Shukran za dhati msomaji wetu kwa kufuatilia matangazo haya ya moja kwa moja.Kuwa na usiku mwema, Alamsiki
Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Besigye asusia kula kulalamikia hatua ya kuzuiliwa kwake gerezani
Besigye, aliyekuwa daktari wa kibinafsi wa Rais Yoweri Museveni, alikamatwa katika mazingira ya kutatanisha mwezi Novemba mwaka jana jijini Nairobi.
Muhtasari
- Zimbabwe yatangaza kulipa fidia raia wa kigeni waliopokonywa mashamba yao
- Marekani na Uingereza zasusia kusaini azimio la akili mnemba AI
- Canada yaapa kujibu ushuru wa Trump kwa bidhaa zinazoingia Marekani
- Israel imeshindwa kutimiza ahadi za kusitisha mapigano - Rais wa Uturuki
- Rais wa Sudan Kusini awafuta kazi viongozi wakuu na mkuu wa ujasusi
- Kiongozi wa CAR azindua 'majaribio' ya sarafu ya meme
- Besigye asusia kula kulalamikia hatua ya kuzuiliwa kwake gerezani
- Trump kukabiliwa na upinzani mkali kutoka Jordan juu ya mpango wa Gaza
- Vitisho havina maana katika kusitisha mapigano - afisa wa Hamas
- Mwalimu amchoma kisu mtoto wa miaka minane nchini Korea Kusini
- Trump atangaza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zote za chuma na alumini zinazoingizwa
- Muungano unaoongozwa na Musk watoa ofa ya $ 97.4bn kwa mtengenezaji wa Chatgpt
- Zaidi ya watu 50 wafariki dunia baada ya basi kuanguka kutoka kwenye daraja Guatemala
- Hamas kuahirisha makubaliano ya kuwaachilia mateka na kulaumu Israel
Moja kwa moja
Na Asha Juma na Mariam Mjahid
Zimbabwe kuwalipa fidia raia wa kigeni waliopokonywa mashamba yao
Zimbambwe imeanzisha tena mpango wa kufiwadia kwa raia wa kigeni ambao mashamba yao yalinyakuliwa wakati wa mradi tata wa serikali.
Waziri wa fedha wa Zimbambwe amethibitisha leo kuwa mashamba 94 yalioidhinishwa kwa mpango wa fidia mwaka jana sasa wamiliki wake wameanza kupokea pesa zao wakiwemo raia 56 kutoka Uholanzi, Denmark,Ujerumani,Uswizi na Yugoslavia.
Kufidia mashamba ambayo yamelindwa na makubaliano ya mali ni suala muhimu itatoa fursa kwa Zimbabwe kuanza upya mazungumzo na mataifa ya magharibi kuhusu kulipa deni .
Waziri huyo Mthuli Ncube amedokeza ametenga dola milioni 20 kufidia na bado wana deni la dola milioni 125.
Hatua ya kuchukua mashamba yaliyokuwa yakimilikwa na wazungu enzi za ukoloni ilipelekea mataifa ya magharibi kuwekea vikwazo na kulazimisha Zimbabwe kulipa fidia wamilki wa ardhi hizo.
Hata hivyo wamiliki wengi wa mashamba yaliyonyakuliwa ni wakazi nchini humo na kufikia sasa hawajalipwa.
Pia unaweza kusoma:
Marekani na Uingereza zasusia kusaini azimio la akili mnemba AI
Uingereza na Marekani zimekataa kusaini azimio la kimataifa kuhusu akili mnemba (AI) katika mkutano wa kimataifa uliofanyika Paris.
Azimio hilo, lililosainiwa na Ufaransa, China, India na nchi nyingine, linahimiza njia ya “wazi,” “kujumuisha,” na “ya kimaadili” katika maendeleo ya AI.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza ilisema kuwa Uingereza haikukubaliana na baadhi ya vipengele vya azimio hilo na itaunga mkono tu mipango inayohusiana na maslahi yake ya kitaifa.
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, alisema kuwa kudhibiti AI kupita kiasi kunaweza “kuua sekta hii” na akasisitiza kuwa sera zinazohamasisha maendeleo ya AI zinapaswa kutiliwa mkazo badala ya usalama.
Uingereza imekuwa mstari wa mbele katika suala la usalama wa AI, ambapo Waziri Mkuu wa zamani, Rishi Sunak, aliongoza mkutano wa kwanza wa Usalama wa AI duniani mwaka 2023.
