Fahamu ndege za abiria zenye kasi zaidi duniani zilizoagizwa na kampuni ya ndege ya American Airlines

Chanzo cha picha, Boom Supersonic
Zitaweza kupaa juu ya bahari kwa kasi ya kilomita 2000 kwa saa, ikiwa ni mara mbili ya ndege za kibiashara zenye kasi zaidi duniani.
Hizi ni ndege aina ya Overture, kizazi kipya cha ndege zenye lengo la kujaza pengo lililoachwa katika soko la anga baada ya kuondoka kwa ndege aina ya Concorde.
Jumanne hii, shirika la ndege la Marekani la American Airlines lilitangaza makubaliano na Boom Supersonic, watengenezaji wa Overture, kununua ndege 20 kati ya hizi, ingawa wakiwa na chaguo mbadala la kuongeza ndege nynegine 40 kama hizo.
Kampuni ya ndege ya American Airlines inatarajia kuwa na idadi kubwa ya ndege za kibiashara duniani ambazo inatarajia kusafiri kutoka Miami hadi London chini ya saa tano au kutoka Los Angeles hadi Honolulu kwa muda wa saa tatu pekee.
Shirika hili la ndege hatahivyo, sio la kwanza kupata aina hii ya ndege, kwani mnamo Juni 2021 United Airlines ilisaini makubaliano na kampuni ya Boom kununua ndege 15, na ndege nyengine 35 za ziada.
Safari za ndege za kibiashara duniani zilisitishwa mwaka wa 2003, wakati ndege ya mwisho aina ya Concorde iliokuwa ikitoa huduma hiyo ilipoacha kufanya kazi, baada ya kuondolewa kwa sababu za kiusalama, mnamo Julai 25, 2000, baada ya ndege aina kama hiyo kuhusika na ajali katika uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris, ajali iliogharimu maisha ya watu 113.
Supersonic na endelevu?
Ndege hiyo aina ya Overture itaundwa kubeba kati ya abiria 65 na 80 na itasafiri kwa takriban kilomita 7,800.

Chanzo cha picha, boom
Kulingana na muundaji wake , ndege hiyo yenye injini nne itaweza kufanya kazi kwenye njia zaidi ya 600 zenye soko kubwa kote ulimwenguni.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Boom inadai kuwa imejumuisha vigezo endelevu vya mazingira katika muundo wake, kwa hivyo lengo lake ni kwa safari zake za ndege kutokuwa na hewa chafu ya kaboni.
Hili ni suala tata kwani sekta ya usafiri wa anga inakosolewa kwa kuwa mojawapo ya sekta zinazochafua mazingira zaidi.
Ikikabiliwa na changamoto hii, kampuni hiyo inadai kufanya utafiti kati ya miradi endelevu ya mafuta ya ndege kwa nia ya kutatua tatizo la utoaji wa gesi chafu.
Kwa sasa, wanasema, mafuta bora ya aina hii kwenye soko hupunguza 80% ya CO2 ikilinganishwa na mafuta ya kawaida.
Muundaji huyo anashirikiana na kampuni ya Prometheus Fuels, ambayo wanasema ina mchakato unaoruhusu kuunda mafuta endelevu kutoka kwa CO2 angani.
Boom Supersonic inadai kuwa mbawa za Overture zimeundwa ili kuboresha mtiririko wa hewa, kupunguza hali ya kuvuta na kuongeza ufanisi wa mafuta .
Kiteknolojia, sio vigumu kuunda ndege yenye kasi zaidi , ijapokuwa changamoto yake ni kutoa huduma ambayo abiria wanaweza kulipia na ambayo haina uchafuzi wa mazingira.
Overture imepangwa kuzinduliwa mnamo 2025, lakini haitarajiwi kuanza kubeba abiria hadi 2029.
Inasakia kuonekana iwapo kufikia wakati huo itaweza kutimiza malengo yake makubwa na iwapo itafanikiwa kuziba pengo la Concorde.












