Mkahawa mpya wa Korea Kaskazini ambao ni raia wa Urusi pekee wanaoweza kuutumia

Chanzo cha picha, Anastasia Samsonova, Getty Images
Eneo jipya la mapumziko katika ufuo wa bahari wa Korea Kaskazini limefunguliwa lakini kwa raia wa Urusi pekee.
BBC ilizungumza na mmoja wa wageni wa kwanza wa kigeni katika Wonsan-Kalma.
Mashine ya propaganda ya Korea Kaskazini imepigia debe eneo la pwani la Wonsan Calma la kitalii, ambalo lilifunguliwa Julai 1, kama sehemu muhimu ya matarajio ya kiongozi Kim Jong-un kukuza sekta ya utalii nchini humo.
Kabla ya ufunguzi wake, hoteli hiyo iliopo ufukweni ilitangazwa kuwa kivutio kwa wenyeji na wageni, lakini muda mfupi baadaye, Korea Kaskazini ilitangaza kuwa wageni, isipokuwa watalii wa Urusi, hawakuruhusiwa kuitumia "kwa sasa".
Hadi sasa, makundi mawili ya watalii wa Urusi wametembelea eneo hilo la kitalii, na kundi jingine linazuru eneo hilo kwa sasa.
Idhaa ya BBC ya Urusi ilizungumza na mtalii wa Urusi aliyetembelea Wonsan Kalma. Alisema "alifurahia likizo bila umati" na kwamba mchanga mweupe wa ufuo "ulilainishwa na kulainisha kila siku kwa usahihi unaofaa
'Kila kitu kilikuwa shwari'

Chanzo cha picha, KCNA
Anastasia Samsonov, 33, afisa anyesimamia masuala ya wafanya kazi , alikuwa miongoni mwa mwa kundi la kwanza la watalii wa Urusi kutembelea Wonsan-Kalma mnamo Julai.
"Kila siku (ufuo) ulisafishwa na kung'aa. Hakuna mahala palipokuwa na doa. Vibanda vilikuwa vipya kabisa, kila kitu kilikuwa safi na nadhifu. Mlango wa kuingia baharini ulikuwa mzuri sana, kwa hiyo ndiyo, ulikuwa ufuo mzuri sana," alituambia.
Alisema kuwa awali, kutokana na baadhi ya matatizo yanayohusiana na kuandaa ziara hiyo, "haikuwa wazi kama Warusi wangeweza kwenda eneo la utalii la pwani au la."
Hapo awali watalii hao walipangiwa kutumia siku yao ya kwanza Pyongyang, mji mkuu, kutembelea vivutio vya jiji kama vile Tao la Ushindi na Kim Il-sung Square, na kisha kuelekea kwenye mapumziko ya bahari siku iliyofuata.
Lakini kwa sababu zisizojulikana, waliwekwa Pyongyang kwa siku ya ziada na kuishia kuchukua treni hadi Wonsan badala ya kwenda na ndege kama ilivyopangwa.
Watalii walifanikiwa kuwashawishi waongozaji kukaa siku ya ziada kwenye eneo la mapumziko la bahari badala ya kutumia siku ya mwisho ya safari yao kwenda Pyongyang, kwa jumla ya siku nne kamili kwenye ufuo.

Chanzo cha picha, Anastasia Samsonova
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ziara hiyo imeandaliwa na shirika la usafiri la Urusi liitwalo Vostok Intour, ambalo hutoa ziara za kwenda Korea Kaskazini.
Ziara hiyo ya siku nane inajumuisha mwongozaji watalii anayezungumza kwa lugha ya kirusi wa watalii na malazi katika hoteli ya nyota nne.
Shirika la usafiri lenye makao yake makuu mjini Vladivostok liliiambia BBC kwamba watalii wote, bila kujali umri au maslahi mahususi, walitakiwa kushiriki katika matembezi na shughuli zilizoainishwa katika mpango wa watalii.
"Ikilinganishwa na nchi nyingine, faida ya kusafiri hapa ni kwamba hakuna watalii wengine. Kwa mfano, unapoenda Thailand kumejaa wgeni.. Kusema kweli, hilo lilikuwa jambo la kushangaza zaidi kuhusu likizo hii," Samsonov alisema.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Urusi vimetaja eneo hilo la mapumziko kama eneo la kipekee la likizo kwa mtazamo wa eneo la majaribio ya makombora, lakini Samsonov alisema hajawahi kuona kitu kama hicho hapo.