Hata hivyo, Andrew Dudfield kutoka Full Fact alieleza kuwa uamuzi wa kutotia saini kwa Uingereza unaweza kuathiri sifa yake kama kiongozi wa dunia katika uvumbuzi wa AI salama na wa kimaadili.
Azimio lililosainiwa na nchi 60 linasisitiza umuhimu wa kupunguza pengo la kidijitali na kuhakikisha AI inapatikana kwa wote, ikiwa ni pamoja na kuwa “wazi,” “salama,” na “ya kuaminika.”
Pia, mjadala kuhusu athari za maendeleo ya AI kwa jamii, mazingira, na utawala uliendelea.
Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, alisisitiza umuhimu wa uvumbuzi, ushirikiano, na teknolojia ya chanzo wazi ili kuendeleza maendeleo ya akili mnemba AI.
Pia unaweza kusoma:
Canada yaapa kujibu ushuru wa Trump kwa bidhaa zinazoingia Marekani
Canada imesema itajibu kwa haraka kwa ushuru wa 25% aliouweka Rais wa Marekani Donald Trump kwa bidhaa za chuma na alumini zinazoingia Marekani, kwa mujibu wa waziri wa viwanda wa Canada.
Rais Donald Trump alisema ataanza utekelezaji wa ushuru huo kuanzia tarehe 12 mwezi Machi.
Canada ni nchi ambayo inauza vyuma hivyo Marekani na Trump ameapa kuongeza ushuru kama sehemu ya mpango wake wa kumanya Marekani kuwa tajiri tena.
Canada, imesema ushuru huu utadhuru sekta za kiuchumi katika nchi zote mbili.
Viongozi wa Canada na wa majimbo wamekemea hatua hii, na baadhi ya wanasiasa wamesema watatoa jibu la kulipiza kwa Marekani ikiwa wataingia madarakani.
Waziri wa Viwanda wa Canada François-Philippe Champagne alisisitiza kuwa biashara za chuma kutoka Canada zimeifanya Amerika Kaskazini kuwa mshindani na salama zaidi kiuchumi.
Licha ya kuwa na mzozo wa kibiashara na Canada na Mexico, Trump alikubali kuahirisha kwa siku 30 utekelezaji wa ushuru huu kwa bidhaa kutoka nchi hizo mbili.
Trump pia ameweka ushuru wa asilimia 10% kwa bidhaa kutoka China, huku China ikijibu kwa haraka dhidi ya bidhaa za Marekani.
Aidha, Trump ameashiria kuwa atafanya hivyo kwa bidhaa kutoka Umoja wa Ulaya, na alieleza kwamba hatakuwa na shida na tishio kwa washirika wa kibiashara wa Marekani kulipiza kisasi.
Pia unaweza kusoma:
Israel imeshindwa kutimiza ahadi za kusitisha mapigano - Rais wa Uturuki
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema Israel imekosa kutimiza ahadi zake kuhusu kusitisha mapigano na kusisitiza Israel ikome kuvamia Palestina.
Aliongeza kuwa Uturuki inaendelea kutuma misaada kwa Gaza na inataka kuanzishwe kwa taifa huru la Palestina.
Naye Rais wa Syria, Ahmed al-Sharaa, amesema Rais Donald Trump ameanza vizuri kipindi chake cha pili, lakini anakosoa mpango wa kuhamisha Wapalestina na kuwapeleka Jordan, akisema kuwa ni uovu mkubwa.
Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, ameitaka jamii ya kimataifa kusaidia ujenzi wa Gaza badala ya kuwahamisha Wapalestina, huku akipinga vikali mpango wa Trump wa kuchukua udhibiti wa Gaza au kuinunua.
Wakati huo huo, mfalme wa Jordan Abdullah amekutana na baadhi ya washauri wakuu wa Rais Donald Trump kabla ya viongozi hao wawili kukutana.
Mfalme Abdullah alifanya kikao na mshauri wa masuala ya kiusalama ya kitaifa Mike Waltz.
Pia unaweza kusoma:
Rais wa Sudan Kusini awafuta kazi viongozi wakuu na mkuu wa ujasusi
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, amewafuta kazi makamu wake wawili, mkuu wa idara ya ujasusi wa nchi hiyo, pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu.
Uamuzi huu ulitangazwa kupitia mfululizo wa amri za rais zilizosomwa na mtangazaji wa runinga ya taifa.
