Yaser Abdel Said: Mwanamume aliyekuwa akisakwa sana na FBI akamatwa

Chanzo cha picha, FBI
Dereva wa taxi ambaye amekuwa akitafutwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya binti zake wawili amekamatwa baada ya kwenda mafichoni kwa miaka 12 iliyopita.
Waranti ya kumkamata Yaser Abdel mwaka 2008 baada ya kuwapiga risasi binti zake, Sarah Yaser Said, 17, na Amina Yaser Said, 18.
Mshukiwa huyo mzaliwa wa Misri aliwekwa kwenye orodha ya shirika la upelelezi la Marekani FBI, ya watu 10 wanaotafutwa zaidi mwaka 2014.
Karibu miaka saba baadae, amekamatwa na kuzuiliwa Justin, Texas, akiwa na jamaa zake wawili.
Mtu huyo aliye na umri wa miaka 63- hivi karibuni atahamishwa Kaunti ya Dallas, ilisema taarifa iliyotolewa na Idara ya FBI Dallas siku ya Jumatano.
Jopo kazi la uhalifu wa ghasia linaloongozwa na FBI mjini Dallas limekuwa likimtafuta kwa muda mrefu Yaser Abdel," alisema ajenti maalum wa FBI Dallas, Matthew DeSarno.
"Wachunguzi hawa wenye tajiriba hawajawahi kuchoka kumtafuta kwani waliahidi kuwapa haki wahasiriwa katika kesi hii."
Mama ya wasichana hao, Patricia Owens, amesema amefurahishwa na hatua ya kukamatwa kwake, na kuambia vyombo vya habari vya mji huo: "Sasa wasichana wanaweza kupumuzika kwa amani ."
FBI pia ilitangaza kuwakamata watu wawili zaidi, kwa mujibu wa ripoti ya CBS DFW.
Islam Said, mwana wa kiume wa mshukiwa, na Yassim Said, ndugu yake mshukiwa walishitakiwa kwa, kumficha mtoro huyo.
Said ameshitakiwa kwa kosa gani?
Uchunguzi wa mauaji ulianzishwa Januari mosi 2008 baada ya Amina na Sarah kupatikana wakiwa wameuawa kwa kupigwa risasi.
Siku hiyo, mshukiwa aliwabeba kwenye taxi wasichana hao kwa kisingizio kwamba anaenda kuwanunulia chakula, FBI inadai.
FBI inasema aliwapeleka hadi Irving, Texas, ambako inadaiwa aliwapiga risasi wasichana hao ndani ya gari. Wote walifariki kutokana na majeraha kadhaa ya risasi.

Chanzo cha picha, FBI
Kabla ya vifo vyao, jamaa wa familia aliwaambia polisi kwamba mshukiwa alitishia "kumdhuru" Sarah kwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu ambaye sio Muislamu, kwa mujibu wa kituo cha habari cha CBC.
Shangazi ya dada hao wawili, Gail Gattrell, ametaja mauaji yao kama "mauaji ya heshima".
Mauaji ya mwanafamilia anayedhaniwa kufedhehesha jamaa zake wakati mwingine husemekana kuwa "mauaji ya heshima" - lakini wakosoaji wanapinga maana inayotolewa kwa mauaji kama hayo.
Idara ya polisi ya Irving ilifanya uchunguzi wa mauaji ya Amina na Sarah na, kufikia Januari 2, 2008 waranti ya kukamatwa kwa Yaser Abdel Said ilitolewa.
Tangu wakati huo, maajenti wa FBI "wamekuwa wakipambana kuwatafutia haki Amina na Sarah",Mkuu wa Idara ya polisi ya Irving Jeff Spivey, alisema.












