Bei ya Mafuta ya kula Afrika Mashariki: Je ni wakati wa kula chukuchuku?

mayai

'Naomba chipsi mayai, nikaangie kuku au leo tutakula ndizi za kukaanga ama samaki wa kukaanga na ugali', haya ndiyo maisha ya wananchi wengi wa Afrika Mashariki yanayohusu vyakula.

Vyakula vingi wanavyopika na kula vinatumia matufa ya kula kuanzia asubuhi kwenye maandazi, chapati, vitumbua, bagia, kababu mpaka jioni kwenye chipsi mayai, wali au ugali na samaki au nyama.

Mahitaji ya mafuta ya kula Afrika Mashariki yanafikia mpaka tani 2.5 milioni kwa mwaka. Kwa Tanzania mahitaji ni wastani wa tani 650,000 licha ya uzalishaji wa ndani ni wastani wa tani 290,000.

Uganda mahitaji kwa mwaka ni wastani wa tani 120,000 ingawa yenyewe inazalisha tani 40,000 tu.

Kenya wanahitaji wastani wa tani za mafuta ya kula 400,000 mpaka 500,000 kwa mwaka lakini wanachozalisha ni robo tatu ya mahitaji.

Kwa upungufu huo nchi hizo zimekuwa zikitumia mamilioni ya dola kuagiza mafuta ya kula kutoka nje hasa katika nchi kama Malaysia, India, Singapore na Indonesia Ukraine, Poland na Belarus.

Mfano Rwanda yenyewe ilitumia mpaka dola milioni 1 kuagiza bidhaa hiyo nje.

Tanzania kwa mwaka yenyewe inatumia mpaka dola 204.7$ milioni kuagiza mafuta ya kula toka nje. Hizi ni gharama kubwa.

Sasa pamoja na mahitaji makubwa na kupendwa sana kwenye mapishi ya Afrika Mashariki, mafuta ya kula sasa, yamekuwa 'kaa la moto' kwa watumiaji wake, kutokana na bei yake kupaa kila uchwao.

Kupanda huku kwa bei, kumeleta vilio karibu katika nchi zote za Afrika Mashariki zikiwemo Tanzania, Kenya, DRC na Uganda na kuibua mjadala mkubwa kuhusu njia gani mbadala na za muda mrefu za kushughulikia suala hili la mafuta ya kula?

Ili kuondoa maumivu ya gharama za kuagiza nje na unafuu wa bei kwa watumiaji.

Bei ya mafuta zikoje Afrika Mashariki?

m

Miaka miwili iliyopita katika nchi za Afrika Mashariki, uliweza kupata mafuta ya kula kwenye dumu la ujazo wa lita 20 mpaka kwa dola 22$, lakini kwa sasa bei ya mafuta ya kula kwa ujazo huo imepaa mpaka mpaka dola 60$ katika baadhi ya maeneo.

Nchini Tanzania katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, bei ya mafuta ya kula kwa dumu la lita 20, imepanda mpaka wastani wa kati ya dola 40$ mpaka dola 55$ (kama tsh 130,000) kutoka wastani wa dola kati ya 25$ na 34$ (kama tsh 75,000).

Kwa bei ya reja reja kwa lita moja katika baadhi ya maeneo mafuta yanauzwa kati ya dola 2.8% mpaka dola 3.2$ (6,500tsh mpaka 7,500tsh).

Nchini Kenya hasa katika jiji la Nairobi bei ya mafuta inakwenda mpaka dola kati ya 50$ na 60$ kutoka wastani wa dola 28$ na 50$ kwa ujazo wa dumu la lita 20.

Ni Februari mwaka 2021 tu lita moja moja ya mafuta ya kula Kenya iliuzwa Ksh236 sawa na dola 2.05$ lakini kufikia Februari 2022, ilipanda mpaka Ktsh 312 sawa na dola 2.71$.

Hali ya bei haitamalaki kwa uzuri pia katika nchi zingine za Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa wa mtandao wa taarifa za bei za bidhaa duniani wa globalproductprices, lita moja ya mafuta ya kula nchini Uganda inauzwa mpaka dola 3.45$ kutoka wastani wa dola 2.5$ mpaka 3$.

Rwanda mafuta yaliuzwa dola 22$ mpaka 35$ kwa lita 20 sasa imefika dola 70$. Kwa ujumla ukilinganisha na bei ya soko la dunia inayofikia dola 2.88$ kwa lita wastani wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki zinaendelea kuwa mwiba.

Kwa nini bei ya mafuta ya kula imezidi kuwa mwiba Afrika Mashariki?

mafuta

Nchi za Afrika Mashariki zinahitaji angalau wastani wa tani 2.5milioni za mafuta ya kula kwa mwaka kutosheleza mahitaji ya wananchi wake wanaokadiriwa kufikia milioni 300 hasa baada ya DRC kujiunga kwenye ukanda huo wa Afrika Mashariki.

Pamoja na mahitaji hayo makubwa, uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula haukidhi mahitaji hivyo kulazimika kuagiza mafuta kutoka katika mataifa ya nje.

Hata hivyo taifa kama Ukraine ambalo ni msambazaji mkubwa wa mafuta ya alizeti duniani imesimamisha shughuli na usafirishaji wa bidhaa hiyo kutokana na vita inayoendelea sasa nchini humo.