Hakukuwa na maelezo yoyote kuhusu sababu za uamuzi huo.
Sudan Kusini ina makamu watano wa rais kama sehemu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2018 yaliyolenga kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Nchi hiyo yenye rasilimali za mafuta ilipata uhuru wa kujisimamia kama taifa mwaka 2011 baada ya kujitenga na Sudan, lakini ilijikuta ikikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya Rais Kiir na makamu wake Riek Machar kugombana.
Makubaliano ya kugawana madaraka ya mwaka 2018 yamekuwa na changamoto nyingi.
Mmoja wa makamu wa rais aliyeondolewa ni James Wani Igga, mwanasiasa mzoefu na jenerali, ambaye amekuwa katika wadhifa huo tangu 2013 na pia alikuwa naibu mwenyekiti wa chama cha SPLM, chama cha rais.
Mwingine ni Hussein Abdelbagi Akol, kutoka muungano wa upinzani (SSOA) ambao si sehemu ya harakati kuu za upinzani za Makamu wa Rais wa Kwanza, Riek Machar. Akol ameteuliwa kuwa waziri wa kilimo, akirithi Josephine Joseph Lagu kutoka muungano wa SSOA ambaye sasa anakuwa makamu wa rais.
Benjamin Bol Mel, ambaye alihukumiwa na Marekani mwaka 2017 kwa tuhuma za rushwa, amepewa nafasi ya Igga kama makamu wa rais.
Mel, ambaye awali alikuwa mjumbe maalum wa rais kwa programu maalum, amekuwa akitajwa kama mmoja anayeweza kumrithi Kiir.
Rais hajateua waekezaji wa nafasi za waziri wa afya na gavana wa jimbo la Equatoria Magharibi, ambao wote wanatoka chama cha Machar.
Pia hajateua mbadala wa kudumu kwa mkuu wa ujasusi, Akec Tong Aleu, ambaye alihudumu miezi minne tu tangu kuteuliwa mwezi Oktoba.
Makubaliano ya amani ya 2018 yanampa rais mamlaka ya kuteua na kufuta kazi maafisa wa serikali katika ngazi za kitaifa na za majimbo.
Rais anaweza kuteua na kufuta kazi maafisa kutoka vyama vingine vya kisiasa kwa idhini ya uongozi wa vyama hivyo.
Haijulikani kama kufutwa kazi kwa gavana wa Equatoria Magharibi na waziri wa afya kulikuwa kumeidhinishwa na kiongozi wa chama chao, Machar. chama cha SPLM-In Opposition hakijatoa maoni kuhusu jambo hili.
Sudan Kusini haijafanya uchaguzi tangu kupata uhuru.
Kura za kwanza za kitaifa zilipangwa kufanyika mwaka 2015, lakini uchaguzi huo haukuweza kufanyika kutokana na mzozo uliozuka mwezi Desemba 2013.
Uchaguzi huo ulipangwa kufanyika mwaka 2022, lakini uliahirishwa kwa miaka miwili na ulitarajiwa kufanyika miezi miwili iliyopita.
Uchaguzi huo uliahirishwa tena, na uongozi wa nchi ulisema kuwa uchaguzi sasa utafanyika mwezi Disemba 2026.
Pia unaweza kusoma:
Kiongozi wa CAR afanyia 'majaribio' sarafu yake ya mtandaoni
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Faustin-Archange Touadéra, amezindua sarafu ya mtandaoni ya meme kwa lengo la kuinua hadhi ya nchi, ambayo ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani.
Sarafu za meme hutumika kujenga umaarufu kwa mtindo wa intaneti au harakati na mashabiki huvutiwa na kukusanya na kuipa thamani yao, lakini ni uwekezaji wa kipekee na unaobadilika kwa haraka.
Touadéra alitangaza uzinduzi wa sarafu hiyo, inayoitwa $CAR, kupitia akaunti yake ya X mwishoni mwa juma na Jumatatu alisema kuwa ilikuwa “mafanikio.”
Hata hivyo, thamani ya sarafu hiyo ilishuka kwa kiasi kikubwa hadi asilimia 90%, kulingana na tovuti maalum.
Mnamo mwaka 2022, CAR ilikubali sarafu ya Bitcoin kama fedha halali, ikawa nchi ya pili duniani baada ya El Salvador kufanya hivyo.
Touadéra alielezea uzinduzi wa sarafu ya meme ya juma hili kama “majaribio” ya jambo linaloweza “kuunganisha watu, kusaidia maendeleo ya kitaifa, na kuweka nchi hiyo jukwaani kimataifa kwa njia ya kipekee.”
Sarafu za meme mara nyingi zimekosoa kwa asili yao ya kubashiri, ambapo watumiaji huunda au kununua kwa matumaini kuwa thamani yao itaongezeka na kupata pesa haraka - lakini wengi huelekea kupoteza pesa zao.
Kabla ya kuapishwa kwake mwezi uliopita, Rais wa Marekani Donald Trump alizindua sarafu yake ya meme ambayo thamani yake ilipanda haraka, na inaripotiwa kwamba ilikusanya mamilioni ya dola kwa ajili yake.
The New York Times imeripoti kuwa sasa inathamani ya robo ya thamani yake ya juu zaidi.
Pia unaweza kusoma:
Besigye asusia kula kulalamikia hatua ya kuzuiliwa kwake gerezani
Kiongozi wa upinzani wa Uganda Dk. Kizza Besigye, amesusia kula katika gereza la Luzira mjini Kampala.
Wasaidizi wake wanasema Besigye analalamikia kuendelea kuzuiliwa kwake kufuatia uamuzi wa mahakama kuu ya nchi hiyo mwezi uliopita uliozuia mahakama za kijeshi kuwahukumu raia.
Harold Kaija, msaidizi wa kisiasa wa chama cha Besigye cha People’s Front for Freedom (PFF), amethibitisha hatua ya kiongozi huyo kususia kula.
"Naam, ni kweli. Ameanza mgomo wa kususua kula. Tunaamini anafanya hivyo hatua ya kuendelea kumshikilia gerezani- anapaswa kuwa nyumbani," Kaija aliambia BBC.
Aliongeza kuwa PFF inashirikiana na mamlaka husika kuhakikisha Besigye anaachiwa huru.
Besigye, aliyekuwa daktari wa kibinafsi wa Rais Yoweri Museveni, alikamatwa katika mazingira ya kutatanisha mwezi Novemba mwaka jana jijini Nairobi pamoja na msaidizi wake wa kisiasa, Obeid Lutale.
Wawili hao baadaye walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi mjini Kampala, ambapo walishtakiwa kwa kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria—mashtaka ambayo wanapinga.
Katika uamuzi wa kihistoria mwezi uliopita, Mahakama ya Juu ya Uganda ilitangaza kuwa ni kinyume cha katiba kwa mahakama za kijeshi kuwahukumu raia, na kuamuru kesi zote hizo kuhamishiwa katika mahakama za kiraia.
Uamuzi huo ulimkasirisha Rais Museveni, ambaye alipuuzilia mbali na kuutaja kuwa "uamuzi usio sahihi" na kuapa kuupinga.
Wakati huo huo, Besigye, mgombea urais mara nne, anatarajiwa kufika mbele ya mahakama ya kiraia leo kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi ya 2022 ambayo anatuhumiwa kufanya maandamano kinyume cha sheria.
Pia unaweza kusoma:
Trump kukabiliwa na upinzani mkali kutoka Jordan juu ya mpango wa Gaza
Donald Trump anatarajiwa kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Mfalme Abdullah wa Jordan katika Ikulu ya White House leo, kwenye mkutano wao wa kwanza tangu rais wa Marekani kupendekeza kuhamisha wakazi wa Gaza hadi Jordan.
Jordan, mshirika mkuu wa Marekani, imekuwa katika kipindi kigumu katikati ya uhusiano wake wa kijeshi na kidiplomasia, na uungaji mkono wa Wapalestina nyumbani.
Tayari ikiwa imejaribiwa na Vita vya Gaza, inasukumwa hadi ukutani na mipango ya Trump kwa amani ya Gaza.
Trump alisema kwamba watu wa Gaza wahamishiwe Jordan na Misri, akimwambia mtangazaji wa Fox News kwamba hawatakuwa na haki ya kurejea nyumbani - maono ambayo, yakitekelezwa, yatakiuka sheria za kimataifa.
Siku ya Jumatatu alisema huenda akazuia msaada kwa Jordan na Misri ikiwa hawatachukua wakimbizi wa Kipalestina.
Baadhi ya wapinzani wakubwa wa kuwahamisha Wagaza hadi Jordan ni Wagaza waliohamia nchi hiyo hapo kabla.
