Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini Israel inakabiliwa na maandamano makubwa zaidi katika historia yake ya miaka 75?
Maelfu ya Waisraeli waliingia barabarani kote nchini mwishoni mwa juma katika kile kinachojulikana kuwa maandamano makubwa zaidi katika historia ya Israel.
Maandamano hayo yanapinga mipango ya serikali kupunguza nguvu za Mahakama ya Juu, ambayo wakosoaji wanasema inadhoofisha uhuru wa mahakama na kutishia demokrasia.
Akitetea mipango yake, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alionyesha kuwa mageuzi hayo yatarejesha uwiano kati ya matawi ya serikali.
Suala hilo limesababisha mgawanyiko mkubwa katika jamii ya Israel na kama kiongozi wa upinzani Yair Lapid alivyoeleza, huu ndio "mgogoro mkubwa zaidi" ambao Israeli imekabiliana nao katika historia yake.
Maandamano hayo yamekuwa yakiendelea kwa wiki 10 na yamekuwa yakiongezeka huku mageuzi yakielekea kuidhinishwa.
Siku ya Jumamosi, waandaaji walisema hadi waandamanaji 500,000 waliingia mitaani nchini humo katika kile gazeti la Haaretz lilichokiita "maandamano makubwa zaidi katika historia ya nchi."
Mjini Tel Aviv pekee, takriban watu 200,000 walisemekana kuandamana siku ya Jumamosi na katika mji wa kaskazini wa Haifa, waliripotiwa kuwa na waandamanaji 50,000.
"Chanzo"
Kama Yolande Knell, mwandishi wa BBC Jerusalem anavyoeleza, "Mabadiliko katika mfumo wa haki ndio msingi wa sera ya muungano mpya wa kidini wa kitaifa wa Israeli unaoongozwa na Netanyahu" ambao uliundwa mnamo Desemba.
"Lengo la mageuzi hayo ni kuipa serikali ushawishi madhubuti juu ya chaguo la majaji na kupunguza uwezo wa Mahakama ya Juu kutoa uamuzi dhidi ya Ofisi ya Waziri Mkuu au kubatilisha sheria," inaongeza.
Chini ya mapendekezo hayo, wanasiasa wangekuwa na jukumu kubwa katika uteuzi wa majaji na kuruhusu Knesset kubatilisha maamuzi ya Mahakama ya Juu kwa wingi rahisi na kuondoa baadhi ya sheria katika ukaguzi wa mahakama kabisa.
Wakosoaji wanasema hii inahatarisha mfumo wa kisiasa, kwani Israel haina katiba na ni bunge pekee linalodhibitiwa na muungano unaotawala.
Katikati ya pambano hili ni Benjamin Netanyahu, ambaye ametawala siasa za nchi hiyo kwa miongo miwili iliyopita.
Licha ya kukabiliwa na kesi kwa madai ya hongo, ulaghai na uvunjaji wa uaminifu, ambayo anakanusha, alichaguliwa tena Novemba 2022 baada ya miezi 18 ya upinzani.
Huu ni muhula wake wa sita kama waziri mkuu na sasa ana wabunge wengi katika Knesset (bunge) akiongoza serikali ya mseto ya vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia na kidini.
Tangu serikali iwasilishe mipango ya mageuzi ya mahakama mwezi Januari, maelfu ya watu wameshiriki katika maandamano makubwa ya kila wiki kupinga sheria mpya, ambayo kwa sasa inajadiliwa katika Knesset.
Kura za maoni zinaonyesha mpango wa serikali haupendwi na Waisraeli wengi wangependelea kuafikiana.
Rais Isaac Herzog, ambaye hasa ana jukumu la kiitifaki, amekuwa akishinikiza kuwepo kwa mazungumzo kati ya serikali na upinzani, akionya kuwa nchi hiyo iko ukingoni mwa "kuporomoka kwa katiba na kijamii."
Washirika wengi wa kigeni wa Israel pia wameelezea wasiwasi wao kuhusu sheria hiyo mpya.
"Punguza mwendo kidogo, labda uwalete watu pamoja, jaribu kujenga maelewano," Balozi wa Marekani nchini Israel Tom Nides alisema mapema Machi.
Serikali imesimama kidete kupinga maandamano hayo kwa madai kuwa yanachochewa na wapinzani wa kisiasa.
Mgawanyiko Mkubwa
Suala hilo linasababisha mgawanyiko mkubwa katika jamii ya Israel na hata askari wa akiba, nguzo kuu kwa jeshi la Israel, wametishia kukataa utumishi wao wa kijeshi kama njia ya kuonyesha upinzani wao.
Jumatatu iliyopita, katika hali ambayo haijawahi kushuhudiwa, makumi ya marubani ya wanajeshi wa akiba katika kikosi cha wasomi wa Jeshi la Wanahewa la Israeli walisema hawataripoti kwa mafunzo.
Baadaye walibadili misimamo na kukubali kuhudhuria na kufanya mazungumzo na makamanda wao.
"Si kawaida kabisa," afisa wa hifadhi aliambia BBC. "Tunaelekea kubaki bila upendeleo katika masuala haya, lakini si mjadala wa kawaida wa kisiasa. Ni mabadiliko makubwa. Tuna wasiwasi kwamba kanuni zetu muhimu za demokrasia zitaharibiwa kabisa."
Wafanyakazi wa sekta ya teknolojia, wanasheria na mabenki pia wameelezea wasiwasi juu ya athari zinazowezekana za mageuzi, ikiwa ni pamoja na uchumi.
Netanyahu anatarajia miswada hiyo kupitishwa kabla ya kikao hiki cha Knesset kukamilika Aprili 4.