Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Israel yasajili askari wa akiba 60,000 kabla ya mashambulizi yaliyopangwa Gaza

Jeshi la Israel linasema kuwa linawasajili askari wa akiba wapatao 60,000 kabla ya mpango wa mashambulizi ya ardhini ili kuuteka mji wote wa Gaza.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma , Lizzy Masinga & Dinah Gahamanyi

  1. Uganda haijakubali kuchukua watu waliofukuzwa kutoka Marekani, afisa wa ngazi ya juu asema

    Afisa mkuu wa Uganda alikanusha Jumatano ripoti ya vyombo vya habari vya Marekani kwamba nchi hiyo imekubali kuwachukua watu waliofukuzwa kutoka Marekani, akisema haina vifaa vya kuwahudumia.

    Iikinukuu nyaraka za ndani za serikali ya Marekani, shirika la habari nchini humo, CBS News liliripoti Jumanne kwamba Washington imefikia makubaliano ya kuwahamisha Uganda na Honduras kama sehemu ya harakati zake za kuongeza kasi ya kuwafukuza wahamiaji katika nchi ambazo hawana uraia.

    "Kwa ufahamu wangu hatujafikia makubaliano kama haya," Okello Oryem, waziri wa maswala ya kigeni aliiambia Reuters kwa ujumbe mfupi wa simu."Hatuna vifaa na miundombinu ya kuwahudumia wahamiaji haramu kama hao nchini Uganda.

    "Serikali ya Honduras haikujibu mara moja ombi la Reuters la maoni juu ya ripoti hiyo.Rais Donald Trump analenga kuwafukuza mamilioni ya wahamiaji walioingia Marekani kinyume cha sheria na utawala wake umetaka kuongeza uhamisho hadi nchi za tatu , ikiwa ni pamoja na kuwatuma wahalifu waliopatikana na hatia nchini Sudan Kusini na Eswatini.

    Ripoti ya CBS ilisema makubaliano na Uganda na Honduras yalitokana na kifungu cha sheria ya uhamiaji ya Marekani ambayo inaruhusu watu wanaotafuta hifadhi kuhamishwa hadi nchi za tatu ikiwa serikali ya Marekani itaamua mataifa hayo yanaweza kusikiliza madai yao kwa haki.

    Soma zaidi:

  2. Mbunge wa Afrika Kusini afyatua risasi kuzima shambulio wakati wa jaribio la utekaji nyara

    Mbunge mashuhuri wa Afrika Kusini alifyatua risasi kuzima shambulio kali la genge dhidi yake na wenzake wawili mjini Cape Town.

    Ian Cameron - pamoja na wajumbe wengine wawili wa kamati ya polisi ya bunge, Lisa Schickerling na Nicholas Gotsell - walikuwa wakirejea kutoka kwa safari ya kikazi wakati gari lao lilipovamiwa katika kitongoji cha Philippi siku ya Jumanne.

    Wavamizi hao walivunja madirisha ya gari hilo kwa matofali na kuwajeruhi Cameron na Gotsell.

    Cameron, ambaye meno yake yalivunjika, alilipiza kisasi kwa kufyatua risasi na kumjeruhi mmoja wa washambuliaji.

    Polisi walisema vijana wawili, wenye umri wa miaka 16 na 18, wamekamatwa walipokuwa wakichunguza kesi ya kujaribu kuua na kujaribu kuteka nyara.

    Uhalifu ni tatizo kubwa nchini Afrika Kusini na nchi hiyo ina moja ya viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani.

    Mmoja wa washukiwa hao alikamatwa akitafuta matibabu katika hospitali siku ya Jumanne huku mwingine akikamatwa shambani mapema Jumatano, polisi walisema, na kuongeza kuwa msako unaendelea kumtafuta mshukiwa wa tatu.

  3. Putin azungumza na Erdogan kuhusu Ukraine na mazungumzo na Trump

    Huduma ya habari ya Kremlin imeripoti kwamba Vladimir Putin alifanya mazungumzo ya simu na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambapo alijadili "maendeleo ya hivi punde kuhusu hali ya Ukraine."

