Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
DeepSeek: Programu ya akili mnemba ya China kwenye rada ya usalama wa Marekani
Maafisa wa Marekani wanafuatilia athari kwa usalama wa taifa baada ya uvumbuzi wa programu ya akili bandia (AI) ya China ya DeepSeek, kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha habari cha Ikulu ya White House, Karoline Leavitt.
Tangazo hilo linakuja wakati kukiwa na ripoti kwamba jeshi la wanamaji la Marekani limepiga marufuku wanajeshi wake kutumia programu ya DeepSeek kwa sababu ya "maswala ya usalama na maadili."
Wakati huo huo, kampuni ya OpenAI inayomiliki programu ya ChatGPT, imeahidi kufanya kazi kwa karibu na serikali ya Marekani ili kuzuia wapinzani kuchukua teknolojia yake.
Mapema wiki hii, programu ya AI DeepSeek iliyoripotiwa kuwa ilitengenezwa kwa gharama nafuu na ina uwezo mkubwa, ilisababisha kudorora kwa hisa za makampuni ya teknolojia ya Marekani huku wawekezaji wakihoji mabilioni ya dola wanazotumia kwenye miundombinu ya AI.
"Nilizungumza na [Baraza la Usalama la Kitaifa] asubuhi ya leo, wanachunguza [athari kwa usalama wa kitaifa]," amesema Bi Leavitt, ambaye pia alirejea matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump siku moja kabla kwamba DeepSeek inapaswa kuiamsha sekta ya teknolojia ya Marekani.
'Hatutaishitaki DeepSeek'
Kampuni ya Marekani ya OpenAI ambayo ndio mtengenezaji wa programu ya ChatGPT, imeeleza siku ya Jumatatu kuwa haina mpango wa kuishitaki kampuni ya akili mnemba ya China ya DeepSeek.
OpenAI inazituhumu kampuni za China kuwa zinajaribu kunakili miundo yenye uwezo mkubwa ya akili mnemba. Lakini Sam Altman, mkuu wa OpenAI alisema kampuni hiyo "haina mipango" ya kuishtaki kampuni ya DeepSeek, ambayo ilileta mjadala huko Silicon Valley.
"Hapana, hatuna mpango wa kushtaki DeepSeek hivi sasa. Tutaendelea tu kutengeneza bidhaa bora na kuongoza ulimwenguni," Altman aliwaambia waandishi wa habari huko Tokyo.
Wavumbuzi wa ChatGPT walionya wiki iliyopita kwamba kampuni za China zinajaribu kwa nguvu nyingi kuiga miundo yake ya AI yenye uwezo wa hali ya juu.
Kwa mujibu wa CNBC, jeshi la wanamaji la Marekani limetuma barua pepe kwa wafanyakazi wake likiwaonya kutotumia programu ya DeepSeek kutokana na "maswala yanayoweza kutokea ya usalama na maadili yanayohusiana na asili na matumizi ya programu hiyo".
Jeshi la majini la Marekani halikujibu maswali ya BBC kuhusu hatua hiyo.
Akizungumza kwenye Fox News, mkuu wa masuala ya teknolojia wa Ikulu ya Marekani, David Sacks, alieleza kuwa DeepSeek inaweza kuwa imetumia mitindo iliyotengenezwa na kampuni ya teknolojia ya AI ya Marekani ifahamikayo kama US OpenAI kupata ubora.
"Kuna ushahidi mkubwa kwamba DeepSeek ilichofanya ni kuchukua maarifa kutoka OpenAI," amesema Bw Sacks. "Nadhani moja ya mambo ambayo utaona katika miezi michache ijayo ni kampuni zetu kuu za AI kuchukua hatua za kuzuia kunakili."
OpenAI iliunga mkono hilo katika taarifa ya baadaye ambayo ilisema: "Kama watengenezaji wakuu wa AI, tunashiriki katika hatua za kuzuia na kulinda milki yetu... na tunaamini tunaposonga mbele ni muhimu kufanya kazi karibu na serikali ya Marekani ili kulinda vyema zaidi wabunifu wetu."
DeepSeek yashambuliwa
Wakati huo huo, DeepSeek inasema imekuwa ikilengwa na mashambulizi ya mtandaoni. Siku ya Jumatatu ilisema itapunguza usajili kwa muda kwa sababu ya "mashambulizi makubwa" kwenye programu yake.
Yuyuan Tantian, chaneli ya mtandao wa kijamii chini ya kituo cha utangazaji cha serikali ya China CCTV, inadai kuwa kampuni hiyo imekabiliwa na mashambulizi "kadhaa" ya mtandao katika wiki za hivi karibuni, na yameongezeka zaidi.
DeepSeek ilipata umaarufu wiki iliyopita baada ya wataalamu wa AI kusifu muundo wake wa AI na watu wakaanza kupakua programu hiyo kwenye simu zao.
Umaarufu wake ulisababisha kuporomoka kwa hisa za teknolojia za Marekani, ambazo nyingi zimepata nafuu na kurudi katika hali zao.
Sekta ya AI ya Marekani ilitikiswa na mafanikio yaliyoonekana, haswa kwa sababu ya maoni yaliyopo kwamba Marekani inaongoza katika kinyang'anyiro hicho.
Kuna mfululizo wa vizuizi vya kibiashara vinavyopiga marufuku China kupata vifaa vya teknolojia ya hali ya juu vinavyotumiwa katika akili mnemba. Hilo liliongeza mjadala.
Ingawa China imeongeza uwekezaji katika teknolojia ya hali ya juu ili kunufaisha uchumi wake, DeepSeek si mojawapo ya makampuni makubwa ya China ambayo yamekuwa yakitengeneza miundo ya AI kushindana na ChatGPT inayotengenezwa Marekani.
Wataalamu wanasema Marekani bado itanufaika kwakuwa ni nyumbani kwa baadhi ya makampuni makubwa ya vifaa vya kitekonolojia na bado haijulikani wazi jinsi DeepSeek ilivyoweka muundo wake na inaweza kufikia umbali gani.
Wakati DeepSeek ikiendelea kutamba sokoni wiki hii, Rais Trump alielezea kuwa huo ni "wito wa uamsho" kwa sekta ya teknolojia ya Marekani, huku akipendekeza kwamba inaweza kuwa ishara "chanya."
"Kama unaweza kuitengeneza kwa gharama nafuu na kufikia matokeo sawa. Nadhani hilo ni jambo zuri kwetu," aliwaambia waandishi wa habari kwenye ndege ya Air Force One.
Pia alisema hana wasiwasi na mafanikio hayo, na kuongeza kuwa Marekani itasalia kuwa yenye nguvu katika sekta hiyo ulimwenguni.
Imetafsiriwa na Martha Saranga