CCM ‘inavyochonga barabara mpya’ baada ya Magufuli

Chanzo cha picha, IKULU
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
Uchaguzi wa Abdulrahman Kinana kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliteka vichwa vya habari katika vyombo vingi lakini habari kubwa zaidi ilipita bila kujadiliwa sana.
Kama ilivyo mara nyingi katika siasa za Tanzania, jambo ambalo lingetakiwa kuchambuliwa vizuri, ndilo ambalo huja kujadiliwa mbele ya safari wakati likianza kufanya yaliyokusudiwa.
CCM imefanya marekebisho ya Katiba yake - kwa mara ya 17 tangu kianzishwe mwaka 1977, na kwa mujibu wa Katibu Mwenezi wake, Shaka Hamdu Shaka, lengo la marekebisho ya safari hii ni "kuongeza udhibiti wa viongozi wa chama na usimamizi wa ilani ya CCM kwenye Serikali za Mitaa".
Linalozungumzwa zaidi ni hatua ya kuwarejesha makatibu wa CCM wa mikoa kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, hivyo kubadili uamuzi ambao vikao hivyo hivyo vilifanya miaka mitano iliyopita kuwaondoa viongozi hao kwenye chombo hicho muhimu cha chama tawala cha Tanzania.
Kuanua jamvi la CCM ya Magufuli

Chanzo cha picha, IKULU
Mabadiliko yaliyotokea Dodoma wiki iliyopita yameanua rasmi jamvi la CCM iliyotaka kutengenezwa na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021. Yeye hakuwa mwandani wa CCM na mara zote hakuwa na imani na mifumo na watu aliowaona kama wanaowakilisha "CCM halisi".
Mmoja wa maswahiba wake wa kisiasa alipata kuniambia kuhusu namna alivyoitwa na Magufuli Ikulu ya Dar es Salaam kuulizwa kuhusu jambo moja muhimu la kisiasa na Rais kumwambia waziwazi kuwa; "sina imani na watu walionizunguka.
Kila ninayetaka kuzungumza naye, naambiwa huyo ni wa Kinana, Lowassa au Kikwete". Ni sababu hiyo ya msingi ambayo pia aliwahi kuidokeza wakati mmoja hadharani, iliyomfanya aamue kukitengeneza chama katika taswira yake.

Ndiyo sababu ya uamuzi uliofanywa kupitia vikao tofauti vya CCM kati ya mwaka 2016 na 2017 vilivyoleta mabadiliko aliyoyataka.
Mojawapo ilikuwa ni kupunguza idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa kuondoa baadhi ya waliokuwa wakiingia kwa mujibu wa nyadhifa zao ikiwamo makatibu wa mikoa. Kwa mabadiliko hayo, idadi ya wajumbe ilipungua kutoka 388 hadi 162.
Sababu iliyotolewa wakati huo - na ikiendana na kauli mbiu yake ya kupunguza matumizi, ilikuwa ni kupunguza gharama za kuendesha vikao, kutunza siri za vikao na kutengeneza chama cha kisasa chenye watu wachache kwenye vyombo vya kufanya uamuzi.
Ni wakati huo pia ndipo baadhi ya wanachama mashuhuri wa CCM walifukuzwa au kusimamishwa uanachama kutokana na matukio yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Katika historia ya CCM, NEC ina nafasi ya kipekee. Matukio mengi makubwa yaliyowahi kutokea katika uhai wa chama hicho ama yalijadiliwa au kumalizikia hapo.
Ni kikao kilichokuwa kikifahamika kwa kuhusisha wajumbe wa aina mbalimbali na ziko simulizi za namna Baba wa Taifa, Julius Nyerere na wenyeviti waliomfuatia walivyokuwa 'wakiteseka' wakiwa kwenye kikao hicho.
NEC ndiko palikokuwa mahali pekee ambako Rais angeweza kuambiwa ukweli wake waziwazi na bila woga kwa sababu ya dhana ya chama kushika hatamu.
Makatibu wa CCM wa mikoa walikuwa wakiaminika kama watu walio karibu na wananchi na wanaojua shida na kero zao.
Makatibu hao walikuwa na kazi ya kuhakikisha chama kinabaki madarakani kwa namna yoyote na pia kuwasilisha kile ambacho wananchi wangependa kuona kinajadiliwa kwenye vikao vya juu.
Cheo hicho pia kilikuwa ni sehemu ya kutengeneza viongozi wajao wa ngazi za juu. NEC ilikuwa ni fursa ya kuonesha uwezo wao na kukijua chama.
Kusimamia Serikali za Mitaa

