Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nchi nyingine zitajibu nini juu ya ushuru wa Trump?
Halikuwa jambo la uongo, Marekani sasa imepandisha ushuru kwa mataifa kadhaa - na huu ndio mwanzo tu.
Mfumo wa biashara ya dunia haujawahi kuwa katika hali hii hapo awali. Huu ni mteremko kuelekea mzozo mpana wa kibiashara.
Lakini cha muhimu zaidi juu ya hatua ambazo Marekani inazichukua, ni jinsi nchi nyingine zitakavyo jibu.
Trump anataka nini?
Trump ana historia ya kupandisha ushuru mara kwa mara - ili kulazimisha mabadiliko ya kidiplomasia, kushughulikia ukosefu wa usawa wa kibiashara au kuongeza mapato makubwa.
Malengo haya kupitia ushuru hayawezi kufikiwa yote kwa wakati mmoja.
Kwa mfano, wakati wa muhula wa kwanza wa vita vyake "dhidi ya China," wanadiplomasia wa nchi za Magharibi walikuwa wakihangaika kutafuta bidhaa za Marekani ambazo wanaweza kununua zaidi, ili kuipa White House ushindi.
Ulaya inaweza kusema kuwa imeongeza ununuzi wake wa bidhaa za Marekani za gesi asilia, au silaha, au sumaku maalumu kwa ajili ya umeme wa upepo.
Lakini mtindo huo uliofanyika, ilimradi tu rais wa Marekani aweze kuwa mshindi katika vita vyake vya kibiashara.
Je, kubadilisha ushuru katika biashara ndio lengo?
Hatua ya Trump, ni kutoa adhabu kwa sababu ya biashara ya dawa ya kulevya ya fentanyl – inayoingizwa Marekani kimagendo kupitia Canada na Mexico, lakini sababu hiyo inaonekana ni kama kisingizio tu ili kuchukua hatua ya "dharura" ambayo kwa kawaida ingehitaji uamuzi wa bunge.
Canada imesema itachukua hatua thabiti dhidi ya Trump, hatua hiyo imefafanuliwa vyema na mgombeaji wa nafasi ya waziri mkuu wa nchi hiyo, Mark Carney.
"Tutalipiza kisasi ... dola kwa dola," ameiambia BBC, akikejeli sababu ya Trump juu ya dawa za kulevya za fentanyl na kusema Canada "itajibu."
Ametoa onyo la kificho kwa taifa lolote linalotaka kukaa kimya na kumtazama tu rais huyo wa Marekani: "Kila la kheri."
Ikiwa Carney atamrithi Justin Trudeau, ataishia kukutana na Trump katika G7, kundi la mataifa saba yenye uchumi mkubwa zaidi duniani.
Akiwa gavana wa zamani wa Benki ya England, Carney alikutana na Trump kwenye mikutano ya G20 na G7. Moja kwa moja alihitimisha kuwa kiongozi huyo wa Marekani anaheshimu tu nguvu.
Katika mazungumzo yangu ya hivi karibuni na wapatanishi wa biashara kutoka Ulaya, wamesisitiza kuwa wanataka ushirikiano, pamoja na mikataba na Marekani. Lakini walikwepa kumkosoa Trump moja kwa moja na hata kwa pendekezo lake la ajabu la kutumia ushuru dhidi ya mshirika wa Nato Denmark juu ya hatima ya Greenland.
Swali Muhimu
Swali muhimu hapa ni ikiwa ulimwengu wote, hata zile nchi zilizo kimya, zitaratibu ushuru wa kulipiza kisasi, kwa biashara za watu wa karibu wa Rais Trump, kama vile Elon Musk.
Kampuni ya Musk ya Tesla, ambayo inatengeneza magari ya umeme, ilionya wiki iliyopita juu ya athari za ushuru wa nipe nikupe.
Onyo hilo linalenga kuzifanya kambi pinzani zinazo izunguka Ikulu na Bunge la Congress, kueleza wasiwasi wao kuhusu athari kwa mauzo ya nje ya bidhaa kutoka katika viwanda vya Marekani, na athari kwa bei za ndani za Marekani.
Lakini matokeo hasa ya hatua hizi za Trump yatategemea mitizamo ya ndani ya Marekani.
Mataifa mengine yanaweza kuhitimisha kwamba siku hizi, kuna chaguzi nyingine ulimwenguni za kuchagua jinsi ya kufanya biashara.
Wakati vitisho vya ushuru vikizidi kuongezeka katika kila upande kwa kadiri siku zinavyosonga, dunia inabaki kuwa ni eneo lenye mashaka.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Mariam Mjahid