    Miongoni mwa mambo mengine, Putin alizungumza juu ya msaada wa Uturuki "katika kufanya mazungumzo kati ya wawakilishi wa Urusi na Ukraine huko Istanbul." "Rais wa Urusi alielezea tathmini yake ya mkutano wa Urusi na Marekani uliofanyika Anchorage,"ilisema huduma habari ya Kremlin ilisema.

    Erdogan ameelezea mara kwa mara nia yake ya upatanishi katika kuleta suluhu ya amani ya vita kati ya Urusi na Ukraine.

    Wajumbe wa Urusi na Ukraine wamefanya mazungumzo huko Istanbul mara kadhaa, lakini matokeo yao pekee yalikuwa kubadilishana kumbukumbu na makubaliano juu ya kukabidhiana kwa wafungwa wa vita na miili ya wafu.

    Putin hivi karibuni alifanya mazungumzo na Rais wa Marekani Donald Trump huko Alaska; Trump pia alimkaribisha Volodymyr Zelensky na viongozi wa Ulaya katika Ikulu ya White House mapema wiki hii.

    Baada ya mikutano hiyo, maafisa wa Marekani walisema Ukraine na Urusi zinaweza kupanga mkutano kati ya Putin na Zelensky, lakini Moscow haijathibitisha taarifa hiyo.

    Soma zaidi:

  4. Israel yasajili askari wa akiba 60,000 kabla ya mashambulizi yaliyopangwa Gaza

    Jeshi la Israel linasema kuwa linawasajili askari wa akiba wapatao 60,000 kabla ya mpango wa mashambulizi ya ardhini ili kuuteka mji wote wa Gaza.

    Afisa wa kijeshi alisema askari wa akiba wataripoti kazini mnamo Septemba na kwamba wanajeshi wengi waliokusanywa kwa ajili ya shambulio hilo watakuwa wanafanya kazi. Waliongeza kuwa wanajeshi tayari wanahudumu katika maeneo ya Zeitoun na Jabalia kama sehemu ya maandalizi ya mpango huo, ambao Waziri wa Ulinzi Israel Katz aliupitisha siku ya Jumanne na utawekwa kwenye baraza la mawaziri la usalama baadaye wiki hii.

    Mamia kwa maelfu ya Wapalestina katika mji wa Gaza wanatarajiwa kuamrishwa kuhama na kuelekea kwenye makazi kusini mwa Gaza.

    Washirika wengi wa Israel wamelaani mpango huo, huku Umoja wa Mataifa na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali yameonya kwamba mashambulizi mengine na uhamisho wa watu wengi zaidi utakuwa na "athari za kutisha za kibinadamu" baada ya miezi 22 ya vita.

    Serikali ya Israel ilitangaza nia yake ya kuliteka eneo lote la Ukanda wa Gaza baada ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas juu ya kusitisha mapigano na kuachiliwa huru kwa mateka kuvunjika mwezi uliopita.

    Wapatanishi wa kikanda wanajaribu kupata makubaliano kabla ya mashambulizi kuanza na wamewasilisha pendekezo jipya la kusitisha mapigano kwa siku 60 na kuachiliwa kwa karibu nusu ya mateka 50 ambao bado wanashikiliwa huko Gaza, ambayo Hamas ilisema imekubali Jumatatu.

    Israel bado haijawasilisha jibu rasmi, lakini maafisa wa Israel walisisitiza siku ya Jumanne kwamba hawatakubali tena makubaliano ya sehemu na kudai yale ya kina ambayo yatawafanya mateka wote waachiliwe. Ni mateka 20 pekee wanaoaminika kuwa hai.

    Unaweza kusoma;

  5. Netanyahu amshutumu Waziri Mkuu wa Australia kwa 'kuisaliti' Israel

    Waziri mkuu wa Israel amemshutumu mwenzake wa Australia kwa "kuisaliti Israeli" na "kutelekeza" jamii ya Wayahudi wa Australia, baada ya siku za mzozo unaoongezeka kati ya nchi hizo mbili.

