Rwanda yaongoza kwa kutoa chanjo ya HPV, waathiriwa wanasemaje?

Saratani ya shingo ya kizazi ni ya nne miongoni mwa saratani zinazowapata wanawake duniani.
Angeline Usanase aligunduliwa kuwa na saratani hiyo akiwa na umri wa miaka sitini na saba.
"Miaka yote nilikuwa wa afya nzuri sana. Lakini mnamo mwaka 2017, niliona matone ya damu, ambayo yalinishangaza sana kwa kuwa nilikuwa nimepitisha umri wa kupata hedhi.
Nilifika kituo cha afya na ndipo waliponishauri nikafanyiwe uchunguzi. Daktari alinieleza kuwa ninao ugonjwa wa saratani katika awamu ya kwanza.
Nilishtuka sana na hata sikutaka kukubali. Wazo la kwanza kunijia akilini lilikuwa kifo. ''
Angeline alianza punde matibabu ili kuzuia kuenea kwa saratani hiyo.
"Baada ya kumaliza matibabu ya dawa yaliyodumu miezi mitatu katika kituo cha afya karibu na nyumbani, niliagizwa kwenda hospitali moja nchini Kenya mnamo mwezi Machi mwaka jana ili kuanza matibabu ya mionzi, kwasababu tiba ya aina hiyo haikuwa inapatikana nchini Rwanda wakati huo".
Matibabu ya saratani nchini Rwanda yanatolewa kwa malipo .
Angeline ni miongoni mwa wachache walionufaika kwa kupata ufadhili wa serikali kusafiri nje ili kutibiwa na hii leo anasema hana saratani tena.

Tangu mwaka 2006, zaidi ya nchi 80 duniani zimezindua chanjo ya HPV.
Chanjo ya HPV inazuia maambukizi ya virusi ambavyo husababisha saratani ya shingo ya kizazi.
Lakini ni nchi chache pekee ndio ambazo zimefanikiwa kuwafikia wasichana wengi zaidi katika kutoa chanjo.
Mwaka 2013, Rwanda alianza kutoa chanjo hii ya HPV kwa wavulana pia.
Chama cha kimataifa kinachokabiliana na virusi vya HPV kinasema, huenda hatua ya Rwanda ikawa kama mfano wa majaaliwa ya kukabiliana na saratani ya shingo ya kizazi.
Soma zaidi kuhusu saratani:

Hata hivyo baadhi ya mila na utamaduni sawa na imani za kidini mara kwa mara zimekua kizingiti dhidi ya jamii kuikumbatia chanjo hii.
"Lazima kwa sababu ni mwanzo wa mradi huu, kulikuwa na habari nyingi tu zisizo za kweli pamoja na dhana potofu. Watu wakisema kuwa chanjo sio nzuri kwa watoto wetu na kuwafanya wawe tasa.
''Haya ni mambo tuliokabiliana nayo hapo awali lakini tunazidi kuwaelimisha watu kupitia watu wanaowaamini katika jamii kama vile wahudumu wa afya, viongozi wa jamii,na sasa tunaweza kusema kuwa dhana hizo potofu hazipo tena''.
Nchi hii imepiga hatua katika kukabili saratani ya shingo ya kizazi na uchunguzi wa ugonjwa huu unatolewa kwa Umma bila gharama yeyote.
Katika hospitali hii ya nyargunga, wanawake mia mbili hamsini wamefika kukaguliwa saratani ya uzazi.

"Saratani ya mlango kizazi ndio hutokea mara nyingi hapa nchini Rwanda na wanawake wengi huja kuchunguzwa wakiwa wamechelewa sana.
Kwa hiyo tuliona umuhimu wa kufanya juhudi zaidi katika kuzuia lakini pia juhudi za kuwatibu wale walioathiriwa na ugonjwa huo''
Nchi nyingine zilizoanzisha chanjo ya HPV ni kama vile Botswana, Uhabeshi, Zimbabwe, miongoni mwa nyingine nyingi zaidi.
Shirika la Afya duniani limeidhinisha ubora wa chanjo hiyo na hakujakuwa na ripoti za athari mbaya za chanjo hiyo.
Watalaamu wanasema matokeo ya sasa, yanatoa matumaini kwamba chanjo iliyozinduliwa muongo mmoja tu huenda ikawa suluhu la kuangamiza ugonjwa huu.
