Takriban watu 45,000 wanaishi wakiwa wamejazana kwenye kambi ya Gaza, karibu na mji wa kaskazini mwa Jordan wa Jerash, mojawapo ya kambi kadhaa za wakimbizi wa Kipalestina huko.
Familia zote eneo hilo mizizi yake ni Gaza: hadi Jabalia, Rafah, Beit Hanoun. Wengi waliondoka baada ya vita vya Waarabu na Israeli vya 1967, wakitafuta makazi ya muda. Vizazi baadaye, bado wamesalia huko.
Soma zaidi:
Vitisho havina maana katika kusitisha mapigano - afisa wa Hamas
Msemaji mkuu wa Hamas anasema kuwa Rais Trump "lazima akumbuke kwamba kuna makubaliano ambayo lazima yaheshimiwe na pande zote mbili" ikiwa anataka mateka wa Israel warejeshwe.
Akizungumza na shirika la habari la Reuters, Sami Abu Zuhri ameongeza kuwa "lugha ya vitisho haina maana na inatatiza mambo".
Siku ya Jumatatu, Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba "mambo yatakuwa mabaya" ikiwa mateka wote waliosalia wa Israeli hawataachiliwa wikendi hii.
Kama ukumbusho, mateka 16 wa Israeli wameachiliwa hadi kufikia sasa, wakisalia 17. Kati ya hao 17, Israel inasema wanane wamekufa.
Soma zaidi:
Mwalimu amchoma kisu mtoto wa miaka minane nchini Korea Kusini
Mwalimu mmoja amemdunga kisu mtoto wa miaka minane katika shule ya msingi nchini Korea Kusini, katika tukio ambalo limeshtua taifa hilo.
Mwalimu huyo wa kike, ambaye yuko katika umri wa miaka 40, alikiri kumdunga kisu mwanafunzi huyo katika mji wa kati wa Daejeon, polisi walisema.
Msichana huyo alipatikana na majeraha ya kuchomwa kisu kwenye ghorofa ya pili ya jengo la shule saa 18:00 kwa saa za huko (09:00 GMT) Jumatatu na kutangazwa kuwa amefariki hospitalini.
Mwalimu alikuwa kando yake akiwa na majeraha ya kuchomwa kisu ambayo polisi walisema huenda alijijeruhi mwenyewe.
Kaimu rais wa Korea Kusini Choi Sang-mok siku ya Jumanne aliamuru uchunguzi kuhusu kesi hiyo na kuzitaka mamlaka "kutekeleza hatua zinazohitajika ili kuhakikisha matukio kama haya hayatokei tena".
Trump atangaza ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zote za chuma na alumini zinazoingizwa
Rais Donald Trump ameamuru kutozwa ushuru wa 25% kwa chuma na alumini zote zinazoingia Marekani katika upanuzi mkubwa wa vikwazo vya biashara vilivyopo.
Ushuru huo, ambao utaongeza gharama za kuagiza bidhaa hizo nchini Marekani, unakuja licha ya onyo la kulipiza kisasi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini Canada - msambazaji mkubwa zaidi wa bidhaa hizo nchini Marekani - pamoja na nchi zingine.
Biashara za Marekani zinazotegemea uagizaji bidhaa hizo pia zimeibua wasiwasi, lakini Trump amesema mipango yake itaongeza uzalishaji wa ndani.
Alionya kuwa hakutakuwa na ubaguzi, akisema "anarahisisha" sheria, ambazo zimepangwa kuanza kutumika tarehe 4 Machi.
"Hili ni jambo kubwa, mwanzo wa kuifanya Marekani kuwa tajiri tena," Trump alisema.
"Taifa letu linahitaji chuma na alumini kutengenezwa Marekani, sio katika nchi za kigeni," aliongeza.
Alipoulizwa kama ushuru unaweza kuongeza bei kwa watumiaji, rais wa Marekani alijibu: "Hatimaye itakuwa nafuu."
"Ni wakati wa viwanda vyetu vikubwa kurejea Marekani...hii ni ya kwanza kati ya nyingi," aliongeza, akipendekeza ushuru mwingine unaweza kuwekwa kwa dawa na chipu za kompyuta.
Marekani ndiyo nchi inayoongoza duniani kuagiza chuma, huku Canada, Brazili na Mexico zikiwa wasambazaji wake wakubwa.