Chanzo cha picha, CCM
CCM imetamka kwamba mabadiliko ya safari hii yana lengo la kusimamia utekelezaji wa ilani kupitia Serikali za Mitaa.
Hili ni eneo linalogusa wananchi wengi zaidi na ni wazi CCM inataka kutumia kipindi hiki kuhakikisha inapambana na kero zinazogusa wananchi wa kawaida - mijini na vijijini.
Mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM ameniambia mwishoni mwa wiki; akitumia lugha ya kimombo -All politics is local- na kwamba kama chama hicho kitaweza kusimamia vizuri utekelezaji wa sera zake kwa kusikiliza wananchi wa kawaida, kitadumu madarakani kwa muda mrefu zaidi.
Pamoja na ukuaji wa uchumi uliotokea katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Tanzania bado ni nchi masikini na wananchi wake wengi wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma muhimu kama maji, afya, elimu na umeme.
Ni wazi kwamba uamuzi wa CCM safari hii una lengo la kuhakikisha inajikita zaidi katika utekelezaji wa mipango ya kuhudumia kada hii ya Watanzania.
Ripoti kadhaa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikionesha kwamba kuna matumizi mabaya ya fedha za umma katika Serikali za Mitaa na kama CCM itaweza kudhibiti ufisadi na matumizi mabaya katika eneo hilo, inaweza kufanya vitu vitakavyorejesha imani ya wananchi kwake.
Kuzuia mwisho wa CCM

Katika sayansi ya siasa, kuna namna mbili ambapo chama cha siasa kinaweza kuondoka madarakani au kufa kisiasa - kwanza ni kwa uchumi kuporomoka na kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi na pili kama chama kitaonekana kuacha njia yake na kufuata mengine.
Hata kwenye hali ngumu kiuchumi, wanachama wanaweza kubaki kama bado wanaamini kwenye misingi lakini kama chama kikiacha misingi, hakiwezi kubaki salama tena.
Kwa namna ambavyo CCM chini ya Magufuli ilivyokuwa ikienda, kulikuwa na uwezekano wa chama hicho ama kupasuka au kuondolewa madarakani endapo hali ya uchumi ingeporomoka. Hiyo ni kwa sababu wapo ambao wangeona CCM si ile waliyokuwa wakiipigania kwa miaka yote. Mabadiliko ya Katiba safari hii yanakifanya chama hicho kurejea kuwa chama ambacho wanachama wake wanajua nini wanakisimamia na pengine watakuwa tayari kubaki nacho kwenye mazingira magumu au rahisi.
Waliokuwa kwenye utendaji wa CCM wakati wa uenyekiti wa Magufuli kila mara walirejea na kunukuu matamshi ya mwenyekiti kuwa ulikuwa ni wakati wa kuleta mabadiliko muhimu, ikiwemo kurejesha nidhamu iliyokuwa imeporomoka hususani katika matumizi ya fedha na kuepusha kufuja mali za chama ambazo baadhi ya viongozi wasio waadilifu walidaiwa kuzigeuza kuwa mali binafsi.
Hali hiyo iliwekwa bayana katika ripoti ya Kamati maalum ya kuhakiki mali za chama iliyoongozwa na Dkt. Bashiru Ally, ambayo matokeo yake yaliuridhisha uongozi wa CCM na kuamua kuteua Dkt. Bashiru kuwa Katibu Mkuu wa CCM Mei, 2018.
Sasa kubwa zaidi ni kwamba CCM imeamua rasmi kufanya tena siasa kama ilivyokuwa miaka ya kabla ya ujio wa Magufuli. Kwa kuwa na makatibu na mifumo ya kawaida ya kufanya siasa, CCM inataka kubaki kuwa chama cha kisiasa.
Ndiyo sababu, huu ni wakati mzuri kuona ni kwa vipi CCM italea Kituo cha Demokrasia (TCD) ambacho sasa kimegeuka kuwa chombo muhimu cha mazungumzo ya kisiasa baina ya vyama vilivyopata usajili na vyenye wabunge. Jumanne ya Aprili 5, 2022, CCM itachukua Uenyekiti wa kituo hicho kwa muda wa mwaka mmoja na itakuwa vyema kutazama ni namna gani mazungumzo baina ya vyama vya shindani yataendelea kuanzia sasa kutoka a nana umuhimu wake katika kuimarisha demokrasia ya vyama vingi.
Kwa miaka sita iliyopita, hakukuwa na majadiliano maana baina ya chama tawala na vile vya upinzani, lakini tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, walau kuna mazungumzo yanaonekana kufanyika na kama CCM imeamua sasa kufanya siasa za ushindani, mwanzo wake utaonekana kuanzia wakati huu watakaoanza kuwa mwenyekiti wa (TCD).