"Hatukuona chochote," anasema. "Hakuna makombora yaliyorushwa tukiwa huko."
Hata hivyo, alikuwa ameona makombora ya kuchezea yakiuzwa kwa dola 40 kila moja, na akasema yalisababisha msisimko mkubwa miongoni mwa watalii.
Nambari ya mfano kwenye vifaa vya kuchezea ilionyesha kuwa ni za kombora la masafa marefu la Hwasong-17.
Msafiri mwingine, Daria, aliandika kwenye Instagram: "Ikiwa una chaguo moja tu kwa likizo ya bahari, ni bora kuchagua mapumziko yaliyojaribiwa, kwa sababu kila kitu hapa bado ni kipya sana na sio aina ya likizo ambayo watalii wa Kirusi wamezoea.
Lakini ikiwa umechoka na bara Asia, Uturuki, na maeneo kama hayo na unatafuta kitu tofauti na kigeni, hii ndiyo unayohitaji."

Chanzo cha picha, getty image
Utalii uliodhibitiwa
Picha za satelaiti na ripoti kutoka kwa televisheni ya shirikisho la Urusi zinaonyesha kuwa eneo la mapumziko linajumuisha vifaa kama vile bustani ya maji na sinema.
Hatahivyo kundi la kwanza la watalii halikuruhusiwa kupata vifaa hivi na walitumia wakati wao mwingi kwenye hoteli na ufukweni.
"Tunaamka asubuhi na kwenda kwa kifungua kinywa. Lakini ikiwa mtu hakutaka, angeweza kuruka kifungua kinywa," Samsonov alisema.
"Kisha, dakika 15 baada ya kiamsha kinywa, tulikuwa tunakusanyika na kupelekwa kwenye ufuo wetu wa kibinafsi kwa magari ya umeme. Tulikuwa na wakati wa kupumzika kwenye ufuo hadi wakati wa chakula cha mchana.
Wakati wa chakula cha mchana, tulikuwa tukipanda gari na kwenda hotelini kubadilisha nguo, kisha kwenda kwenye mgahawa au kula chakula cha jioni hotelini. Baada ya hapo, tungeweza kurudi ufukweni, ingawa wengine hawakutaka kwenda kwenye ufuo wa joto."
Aliongeza kuwa ufuo huo ulikuwa karibia hauna watu na kwamba wageni wa Korea Kaskazini walizuru nyakati za wikendi. Ziara yao ilienda sambamba na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov katika eneo la mapumziko.
"Siku ya mwisho, watoto wa umri wa miaka 10 hadi 14, inaonekana kutoka kambi ya michezo au burudani, walizuru eneo hilo. Walikuwa wakiogelea baharini na walimu wao au wakufunzi na kujifunza kuogelea. Hatukuweza kupinga na tukajiunga nao. Kwa kweli, hakuna mtu aliyetuzuia - tukawasalimia, na msichana alizungumza nami kwa Kiingereza na akauliza jinsi nilivyokuwa," Samsoniva.
Kulingana na Samsonov, pamoja na viongozi, mlinzi alikuwa nasi .
"Tuliuliza mwongozaji kwa nini mipango kama hiyo ilikuwa muhimu," alisema.
Maelezo ni kwamba wenyeji hawakuzoea kuona watalii hata kidogo. Tulipotembea barabarani, walitutazama kwa mshangao mkubwa kwa sababu nchi ilikuwa imefungwa kwa muda mrefu.
Waelekezi hao walisema kuwa hii ilikuwa ni kuzuia makabiliano ya ghafla na wenyeji na kujenga hofu ndani yao."
Alikumbuka tukio moja maalum ambapo wenyeji waliogopa sana - kwa mfano, wakati mtalii mwanamke alipogonga mlango wa chumba cha watalii, bila kutarajia mtu yeyote kuwa hapo. Lakini mlango ulipofunguliwa na kumwona mgeni, aliogopa na kukimbia.
Vikwazo na tuhuma
Kulingana na Andrei Lankov, mtaalam wa uhusiano wa Korea Kaskazini na Urusi na profesa katika Chuo Kikuu cha Kookmin huko Seoul, hata kwa raia wa China, mshirika mkuu wa Korea Kaskazini na mshirika wa kiuchumi, hoteli hiyo kwa sasa ni vigumu kufikia.
