hutoa jumbe za sauti kama kawaida yake- hadi sasa hajasema chochote.

Putin kusamehe 'usaliti'?

th

Chanzo cha picha, Reuters

Ujumbe unakinzana wa Vladimir Putin umekuwa ukizua hisia na kubadilisha mitazamo ya rais wa Urusi.

Hata hivyo, usitarajie kwamba Rais Putin atakubali kwamba mambo yalikuwa mabaya. Kukubali makosa sio mtindo wake.

Je, ni hatua gani itakayofuata ya rais wa Urusi? Kidokezo, pengine, kilikuja katika toleo la hivi punde zaidi la kipindi cha habari cha televisheni Urusi Jumapili usiku.

Akiripoti juu ya ghasia za Wagner, mtangazaji alicheza dondoo kutoka kwa mahojiano ya zamani ya Putin.

"Je, unaweza kusamehe?"

"Ndiyo. Lakini si kila kitu," Putin anajibu.

"Ni nini huwezi kusamehe?"

"Usaliti."

Iwapo Yevgeny Prigozhin alitazama mahojiano hayo hapo nyuma kabla ya uasi wake basi anajua jibu ya kile kinachoweza kumkumba katika siku zijazo endapo mkataba wake na Putin kumaliza uasi hautatekelzwa na Kremlin.

Putin alijenga 'zimwi'linalomrudia

th

Chanzo cha picha, EPA

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell anasema uasi wa kundi la Wagner mwishoni mwa juma unaonyesha mpasuko katika nguvu za kijeshi za Urusi.

"Mfumo wa kisiasa unaonyesha udhaifu, na nguvu za kijeshi zinapungua," aliwaambia waandishi wa habari huko Luxembourg kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa EU.

"Mnyama huyo ambaye Putin aliunda na Wagner, mnyama huyo anamng'ata sasa - mnyama huyo anamtishia muumbaji wake," Borrell alisema kuhusu mkuu wa Wagner Yevgeny Prigozhin, akiongeza kuwa "si jambo zuri" kuona nchini yenye nguvu ya nyuklia kama Urusi ikitokomea " katika awamu ya machafuko ya kisiasa".

Uasi wa Wagner unaonyesha Putin alifanya makosa makubwa juu ya Ukraine - Nato

TH

Chanzo cha picha, Reuters

Wakati huo huo katibu mkuu wa Nato Jens Stoltenberg, amesema uasi uliositishwa na wanajeshi wa Wagner mwishoni mwa juma ni "dhihirisho jingine la kosa kubwa la kimkakati" ambalo Vladimir Putin alifanya kwa kuivamia Ukraine.

Stoltenberg, ambaye anaongoza muungano wa kijeshi wa nchi 31 zikiwemo Uingereza na Marekani, ameelezea matukio ya mwishoni mwa juma kama "suala la ndani la Urusi".

"Wakati Urusi inaendelea na mashambulizi yake, ni muhimu zaidi kuendeleza msaada wetu kwa Ukraine," aliwaambia waandishi wa habari huko Vilnius, mji mkuu wa Lithuania.