Jinsi kiongozi wa upinzani Uganda alivyotoweka nchini Kenya na kuishia katika mahakama ya kijeshi

    • Author, Wycliffe Muia
    • Nafasi, BBC News, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Tukio la kutekwa kwa kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye alipokuwa ziarani nchini Kenya karibu wiki mbili zilizopita limezua shutuma nyingi na hofu ya mabadilishano ya siri ya taarifa za kijasusi kati ya mataifa hayo mawili jirani.

Washirika wa Besigye na mkewe wamefichua jinsi kinara huyo wa upinzani alivyoshawishiwa kukutana na watekaji nyara wake, wanaosemekana kujifanya maajenti wa usalama wa Kenya.

Ripoti zinasema alifuatiliwa tangu alipopanda ndege katika uwanja wa ndege wa Entebbe nchini Uganda kuelekea mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ambako alitekwa nyara, kurudishwa nyumbani(Uganda) bila kufuata utaratibu wa kisheria na hatimaye kufikishwa katika mahakama ya kijeshi.

Wakati Kenya ikisisitiza kuwa haikuhusika kwa vyovyote na kutekwa kwa Besigye na inachunguza tukio hilo, Uganda inashikilia kuwa Kenya ilikuwa na ufahamu kamili wa mpango huo, ikitoa mfano wa mawasiliano ya kijasusi yaliyolenga kumsaka Besigye.

Kwa leo anatarajiwa kufikishwa tena katika mahakama ya kijeshi mjini Kampala, tunaangazia tunachojua kufikia sasa.

Kizza Besigye ni nani?

Besigye amegombea na kushindwa katika chaguzi nne za urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu 1986.

Hajashiriki siasa hivi majuzi, na hakugombea uchaguzi wa 2021.

Lakini mapema mwaka huu, alianzisha chama kipya, People’s Front for Freedom (PFF) baada ya kujitenga na Forum for Democratic Change (FDC), alichokianzisha miongo miwili iliyopita.

Mwanasiasa huyo wa upinzani kwa miaka mingi amezuru Kenya na kufanya shughuli zake kwa uhuru, wakati mwingine kuhudhuria matukio ya hadhi ya juu - hata wakati alipokuwa mpinzani na mkosoaji mkuu wa Museveni.

Besigye alitoweka katika mazingira gani?

Besigye alikuwa amezuru Nairobi kuhudhuria uzinduzi wa kitabu cha mwanasiasa wa upinzani nchini Kenya Martha Karua.

Mwanasiasa huyi wa Uganda mwenye umri wa miaka 68 alitua jijini Nairobi asubuhi ya tarehe 16 Novemba na kuchukua teksi hadi katika hoteli moja mtaani Hurlingham. Aliandamana na mshirika wake wa muda mrefu Hajj Obeid Lutale.

Saa chache baadaye, aliondoka hotelini, akapanda teksi na kuelekea Riverside Drive, kilomita 5 (maili tatu) kutoka hoteli yake, kwa mkutano wa faragha, kulingana na washirika wake wa kisiasa.

Hii ilikuwa mara ya mwisho kuonekana hadi alipoibuka tena Uganda siku nne baadaye.

Dereva wake wa teksi alisema alimsubiri mwanasiasa huyo mkongwe kwa zaidi ya saa 12, kabla ya kuamua kuondoka aliposhindwa kuwasiliana naye kwa njia ya simu.

Timu ya Besigye nchini Uganda ilianza kutoa taarifa za kuhofia hali yake baada ya simu za kiongozi wao kutopokelewa.

Kutoweka kwake kuligonga vichwa vya habari na kuibua taharuki katika eneo hilo, huku mkewe Winnie Byanyima, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na VVU na Ukimwi, akitumia mitandao ya kijamii kuripoti kuwa mumewe "alitekwa nyara" jijini Nairobi.

Siku iliyofuata, kiti chake alichokuwa ametengewa wakati wa uzinduzi wa kitabu, ambapo alitarajiwa kuwa mmoja wa mzungumzaji, kilibaki tupu huku waandaaji wa hafla hiyo wakipaza sauti kuhusu kutofika kwake.

Besigye alitoweka vipi?

Besigye na rafiki yake Lutale walifika katika ghorofa hiyo kando ya Riverside Drive ambapo alitakiwa kukutana na raia wa Uganda ambaye hakutambulika na raia mwingine wa Uingereza ambaye hakujulikana, kulingana na Bi Byanyima.

