Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini hatua ya usitishaji vita Gaza inasuasua?
- Author, Paul Adams
- Nafasi, BBC diplomatic correspondent
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Hamas imetangaza kuchelewesha kutoa kundi lijalo la mateka, siku chache kabla ya kuliachia kundi hilo, huku ikitoa taarifa rasmi kwenye Telegram, ikisema kuwa tangazo lao ni "onyo" kwa Israel na kusema wanatoa "muda wa kutosha kwa wasuluhishi kuishinikiza Israeli kutimiza wajibu wake."
Hamas inasema "mlango uko wazi" kwa kutolewa kwa mateka kama ilivyopangwa siku ya Jumamosi.
Inaonekana kuwa Hamas inatoa muda ili kutatuliwa kwa mkwamo huu.
Lakini ni nini hasa kukwama huku?
Hamas imeorodhesha malalamiko kadhaa, kuchelewesha kurudi kwa watu waliokimbia, kuendelea kufyatua risasi dhidi yao na kushindwa kuruhusu kuingia kwa aina fulani za misaada ya kibinadamu.
Viongozi wengine wa Kipalestina wasioungana na Hamas wameelezea kukataa kwa Israel kutoa ruhusa kwa karvani kuingia Gaza ili kutoa makazi ya muda kwa Wapalestina wengi ambao nyumba zao zimeharibiwa.
Wakati ambapo serikali ya Israeli inajadili hadharani njia za kuwahamasisha raia kuondoka Gaza, kushindwa kutoa vibali kwa makazi ya muda kutachochea hofu za Wapalestina za kutolewa kwa nguvu.
Hofu ambayo kwa Donald Trump inazidi kuwa kubwa, karibu kila siku.
Kilichoanza kama pendekezo tu kwamba Wapalestina wengi wanapaswa kuondoka wakati Gaza inajengwa tena, kimegeuka kuwa ombi la rais kwamba wote wanapaswa kuondoka na Marekani ichukue usimamizi wa Gaza.
Kadhalika Trump anapoongeza msimamo wake, Hamas inaweza kuwa inajiuliza kama inafaa kuendelea na mazungumzo ya hatua ya pili ya mapatano ya kusitisha mapigano. Ni kwa ajili ya nini hasa mazungumzo haya?
Iwapo Trump ni mkweli, Wapalestina wanajua kwamba itakuwa juu ya Israel kuhakikisha Gaza inakuwa bila raia. Kuwanyima makazi hakutoshi. Hii itahitaji karibu kabisa kutumia nguvu.
Sasa Trump amesema kuwa ikiwa mateka wote walioshikiliwa Gaza hawatarudishwa ifikapo Jumamosi, atapendekeza kufuta mapatano ya kusitisha mapigano na "kila kitu kitavunjika."
Lakini alisema anazungumza kwa niaba yake mwenyewe na "Israel inaweza kupuuza hili."
Ikiwa vita vitarejelewa, Hamas inaweza kuwa inajiuliza kuna faida gani ya kuachilia mateka waliobaki.
Kwa jamaa na marafiki wa mateka, mkwamo huu wa sasa, na kuingilia kwa Trump, ni sababu ya wasiwasi mpya.
"Kila tamko au matangazo, bila shaka, yanafanya Hamas kuwa wagumu zaidi," Dudi Zalmanovich aliiambia BBC. Mpwa wa mkewe, Omer Shem Tov, bado anashikiliwa na Hamas.
"Ningependa aache kuwa na msimamo mkali," Bwana Zalmanovich alisema kuhusu Trump.
Israel ina mashaka yake kuhusu mantiki ya vitisho vya Hamas vya kuchelewesha hatia hiyo.
Kuonekana kwa mateka waliokonda mwishoni mwa juma kumeongeza hofu kwamba Hamas inaweza kutaka dunia isione wengine walioko katika hali mbaya zaidi.
Juu ya vita inayohusisha wapiganaji wa Hamas wakiwa wamejihami vizuri wakitembea mchana, na tahadhari kutoka kwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, kwamba kundi hili limeajiri wanajeshi wengi kama ilivyopoteza wakati wa vita, si Waisraeli wote wanaamini kwamba mapatano ya kusitisha mapigano yanaweza au hata yanapaswa kudumu.
Bado ni mapema kusema ikiwa mchakato huu uliojadiliwa kwa makini, na kupangwa hatua kwa hatua, uko karibu kuanguka, kama wengi wanavyotabiri, lakini baada ya kuanza vizuri, unakutana na shinikizo kubwa zaidi.