    Benjamin Netanyahu alisema Jumanne kwamba historia itamkumbuka Anthony Albanese "kwa kile alichosema: mwanasiasa dhaifu".

    Australia ilimzuia mwanachama wa siasa kali za mrengo wa kulia wa muungano unaotawala wa Netanyahu kuingia nchini humo siku ya Jumatatu, na Israel nayo ikabatilisha viza za wawakilishi wa Australia kwa Mamlaka ya Palestina.

    Waziri wa Uhamiaji wa Australia Tony Burke alisema Netanyahu "ameikosoa" Canberra hivi karibuni akitangaza kuwa itaungana na Uingereza, Ufaransa na Canada katika kutambua taifa la Palestina.

    "Nguvu hazipimwi kwa ni watu wangapi unaoweza kulipua au ni watu wangapi unaweza kuwaacha wakiwa na njaa," Burke aliambia Shirika la Utangazaji la Australia Jumatano.

    Albanese baadaye aliwaambia waandishi wa habari kwamba "hachukulii vitu hivi kibinafsi". "Ninawaheshimu viongozi wa nchi nyingine, nashirikiana nao kwa njia ya kidiplomasia," alisema.

    Kiongozi wa upinzani wa Israel alikosoa matamshi ya Netanyahu, na kuyataja kuwa ni "zawadi" kwa kiongozi huyo wa Australia. Yair Lapid aliandika kwenye X: "Jambo ambalo linaimarisha zaidi kiongozi katika ulimwengu wa kidemokrasia leo ni makabiliano na Netanyahu, kiongozi mwenye sumu zaidi ya kisiasa katika ulimwengu wa Magharibi.

    Unaweza kusoma;

  6. Waziri wa Afrika Kusini akosolewa vikali kuhusu chuki za ubaguzi wa rangi

    Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa Afrika Kusini Gayton McKenzie amekuwa mwepesi wa kuwatangaza na kuwalaumu watu wengine kwa ubaguzi wa rangi lakini yeye mwenyewe sasa ametajwa kuwa mbaguzi wa rangi - mashtaka ambayo anayakanusha.

    Mara nyingi anaonekana kama mtu wa kukatisha tamaa kwa jumuiya ya machotara chini humo, wanaotambuliwa kama watu wenye asili mchanganyiko wanarejelewa kulingana na sensa ya watu Afrika Kusini .

    Lakini maoni ya zamani aliyotoa McKenzie kwenye mitandao ya kijamii, akitumia neno la kukera sana akimaanisha watu weusi, yamezua dhoruba ya kisiasa.

    Ana hadi mwisho wa Jumatano kujibu kwa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Afrika Kusini (SAHRC), ambayo inamtaka waziri kufuta jumbe hizo zinazokera na kuomba radhi kwa umma, miongoni mwa matakwa mengine.

    "Mchotara" ilikuwa ni uainishaji uliotolewa kwa watu wa urithi mchanganyiko chini ya ubaguzi wa rangi. Mfumo huu uliunda utawala wa kikabila uliotekelezwa kisheria ambao uliweka matabaka na uliwaona watu weupe juu na watu weusi chini, na Wahindi na watu weusi akatika tabaka la katikati.

    Licha ya ubaguzi wa rangi kukomeshwa miongo mitatu iliyopita , urithi wake mchungu unaendelea katika uchumi na siasa za nchi hiyo.

    Muungano wa Patriotic wa McKenzie (PA) umevutia uungwaji mkono miongoni mwa watu weusi, na kushinda uwakilishi bungeni katika uchaguzi mwaka jana.

    "Kwa mara ya kwanza kuna watu weusi pia wanaenda bungeni kupitia Muungano wa Patriotic Alliance," McKenzie alisema, baada ya matokeo kutangazwa.

