Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Kenya 2022: Uchaguzi wa Kenya una maana gani kwa Tanzania na Afrika Mashariki?
- Author, Na Mohammed AbdulRahman.
- Nafasi, Mchambuzi
Uchaguzi mkuu wa Kenya uliopangwa kufanyika Agosti 9, 2022 ni suala linalofuatiliiwa kwa karibu na kwa kuzingatia kwamba matokeo yatakuwa na athari kubwa. Kenya ambalo ni Taifa kubwa kubwa zaidi kiuchumi miongoni mwa mataifa ya Afrika Mashariki, litamchagua rais mpya wa tano na viongozi wengine wa uwakilishi huku mafanikio ya uchaguzi huo yakitarajiwa kuwa dira ya demokrasia, ambayo imezorota katika nchi kadhaa jirani.
Viongozi wa baadhi ya mataifa katika kanda ya AfrikaMashariki wamezifanyia marekebisho katiba zao zilizokuwa awali na ukomo wa utawala wa miaka kumi na kuondoa kikomo hicho ili kujifungulia njia ya kuwawezeshaa kubakia madarakani kwa muda mrefu zaidi. Hao ni Pamoja na viongozi wa Uganda na Rwanda. Rais Kagame wa Rwanda aliwahi kusema wakati wa mabadiliko ya katiba yaliyomruhusu kuongoa zaidi ya miwili kuwa uamuzi huo ni kuzingatia matakwa ya Wanyarwanda walimuomba kufanya hivyo.
Kenya ni nchi iliyoheshimu katiba yake na Rais Uhuru Kenyatta anasubiri kumkabidhi madaraka yule atakayekuwa mrithi wake, mshindi wa uchaguzi huo. Washindani wawili wakuu ni Wazri mkuu wa zamani, Rais Odinga, aiyeteuliwa na Muungano wa Azimio la Umoja, akiungwa mkono na Uhuru Kenyatta awe mrithi wake. Chama cha Jubilee cha Kenyatta ni sehemu ya Azimio la Umoja. Mpinzani wake ni Makamu wa Rais William Ruto, mgombea wa Muungano wa Kenya Kwanza, aliyehitilafiana na Kenyatta.
Uamuzi wa Kenyatta wa kuheshimu katiba ni jambo la kupongezwa, lakini sababu kubwa ni uhuru wa mahakama ambayo ni taasisi ya kusimamia sheria. Itakumbukwa yaliotokea katika uchaguzi wa 2017, wakati Jaji mkuu wa wakati ule, David Maraga alipotangaza kwamba matokeo ya uchaguzi ni batili kufuatia dosari zilizotokea katika uchaguzi huo hilo. Hatua ya mahakama kuu ilitokana na malalamiko yaliowasilishwa na mgombea wa upinzani Raila Odinga. Pia pamoja na kampeni kali ya uchaguzi wagombea wote wakuu Raila Odinga na William Ruto wametoa wito wa amani kuliepusha taifa na janga la machafuko ya uchaguzi wa 2007/2008.
Ujumbe kwa Tanzania
Mafanikio ya uchaguzi ujao nchini Kenya yatakuwa na ujumbe mahsusi kwa jirani yake mkubwa Tanzania ambayo tangu iliporudi kwenye mfuo wa vyama vingi vya siasa 1992 na kufuatiwa na uchaguzi wa kwanza 1995, mchakato wa uchaguzi umedhibitiwa na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Matokeo yake ni kushindwa kuimarika kwa taasisi muhimu katika ujenzi wa demokrasia imara, huku nguzo kuu ikiwa ni mahakama.
Wanaharakati wamekuwa wakitaja sababu za kutopatikana mafanikio kuwani Pamoja na Rais kuwa na madaraka ya kupita kiasi yakimpa nguvu miongoni mwa mengine kuteua Tume ya Uchaguzi, inayoangaliwa kuwa ni mzizi wa kutopatikana haki katika uchaguzi. Tume ya Uchaguzi huteuliwa na Rais na matokeo ya uchaguzi wa Rais yanapotangazwa hayawezi kupigwa kama ilivotokea Kenya 2017.
Wanaharakati wanadai dawa mjarab ni kuwepo Katiba mpya itakayofungua njia ya kupatikana Tume Huru ya Uchaguzi itakayosimamia uchaguzi huru na wa haki. Tanzana ilishuhudia uamuzi wa mpiga kura kutoheshimiwa, baada ya nguvu ya dola kutumika kuhakikisha matokeo ya uchaguzi yanakipa ushindi mkubwa chama tawala CCM na kuvikandamiza vyama vya upinzani. Wadadisi wanaueleza uchaguzi wa 2020 wakati wa uongozi wa Rais John Pombe Magufuli aliyefariki Machi 2021 kuwa ndiyo uliokuwa mbaya kabisa kuwahi kuonekana tangu Tanzania irejeshe mfumo demokrasia ya vyama vingi vyama siasa.