Soma zaidi:
Muungano unaoongozwa na Musk watoa ofa ya $ 97.4bn kwa mtengenezaji wa Chatgpt
Muungano wa wawekezaji unaoongozwa na Elon Musk ulitoa ofa ya $97.4bn kununua OpenAI, watengenezaji wa ChatGPT.
Wakili wa bilionea huyo, Marc Toberoff, alithibitisha kuwa aliwasilisha ofa ya "mali zote" za kampuni ya Musk kwa bodi yake Jumatatu.
Ofa hiyo ni mabadiliko ya hivi punde katika vita vya muda mrefu kati ya Musk, mtu tajiri zaidi duniani ambaye pia yuko karibu sana na Rais wa Marekani Donald Trump, na mkurugenzi mtendaji wa Open AI Sam Altman juu ya mustakabali wa teknolojia hii mpya ya AI inayovuma.
Akijibu ofa hiyo, Altman aliweka ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Musk wa X : akisema "hapana, asante lakini tutanunua twitter kwa $9.74 bilioni ukipenda."
OpenAI inasifiwa sana kwa kusaidia katika utengenezaji wa zana za kijasusi kwa kutumia akili mnemba na kuibua uwekezaji mkubwa katika sekta hiyo.
Musk na Altman walianzisha kampuni hiyo mnamo 2015 kama kampuni isiyo ya faida, lakini uhusiano wao umezorota tangu mkuu wa Tesla na X alipojiondoa kwenye kampuni hiyo mnamo mwaka 2018.
Soma zaidi:
Zaidi ya watu 50 wafariki dunia baada ya basi kuanguka kutoka kwenye daraja Guatemala
Takriban watu 54 wamefariki dunia baada ya basi kuanguka kutoka kwenye daraja nje kidogo ya Jiji la Guatemala, wazima moto walisema.
Basi hilo, lililokuwa likielekea mji mkuu kutoka idara ya El Progresolilikuwa na abiria 75, na lilianguka chini ya bonde lenye urefu wa mita kadhaa na kutumbukia kwenye mfereji wa maji taka, kulingana na idara ya zima moto ya eneo hilo.
Miongoni mwa waliofariki ni watoto wadogo.
Miili ya wengi kati ya 54 waliofariki, akiwemo dereva wa basi, iko katika chumba cha kuhifadhi maiti cha muda karibu na eneo la ajali, wazima moto walisema.
Huduma za dharura zilisema takriban watu wengine 15 waliokolewa wakiwa na majeraha mabaya, ingawa idadi kamili ya walionusurika haijulikani.
Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha ukubwa wa ajali hiyo, huku basi hilo likipinduka na waokoaji wakiondoa miili ya marehemu na walionusurika.
Taratibu za kutambua miili hiyo zimeanza na mamlaka imeanza kuandaa orodha za majina ya marehemu.
Pia unaweza kusoma:
Hamas inasema itaahirisha makubaliano ya kuwaachilia mateka na kulaumu Israel
Msemaji wa kundi la Hamas amesema kundi hilo linaahirisha kuachiliwa tena kwa mateka wa Israeli, likilaumu kile anachosema ni ukiukaji wa Israel wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Mateka watatu wanaoshikiliwa huko Gaza wanatarajiwa kuachiliwa siku ya Jumamosi kwa mabadilishano ya wafungwa zaidi wa Kipalestina wanaoshikiliwa nchini Israel.
Waziri wa Ulinzi wa Israeli Israel Katz aliita tangazo la Hamas "ukiukaji kamili wa makubaliano ya kusitisha mapigano".
Mshirika mkuu wa Israel Rais wa Marekani Donald Trump amependekeza usitishaji vita unapaswa kufutwa ikiwa "mateka" wote wanaoshikiliwa Gaza hawatarudishwa ifikapo Jumamosi.
"Nimesema warudishwe ifikapo saa sita Jumamosi... wote, si wawili, mmoja watatu na wanne na wawili," alisema.
“Najisemea mwenyewe,” alisisitiza. "Israel inaweza kuibatilisha."
Mateka 73 waliochukuliwa wakati wa shambulio la Hamas dhidi ya Israeli tarehe 7 Oktoba 2023, na wengine watatu waliochukuliwa muongo mmoja kabla, bado wanazuiliwa huko Gaza.
Ikiwa mateka hawataachiliwa, Trump aliongeza, "Mabaya yatatokea."
Alipoulizwa kama alimaanisha kulipiza kisasi kutoka kwa Israeli, alisema: "Utajua, na watajua pia. Hamas watajua ninachomaanisha."
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja