Ligi Kuu Uingereza: Nani kutwaa ubingwa Arsenal, Liverpool au Man City?

gbv
Maelezo ya picha, Kuna pointi moja tu inayowatenganisha Arsenal, Liverpool na Manchester City zikiwa zimesalia mechi 10 kabla ya msimu wa 2023-24 wa Ligi Kuu ya Uingereza kumalizika.

Baada ya kisanga cha sare kati ya Liverpool na Manchester City kwenye uwanja wa Anfield siku ya Jumapili, sasa ni wakati mzuri wa kutathmini mbio za kusisimua za kuwania taji la Ligi Kuu ya Uingereza huku zikiwa zimesalia mechi 10.

Kwa mara ya kwanza tangu 2014, pointi moja pekee ndio inatenganisha timu tatu za juu baada ya michezo 28 iliyochezwa.

Timu tatu za juu hazitocheza ligi kuu kwa muda wa wiki tatu - kwa sababu ya robo fainali ya Kombe la FA na mapumziko ya kimataifa. Watakaporejea Liverpool itacheza na Brighton na Manchester City itaikaribisha Arsenal Jumapili Machi 31.

Kikosi cha Pep Guardiola cha City kinatisha huku kikipania kuweka rekodi ya ligi kuu ya Uingereza ya kutwaa mataji manne mfululizo. Tangu walipofungwa 1-0 na Aston Villa mwezi Disemba - wameshinda mara 10 katika mechi 13 za ligi.

Kwa upande wa Liverpool, kipigo cha 3-1 kutoka kwa Arsenal Februari 4 kinasalia kuwa kipigo pekee ndani ya ligi katika mechi zao tisa hadi sasa toka 2024.

Kikosi cha Liverpool chini ya Jurgen Klopp bado kina safari ya kwenda katika uwanja wa Goodison Park kwa dabi ya Merseyside dhidi ya Everton.

Kwa upande wa Arsenal, ingawa wikiendi hii wamemaliza wakiwa kileleni mwa jedwali, Simon Gleave, mchambuzi wa soka anasema.

Ni mbio za farasi wawili, City na Liverpool watakuwa mstari wa mbele wa kinyang’anyiro huku Arsenal ama washika bunduki, itakuwa na ratiba ngumu zaidi.

"Arsenal wamebakiwa na mechi sita katika Premier League, tano kati ya hizo ni ugenini. Manchester City wana mechi sita, nne kati ya hizo ni nyumbani. Liverpool pia wamebakisha mechi sita na tatu kati ya hizo wako nyumbani," anasema Gleave.

Historia inasemaje?

gnb

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Ni mara chache sana imetokea timu tatu katika ligi kuu ya Uingereza kuwania taji zikiwa zimetenganishwa na pointi mbili kuelekea mwisho wa msimu.

2013-14: Hadi kufikia Mei 6, 2014 pointi mbili pekee ziliwatenganisha Liverpool, Man City na Chelsea, lakini City walishinda mchezo wao wa kiporo na kuipita Liverpool - na hatimaye kunyakua ubingwa.

2001-02: Tarehe 23 Aprili 2002, Arsenal walikuwa mbele ya Liverpool kwa pointi moja huku Man Utd wakiwa nyuma kwa pointi moja.

Lakini Arsenal walikuwa na mchezo wa kiporo na walishinda mechi 11 mfululizo na kutwaa ubingwa kwa kuifunga United kwenye uwanja wa Old Trafford.

1995-96: Zikiwa zimesalia mechi nane Man Utd walikuwa na pointi 61 huku Newcastle na Liverpool wakiwa na pointi 59 katika nafasi ya pili na ya tatu. Lakini kikosi cha Sir Alex Ferguson kilishinda na kutwaa ubingwa.

Watabiri wanapendekeza nini?

hgb

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Kampuni ya data za michezo Opta, wameweka utabiri wao kwa kutabiri mechi za kushindwa, kushinda na droo kwa kutumia michezo ya nyuma na ushindani wa sasa na kuja na matokeo yao.

Opta inaiweka Man City katika asilimia 46 ya kushinda taji la Ligi Kuu ya Uingereza, Liverpool asilimia 35 na Arsenal asilimia 19.

Kampuni ya data za michezo Gracenote nayo imetabiri kila matokeo ya mechi - kushinda, sare au kushindwa - kwa kutumia takwimu za Euro Club Index.

Jedwali la mwisho la Ligi Kuu kwa utabiri wa Gracenote. Inaiweka Man City katika asilimia 44 ya kushinda, Liverpool asilimia 37 na Arsenal 19.

Iwapo kutakuwa na sare, ligi inaamuliwa kwa tofauti ya mabao, kisha mabao ya kufunga, kisha pointi nyingi katika mechi walizocheza wao kwa wao, kisha mabao mengi ya ugenini katika mechi ya wao kwa wao.

Chochote kitakachotokea, hakika kutakuwa na panda shuka nyingi kati ya sasa hadi siku ya mwisho ya ligi tarehe 19 Mei.