"Hapa kwetu, mambo ya Covid yalikuwa tayari yamesababisha bei ya mafuta kupanda kutoka 2,200Ksh mpaka 4,500Ksh ndani ya miaka miwili. Baada ya uvamizi (wa Ukraine) bei imepanda mpaka 5,100Ksh (dola 44$) ndani ya wiki moja", alinukuliwa na chombo cha habari cha Busness Daily cha Kenya, Mmoja wa viongozi wa sekta hiyo ya mafuta Abdulghani Alwojih.

Ukiacha vita vya Ukraine na sababu zingine za kiusalama pamoja na zile za kiuchumi na kisera, zipo sababu zingine kubwa mbili zinazotajwa wazi kuwa na mkono wake kwenye hili la kupanda kwa bei ya mafuta ya kula katika ukanda huu; mabadiliko ya hali ya hewa katika baadhi ya maeneo yanayozalisha malighafi ya mafuta ya kula pamoja na uwepo wa janga la Corona.

Kutokana na Covid-19 Malaysia pia ilipunguza uzalishaji wake kama ilivyo kwa Indonesia. Hilo limeongeza kuni za kupanda kwa 'moto' wa bei kutokana na uzalishaji wake kwenye soko la mafuta hayo.

Aghalabu kukuta sababu zote zinasadifu ukweli wa hali halisi ulivyo, wapo wanaotumia mwanya huo huo kwa manufaa binafsi kama anavyoeleza mtaalam wa masuala ya biashara kutoka chuo kikuu cha Ushirika, Moshi, Daktari Izack Kazungu; "Corona sawa, hali ya hewa sawa na vita ya Ukraine ni kweli imeendelea kuleta athari nyingi, lakini wapo wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitumia mwanya huo kuongeza bei kiholela".

Kwa nini ni muhimu kushughulika na mafuta ya kula sasa?

m

Mwiba wa mafuta ya kula haupaswi kuachwa ukaozea ndani. Unapaswa kutolewa mapema hata kama utalazimika kutolewa kwa maumivu.

Wiki iliyopita Rais wa Tanzania, alimtaka waziri wake wa fedha, Mwigulu Nchemba kushughulikia suala la mafuta ya kula.

Mara kadhaa pia viongozi wa nchi zingine kama Uhuru Kenyatta wa Kenya na Paul Kagame wa Rwanda wamewahi kusikika wakizungumzia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo na bidhaa zingine za vyakula.

"Serikali za Afrika Mashariki, hazina namna ya kukwepa kulivaa hili, kwa manufaa ya muda mrefu, hata kama litawakosesha mapato ama kuwafanya kuingia gharama kubwa, hakuna njia ya mkato", anasema Dr. Izack Kazungu.

Wataalam wanataja mambo matano makubwa yanayoweza kusaidia kuleta suluhu ya muda mrefu na kuboresha sekta ya mafuta ya kula; kuwekeza katika uzalishaji wa mafuta kupitia kilimo cha kisasa cha mazao ya mafuta kama alizeti, pamba, nazi, mawese, karanga, korosho na ufuta. P

ili kuboresha sekta ya mifugo na uvuvi kwa ajili ya kupata kwa wingi mafuta yatokanayo na wanyama na samaki.

Suala lingine ni kuondoa tozo ama kodi zinazoongeza mzigo kwenye biashara ya mafuta ama shughuli za sekta ya mafuta ya kula wakati la nne ni kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya umeme na tano ni unafuu wa mafuta ya petroli na dizeli na kuboresha miundo mbinu ya usafirishaji.

"bado kuna mambo mengi ya kufanya hasa kwa upande wa serikali (Kenya) kwa mfano, kwa kupunguza 3% ya tozo ya RDL na IDF, kupitia gharama za mafuta (Petrol na Dizeli) na nishati ya umeme kama hatua zinazoweza kuchukuliwa', alisema Alwojih.

,

Kwa upande wa Tanzania, Juhudi za kupunguza pengo la mahitaji ya mafuta ya kula lilishaanza kwa msukumo wa waziri mkuu, Kassimu Majaliwa. Pamoja na zao la alizeti linalotiliwa mkazo, nchi hiyo imeanza kutekeleza mikakati ya kuendeleza zao la michikichi kwa kuanzisha Kituo Maalum cha Utafiti wa Mchikichi cha Kihinga.

Waziri mkuu huyo alisema kuwa hadi kufikia Mei, 2021 jumla ya mbegu 5,630,376 za chikichi na miche milioni 1.5 imezalishwa na kusambazwa katika Mikoa ya Kigoma, Katavi, Kagera, Rukwa, Mbeya, Pwani na Ruvuma.

Wakati hatua zinazofanana na hizi za Serikali za Afrika Mashariki zikendelea kuchukuliwa na kusubiriwa matokeo yake, je kwa sasa wananchi takribani 300 milioni wa ukanda huu waanze kufikiria kula 'vyakula vya chuku chuku" kwa maana ya visivyoungwa na mafuta na waendelee kuumia kwa bei za mwiba?

Pengine vyakula vya kuchemsha tu, kuoka, kuchoma ama vinavyotengeneza mafuta yake wakati wa kupika vinaweza kuwa mbadala kwa wakati huu. Ingawa matumizi ya karanga za kusaga, korosho au nazi hayawezi kupuuzwa.