Shinikizo yazidi kwa Rais Biden kujibu mashambulizi ya wanamgambo wa Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Haijabainika ni umbali gani Marekani inaweza kufika, lakini hali hiyo ni ukumbusho wa kile kilichotokea baada ya mashambulizi ya Desemba 2019, wakati wanamgambo wa Iraq waliporusha makombora kwenye kambi ya Marekani huko Kirkuk, na kumuua mwanakandarasi wa Marekani.
Baada ya shambulio hilo, Marekani ililipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi makubwa ya anga kwenye kambi ya wanamgambo kwenye mpaka wa Iraq na Syria, na kuua wanachama 25.
Mazishi yao yalizua maandamano ya wanamgambo wa Shia wanaoiunga mkono Iran na wafuasi wake, ambao walivamia ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.
Msururu huu wa matukio ulichangia pakubwa katika uamuzi wa Rais wa zamani Donald Trump kumuua mmoja wa makamanda wakuu wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC), Jenerali Qasem Soleimani.
Marekani na Iran zimesema mara kwa mara katika miezi michache iliyopita kwamba hazitaki kusambaa kwa vita zaidi katika eneo hilo.
Bila shaka kutakuwa na mahesabu mengi na uwezekano wa kubadilishana ujumbe nyuma ya pazia kati ya Tehran na Washington, lakini kilichotokea katika Mnara wa 22 kinafanya iwe vigumu zaidi kwa Marekani kusitisha majibu yake kwa "washukiwa wa kawaida tu".
Swali linabaki, je, Marekani itafanya kitu sawa wakati huu shinikizo linapozidi kwa utawala wa Biden kuijibu moja kwa moja Iran kama muungaji mkono wa makundi haya?















