Uchaguzi wa Nigeria 2023: Kura zinahesabiwa lakini matokeo ya mwisho yanaweza kuchukua siku kadhaa

Chanzo cha picha, BB/GIFT UFUOMA
Shughuli ya kuhesabu kura inaendelea katika uchaguzi wa rais wa kinyang’anyiro kikali zaidi nchini Nigeria tangu utawala wa kijeshi ulipomalizika mwaka 1999.
Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilionekana kuwa juu, huku vijana wengi wa wapiga kura wa mara ya kwanza wakifika kabla ya mapambazuko kupiga kura.
Upigaji kura wa Jumamosi ulitawaliwa na ucheleweshaji wa muda mrefu katika vituo vya kupigia kura, pamoja na ripoti zilizosambaa za unyakuzi wa masanduku ya kura na mashambulizi ya watu wenye silaha.
Na baadhi ya vyama vimeibua hofu juu ya madai ya ukiukwaji wa sheria, jambo ambalo linaweza kusababisha matokeo yenye utata.
Uchaguzi huo ni zoezi kubwa zaidi la kidemokrasia barani Afrika, huku watu milioni 87 wakistahili kupiga kura.
Siasa zimetawaliwa na vyama viwili - chama tawala cha APC na PDP - tangu kurejeshwa kwa demokrasia ya vyama vingi miaka 24 iliyopita.
Lakini wakati huu, pia kuna changamoto kubwa kutoka kwa mgombea wa chama cha tatu katika kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Muhammadu Buhari – Peter Obi wa chama cha Labour, ambaye anaungwa mkono na vijana wengi.
Makumi kwa maelfu ya vituo vya kupigia kura vinahesabu matokeo, ambayo yatakusanywa na kutumwa kwenye makao makuu ya uchaguzi katika mji mkuu Abuja.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Matokeo ya mwisho hayatarajiwi hadi angalau Jumanne.
Katika mkutano na waandishi wa habari Jumamosi, mkuu wa uchaguzi, Mahmood Yakubu, aliomba radhi kwa kucheleweshwa kwa upigaji kura, lakini alisema kwamba kila mtu ambaye alikuwa kwenye foleni ifikapo 14:30 saa za nchi hiyo (13:30 GMT) ataruhusiwa kupiga kura, ingawa vituo vya kupigia kura vilipaswa kufungwa rasmi wakati huo.
Wapiga kura katika jiji kubwa zaidi, Lagos, walishangilia wakati maafisa wa uchaguzi walipowasili katika kituo cha kupigia kura katika kitongoji cha Lekki karibu saa nne baada ya shughuli ya kupiga kura kufungwa rasmi.
"Kama Mnigeria unatarajia tukio lolote, kwa hivyo nilitoka na benki yangu ya umeme na chupa ya maji. Nitasubiri hadi wafike ili niweze kupiga kura," mpiga kura wa kwanza Edith aliiambia BBC.
"Kama Mnigeria unatarajia tukio lolote, kwa hivyo nilitoka na kihifadhi umeme na chupa ya maji. Nitasubiri hadi wafike ili niweze kupiga kura," mpiga kura wa kwanza Edith aliiambia BBC.
Taarifa zilizosambaa za mashambulizi ya silaha katika vituo vya kupigia kura
Siku ya uchaguzi kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya amani, lakini kumekuwa na ripoti kutoka Lagos za ghasia na masanduku ya kura kuibwa.
Baadhi ya wapiga kura walilalamikia kushambuliwa na kufukuzwa walipokuwa wamekusanyika kupiga kura.
Katika maeneo mengine, watu waliripotiwa kuombwa ama kumpigia kura mgombea fulani au kuondoka katika kituo cha kupigia kura.
Bw Yakubu alisema kuwa watu waliokuwa na silaha pia walishambulia baadhi ya vitengo vya kupigia kura katika jimbo la kusini la Delta na jimbo la kaskazini la Katsina, ambapo mashine za kuthibitisha kadi za wapiga kura zilibebwa na watu wasiojulikana.
Baadaye kuliletwa mashine zingine na usalama kuimarishwa ili kuruhusu upigaji kura kufanyika, aliongeza.