    Rais Cyril Ramaphosa alijumuisha muungano wa PA katika serikali yake ya muungano wa vyama vingi baada ya chama chake cha African National Congress (ANC) kupoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza.

    Soma zaidi:

  7. Raia 140 waliuawa na waasi DRC licha ya mchakato wa amani - Ripoti

    Waasi wa M23 waliwaua takriban watu 140 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwezi uliopita katika moja ya vitendo vya ukatili mbaya zaidi wa kundi hilo lililojihami tangu kuibuka tena mwishoni mwa 2021, Human Rights Watch imesema katika ripoti yake.

    Waasi hao hapo awali walikanusha vikali kuhusika na mauaji haya, wakitaja mashtaka hayo kuwa "upotoshaji wa wazi".

    Haikujibu ombi la kutoa maoni juu ya ripoti hiyo, shirika la haki za binadamu lilisema.

    Hii ni licha ya mchakato wa amani, uliosimamiwa na Marekani na Qatar, kumaliza mzozo katika eneo hilo.

    Mashuhuda waliambia kikundi cha utetezi kwamba waasi wanaoungwa mkono na Rwanda "waliwaua" wakazi wa eneo hilo, wakiwemo wanawake na watoto, wengi wao kutoka kabila la Wahutu katika eneo la Rutshuru, karibu na Mbuga ya Kitaifa ya Virunga.

    Mauaji hayo yanayodaiwa kutekelezwa yanaonekana kutokea wakati wa kampeni ya M23 dhidi ya kundi la Wahutu wenye silaha, FDLR, lililoundwa na wahusika wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika nchi jirani ya Rwanda.

    HRW ilisema jumla ya mauaji mwezi Julai yanaweza kuzidi 300, na kuthibitisha matokeo kama hayo ya Umoja wa Mataifa mapema mwezi huu.

    Mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23 yaliongezeka mwezi Januari, wakati waasi hao walipoteka sehemu kubwa ya mashariki yenye utajiri wa madini, ukiwemo mji mkuu wa eneo la Goma.

    Maelfu ya watu wameuawa na mamia kwa maelfu ya raia kulazimishwa kuyaacha makazi yao katika vita vinavyoendelea, Umoja wa Mataifa unasema.

    Unaweza kusoma;

  8. Mchina afungwa Marekani kwa kupeleka silaha Korea Kaskazini

    Korea Kaskazini imepigwa marufuku kufanya biashara ya silaha na zana za kijeshi chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa

    Raia wa China amehukumiwa kifungo cha miaka minane jela kwa kosa la kusafirisha silaha na vifaa vingine vya kijeshi kwenda Korea Kaskazini, wizara ya sheria ya Marekani imesema.

    Shenghua Wen, 42, alipokea takriban $2m (£1.5m) kutoka kwa maafisa wa Korea Kaskazini ili kusafirisha bidhaa hizo kutoka California, kulingana na taarifa kutoka kwa shirika hilo siku ya Jumatatu.

    Mkazi wa Ontario, California, Wen amezuiliwa tangu Desemba 2024. Alikiri hatia mnamo Juni kwa kula njama ya kukiuka Sheria ya Kimataifa ya Uwezo wa Kiuchumi wa Dharura na kuwa wakala haramu wa serikali ya kigeni.

    Kesi ya Wen inaonyesha mbinu mbalimbali ambazo Korea Kaskazini inazitumia vikwazo vya kimataifa kwa biashara yake ya silaha.

    Ikimtaja Wen kama "mgeni haramu", wizara ya sheria ilisema aliingia Marekani kwa viza ya wanafunzi mwaka wa 2012 na kusalia nchini baada ya viza yake kuisha Desemba 2013.

    "Kabla ya kuingia Marekani, Wen alikutana na maafisa wa serikali ya Korea Kaskazini katika ubalozi wa Korea Kaskazini nchini China," shirika hilo lilisema. "Maafisa hawa wa serikali walimuelekeza Wen jinsi ya kununua bidhaa kwa niaba ya Korea Kaskazini."

    Maafisa wawili wa Korea Kaskazini waliwasiliana na Wen kupitia jukwaa la ujumbe mtandaoni mwaka wa 2022 na kumwambia apitishe silaha na bidhaa nyingine kutoka Marekani hadi Korea Kaskazini, kulingana nawizara ya sheria.

    Unaweza pia kusoma:

  9. Marekani yafikia makubaliano na Uganda pamoja na Honduras kuwapeleka wahamiaji katika nchi hizo

    Marekani imefikia makubaliano na Honduras na Uganda kuwapeleka wahamiaji katika nchi hizo kama sehemu ya kukabilia na wahamiaji haramu, kulingana na nyaraka zilizopatikana na mshirika wa BBC wa Marekani CBS.

    Uganda imekubali kuchukua idadi isiyojulikana ya wahamiaji wa Kiafrika na Asia ambao walikuwa wameomba hifadhi kwenye mpaka wa Marekani na Mexico, wakati Honduras itapokea mamia ya watu waliofukuzwa wa nchi zinazozungumza Kihispania, CBS inaripoti.

    Hatua hiyo ni sehemu ya jaribio la utawala wa Donald Trump kutaka nchi nyingi zaidi zikubali wahamiaji waliofukuzwa nchini humo ambao si raia wao.

    Wanaharakati wa haki za binadamu wamelaani sera hiyo, wakisema wahamiaji wanakabiliwa na hatari ya kutumwa katika nchi ambako wanaweza kudhurika.

    Chini ya makubaliano hayo, Uganda imekubali kuwapokea wahamiaji waliofukuzwa Marekani almuradi wasiwe na historia ya uhalifu, lakini haijulikani nchi hiyo hatimaye itachukua wangapi, kulingana na CBS.

    Honduras ilikubali kupokea wahamiaji wa zaidi ya miaka miwili, ikiwa ni pamoja na familia zinazosafiri na watoto, lakini nyaraka zinaonyesha inaweza kuamua kukubali zaidi.

    Mikataba yote miwili ni sehemu ya shinikizo kubwa la utawala wa Trump wa kupanga mipango ya kufurushwa kwa wahamiaji na kupelekwa katika nchi mbalimbali kwenye mabara kadhaa - ikiwa ni pamoja na yale yenye rekodi tata za haki za binadamu.

    Kufikia sasa, mataifa kadhaa yamekubali kuwapokea wahamiaji waliofukuzwa kutoka mataifa mengine.

    Soma zaidi:

  10. Mwanamke wa Peru aficha dawa za kulevya kwenye kifaa cha kujifurahisha kingono

    Mwanamke mmoja wa Peru ameshtakiwa kwa kujaribu kusafirisha dawa za kulevya aina ya Cocaine za thamani ya $70,000 (£52,000) hadi Bali, zikiwa zimefichwa kwenye nguo yake ya ndani na kifaa cha kujifurahisha kingono.

    Mwanamke huyo, ambaye alitambuliwa tu na herufi za kwanza za NS, alizuiliwa na maafisa wa forodha ambao walihisi kuwa ana wasiwasi, polisi walisema.

    "Mihadarati hiyo ilifichwa kwenye vifurushi sita vya plastiki vilivyofungwa kwa mkanda mweusi ndani ya sidiria ya rangi ya kijani, vifurushi vitatu kama hivyo vilipatikana kwenye chupi nyeusi na kifaa cha kujifurahisha kingono ambacho kiliingizwa mwilini mwake," Radiant, mkurugenzi wa kitengo cha mihadarati katika polisi wa Bali, aliwaambia waandishi wa habari.

    Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 42 ameshtakiwa chini ya sheria za dawa za kulevya nchini Indonesia, na iwapo atapatikana na hatia anaweza kukabiliwa na hukumu ya kifo.

    Soma zaidi:

  11. Qatar yasema DRC, M23 bado 'wanashiriki' katika mchakato wa amani

    Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na waasi wa M23 hawajajiondoa katika mchakato wa amani licha ya kukosa kufikia makubaliano siku ya mwisho iliyopangwa, mpatanishi wa Qatar alisema Jumanne.

    "Pande zote mbili zinashirikiana vizuri. Tunashirikiana nao pia... na tumejitolea katika mchakato huo," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Majed al-Ansari aliambia mkutano wa kawaida wa habari.

    Serikali ya Congo na waasi wa M23 walitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Julai yenye lengo la kukomesha kabisa mapigano ambayo yamesababisha vurugu mashariki mwa DRC.

    Chini ya masharti ya makubaliano hayo yaliyofuatia mazungumzo ya Qatar, pande hizo mbili zilipaswa kuanza mazungumzo ya amani Agosti 8 na kukamilisha makubaliano ifikapo tarehe 18 Agosti.

    Licha ya muda uliopangwa kufikia kikomo, Ansari alisema bado kuna nia ya kuendelea na mchakato huo.

    Siku ya Jumapili, afisa wa Qatar aliiambia AFP kwa sharti la kutotajwa jina kwamba rasimu ya mpango wa amani imetolewa na DRC na waasi wa M23 kabla ya duru nyingine ya mazungumzo inayotarajiwa kufanyika Doha katika siku zijazo.

    Soma zaidi:

  12. Salah na Rogers washinda Tuzo za Chama cha Wanasoka wa Kulipwa

    Winga wa Liverpool, Mohamed Salah ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA), huku kiungo wa Aston Villa, Morgan Rogers akichaguliwa kuwa mchezaji bora chipukizi wa mwaka.

    Meneja wa zamani wa England Sir Gareth Southgate ndiye mpokeaji wa tuzo ya PFA 2025 kwa mchango wake katika soka na mafanikio akiwa na timu ya taifa.

    Salah, 33, ndiye mchezaji wa kwanza kushinda tuzo hiyo mara tatu baada ya kuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Liverpool msimu uliopita.

    Alipoulizwa kama alikuwa na matamanio ya kushinda tuzo wakati akikulia Misri, alisema: "Ni kweli nilitaka kuwa mchezaji wa mpira wa soka na nilitaka kuwa maarufu na kutunza familia yangu, lakini hufikirii mambo makubwa wakati bado uko Misri.

    "Unapokua, unaanza kuona mambo kwa njia tofauti, kuwa na tamaa na unaanza kuwa na mtazamo mpana."

    Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Primia msimu wa 2024-25.

    Mchezaji mwenzake wa Reds Alexis Mac Allister, nahodha wa Manchester United Bruno Fernandes, mshambuliaji wa Newcastle Alexander Isak, mshambuliaji wa Chelsea Cole Palmer na kiungo wa kati wa Arsenal Declan Rice pia walikuwa kwenye orodha ya walioteuliwa.

    Soma zaidi:

  13. Makumi ya wahamiaji wa Afghanistan kutoka Iran wafariki katika ajali ya basi

    Ajali ya trafiki magharibi mwa Afghanistan imeua watu 73, wakiwemo watoto 17, wengi wao wakiwa kwenye basi lililokuwa limewabeba wahamiaji wa Afghanistan waliofukuzwa kutoka Iran, afisa wa Taliban alithibitisha kwa BBC Pashto.

    Basi hilo lililokuwa likielekea Kabul lilishika moto Jumanne usiku baada ya kugongana na lori na pikipiki katika mkoa wa Herat, alisema Ahmadullah Mottaqi, mkurugenzi wa habari na utamaduni wa Taliban huko Herat.

    Kila mtu ndani ya basi aliuawa, pamoja na watu wawili kutoka kwa magari mengine, alisema.

    Katika miezi ya hivi karibuni Iran imeongeza kasi ya kuwafukuza wahamiaji wa Afghanistan wasio na vibali ambao wamekimbia migogoro katika nchi yao.

    "Abiria wote walikuwa wahamiaji ambao walikuwa wamepanda gari huko Islam Qala," msemaji wa gavana wa mkoa Mohammad Yousuf Saeedi aliiambia AFP, akimaanisha mji karibu na mpaka wa Afghanistan na Iran.

