Chris Sutton: 'Mohamed Salah ni bora kwa sasa kuliko Lionel Messi na Cristiano Ronaldo'

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah "ni mchezaji bora wa dunia" kwa sasa , anasema mshambuliaji wa zamani wa Blackburn Chris Sutton.
Goli la Salah dhidi ya Manchester City limeelezewa kama "moja ya magoli bora kabisa yaliyowahi kufungwa kwenye ligi kuu England" kwa mujibu wa mshambuliaji wa zamani wa England Alan Shearer.
Mmisri huyo mwenye miaka 29 amefunga mabao 9 katika michezo 9 msimu huu.
"Kwa sasa, ni bora kuliko [Lionel] Messi na [Cristiano] Ronaldo," alisema Sutton.
Baada ya kufunga goli lake la 100 katika ligi kuu England mwezi Septemba , Salah alifunga moja ya mabao yake bora kabisa katika mechi dhidi ya Manchester City.
Mmisri huyo alitengeneza bao la kwanza lililowekwa kimiani na Sadio Mane baada ya kucheza vyema, lakini Phil Foden na Kevin de Bruyne waliisaidia Man City kupata ssare na alama moja muhimu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sutton alisema kiwango bora cha Salah cha kila siku, ndicho kinachomfanya awe mchezaji bora wa dunia kwa sasa.
Mbali na mabao `yake 9 aliyofunga kwenye mashindano yote, Salah ambaye bado hajasaini mkataba mpya ametoa pasi tatu za mabao mpaka sasa.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Chelsea ana wastani wa mabao 21 kwa msimu katika misimu mitatu iliyopita ya ligi kuu akifunga mabao 32 katika msimu wa 2017-2018.
"Takwimu zake zimekuwa bora katika misimu kadhaa iliyopita," Sutton alisema.
"Kufanya hivyo uwanjani , ambapo amekuwa akifanya kwa miaka mingi, inakuonyesha alivyo na uwezo na akili.
"Muendelezo wa anachofanya ndio kitu cha kuangalia, na amekuwa akifanya hivyo msimu baada ya msimu wakati wengine viwango vyao vikiporomoka na Liverpool mpaka sasa hawajampa mkataba mpya."
'Nimekuwa nikimsifia tangu tukiwa sote Fiorentina'

Chanzo cha picha, Getty Images and BBC Sport
Mlinzi wa zamani wa England Micah Richards - ambaye amecheza na Salah kwneye kikosi cha Fiorentina ya Italia mwaka 2015 - anamuunga mkono mshambuliaji wa Celtic kuhusu ubora wa Salah.
"Nimekuwa nikisema Salah ni mchezaji wa kiwango cha dunia," alisema Richards
"Kila mmoja alinicheka. Nimekuwa nikimsifu tangu akiwa Fiorentina.
"Nilivyomuona mazoezini, nilisema, 'huyu mtu ni hatari'. Anaweza kukokota mpira na kuwapita wachezaji watano na kumfunga kipa.
"Unaweza kumpa mpira katika mazingira magumu ama ya kubanwa kwa kadri unavyotaka, lakini ataupokea vizuri. Pia alikuwa mchoyo mazoezini akijua kwamba angeweza kufunga.
"Nilijaribu kuwaambia watu miaka ya nyuma lakini hakuna aliyetaka kunisikiliza - niliona uwezo wake na sasa , sishangai kile anachokifanya."













