Ushindi wa Kaizari Sassou-Nguesso ni kuwa ujumbe bado yupo

Na Mohammed AbdulRahman
Mchambuzi
Rais Denis Sassou-Nguesso wa Jamhuri ya Congo (Brazzaville) ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa Rais uliofanyika Jumapili Machi 20. Tume huru ya uchaguzi ilisema kiongozi huyo amejinyakulia asilimia 88 ya kura, akimuacha mbali mgombea mkuu wa mpinzani Guy-Brice Parfait Kolelas akiwa na asilimia 7.84.
Ushindi huo wa kishindo ni jambo lililotarajiwa lakini kilichokuwa kikisubiri ni kwa kiwango gani.
Uchaguzi ulifanyika licha ya kifo cha mgombea mkuu wa upinzani Guy- Brice Parfait Kolelas. Kolelas alisafirishwa kwenda Ufaransa mnamo mkesha wa siku ya uchaguzi , akiugua Covid-19 na akafariki ndani ya ndege akiwa njiani.
Pamoja na wanasiasa wengine wa upinzani kuususia uchaguzi huo kwa madai ya kutopewa nafasi sawa za ushindani na Rais aliye madarakani, Kolelas na wagombea wengine watano walishiriki , wakisisitiza lisingekuwa jambo la busara kumuachia uwanja Sassou- Nguesso, licha ya kuwepo dalili zote za mizengwe kuhakikisha anatangazwa mshindi.
Kimsingi kuna kifungu cha katiba kinachotaja juu ya kufutwa matokeo pindi mgombea mmoja anafariki, lakini Tume ya uchaguzi ilisema safari hii, kifungu hicho hakina uzito.

Alivyopanda ngazi hadi kutwaa madaraka
Mwanajeshi huyo kamanda wa zamani wa kikosi cha askari wa miamvuli, alikuwa sahibu mkubwa wa mwanajeshi mwenzake Kapteni Marien Ngouabi na kwa pamoja wakashirikiana kuupindua utawala wa Alphonse Massamba Debat 1968.
Congo Brazzaville ikaitwa Jamhuri ya watu wa Congo, na kuongozwa na Chama cha wafanyakazi cha nadharia kisoshalisti - Parti Congolese du Travail-PCT.
Ngouabi aliuwawa 1977 kwenye makazi yake Ikulu 1977 katika mazingira ya kutatanisha.
Wadadisi wanaashiria kulikuwa na uhasama wa kuwania madaraka ndani ya PCT kati ya Nguesso na Joachim Yombi Opango aliyemrithi Ngouabi na Sassou -Nguesso, aliyeshikilia wadhifa wa Waziri wa ulinzi. Opango alilazimishwa kujiuzulu na Sassou-Nguesso akatwaa madaraka.
Mwaka 1991 aliruhusu mfumo wa vyama vingi na akashindwa na Pascal Lissouba katika uchaguzi uliofanyika mwaka mmoja baadae .
Sassou-Nguesso alirudi madarakani kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati wanamgambo wake " Cobra" walipoyashinda majeshi ya serikali ya Lissouba 1997.
Mbali na kusaidiwa na majeshi ya Angola, wengi wanaamini Ufaransa ilikuwa na mkono wake.
Lengo lilikuwa ni kudhibiti utajiri wa mafuta kupitia kampuni lake kubwa la Total. Jamhuri ya Congo ni mchimbaji mkubwa watatu wa mafuta barani Afrika , kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kadhia ya kuuwawa Ngouabi, inafanana na ile ya Thomas Sankara wa Burkina faso na rafiki yake mkubwa Blaise Compaore.
Sababu hasa kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi ilikuwa ni kinyanganyiro cha kuwania madaraka na ushawishi kutoka nje.
Wote wawili Sassou-Nguesso na Compaore waliachana na sera za kimapinduzi na kufuata mfumo wa kipepari, wakijenga uhusiano wa karibu na viongozi wa Ufaransa.
Hatua kali kuwadhibiti wapinzani

