Wanafunzi wafundwa kuhusu afya ya uzazi kupunguza mimba za utotoni

- Author, Aboubakar Famau
- Nafasi, BBC Africa, Tanzania
Zaidi ya wanafunzi mia moja katika maeneo mbalimbali mkoani Singida, nchini Tanzania wamemaliza mafunzo ya siku tatu yaliyolenga kutoa elimu ya afya ya uzazi.
Mafunzo hayo yametolewa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya na shirika lisilo la kiserikali la World Vision, huku yakiwa na lengo la kupunguza mimba za utotoni mkoani humo.
Waandaaji wa mafunzo hayo, wanatarajia kwamba wanafunzi hao watatumia vyema mafunzo walioyapata katika kipindi cha siku tatu ili kuepukana na janga la mimba za utotoni, ambapo mkoa wa Singida unatajwa kama miongoni mwa mikoa mitano yenye asilimia kubwa ya mimba za utotoni.
Mikoa mengine ni pamoja na Shinyanga, Dodoma, Tabora na Mara.

Penina Masanja ni miongoni mwa wanafunzi waliopata mafunzo hayo anasema hivi SAS's amepata hamasa baada ya kupata elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi.
Mbali na suala la mimba za utotoni imebainika pia kwamba changamoto nyingine wanazokumbana nazo watoto wa kike ni pamoja na ukosefu wa taulo pindi wanapokuwa katika siku zao.
Nasra Mohamed ni miongoni mwa wanafunzi waliohitimu mafunzo hayo anaelezea jinsi alivyowahi kukatisha masomo baada ya kukosa sodo.
"Tulikuwa tunapata tabu sana kipindi cha mwanzo maana yake tulikuwa hatuna uwezo wa kununua taulo za kike, lakini baada ya kupewa tunaona kuna mabadiliko makubwa kwa wanafunzi," anasema Nasra.
Licha ya juhudi zinazofanywa na serikali na mashirika mbalimbali kutokomeza tatizo la mimba za utotoni, lakini inaonekana bado lipo katika baadhi ya maeneo.

Tumaini Fredy ambae ni mtaalamu kutoka shirika la World Vision Tanzania anasema kambi hizi za kuwafunda watoto waliofikia umri wa balehe katika masuala ya afya ya uzazi na mimba za utotoni, mpaka sasa imefanyika katika mkoa wa Singida na Shinyanga ambapo hivi sasa wahitimu wanategemewa kwenda kutoa elimu kwa wenzao.