    Polisi wa Herat walisema ajali hiyo ilitokea kwa sababu ya "kasi na uzembe" wa dereva wa basi hilo, AFP iliripoti.

    Ajali za trafiki ni za kawaida nchini Afghanistan, ambapo barabara zimeharibiwa na miongo kadhaa ya migogoro na kanuni za kuendesha gari hazitekelezwi inavyostahili.

    Tangu miaka ya 1970, mamilioni ya Waafghanistan wamekimbilia Iran na Pakistan, na mawimbi makubwa wakati wa uvamizi wa Soviet nchini Afghanistan mnamo 1979 na kufuatia kurejea kwa Taliban madarakani mnamo 2021.

    Hii imechangia kuongezeka kwa hisia za chuki dhidi ya Afghanistan nchini Iran, huku wakimbizi wakikabiliwa na ubaguzi wa kimfumo.

    Iran hapo awali ilikuwa imetoa makataa ya Julai kwa Waafghanistan wasio na vibali kuondoka kwa hiari.

  14. Vichwa sita vilivyokatwa vyapatikana barabarani nchini Mexico

    Vichwa sita vilivyokatwa vimepatikana kwenye barabara katikati mwa Mexico, katika eneo ambalo kwa kawaida halihusishwi na vurugu za magenge ya wahalifu.

    Mamlaka za eneo hilo ziligundua tukio hilo la kutisha mapema Jumanne asubuhi kwenye njia inayounganisha majimbo yenye amani ya Puebla na Tlaxcala.

    Polisi hawajatoa sababu za mauaji hayo au kusema ni kundi gani kati ya wahalifu wanaofanya kazi nchini Mexico ambalo huenda lilitekeleza mauaji hayo.

    Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa blanketi iliachwa kwenye eneo la tukio na ujumbe ukitoa onyo kwa magenge yanayopingana na ambayo inaonekana ilitiwa saini na kikundi kiitwacho "La Barredora", ikimaanisha kufagia.

    Ni jina sawa na kundi la wahalifu lisilojulikana sana linaloendesha shughuli zake katika jimbo la magharibi la Guerrero lakini haijabainika iwapo walihusika na shambulio hilo au kwa nini.

    Ofisi ya mwendesha mashtaka wa eneo hilo ilisema vichwa vilivyopatikana Tlaxcala ni vya wanaume na imeanzisha uchunguzi kuhusu mauaji hayo, kulingana na shirika la habari la AFP.

    Pamoja na biashara haramu ya madawa ya kulevya, kuna suala la mafuta ya magendo katika eneo hilo ambayo inazalisha mabilioni ya dola kwa mwaka kwa makundi yanayoendesha shughuli hiyo haramu.

    Mnamo mwezi Juni, miili ya watu 20 - wanne kati yao waliokatwa vichwa - ilipatikana huko Sinaloa, jimbo lililokumbwa na ghasia za magenge.

    Vijana saba wa Mexico pia waliuawa kwa kupigwa risasi kwenye sherehe za Kanisa Katoliki katika jimbo la kati la Guanajuato mnamo mwezi Mei.

    Vurugu kati ya makundi ya wapiganaji zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, huku mamia kwa maelfu ya watu wakiuawa na makumi ya maelfu kupotea tangu serikali ilipoanza kutumia jeshi la Mexico dhidi ya magenge mnamo mwaka 2006.

    Soma zaidi:

  15. Israel inadai kuachiliwa kwa mateka wote wa Gaza huku ikitiliwa shaka iwapo itakubali pendekezo la kusitisha mapigano

    Israel inataka kuachiliwa huru kwa mateka wote 50 wanaoshikiliwa huko Gaza, afisa mmoja wa Israel amesema, na kusababisha wasiwasi iwapo itakubali pendekezo jipya la kusitishwa kwa mapigano kwa siku 60 ambalo Hamas ilikubali Jumatatu.

    Pendekezo hilo, lililotolewa na Qatar na Misri, litashuhudia kuachiliwa kwa karibu nusu ya mateka na "inakaribiana" na pendekezo la Marekani ambalo Israel ilikuwa imekubali hapo awali, kulingana na Qatar.

    Israel haijaikataa waziwazi - lakini msemaji wa serikali ya Israel David Mencer aliiambia BBC kwamba haipendezwi na "mkataba wa nusu nusu".

    "Mambo yamebadilika sasa. Waziri mkuu ameweka mpango wa mustakabali wa Gaza," Mencer alisema.

    Duru za Palestina zilisema pendekezo hilo litashuhudia mateka 10 walio hai na 18 waliokufa wakikabidhiwa Israel huku pande zote zikijadiliana usitishaji wa kudumu wa mapigano na kurejea kwa mateka wengine.

    Israel inaamini kuwa ni mateka 20 tu kati ya 50 ambao bado wako hai baada ya miezi 22 ya vita.

    Baadaye wiki hii, baraza la mawaziri la Israel linatazamiwa kuidhinisha mpango wa jeshi kuukalia kwa mabavu mji wa Gaza, ambapo mashambulizi makali ya Israel tayari yamewafanya maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza nia ya Israel ya kuteka Gaza yote - ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo wakazi wake wengi wa Wapalestina milioni 2.1 wametafuta hifadhi - baada ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano kusambaratika mwezi uliopita.

    Soma zaidi:

  16. Urusi yapuuzilia mbali kufanya mazungumzo na Zelensky

    Ikulu ya Urusi imepuuzilia mbali mazungumzo kuhusu mkutano kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na Volodymyr Zelensky wa Ukraine, huku Donald Trump akitoa wito kwa viongozi hao wawili kukutana ili kujadili kumaliza vita nchini Ukraine.

    Shinikizo la kufanyika kwa mkutano baina ya nchi hizo mbili linakuja baada ya rais wa Marekani kukutana na Putin mjini Alaska wiki iliyopita, na kuwakaribisha viongozi saba wa Ulaya na Zelensky katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu.

    Trump alikiri mzozo huo ulikuwa "vigumu" kusuluhisha na akakubali kuwa inawezekana rais wa Urusi hakutaka kumaliza uhasama.

    "Tutajua kuhusu Rais Putin katika wiki kadhaa zijazo," alisema Jumanne. "Inawezekana kwamba hataki kufanya makubaliano."

    Putin alikabiliwa na "wakati mgumu" ikiwa ndivyo ilivyokuwa, Trump aliongeza, bila kutoa maelezo yoyote.

    Rais wa Urusi siku ya Jumatatu alimwambia Trump kuwa yuko "sawa" na wazo la mazungumzo ya moja kwa moja na Ukraine, lakini siku iliyofuata Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov alipuuzilia mbali ahadi hiyo hatua ambayo tayari haijaeleweka.

    Mkutano wowote ungepaswa kutayarishwa "hatua kwa hatua... kuanzia ngazi ya wataalam na baada ya hapo kupitia hatua zote zinazohitajika", alisema, akirudia maneno ya mara kwa mara ya Urusi.

    Dmitry Polyanskiy, naibu mwakilishi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, aliiambia BBC "hakuna mtu [aliyekataa]" fursa ya mazungumzo ya moja kwa moja, "lakini haipaswi kuwa mkutano kwa ajili tu ya mkutano uwe umefanyika".

    Siku ya Jumanne, iliripotiwa kwamba Putin alikuwa amependekeza kwa Trump kwamba Zelensky anaweza kusafiri hadi Moscow kwa mazungumzo, jambo ambalo Ukraine haikuweza kukubali kamwe.

    Pendekezo hilo linaweza kuwa ni njia ya Urusi ya kuweka chaguo lisilowezekana ambalo Ukraine haiwezi kukubaliana nalo.

    Soma zaidi:

  17. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni taraehe 20/08/2025