Sassou-Nguesso amekuwa havumilii upinzani wa aina yoyote dhidi ya utawala wake.
Wapinzani na wanaharakati kadhaa wa haki za wako magerezani akiwemo Mkuu wa zamani wa majeshi Jean-Marie Michel Mukoko aliyehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa mashtaka ya kuhatarisha usalama wa taifa. Mwingine ni André Okombi Salissa, waziri wa zamani aliyethubutu kumpinga na akajitokeza kushindana naye katika uchaguzi wa 2017.
Kwa upande mwingine alikataa kuwaalika waangalizi wa Umoja wa mataifa na Umoja wa Ulaya kuangalia uchaguzi na wizara ya ndani ikawanyima kibali wajumbe wa Kanisa Katoliki kuwa waangalizi. Mbali na hayo mnamo siku ya uchaguzi mawasiliano yote kwa kutumia internet yalifungwa. Mtindo huu mpya umeanza kutumika katika nchi nyingi za Afrika wakati wa uchaguzi , ikiwa ni pamoja na Uganda wakati wa uchaguzi wa Januari mwaka huu.
Sassou-Ngueso anashutumiwa vikali kwa utawala mbaya , umasikini, njaa, rushwa na ukosefu wa usawa miongoni mwa jamii ambayo hainuafaiki na utajiri wa mafuta ya nchi hiyo, wakati familia yake ikijitajirisha na kuwekeza nchini Ufaransa.
Sababu nyingine ya kubaki madarakani muda wote huu, ni uamuzi wa kuibadili katiba 2015 kwa kuitisha kura ya maoni ili aweze kuendelea, akifuata mkondo wa baadhi ya marais wenzake barani Afrika. Wote walifanya hivyo wakati muhula wa kila mmoja wao ulipokaribia kumalizika. Mtindo huo unaendelea. Mfano wa karibuni ni ule wa Marais wa Cote d´Ivoire (Ivory Coast) na Guinea Alassane Ouattara na Alpha Conde.
Jumuiya za kiraia na mashirika ya haki za binadamu katika Jamhuri ya Congo yametoa wito wiki hii kuitaka Ufaransa wanayodai inamlinda kisiasa Sassou-Nguesso ,ilaani kuzorota kwa hali ya kisiasa na kijamii katika taifa hilo la ukanda wa Afrika kati.
Ajiunga na safu ya vigogo

Ushindi wa Sassou Nguesso wa asilimia 88 uliotangazwa na Waziri wa ndani, baada ya kupokea matokeo kutoka Tume ya Uchaguzi ilioteuliwa na Rais mwenyewe ni wa kishindo. Chini ya utaratibu unaohusiana na uchaguzi waziri wa ndani ndiye anayeratibu uchaguzi. Mfumo huo hutumika katika nchi nyingi za kiafrika zilizokuwa makaloni ya Ufaransa.
Akiwa na umri wa miaka 77 ana miaka 36 madarakani, anajiunga na kilabu ya vigogo,kundi la kina Teodoro Obiang Nguema wa Guinea ya Ikweta, Paul Biya wa Cameroon na Yoweri Museveni wa Uganda wanaohesabika kuwa viongozi waliotawala muda mrefu barani Afrika. Nguema ametimiza miaka 40 madarakani, Biya 38 na Museveni aliyeanza muhula mwengine baada ya kushinda uchaguzi mwezi Januari ameshatawala kwa miaka 35.
Binafsi Sassou Nguesso anadai usalama wa Congo unamtegemea yeye, msemo alioutumia kama kauli mbiu wakati wa kampeni yake ya uchaguzi. Kuna wasiwasi juu ya kujihusisha wanawawe katika siasa. Binti yake Claudia na mwanawe wa kiume Denis Christel wote ni wabunge katika bunge la taifa. Pia Claudia ni mshauri wake maalum wa masuala ya mawasiliano, lakini amekanusha uvumi uliozagaa kwamba anamuandaa Christel kuwa mrithi wake.
Kilichodhihirika baada ya uchaguzi huu, ni kwamba bado demokrasia ni mtihani kwa wananchi wa jamhuri ya Congo. Lakini vyovyote itakavyokuwa, kwa hivi sasa wakati akijitayarisha kuanza muhula mwengine tena wa miaka mitano, "Kaizari" Denis Sassou-Nguesso kama wafuasi wake wanavyopenda kumwita haoneshi dalili ya kustaafu. Bado yupo .













