Kimbunga Florence bado tishio maisha ya watu huko Marekani

Idadi kubwa ya watu inahofiwa kwamba huenda watakufa Pwani mashariki nchini Marekani kutokana na madhara makubwa ya kimbunga Florence. Taasisi ya majanga ya FEMA imearifu kuwa upepo utokanao na Kimbunga utasababisha mafuriko makubwa katika maeneo hayo.
Taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinasema kuwa mvua kubwa ,upepo mkali na radi vimeendelea kusambaa maeneo ya Pwani ya kaskazini mwa jimbo la Carolina.
Kitengo cha kukabiliana na vimbunga nchini Humo,kimearifu kuwa kasi ya upepo kwa sasa imefikia kilomita 165 kwa saa.
Rais Donald Trump ametangaza hali ya hatari katika maeneo ya Kaskazini na kusini mwa jimbo la Carolina ambapo pia eneo kubwa la Washington DC limechukua pia tahadhali.
Kimbunga hicho kinachotajwa kibaya kuwahi kutokea siku ya ijumaa kinatarajiwa kuyapiga maeneo ya pwani ya mashariki.
Mkurugenzi wa kitengo cha majanga Kaskazini mwa jimbo la Carolina Mike Sprayberry, anasema kuwa wamejiandaa vilivyo na hasa kutokana na uzoefu walioupata mwaka 2016 kuhusiana na kuokoa idadi kubwa ya watu. ''Tulipata somo wakati wa Kimbunga Matthew,tulikuwa tukiwatumia wataalam wetu wa masuala ya mafuriko,na hali ya hewa ambapo ilikuwa taarifa maalumu na za uhakika zinafikishwa kwa wananchi ambao wapo katika hatari na kisha wanaokolewa wakiwa katika eneo moja,na kisha kuwafuata wale ambao utabiri unaonyesha kwamba watafikiwa na madhara baadaye,hivyo mbinu hiyo tunaitumia tena safari hii''.Mike Sprayberry.
Hata hivyo kasi hiyo inatarajiwa kupungua hadi kitovu cha kimbunga hicho kitakapo fika maeneo ya Pwani. Takribani watu million 1.7 wameyahama maeneo yao katika maeneo ya Georgia, Kaskazini na Kusini mwa Carolina, Virginia na Maryland,huku hali ya tahadhari ikiwa tayari imetangazwa katika maeneo hayo.








