BBI: Rege yazimwa huku maoni mseto yakitolewa kuhusu uamuzi wa korti

bb

Chanzo cha picha, Ikulu kenya

Muda wa kusoma: Dakika 3

Mahakama ya rufaa nchini Kenya imeafiki uamuzi wa mahakama kuu kwamba mchakato wa kuirekebisha katiba nchini humo maarufu kama BBI ulikiuka katiba na ni kinyume cha sheria.

Katika uamuzi wa wengi siku ya ijumaa majaji sita katika jopo la majaji saba wakiongozwa na rais wa korti hiyo Daniel Musinga walikosoa vikali mchakato na taratibu zilizofuatwa na kutumiwa kuanzisha, kupigia debe na kuwasilisha mswada wa BBI bungeni wakisema taratibu hizo zilikiuka katiba na sheria za Kenya

Majaji hao hata hivyo waliondoa maamuzi mengine yaliyotolewa na mahakama kuu kama uamuzi uliosema kwamba rais Uhuru Kenyatta alikuwa amekiuka sura ya sita ya katiba ya nchi hiyo

Maelezo ya sauti, Je ripoti ya BBI ndio suluhisho la amani na umoja wa kudumu Kenya

Wote kwa pamoja pia waliweka kando uamuzi wa wenzao wa mahakama kuu kwamba rais alikiuka sura ya sita ya katiba kwa kuanzisha mchakato wa BBI.

Majaji wote waliafiki kwamba muundo wa kimsingi unafaa kutumika katika maamuzi kuhusu marekebisho ya katiba ya Kenya.

Watano kati yao walisema kanuni ya muundo wa kimsingi inalemaza kwa kiasi fulani marekebisho ya katiba ya Kenya. Majaji Hannah Okwengu na Fatuma Sichale hata hivyo walitofautiana na uamuzi huo.

Majaji wote waliafiki kwamba kesi ya kiraia inaweza kufunguliwa dhidi ya rais aliye madarakani lakini jaji Francis Tuiyott alitofautiana na wenzake.

Majaji wote pia walikubali kwamba rais hana mamlaka ya kuanzisha mchakato wa kuirekebisha katiba. Pia korti hiyo iliamuru kwamba kamati maalum iliyosimamia mchakato wa BBI haikuwa na mamlaka ya kuanzisha mchakato wa kuirekebisha katiba.

Majaji sita waliamuru kwamba katiba haiwezi kufanyiwa kura ya maamuzi bila kuwahusisha wananchi. Jaji Sichale hata hivyo alitofautiana nao.

Maelezo ya video, Bwana Ruto amesema kufutwa kwa safari yake ni hatua ya kumdunisha

Jaji Sichale pia alitofautiana na uamuzi wa wengi kwamba tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini humo IEBC haikuwa na idadi ya kutosha ya makamishna kuendesha zoezi la kuhakiki saini zilizokusanywa kutoka kwa Wakenya na majukumu mengine ya kiutawala yaliyohusiana na utaratibu mzima wa BBI.

"Zuio la kudumu hivyo basi linatolewa kuizuia IEBC kuandaa kura ya maoni kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba wa 2020'', Majaji hao wamesema.

Katika uamuzi wao, majaji walionekana kufanya kuwa vigumu hata zaidi kuirekebisha katiba kupitia juhudi za wananchi ama za watu wengi. Wengi walimkosoa rais kwa kujaribu kuendesha mchakato wa kuirekebisha katiba kupitia jitihada za wengi, mkondo ambao unafaa tu kutumiwa na mwananchi wa kawaida.

Naibu wa Rais William Ruto asherehekea uamuzi

Miongoni mwa watu ambao maoni yao yalikuwa yametarajiwa na wengi nchini kuhusu uamuzi wa kesi hiyo ni naibu wa rais William Ruto.

wrs

Kama ilivyotarajiwa, kuzimwa kwa 'rege' ya BBI imekuwa kama wimbo mtamu kwa maskio yake. Ruto alitumia ukurasa wake wa Twitter kueleza alivyohisi. Alisema Mungu ameshuka kuwasaidia watu wanyonge na maskini ili kuilinda katiba.

Katika ujumbe wake Ruto pia aliongeza kwamba wakati sasa umewadia kwa wanyonge aliowaita 'hustlers' kuangazia njia za kuboresha hali zao kiuchumi kupitia mbinu yake ya 'Bottoms up' ambayo amekuwa akiipigia debe katika mikutano yake ya kisiasa .

Ruka X ujumbe, 1
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe, 1

Kwa naibu wa rais, uamuzi wa korti ya rufaa utakuwa kama ithibati kwa wafuasi wake na msimamo wake tangia mwanzo wa mchakato wa BBI kwamba lengo zima la BBI halikuwa zuri na hasa kwake kisiasa. Mwafaka wa 'Handshake' uliozaa BBI umelaumiwa kwa kuleta mgawanyiko mkubwa kati ya Ruto na rais Uhuru Kenyatta.

Mchakato mzima wa BBI ulionekana na kambi ya Ruto kama njia ya upande wa kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kuelekeza walivyoataka siasa za uchaguzi wa mwaka ujao.

Raila Odinga:Huu sio mwisho wa majadiliano

Kiongozi wa ODM Raila Odinga alikuwa tayari amedokeza jinsi atakavyopokea uamuzi wa korti. Siku ya Alhamisi alikuwa amesema kwamba hana nia ya kwenda katika mahakama ya juu zaidi nchini kukata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa leo.

ro

Ujumbe wake huo ulitafsiriwa na wadadisi kama njia ya kuwatayarisha wafuasi wake kustahimili makali ambayo yameambatana na kuzimwa kwa 'rege' ambayo Raila amekuwa akikariri kwamba hakuna anayeweza kuizima.

Ruka X ujumbe, 2
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe, 2

Katika ujumbe wake kupitia twitter Odinga amesema pande husika zitatathmini uamuzi wa majaji na hatua ya kutupiliwa mbali kwa BBI sio mwisho wa majadiliano kuhusu hatima ya nchi ambayo Wakenya wanaitaka.

Uamuzi huo pia utakuwa na athari katika mkondo na semi za kisiasa nchini humo kwani mageuzi ya katiba yangefanikisha mabadiliko ya muundo wa serikali hatua ambayo ingeweza kutumiwa kama chambo kujenga miungano ya kisiasa wakati taifa hilo linapojitayarisha kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao.