Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Urusi yashambulia mfumo wa usafirishaji gesi wa Ukraine

Wizara ya Nishati ya Ukraine iliripoti kwamba Urusi ilipiga moja ya vifaa vya mfumo wa usafirishaji wa gesi wa Ukraine wakati wa shambulio la usiku.

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Urusi yashambulia mfumo wa usafirishaji gesi wa Ukraine

    Wizara ya Nishati ya Ukraine iliripoti kwamba Urusi ilipiga moja ya vifaa vya mfumo wa usafirishaji wa gesi wa Ukraine wakati wa shambulio la usiku.

    Kiwango cha uharibifu kinatathminiwa.

    Wakati huo huo, Reuters inaripoti, ikitaja vyanzo viwili vya habari, kwamba shambulizi la Urusi lililenga kituo cha gesi ambacho kina jukumu muhimu katika kusukuma gesi kwenye vituo vya kuhifadhi.

    Tangu uvamizi wa Urusi, imekuwa ikilenga miundombinu ya nishati ya Ukraine, na kusababisha nchi hiyo kukumbwa na matatizo makubwa mara kwa mara na usambazaji wa umeme.

  2. Bolsonaro alipanga kukimbilia Argentina, polisi wa Brazil wasema

    Polisi nchini Brazil wamemshutumu Rais wa zamani Jair Bolsonaro, 70, na mtoto wake wa kiume Eduardo mwenye umri wa miaka 41 kwa kuzuia sheria.

    Wanadai kuwa wawili hao walijaribu kuingilia kati kesi inayoendelea kwa sasa dhidi ya Bolsonaro, ambapo anatuhumiwa kuongoza jaribio la mapinduzi baada ya kushindwa katika uchaguzi wa urais wa 2022.

    Polisi wanasema wamepata hati kwenye simu ya mkononi ya Jair Bolsonaro ambayo inaeleza kwamba alipanga kukwepa kesi ya uhalifu kwa kutafuta hifadhi nchini Argentina.

    Pia wanamtuhumu Eduardo Bolsonaro kwa kushawishi utawala wa Trump kwa niaba ya baba yake, jambo ambalo wanasema lilisababisha Marekani kuweka ushuru wa adhabu kwa bidhaa za Brazil.

  3. Nyota wa muziki wa Ghana Shatta Wale azuiliwa kwa manunuzi ya Lamborghini

    Mwanamuziki maarufu wa Ghana Shatta Wale amezuiliwa katika uchunguzi wa ushuru unaohusishwa na ununuzi wake wa gari la kifahari, uongozi wake umesema.

    Lamborghini ya njano ya Wale ilikamatwa mapema mwezi huu kwa ombi la Marekani, ambayo ilidai kuwa gari hilo lilikuwa limezuiwa kutokana mapato ya biashara ya uhalifu.

    Mtandao huo unadaiwa kumhusisha Mghana mwingine, Nana Kwabena Amuah, ambaye anatumikia kifungo cha miaka saba jela nchini Marekani kwa makosa ya ulaghai.

    Uongozi wa Wale haukutaja madai ya Marekani katika taarifa yao, ukisema badala yake msanii huyo alizuiliwa kwa sababu ya "masuala ya kodi".

    Katika taarifa iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii, timu ya Wale ilisema "alijisalimisha kwa hiari" kwenye Ofisi ya Uhalifu wa Kiuchumi ya Ghana (Eoco) Jumatano alasiri.

    Eoco bado haijajibu ombi la BBC la kutoa maoni. Wale, jina halisi Charles Nii Armah, ni mmoja wa wasanii mashuhuri wa Ghana.

    Amejenga taaluma yenye mafanikio makubwa kwenye dancehall ya Jamaica, na akakuza utambulisho wake kimataifa kwa kushirikiana na Beyoncé kwenye wimbo wake wa 2019.

    Baada ya gari lake aina ya Lamborghini kukamatwa mapema mwezi huu katika uchunguzi unaohusishwa na Nana Kwabena Amuah, Wale alikanusha kuwa hajui au ana uhusiano na Mghana huyo.

    Alisema alikuwa "mmiliki wa tatu" wa gari hilo la $150,000 (£110,000) na kwamba hajui ni nani aliyelisafirisha nchini humo.

    Eoco alisema gari hilo litarejeshwa Marekani kusaidia kurejesha wamiliki.

    Amuah na washirika wake walijifanya wachuuzi kulaghai takriban mashirika 70 ya umma na ya binafsi kote nchini, rekodi za mahakama ya Marekani zinaonesha.

    Siku ya Jumatano, usimamizi wa Wale waliwataka mashabiki kuwa watulivu na kuepuka uvumi huku mwanamuziki huyo akisalia kizuizini.

  4. Kasisi wa zamani apatikana na hatia ya mashambulizi 17 ya aibu

    Kasisi wa zamani anayeshtakiwa kwa kuwadhulumu waumini wa kikundi cha kanisa alichoongoza amepatikana na hatia ya makosa 17 ya unyanyasaji wa aibu dhidi ya wanawake tisa.

    Chris Brain, mwenye umri wa miaka 68, alikuwa mkuu wa Huduma ya (NOS), vuguvugu la kiinjilisti lenye ushawishi lililo na makao yake huko Sheffield katika miaka ya 1980 na 90.

    Hakupatikana na hatia ya mashtaka mengine 15 ya unyanyasaji wa aibu, huku majaji wakiendelea kujadili mashtaka mengine manne ya udhalilishaji na shtaka moja la ubakaji.

    Akiwa amevalia suti nyeusi na shati jeusi, Brain hakuonesha hisia zozote wakati jaji akitoa maamuzi.

    Baraza la majaji walitarajiwa kurejea mahakamani siku ya Alhamisi kuendelea na mashauri yao kuhusu mashtaka yaliyosalia.

    Wakati wa kesi hiyo, mwendesha mashtaka Tim Clark KC alisema baadhi ya wanawake hao walidhulumiwa kingono baada ya kuandikishwa kwenye kikundi kinachojulikana kama "timu ya nyumbani" iliyoshtakiwa kwa kumtunza Brain na familia yake.

    Aliiambia mahakama kuwa kundi hilo lilijulikana miongoni mwa wanachama wa NOS kama "watawa wa Lycra" baada ya mashahidi kuripoti kumuona mshtakiwa akiwa amezungukwa na wanawake wa kuvutia waliovalia nguo za ndani nyumbani kwake.

    Mahakama iliambiwa kwamba wanawake hao walitakiwa kufanya kazi za nyumbani katika nyumba aliyokuwa akiishi pamoja na mkewe na bintiye, mwendesha mashtaka alisema, pamoja na kumburudisha kwa mapenzi.

  5. Papa Leo wa XIV atasafiri kwenda Lebanon ikiwa ni safari ya kwanza ya kimataifa

    Papa Leo wa 1XIV anajiandaa kusafiri hadi Lebanon baadaye mwaka huu, ambayo inaweza kuwa safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuchaguliwa kuwa mkuu wa Kanisa Katoliki mwezi Mei.

    Askofu Mkuu Paul Sayah, naibu wa kiongozi wa ngazi ya juu kabisa wa Kanisa Katoliki nchini Lebanon, aliiambia BBC kuwa Vatican "inatathmini" safari hiyo lakini kanisa bado linasubiri tarehe rasmi.

    Ziara hiyo itaashiria wakati muhimu kwa Papa wa kwanza wa Marekani, ambaye amesisitiza mara kwa mara amani katika Mashariki ya Kati na kuwepo kwa madhehebu mbalimbali.

    "Lebanon ni nchi yenye tamaduni nyingi, yenye dini nyingi na ni mahali pa mazungumzo," Askofu Sayah alisema.

    "Ni moja ya mazingira adimu ambapo Waislamu na Wakristo wanaishi pamoja na kuheshimiana... hivyo inatuma ujumbe kwa ukanda huo."

    Kumekuwa na tetesi kuhusu ziara ya kwanza ya Papa ambayo huashiria msimamo wake.

    Safari kuu ya kwanza ya Baba Mtakatifu Francisko nje ya Roma, hadi kisiwa cha Lampedusa nchini Italia mwaka 2013, iliweka mazingira ya kuzingatia kwa suala la uhamiaji na jamii zilizotengwa.

    Katika miongo ya hivi karibuni, safari za nje zimekuwa zikizingatiwa na papa, na hivyo kuwaruhusu mapapa kuungana na Wakatoliki duniani kote, kueneza ujumbe wao na kushiriki katika diplomasia.

    Katika miaka yake 12 kama papa, Francis alitembelea nchi 68 katika safari 47 za nje, mara nyingi akichagua maeneo yenye jamii masikini, ambayo alielezea kama "sehemu muhimu " za Kanisa.

    Lebanon, maoa ya zaidi ya Wakatoliki milioni mbili na inayojulikana kwa utofauti wake wa kidini, kwa muda mrefu imekuwa na uzito wa mfano kwa Kanisa. Kufika huko kwa papa huko pia kunnaweza kumuweka Leo karibu na vita huko Gaza na mzozo mkubwa wa Israeli na Palestina.

    "Kila mtu anazungumza na Israel lakini Israel haisikii. Netanyahu haonekani kusikiliza sana, lakini kadiri [viongozi wanavyozungumza] ndivyo inavyokuwa bora," Askofu Sayah alisema.

    "Ikiwa Papa ataongeza sauti yake na wasiwasi, nadhani kuna uwezekano wa kuwa na athari fulani."

    Papa Leo tayari ametoa tahadhari kwa juhudi za kuwafikia watu na imani nyingine.

    Moja ya mikutano yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa kwake ilikuwa na wajumbe wa dini mbalimbali, ambapo alisifu "mizizi ya Kiyahudi ya Ukristo" na kuheshimu "kujitolea kwa mazungumzo na udugu" kati ya Wakatoliki na Waislamu. Amesisitiza mara kwa mara Wakristo, Wayahudi, na Waislamu "kusema hapana kwa vita na ndio kwa amani".

    Soma zaidi:

  6. Mtu mzee zaidi aliye hai duniani atimiza miaka 116

    Mtu mzee zaidi duniani anasheherekea miaka 116. Ethel Caterham, anayeishi katika nyumba ya kulea wazee huko Lightwater, Surrey, alikua mtu mzee zaidi aliyeishi kufuatia kifo cha mtawa wa Brazili Dada Inah Canbarro Lucas mwenye umri wa miaka 116.

    Alizaliwa tarehe 21 Agosti 1909, ndiye wa mwisho wa kizazi cha Edward VII. Mjukuu wa vitukuu wake Charles III alimtumia Bi Caterham kadi ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 115 mnamo 2024.

    Bibi Caterham alizaliwa miaka mitatu kabla ya maafa ya Titanic, miaka minane kabla ya Mapinduzi ya Urusi na aliishi katika vita viwili vya dunia.

    Mzaliwa wa Shipton Bellinger, Hampshire, mtoto wa pili kutoka mwisho kati ya watoto wanane, alilelewa huko Tidworth huko Wiltshire.

    Akiwa kijana alifanya kazi za ndani nchini India, na baadaye aliishi Hong Kong na Gibraltar pamoja na mume wake Norman, luteni kanali katika jeshi.

    Taarifa iliyotolewa na nyumba iliyomtunza ilisema: "Ethel na familia yake wanashukuru sana kwa ujumbe wote wa fadhili na shauku iliyooneshwa kwake wakati anasheheherekea siku yake ya kuzaliwa ya miaka 116 mwaka huu.

    "Ethel atatumia siku hiyo kimya kimya na familia yake ili aweze kufurahia kwa namna yake mwenyewe.

    Asante tena kwa salamu nzuri za heri katika siku hii maalum." Mtu mzee zaidi aliyewahi kuishi, ambaye umri wake unaweza kuthibitishwa, alikuwa Mfaransa Jean Louise Calment, aliyefariki mwaka 1997 akiwa na umri wa miaka 122 na siku 164.

  7. Jeshi la Sudan lakanusha kushambulia msafara wa misaada katika eneo lililokumbwa na njaa

    Jeshi la Sudan limekanusha madai ya kushambulia kwa mabomu msafara wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ukipeleka msaada katika eneo lililokumbwa na njaa katika jimbo la Darfur nchini humo.

    Wapiganaji wa RSF walilaumu jeshi kwa shambulio la anga la Jumatano katika mji wa Mellit, ambao uko chini ya udhibiti wa RSF.

    WFP haikutoa maelezo mengi kuhusu shambulio hilo, lakini ilisema malori matatu katika msafara huo wa magari 16 yameharibika na kushika moto.

    Wafanyakazi wote waliokuwa wakisafiri katika msafara huo walikuwa salama, iliongeza.

    Sudan ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Aprili 2023 baada ya mzozo mkali wa madaraka kuzuka kati ya jeshi na RSF, na kusababisha moja ya mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

    RSF haina kikosi cha anga, lakini pande zote mbili hutumia droni.

    Shambulio hilo ni la hivi karibuni zaidi katika msururu wa mashambulizi dhidi ya operesheni za kibinadamu nchini Sudan.

    Unaweza kusoma;

  8. Tazama : Video iliyopigwa kutoka angani ya kanisa la Uswidi lililodumu kwa miaka 113 ilihamishiwa eneo lingine

    Kanisa moja llililodumu kwa miaka miaka 113 kaskazini mwa Uswidi limewasili katika eneo lake jipya baada ya safari ya siku mbili za kuhamishwa.

    Video ya angani inaonyesha kanisa likiinuliwa kwenye trela maalum, huku kanisa likisogezwa kilomita 5 chini ya barabara kwa kasi ya 500m kwa saa, na vitu vya barabarani kama vile taa na alama kuondolewa ili kuruhusu kupitishwa kwa kanisa hilo.

    Kanisa la Kiruna lilikuwa katika hatari ya kuzama baada ya zaidi ya miaka mia moja ya shughuli za uchimbaji madini zinazofanyika katika eneo jirani.

    Kanisa lina uzito wa tani 672, urefu wa 35m na upana wa 40m.

    Lilihamishwa kwa ukamilifu, pamoja na minara yake, badala ya kubomolewa na kuunganishwa tena baadaye.

    Wakati mmoja lilipigiwa kura kuwa jengo bora zaidi lililojengwa kabla ya mwaka 1950.

    Uhamishaji wake unakadiriwa kugharimu mabilioni ya dola.

  9. Urusi yaanzisha mashambulizi mapya magharibi mwa Ukraine

    Urusi imerusha mamia ya ndege zisizo na rubani na makombora magharibi mwa Ukraine usiku kucha katika moja ya mashambulizi makubwa zaidi ya mabomu katika wiki za hivi karibuni, maafisa wa Ukraine wamesema.

    Mashambulizi hayo yaliripotiwa huko Zaporizhzhia, Dnipropetrovsk, na Lviv, ambapo mtu mmoja aliuawa na wengine kujeruhiwa.

    Waziri wa Mambo ya Nje Andrii Sybiha alisema shambulizi hilo lilionyesha ni kwa nini juhudi za kidiplomasia za kumaliza vita na ulinzi mkali wa anga ni "muhimu".

    Hilo linatokea wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amependekeza Uswizi, Austria au Uturuki kama mahali panapowezekana kwa mazungumzo ya amani na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin.

    Soma zaidi:

  10. Makubaliano ya Congo na M23 kurudisha udhibiti wa serikali katika maeneo yanayokaliwa na waasi

    Makubaliano ya amani yaliyopendekezwa kati ya serikali ya Congo na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda yanataka kurejesha udhibiti wa serikali katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi, kulingana na nakala ya rasimu iliyoonekana na Associated Press.

    Rasimu hiyo ambayo ilipendekezwa na Qatar, inaeleza mchakato wa awamu tatu wa kufikia amani. Pendekezo hilo litajadiliwa chini ya upatanishi wa pande zote mbili huko Doha katika siku zijazo. Wale waliohusika moja kwa moja katika juhudi za kuleta amani walithibitisha hilo kwa AP.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Maxime Prévot, aliwaambia waandishi wa habari Jumanne kwamba Rais wa Congo Felix Tshisekedi hajaridhishwa na rasimu ya makubaliano.

    "Awamu mpya ya majadiliano itaanza saa na siku zijazo huko Doha. Rais Tshisekedi alinithibitishia kuwa yaliyopendekezwa si ya kuridhisha. Hilo ni jambo muhimu kulikumbuka," alisema Prévot.

    Kiongozi wa kisiasa wa M23 Bertrand Bisimwa alisema kundi hilo "linalenga kutekeleza Azimio la Doha katika hatua ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa wafungwa."

    Mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23 yaliongezeka mwezi Januari, wakati waasi hao walipoteka sehemu kubwa ya mashariki yenye utajiri wa madini, ukiwemo mji mkuu wa eneo la Goma.

    Maelfu ya watu wameuawa na mamia kwa maelfu ya raia kulazimishwa kuyaacha makazi yao katika vita vinavyoendelea, Umoja wa Mataifa unasema.

    Unaweza kusoma

  11. Arsenal yaipokonya Tottenham Hotspur Eberechi Eze mdomoni

    Hatua ya kushangaza ya Arsenal ya kumnyakua Eberechi Eze kutoka kwa mahasimu wao Tottenham Hotspur ni isiyo na huruma na kuonyesha huu ndio msimu ambao wamepanga kujinyakulia zawadi kubwa zaidi.

    Spurs walikuwa tayari kuzindua zulia jekundu kumkaribisha mshambuliaji wa Crystal Palace wa Uingereza siku ya Jumatano, makubaliano hayo yalikamilika na dalili zote zilionyesha kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alikuwa tayari kuhama.

    Baadaye ilibainika kuwa Arsenal walikuwa wakitathmini jeraha la goti la mshambuliaji Kai Havertz, ambalo linaweza kuwatia doa katika safu yao ya mashambulizi - udhaifu ambao ulikuwa na athari kubwa katika kikosi cha kocha Mikel Arteta kumaliza akiwa mikono mitupu kwa mwaka wa tano mfululizo msimu uliopita.

    Badala ya kwendea chaguo la gharama ya chini la kutafuta wa mkopo kama ilivyotarajiwa, Arsenal walijitokeza kwa mtindo wa aina yake kwa kuandaa pauni milioni 60 ili kumleta Eze Uwanja wa Emirates akiwa tu anakaribia kuingia mikononi mwa Spurs.

    Uhamisho wa Eze kwenda Arsenal, ambao sasa unatarajiwa kukamilishwa kwa mafanikio, sio tu pigo kubwa la kisaikolojia lililolenga London kaskazini huko Spurs.

    Ni ishara tosha kwamba hawana nia ya kubahatisha kwenye lengo lao la kujiimarisha katika kuwania taji la Ligi Kuu, pamoja na kujiweka sawa kwenye Ligi ya Mabingwa kwa mara nyingine tena baada ya kutinga nusu fainali msimu uliopita.

    Ni mkakati tofauti kabisa wa kukabiliana na hali mbaya iliyoikumba Arsenal msimu uliopita, wakati kushindwa kwao kutatua tatizo lililo wazi - yaani kusajili mshambuliaji imara - kuliigharimu pakubwa.

    Spurs walidhani walikuwa wameshamchukua Eze, uwezekano wa makubaliano ya pesa pamoja na Richarlison ulijadiliwa, lakini Arsenal walijitokeza kwa kasi kubwa mara tu walipokabiliwa na uwezekano wa Havertz kuachwa nje.

    Arsenal wamekuwa wakihusishwa na Eze majira yote ya kiangazi, lakini ilifikiriwa kuwa nia yao ilikuwa imefifia mara Ethan Nwaneri alipokubali mkataba mpya wa miaka mitano, pamoja na kumsajili winga wa Chelsea Noni Madueke kwa mkataba wa £48.5m.

    Jeraha la Havertz, na matokeo yake yanayoweza kutokea, yaliamsha hamu yao na kuwaacha Spurs wakiwa wameduwaa.

    Soma zaidi:

  12. Mwanajeshi wa Marekani ahukumiwa kwa kufanya ujasusi kwa ajili ya China

    Baharia wa Jeshi la Wanamaji la Marekani huko California amehukumiwa kwa kosa la ujasusi kwa kuuza siri za kikosi hicho kwa afisa wa China ambaye alimsajili kupitia mtandao ya kijamii.

    Jinchao Wei, 25, alipatikana na hatia ya mashtaka sita, ikiwa ni pamoja na ujasusi, njama ya kufanya ujasusi, na usafirishaji haramu wa data za siri kuhusu meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani.

    "Vitendo vya mshtakiwa vinawakilisha usaliti mkubwa wa uaminifu aliopewa kama mwanajeshi wa Marekani," Mwanasheria wa Marekani Adam Gordon alisema katika taarifa yake baada ya hukumu kusomwa.

    "Kwa kufanya biashara ya siri za kijeshi kwa Jamhuri ya Watu wa China kwa ajili ya pesa taslimu, alihatarisha sio tu maisha ya wanamaji wenzake bali pia usalama wa taifa zima na washirika wetu."

    Wei, anayejulikana pia kama Patrick Wei, alikamatwa mnamo Agosti 2023 kwa mashtaka ya ujasusi alipokuwa akiwasili kufanya kazi kwenye meli ya mashambulizi ya amphibious, USS Essex.

    Raia wa Marekani kwa kuandikishwa uraia, Wei alikuwa fundi mitambo na mwenye kibali cha usalama, na pia alipata taarifa nyeti kuhusu meli hiyo na nyingine zilizokuwa eneo la Pasifiki.

    Wakati wa kesi yake ya wiki nzima, waendesha mashtaka waliwasilisha ushahidi ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya simu, jumbe za kielektroniki, na jumbe za sauti ambazo Wei alibadilishana na mhudumu wake wa Kichina.

    Wei alimwita mhudumu huyo wa Kichina "Big Brother Andy" na kuomba waweke uhusiano wao kuwa siri kwa kutumia programu nyingi zilizosimbwa kuwasiliana na kukubali malipo. Wei pia alitumia kompyuta mpya na simu ya mhudumu wake.

    Soma zaidi:

  13. Israel yaidhinisha mradi wa makazi ya Ukingo wa Magharibi wenye utata

    Israel imetoa idhinisho la mwisho kwa mradi wa makazi wenye utata ambao utaondoa kabisa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Jerusalem Mashariki na kugawanya eneo hilo mara mbili.

    Ujenzi katika eneo la E1 umesitishwa kwa miongo miwili huku kukiwa na upinzani mkali wa kimataifa. Wakosoaji wanaonya kuwa mpango huo utaondoa matumaini ya kuwepo kwa taifa la Palestina.

    Siku ya Jumatano, kamati ya wizara ya ulinzi iliidhinisha mpango wa nyumba 3,400 katika eneo la E1. Waziri wa fedha wa mrengo wa kulia mwenye msimamo mkali Bezalel Smotrich, ambaye alizindua mpango huo wiki jana, alisema wazo la taifa la Palestina "linaondolewa".

    Mamlaka ya Palestina ililaani hatua hiyo ikisema kuwa ni kinyume cha sheria na itaharibu matarajio ya kupatikana kwa suluhisho la serikali hizo mbili.

    Hatua hiyo inafuatia kuongezeka kwa idadi ya nchi zilizosema zitatambua taifa la Palestina, ambalo Israel imelaani.

    Israel imejenga takriban makazi 160 ya Wayahudi 700,000 tangu ilipoikalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki - ardhi ambayo Wapalestina wanataka, pamoja na Gaza, kwa taifa linalotarajiwa - wakati wa vita vya Mashariki ya Kati vya 1967. Takriban Wapalestina milioni 3.3 wanaishi kando yao.

    Makazi hayo ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa - msimamo ulioungwa mkono na maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki mwaka jana.

    Serikali za Israel zilizofuatana zimeruhusu kuendelezwa kwa makazi. Hata hivyo, upanuzi umeongezeka kwa kasi tangu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliporejea madarakani mwishoni mwa 2022 akiwa mkuu wa muungano wa mrengo wa kulia, unaounga mkono walowezi, pamoja na kuanza kwa vita vya Gaza vilivyochochewa na shambulizi la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israel.

    Soma zaidi:

  14. Jeshi la Israel lasema hatua za kwanza za kushambulia mji wa Gaza zimeanza

    Jeshi la Israel linasema limeanza "hatua za awali" za mashambulizi ya ardhini yaliyopangwa kuuteka na kukalia kwa mabavu mji wote wa Gaza na tayari wameshikilia viunga vyake.

    Msemaji wa jeshi alisema kuwa wanajeshi tayari wanaendelea kupanga mikakati yao katika maeneo ya Zeitoun na Jabalia ili kuweka msingi wa mashambulizi hayo, ambayo Waziri wa Ulinzi Israel Katz aliidhinisha siku ya Jumanne na yatajadiliwa kwenye baraza la mawaziri la usalama baadaye wiki hii.

    Takriban wanajeshi wa akiba 60,000 wameitwa kuanzia mwanzo wa Septemba ili kuwaachilia walio kazini kwa ajili ya operesheni hiyo.

    Hamas imeishutumu Israel kwa kukwamisha makubaliano ya kusitisha mapigano kwa ajili ya kuendeleza "vita vya kikatili dhidi ya raia wasio na hatia", shirika la habari la Reuters liliripoti.

    Mamia kwa maelfu ya Wapalestina katika mji wa Gaza wanatarajiwa kuamriwa kuhama na kuelekea kwenye makazi kusini mwa Gaza huku matayarisho ya Israel yakiendelea.

    Washirika wengi wa Israel wamelaani mpango huo, huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akionya Jumatano kwamba "unaweza tu kusababisha maafa kwa wote wawili na hatari ya kulitumbukiza eneo lote katika mzunguko wa vita vya kudumu".

    Wakati huo huo, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ilisema kuhamisha watu zaidi na kuongezeka uhasama kuna "hatarisha kuzidisha hali ambayo tayari ni janga" kwa wakazi milioni 2.1 wa Gaza.

    Serikali ya Israel ilitangaza nia yake ya kuliteka eneo lote la Ukanda wa Gaza baada ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas juu ya kusitisha mapigano na kuachiliwa huru kwa mateka kusambaratika mwezi uliopita.

    Soma zaidi:

  15. Hujambo. Karibu karibu matangazo yetu ya moja kwa moja mimi ni Asha Juma.