Haya hivyo, viongozi kadhaa wa serikali ya chama tawala CCM mara kadhaa wamekuwa wakisema kuwa uchaguzi ulifanyika kwa kufuata taratibu zote na kwamba wanaolalamika wafungue mashauri mahkamani.
Mrithi wa Magufuli, Rais Samia Suluhu Hassan aliyeingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake, sasa anaonekana kubadili dira. Wakati Magufuli aliondoa uwezekano wa kuwa na Katiba mpya akisisitiza sio kipaumbele bali muhimu ni maendeleo, Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha ishara ya kulizungumzia suala la katiba mpya na kupata baraka za chama chake tawala.
Wengi wanaashira kuwa pindi uchaguzi wa Kenya utafanyika katika hali iliyo shwari, utakuwa chachu katika mchakato wa kuimarishwa demokrasia nchini Tanzania. Wakisifia mafanikio yaliopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia katika kipindi kifupi, katika sekta mbali mbali, raia wa kawaida nchini humo wamekuja na msemo " Mama anaupiga mwingi" wakilinganisha na mchezo maridadi wa kandanda.
Swali linalosalia ni je kweli atahakikisha anamaliza kiu ya Watanzania kutaka katiba mpya itakayowafungulia mlango wa kuwa na demokrasia imara zaidi?
Miongoni mwa mafanikio yake mengine ni kurekebisha haraka uhusiano wa kidugu na Kenya ambao ulizorota kipindi cha Rais Magufuli. Hatua yake imeipa msukumo mkubwa biashara ya nchi hizi mbili, na pasina shaka anatarajia kuendeleaa ushirikiano huo na yeyote atakayeibuka kuwa mshindi.
Matumaini ya nchi nyingine za Kanda
Kenya ni nchi muhimu panapohusika biashara ya kanda, kwa sababu ya kutumiwa kwa bandari yake ya Mombasa na wengi wa majirani zake. Kwa mfano Uganda isiyo na bahari inategemea kwa kiwango kikubwa bandari ya Mombasa kwa usafirishaji wa bidhaa inazosafirisha kwenda nje na zile inazoagiza kutoka ng'ambo. Kenya ni mshirika mkubwa wa biashara wa Uganda na Wagombea wote wawili wakuu; Raila ana Ruto walikwenda Kampala kwa nyakati tafauti kuonana na Rais Museveni, tukio linaloashiria kila mmoja anatafuta kuungwa mkono na kiongozi huyo jirani na mkongwe.
Rwanda ni nchi nyingine ambayo inategemea kwa upana mkubwa uagizaji bidhaa kutoka Kenya. Kwa mujibu wa takwimu za 2019, Rwanda iliagiza bidhaa za thamani za dola milioni 278.45 za Marekani kutoka Kenya.
2021 Burundi mwanachama mwengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ilisaini mkataba wa kuimarisha ushirikiano wa biashara na maendeleo Kenyatta. Tangu ilipojiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki Aprili 2022, Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo (DRC) imeonesha ishara ya kufungua zaidi milango ya kiuchumi kwa wawekezaji.
Kenya imekuwa kipaumbele kwa kwa serikali ya Rais Felix Tshisekedi. Mwishoni mwa 2021 ujumbe wa wafanya biashara wa nchi hizo mbili ulikutana nchini Kongo kutathmini nafasi za uwekezaji na kibiashara.
Sambamba na Kongo inaizingatia Kenya kuwa mshirika wa kuaminika katika kusimamia amani nchini humo. Mbali ya wanajeshi wa Kenya kushiriki katika ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa (MONUSCO), Rais Uhuru Kenya alianzisha juhudi mwezi Aprili za kuundwa kikosi cha mataifa ya Jumuiya ya Afrika Masharki, kulisaidia jeshi la Kongo, kufuatia mashambulio mapya ya kijeshi ya waasi wa M23.
Lakini hadi sasa kuundwa kwa kikosi hicho kunakabiliwa na kizingiti kutokana na Kongo kukataa kabisa Rwanda isiwemo katika kikosi hicho ikiishutumu kuwaunga mkono waasi hao, madai ambayo Rwanda inaendelea kuyakanusha.
Kenya kwa hivyo inabakia mshirika muhimu wa kanda kibiashara na kiuchumi na yeyote Hapana shaka yeyote atakayemrithi Rais Uhuru Kenyata, iwe ni Raila Odinga au William Ruto atakuwa na wajibu wa kuendeleza ushirika. Matumaini ya wakaazi katika kanda hii sawa na wakenya kwa jumla, ni kwamba uchaguzi wa Agosti 9, 2022 utakuwa wa amani na utulivu.
Kwa wanaharakati katika nchi jirani wana matarajio kwamba Kenya itakuwa pia na nafasi kubwa ya kuwa usukukani sio tu wa kiuchumi lakini wa kisiasa, panapohusika na vuguvugu lao la kupigania demokrasia na haki za binadamu katika nchi zao.
Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma: