CCM:Chama tawala chini ya Rais Samia kitakuwa cha namna gani?

tz
    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mchambuzi

Rais Samia Suluhu Hassan amepata ushindi wa asilimia mia moja ya wapiga kura wote -avuka kigingi kingine cha Uongozi katika chama ambacho sehemu kubwa ya uongozi wake wa juu ni wanaume.

Wajumbe 1862 ambao ni sawa na asilimia 99 ya wajumbe wa Chama cha Mapinduzi .

CCM wamekutana hii leo jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wa chama hicho na kumchagua rais Samia Suluhu Hassan kuwa mwenyekiti wa Chama hicho.

Rais Samia anajaza nafasi hiyo baada ya kuachwa wazi na hayati John Pombe Magufuli ambae alifariki tarehe 17 mwezi Machi mwaka huu.

Ni mara ya kwanza kwa wajumbe wa chama hicho tawala kukutana baada ya kifo Dkt. Magufuli lakini pia ni kikao cha kwanza kwa Samia kuhudhuria kama rais wa Tanzania.

Hii ni hatua ya kihistoria katika chama hicho kuongozwa na mwanamke katika nafasi yake ya juu kabisa.

Wengi wanasubiri kwa hamu kuona ni mabadiliko gani atakayofanya mwenyekiti mpya baada ya kukabidhiwa mikoba ya kukuongoza Chama hicho kikongwe Afrika Mashariki kwa miaka mitano.

Mabadiliko yanayotarajiwa hivi sasa ni zaidi katika safu ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

Mbali na kupigwa kura ya mwenyekiti, pia kumekuwa na upigaji kura ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka nafasi mbili ambazo zilikuwa wazi.

Swali ambalo watu wengi wanajiuliza sasa ni kuhusu CCM itakuwa vipi chini ya uongozi wa Rais Samia ambaye amechukua nafasi ya hayati Rais John Magufuli aliyefariki dunia ghafla mnamo Machi 17 mwaka huu.

Kabla ya kufika huko, ni vizuri kwanza tukaifahamu CCM anayokabidhiwa kuiongoza.

CCM inayobebwa na dola, isiyopendwa na vijana

ccm

Chanzo cha picha, Getty Images

Samia amekabidhiwa Uenyekiti wa CCM miezi michache tu baada ya chama chake kuibuka na ushindi katika Uchaguzi Mkuu unaoelezwa kuwa "usiokuwa wa kidemokrasia' kuliko mwingine wowote katika historia ya chaguzi za vyama vingi hapa nchini.

CCM iliibuka na ushindi - Tanzania na Zanzibar, mbele ya malalamiko ya wapinzani kukatwa majina, wingi wa kura bandia, viongozi wa upinzani kushambuliwa na wengine kukimbilia nje ya nchi na tuhuma za wagombea wa upinzani kushawishiwa au kutishwa kujiunga na chama tawala.

Zanzibar, anakotoka Samia, aliyekuwa mgombea wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, hayati Seif Shariff Hamad, alipata chini ya asilimia 20 ya kura zote zilizopigwa - jambo ambalo wafuatiliaji wa siasa za Zanzibar hawalioni kama linawezekana kwa muktadha wa siasa za huko.

Ingawa kuna wasioitaka CCM kwa sababu tu kimekaa madarakani muda mrefu na wangetamani mabadiliko; kiu ya kawaida ya mwanadamu, baadhi ya vitendo vilivyotokea katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, vimewatia sababu nyingine zaidi ya kutaka CCM iondoke.

Samia anarithi CCM ambayo vijana wengi hawataki kuhusishwa nayo - ingawa wanatengeneza zaidi ya nusu ya wapiga kura wote, iliyogawanywa na siasa za minyukano za takribani miaka 20 sasa na inayohitaji kujitenganisha na dola ili ionekane inasimama kama chama cha siasa.

Minyukano ndani ya CCM ilianza tangu wakati wa Mkapa lakini ilichochewa zaidi wakati wa Kikwete ambako ilifikia wakati chama kikataka kujivua gamba na kuibua mgogoro ambao hatma yake ilikuwa kwa wana CCM kuimba hadharani kuwa wana imani na mtu asiyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho.

Minyukano hiyo iliendelea wakati wa Uenyekiti wa Magufuli, ambaye ni kama alitaka kutengeneza kilichoanza kuitwa CCM Mpya - akiachana na watu waliofahamika kama wana CCM kindakindaki na kuchukua wanachama kutoka vyama vya upinzani na watu wengine walioonekana kama wageni kwenye chama.

Wakati Magufuli anafariki dunia, aliyekuwa Katibu Mkuu wake wa mwisho, Dk. Bashiru Ally na Katibu Mwenezi, Humphrey Polepole, walikuwa hawajawahi kuwania nafasi yoyote ya kiuchaguzi katika ngazi za juu za CCM kabla hawajateuliwa kushika nyadhifa zao hizo.

Kama Magufuli angeendelea na uongozi wake mpaka mwisho, kulikuwa na uwezekano kuwa CCM hii ya sasa kama inavyoonekana, ingekuwa na mwonekano tofauti na viongozi na vinara wake wangekuwa watu ambao hawajazoeleka sana machoni na masikioni mwa Watanzania.

Magufuli alichaguliwa kuwa Mwenyekiti akiwa hajawahi kuwa hata mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na pengine tabia yake hiyo kama kiongozi wa chama iliakisi historia yake ya nyuma kama mtu asiye kada wa chama na asiye na fungamano na chama hicho. Kwa kawaida, CCM huakisi taswira ya Mwenyekiti wake.

Nini kinatarajiwa katika CCM ya Samia?

S

Chanzo cha picha, CCM

Tofauti na mtangulizi wake, Samia ni mtu ambaye amelelewa na kukulia ndani ya CCM. Hadi anakuwa Rais wa Tanzania, Samia alishakuwa mjumbe wa NEC na Kamati Kuu ya CCM kwa takribani miongo miwili.

Kwa sababu hiyo, haitarajiwi kwamba Samia atakwenda nje ya chama kutafuta viongozi au kujaribu kutengeneza "CCM Mpya" kama mtangulizi wake. Badala yake, anaweza kuingiza maingizo mapya katika uongozi kwa ajili ya kwenda na maono yake lakini wakawa ni watu wanaokijua chama na tamaduni zake.

Wanaomfahamu Samia wanamweleza kama mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa wa kusikiliza hoja tofauti - sifa aliyoionyesha wazi wakati wa Bunge Maalumu la Katiba ambako alisimamia mikutano migumu kwa hoja akiwa Makamu Mwenyekiti wa chombo hicho.

CCM ya Magufuli ilikuwa ikijulikana kwa kufanya vikao vifupi na visivyo na mijadala mikali tofauti na ilivyokuwa wakati wa Kikwete na inatarajiwa kwamba Samia ataachia wana CCM waambiane ukweli kupitia vikao halali vya chama kama ulivyo utaratibu wa muda mrefu wa chama hicho.

Ingawa ilikuwa haisemwi hadharani, wajumbe wa vikao vya juu vya CCM hawakuwa wakiridhishwa na tabia ya Magufuli kupeleka vikao vyao kufanyikia Ikulu ambako mazingira yake hayakuwa 'rafiki' kwa sababu ya ulinzi mkali na protokali nyingine za dola.

Tutarajie kwamba katika CCM ya Samia, siasa za ushindani baina ya chama tawala na upinzani zitarejea walau katika zama za Rais Kikwete au walau katikati ya Kikwete na Mkapa.

Wapo washauri ndani ya CCM wanaoamini kwamba inaweza kuwa hatari kwa chama hicho kurejea haraka kuwa huru kama ilivyokuwa wakati wa Kikwete kwa sababu nchi iimetoka katika utawala wa Magufuli ambao wigo wa kufanya siasa ulibinywa na hivyo kama utatanuliwa sana, udhibiti unaweza kuwa tatizo.

Kabla ya kuingia kwenye siasa moja kwa moja, Samia aliwahi kufanya kazi katika sekta binafsi na kuna dalili kwamba atajitahidi kuifanya iwe taasisi ya kisasa yenye vyanzo vyake vya mapato na inayojitegemea.

Wapi ilipo kete yake muhimu kisiasa?

Samia ndiye sasa mwanamke wa kwanza katika historia kuwa Mwenyekiti wa CCM. Tafiti nyingi za ndani za CCM zimekuwa zikionyesha kwamba bado kinaungwa mkono na wanawake katika makundi tofauti na hili ni eneo ambalo huenda akalitumia vizuri.

Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, timu ya kampeni ya Samia aliyekuwa mgombea mwenza iliundwa pia na wanawake wengi vijana na alitengeneza nao uhusiano uliofanya awe anaalikwa katika matukio mengi ya akinamama - ikiwamo Siku ya Wanawake Duniani alikoalikwa kuwa mgeni rasmi mwaka huu.

Katika hotuba yake bungeni, Samia alitamka hadharani kwamba katika mambo yake yote ya kisiasa, jambo lililo karibu zaidi na moyo wake ni lile la kuzuia vifo vya wanawake wajawazito na watoto.

Kuna sababu zote kuamini kwamba Samia atajitahidi kuifanya CCM iwe rafiki na karibu kwa wanawake, jambo ambalo litakuwa na faida ya kukizimua chama chake na kuingiza wanachama wapya ambao pengine bila juhudi za makusudi za kusaidia wanawake, wasingeweza kujiunga.

Kundi hili la wanawake litagusa pia kundi la jumla la vijana na tayari Samia ameshaonyesha kulifahamu kwa kuzungumza misemo kama "Ukizingua nami nakuzingua" ambao kundi la vijana linaweza kujihusisha nalo.

Kauli zake za mwanzo kama Rais zinamwonesha kama Mwenyekiti atakayekuwa karibu na biashara na wawekezaji - na kama eneo hilo litafanya vizuri, anaweza kujikuta akisaidia katika kupambana na tatizo la ajira linaloathiri vijana wengi hapa nchini.

Nafasi ya Zanzibar ndani ya CCM

Wanachama wa CCM

Jambo moja la wazi ambalo linajulikana kuhusu Samia ni kwamba ni mtu anayeamini kwamba CCM na Muungano kwa ujumla utakuwa imara kama nafasi ya Zanzibar itathaminiwa katika vyombo hivyo viwili.

Kama Rais wa kwanza kutoka Zanzibar tangu mwaka 1995, Samia anafahamu kwamba hii ni fursa ya kipekee kwake kusimika nafasi ya visiwa hivyo katika Muungano; na ni wazi kuwa atateua watu na kufanya kila kitu kwa kuzingatia kwamba Tanzania inaundwa na nchi mbili.

Kwa vyovyote vile, mzaliwa huyu wa Makunduchi, atahakikisha Zanzibar inapata hadhi na heshima yake katika wakati ambao yeye atakuwa Mwenyekiti wa CCM.