Lakini upigaji kura uliahirishwa hadi Jumapili katika vituo 141 vya kupigia kura katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Bayelsa kusini mwa nchi kwa sababu ya kutatizwa kwa shughuli hiyo.
Katika jimbo la kaskazini-mashariki la Borno, Bw Yakubu alisema kwamba wanamgambo wa Kiislamu waliwafyatulia risasi maafisa wa uchaguzi kutoka kilele cha mlima eneo la Gwoza, na kuwajeruhi maafisa kadhaa.

Chanzo cha picha, AFP
Hatua ya kuelekea kwenye uchaguzi huo iligubikwa na uhaba wa fedha uliosababishwa na jaribio lisilofanikiwa la kuunda upya sarafu hiyo, na kusababisha machafuko makubwa katika benki na mashine za kutolea fedha huku watu waliokata tamaa wakitafuta kupata pesa zao.
Noti mpya zilianzishwa ili kukabiliana na mfumuko wa bei, na pia ununuzi wa kura. Katika mkesha wa uchaguzi mjumbe wa Baraza la Wawakilishi alikamatwa akiwa na takriban $500,000 (£419,000) taslimu, na orodha ya watu aliotakiwa kuwapa, polisi wanasema.
Yeyote atakayeshinda atalazimika kukabiliana na uundaji upya wa sarafu, uchumi unaoporomoka, ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana, na ukosefu wa usalama ulioenea ambao ulisababisha 10,000 kuuawa mwaka jana.
Wapiga kura pia walipiga kura zao kwa maseneta 109 katika serikali kuu na wabunge 360 wa baraza la wawakilishi, na kura nyingine ikipigwa kwa magavana wa majimbo mnamo mwezi Machi.
Uchaguzi huo umeshuhudia hamu kubwa kutoka kwa vijana - theluthi moja ya wapiga kura wanaostahiki wako chini ya 35.
Bw Obi, mwenye umri wa miaka 61, anatumai kuvunja mfumo wa vyama viwili vya Nigeria baada ya kujiunga na chama cha Labour mwezi Mei mwaka jana.
Ingawa alikuwa katika chama cha PDP kabla ya wakati huo, anaonekana kama sura mpya na anafurahia kuungwa mkono na baadhi ya sehemu za vijana wa Nigeria, hasa kusini.
Mfanyabiashara huyo tajiri aliwahi kuwa gavana wa Jimbo la Anambra kusini-mashariki kutoka 2006 hadi 2014.
Wafuasi wake, wanaojulikana kama "OBIdients", wanasema yeye ndiye mgombea pekee mwenye uadilifu, lakini wakosoaji wake wanahoji kuwa kura yake ilipotea bure kwani yeye hana uwezekano wa kushinda.
Badala yake, PDP, ambayo ilitawala hadi 2015, inataka Wanigeria kumpigia kura Atiku Abubakar, 76 - mgombea pekee mkuu kutoka
Amewahi kugombea kiti cha urais mara tano kabla – lakini zote ameshindwa. Amekuwa akikabiliwa na tuhuma za ufisadi na uhuni, jambo ambalo anakanusha.
Sehemu kubwa ya kazi yake imetumika katika maeneo ya madaraka, akiwa amefanya kazi kama mtumishi wa ngazi ya juu serikalini, makamu wa rais na mfanyabiashara maarufu.
Watu wengi wanaona uchaguzi huo kama kura ya maoni kuhusu APC, ambayo imesimamia kipindi cha matatizo ya kiuchumi na kuzorota kwa ukosefu wa usalama.
Mgombea wake, Bola Tinubu, 70, anasifiwa kwa kujenga kitovu cha kibiashara cha Nigeria Lagos, wakati wa mihula yake miwili kama gavana hadi 2007.
Anajulikana kama baba wa kisiasa katika eneo la kusini-magharibi, ambako ana ushawishi mkubwa, lakini kama Bw Abubakar, pia amekumbwa na madai ya rushwa kwa miaka mingi na afya mbaya, ambayo yote anakanusha.
Mgombea anahitaji kuwa na kura nyingi zaidi na 25% ya kura zilizopigwa katika thuluthi mbili ya majimbo 36 ya Nigeria ili kutangazwa mshindi.
Vinginevyo, kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi ndani ya siku 21 - ya kwanza katika historia ya Nigeria.