"Kufikia mwaka wa 2017-2018, uongozi wa Korea Kaskazini ulikuwa unajiandaa kufungua milango yake kwa ulimwengu, pamoja na kutoridhishwa fulani," anasema.
"Walikuwa wakipanga kuanzisha mawasiliano na nchi za nje, kuvutia wawekezaji kutoka nje, na kuanzisha miradi ya pamoja."
"Kulikuwa na matumaini wakati huo, lakini matumaini hayo yalikatishwa na ukweli wa vikwazo," Lankov anaendelea.
"Vikwazo hivyo viliwekwa rasmi kabla ya hapo, lakini vilitekelezwa kwa dhati mwaka wa 2017-2019. Hayo yalipotokea, ilionekana wazi kuwa biashara na ulimwengu wa nje ilikuwa itakuwa ngumu kwa sababu zilizo nje ya udhibiti wa serikali ya Korea Kaskazini."
Anaamini maendeleo haya yameibua swali la msingi zaidi ndani ya nchi: Kwa nini kuingiliana na wageni? Kwa maoni yake, serikali ya Korea Kaskazini kwa makusudi inaweka ukomo wa idadi ya watalii na inadhibiti kwa karibu mienendo yao.
Ziara ya utalii inajumuisha nini?
Kulingana na tovuti ya Vostok Intour, ziara hiyo ya siku nane, inajumuisha mwelekezaji anayezungumza Kirusi na milo mitatu kwa siku.
Ratiba hiyo ni pamoja na "kufurahia mandhari nzuri" kutoka eneo la mapumziko la Masikryong, "kutembea chini ya moja ya mitaa ya Pyongyang" ili "kujionea maisha ya kila siku ya Wakorea," na kutembelea Mnara wa Uhuru, wakfu kwa askari wa Soviet waliokufa wakati wa ukombozi wa Peninsula ya Korea kutoka kwa Japan . Ziara hiyo pia inajumuisha kutembelea duka la kumbukumbu.
Gharama ya kukaa siku mbili kwenye ziara hii ni takriban 148,000 rubles (US $ 1,850) kwa kila mtu, wakati kukaa siku moja kunagharimu rubles 176,000 (US $ 2,200) kwa kila mtu.
Kwa kuongezea, wasafiri lazima wapange safari yao wenyewe hadi Vladivostok kwa safari ya ndege kwenda Pyongyang, na hivyo kuweka gharama ya jumla kuwa takriban rubles 200,000 (US$2,500) kwa kila mtu.
Likizo ya pwani yenyewe huchukua siku nne tu.
Kulingana na Samsonov, hakuna gharama za ziada, isipokuwa kwa ununuzi wa zawadi. Mbali na makombora ya kuiga, sare za Olimpiki za Korea Kaskazini pia zilipendwa na watalii, alisema.
Likizo na vikwazo vingi
Samsonov aliongeza kuwa likizo hiyo ilikuja na vikwazo, ikiwa ni pamoja na mtandao wa gharama ya juu sana, udhibiti wa harakati za watalii na vikwazo katika shughuli zao.
Kwa mfano, aliiambia BBC kwamba waelekezi hawakuruhusu watalii kupiga picha za maeneo ya ujenzi. Ratiba zote zilikuwa zimepangwa isipokuwa pale ambapo mamlaka ya Korea Kaskazini iliamua kuzibadilisha.
Utalii wa Urusi kwa Korea Kaskazini unaongezeka, lakini bado ni mdogo ikilinganishwa na maeneo mengine. Takwimu za walinzi wa mpaka wa Shirikisho la Usalama la Urusi zinaonyesha kuwa karibu watalii 1,500 wa Urusi walitembelea Korea Kaskazini mnamo 2024.
Kinyume chake, zaidi ya watu milioni 7.6 walitembelea Uturuki na karibu milioni 1.9 walitembelea China.
Hatahivyo idadi ya watalii inaongezeka. Katika robo ya pili ya 2025, karibu Warusi 3,000 waliingia Korea Kaskazini (1,673 kati yao kama watalii) - idadi ambayo haijaonekana tangu 2011, kabla ya vikwazo vya utalii kuwekwa.












