Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Sudan: Uhasama wa uongozi wa kijeshi kiini cha mapigano huko Khartoum
By Beverly Ochieng, BBC Monitoring, Nairobi
Mapigano ambayo yamezuka katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum na kwingineko nchini humo ni matokeo ya moja kwa moja ya mvutano mkali wa madaraka ndani ya uongozi wa kijeshi wa nchi hiyo.
Kuna mapigano katika maeneo muhimu ya kimkakati katika mji mkuu huku wanachama wa kikosi cha kijeshi - Vikosi vya Msaada wa dharula (RSF) - na wanajeshi wa kawaida wakipigana.
Hapa ndio unahitaji kujua zaidi.
Nini historia ya mapigano?
Tangu mapinduzi ya Oktoba 2021, Sudan imekuwa ikiendeshwa na baraza la majenerali na kuna wanajeshi wawili katikati ya mzozo huo.
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye ni mkuu wa majeshi na kwa hakika ni rais wa nchi hiyo.
Na naibu wake na kiongozi wa RSF, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti.
Wametofautiana katika mwelekeo ambao nchi inaenda na hatua inayopendekezwa kuelekea utawala wa kiraia.
Mojawapo ya hoja kuu muhimu ni juu ya mipango ya kujumuisha askari 100,000 wa RSF katika jeshi na ambao wangeongoza kikosi kipya.
Kwa nini yote yalianza Jumamosi?
Ghasia hizo zinafuatia siku za mvutano huku wapiganaji wa RSF wakisambazwa tena nchini kote katika hatua ambayo jeshi liliona kama tishio.
Kumekuwa na matumaini kwamba mazungumzo yanaweza kutatua hali hiyo lakini hayajawahi kutokea.
Haijabainika ni nani alifyatua risasi ya kwanza Jumamosi asubuhi lakini kuna hofu kwamba hali hii itazidi kuwa mbaya.
Wanadiplomasia wamezitaka pande hizo mbili kusitisha mapigano.
Unakifahamu kikosi cha Msaada wa dharula (RSF)?
RSF iliundwa mwaka wa 2013 na ina asili yake katika wanamgambo mashuhuri wa Janjaweed ambao walipambana kikatili na waasi huko Darfur.
Tangu wakati huo, Jenerali Dagalo ameunda kikosi chenye nguvu ambacho kimeingilia kati migogoro nchini Yemen na Libya na kudhibiti baadhi ya migodi ya dhahabu ya Sudan.
Pia kimeshutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya zaidi ya waandamanaji 120 mnamo Juni 2019.
Kikosi hicho chenye nguvu nje ya jeshi kimeonekana kuwa chanzo cha kukosekana kwa utulivu nchini humo.
Kwa nini jeshi limeshika hatamu?
Mapigano haya ni kipindi cha hivi karibuni zaidi katika mivutano iliyofuatia baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais wa muda mrefu Omar al-Bashir mnamo 2019.
Kulikuwa na maandamano makubwa ya mitaani yakitaka kukomeshwa kwa utawala wake wa takriban miongo mitatu na jeshi lilipanga mapinduzi ili kumuondoa.
Lakini raia waliendelea kudai nafasi katika mpango wa kuelekea utawala wa kidemokrasia.
Serikali ya pamoja ya kijeshi na ya kiraia ilianzishwa wakati huo lakini ilipinduliwa katika mapinduzi mengine mnamo Oktoba 2021.
Na tangu wakati huo ushindani kati ya Jenerali Burhan na Jenerali Dagalo umeongezeka.
Mpango mkakati wa kurejesha mamlaka mikononi mwa raia ulikubaliwa Desemba mwaka jana lakini mazungumzo ya kukamilisha makubaliano hayo yameshindikana.
Nini kinaweza kutokea sasa?
Ikiwa mapigano yataendelea basi yanaweza kusambaratisha zaidi nchi hiyo na kuzidisha machafuko ya kisiasa.
Wanadiplomasia, ambao wamekuwa na jukumu muhimu katika kujaribu kuhimiza kurejeshwa kwa utawala wa kiraia, watakuwa na shauku kubwa ya kutafuta njia ya kuwapata majenerali hao wawili na kuanzisha mazungumzo.
Wakati huo huo, watakuwa Wasudan wa kawaida ambao watalazimika kuishi katika kipindi kingine tena cha kutokuwa na uhakika wa maisha yao.