Raia huyo wa Uingereza alidaiwa kutaka kumtambulisha Besigye kwa kundi la wafanyakazi wenzake na wafanyabiashara, ambao walikuwa wameonyesha nia ya kusaidia kifedha PFF, alisema.

Ndani ya chumba hicho kulikuwa na boksi ambalo lilionekana kuwa na pesa nyingi. Mmoja wa majeshi alikuwa na bunduki mbili.

Muda mfupi baada ya utambulisho mfupi, wanaume wanane waliovalia nguo za kawaida waliosema kuwa walikuwa maafisa wa polisi wa Kenya walibisha mlango na kumwambia Besigye na mshirika wake kwamba walikuwa wamekamatwa, Bi Byanyima aliambia runinga ya Citizen ya Kenya.

Mkuu huyo wa upinzani alijaribu kueleza kuwa hakuwa na uhusiano wowote na vitu vilivyokuwa ndani ya chumba hicho, lakini maafisa wa usalama hawakusikiliza.

Wanaume wanne kati ya hao waliwaingiza Besigye na Lutale kwenye gari lenye nambari za usajiliza Kenya na kuwasafirisha nyakati za usiku kuelekea mpaka wa Uganda.

"Ni wazi ilikuwa operesheni iliyopangwa vyema," Bi Byanyima aliongeza.

Kabla ya kumsafirisha hadi Uganda, wanaume hao wanne waliacha kuzungumza Kiswahili na kuanza kuzungumza lugha za Uganda, Kiganda na Runyankole.

Wawili hao waliokuwa mateka walisafirishwa hadi Uganda bila mali zao, zikiwemo pasi zao za kusafiria, ambazo baadaye zilichukuliwa na maafisa wa chama cha Besigye kutoka hoteli ya Nairobi.

Msemaji wa PFF Ibrahim Ssemujju Nganda aliambia gazeti la The Monitor la Uganda kwamba Besigye na rafiki yake walipitia kituo cha mpakani cha Malaba bila kusimama kwa ukaguzi wa kawaida wa usalama.

"Walibadilisha magari tu. Gari lililokuwa na nambari ya usajili ya Kenya liliachwa kwenye kituo cha mpakani cha Malaba na kuhamia kwenye gari lingine lenye nambari [a] za usajili za Uganda," alisema.

Kwa nini Besigye alichukuliwa Nairobi na je iliwekewa mtego?

Waziri wa Habari wa Uganda Chris Baryomunsi alisema wapelelezi walikuwa wamekusanya taarifa za kutosha kumkamata Besigye akiwa Nairobi.

Alisema mamlaka ya Kenya imewezesha operesheni hiyo, ingawa maafisa wa Nairobi wanasisitiza kuwa hawajui lolote kuihusu.

Besigye sasa anahukumiwa mjini Kampala na wala sio Nairobi kwa sababu uhalifu uliopangwa ulikuwa "dhidi ya Uganda na sio Kenya", msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Jenerali Felix Kulayigye aliambia podcast ya BBC Africa Daily.

"Tuna mfumo wa kisheria na wenzetu nchini Kenya kushughulikia masuala ambayo yanatishia usalama wa kikanda," aliongeza.

Hata hivyo, hakueleza kwa nini hakukuwa na mchakato wa kuwarejesha.

Ripoti zinaonyesha kuwa kukamatwa kwa Besigye kulipangwa kwa miezi kadhaa na kutekelezwa kwa msaada wa baadhi ya watu waliokuwa karibu naye.

Waandalizi wa mkutano huo wanasemekana kuwa raia wa Uingereza na afisa mkuu wa jeshi la Uganda, ambao wote walikuwa wanajulikana sana na Besigye, vyombo vya habari vya Uganda viliripoti.

Mkewe alidai raia huyo wa Uingereza ambaye alikuwa kwenye mkutano huo alikuwa "mhudumu wa kulipwa ambaye alijaribu kutega bunduki" kwa Besigye.

Kwa nini Besigye anashtakiwa katika mahakama ya kijeshi?

Kwa miongo kadhaa, mamia ya raia wamehukumiwa katika mahakama za kijeshi za Uganda, ingawa Mahakama ya Kikatiba imetoa uamuzi dhidi ya hilo.

Besigye, ambaye si mgeni katika mahakama za kijeshi, amerejea huko kwa sababu ajifikisha mbele ya mahakama za kijeshi, Brig Kulayigye aliambia BBC.

Wiki iliyopita, yeye na washtakiwa wenzake walifikishwa katika mahakama ya kijeshi ya Makindye baada ya kuzuiliwa kwa muda wa siku nne.

Wanakabiliwa na mashtaka manne ambayo ni pamoja na kupatikana na bastola mbili na risasi, na kutaka kununua silaha kutoka kwa wageni katika jiji la Uswizi la Geneva, mji mkuu wa Ugiriki, Athens, na Nairobi.

Wawili hao walikana mashtaka yote.

Besigye alipinga kuhukumiwa na mahakama ya kijeshi, akisema kuwa ikiwa kuna mashtaka dhidi yake, anapaswa kuhukumiwa katika mahakama ya kiraia.

Mawakili wake pia walidai kuwa makosa yanayodaiwa yalifanywa nje ya Uganda na kwa hivyo walifikishwa katika mahakama ya kijeshi kinyume cha sheria.

Lakini mahakama ilitupilia mbali ombi la mawakili hao na kuruhusu kesi hiyo kuendelea.

Washtakiwa wameshikiliwa katika gereza kuu la Luzira hadi tarehe 2 Desemba.

Agather Atuhaire, wakili wa Uganda na mwanaharakati wa haki za binadamu, aliambia BBC kwamba Kenya ilipaswa kumkamata Besigye na kumrejesha Uganda kufuatia sheria zinazoongoza mchakato huo.

Bi Byanyima alisema hakutarajia mumewe kupata haki.

Lakini Brigedia Kulayigye alisema mahakama ya kijeshi "siyo mahakama ya kangaroo".

"Haki itapatikana."

Je, suala hilo limeathiri uhusiano kati ya Kenya na Uganda?

Mamlaka ya Kenya imekuwa katika hali ya ati ati kukana ufahamu wowote kuhusu operesheni hiyo na kukaa kimya, huku maafisa wa Uganda wakisema kuwa kuna taarifa nyingi za kijasusi kati ya nchi hizo mbili.

“Serikali ya Uganda ilikuwa inawasiliana na serikali ya Kenya, vinginevyo ungemkamata vipi mtu katikati ya jiji la Nairobi kisha umrudishe Uganda iwe kwa njia ya uwanja wa ndege au ardhini bila ya kuungwa mkono na serikali huko Kenya?" Waziri wa Habari Baryomunsi aliiambia NBS TV ya Uganda.

Wakenya wengi wanauliza kuhusu asili ya uhusiano wa kiusalama kati ya nchi hizo mbili na ikiwa kungekuwa na ufichuzi kamili kwamba Besigye angefunguliwa mashtaka katika mahakama ya kijeshi.

Jumanne iliyopita, Kaimu Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Kenya Musalia Mudavadi alijizuia kutoa majibu ya wazi kwa wanahabari, akiomba kwamba nchi yake isihukumiwe “vikali sana”.

Mudavadi, ambaye pia ni kaimu waziri wa mambo ya ndani, alisema Kenya ni nchi iliyo wazi, ambayo inairuhusu "mambo mengi". Lakini akaonya wageni dhidi ya kusababisha mpasuko kati ya Kenya na nchi zao.

Alisema suala la Besigye litatatuliwa kidiplomasia, akielezea Uganda kama "mshirika muhimu wa Kenya".

Kukiri kwa Uganda kwamba Kenya ilihusika katika utekaji nyara huo kumeifanya serikali ya Kenya kukabiliwa na mzozo nchini Uganda na nyumbani.

Baadhi ya raia wa Uganda wamefanya maandamano nje ya ubalozi wa Kenya mjini Kampala huku wengine wakitishia kususia bidhaa za Kenya.

Kushikiliwa kwa Besigye kunafuatia msururu wa matukio ya utekaji nyara na kutoweka nchini Kenya, ikiwa ni pamoja na kuwatimua kwa lazima wakimbizi wanne wa Kituruki hadi Ankara, ambako walikabiliwa na tuhuma za kula njama dhidi ya Rais Recep Tayyip Erdogan.

Taarifa ya ziada ya Alan Kasujja

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi