Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump akataa kutuma wanajeshi wa Marekani nchini Ukraine kama sehemu ya dhamana ya usalama

Rais wa Marekani Donald Trump ametaa kutuma wanajeshi wa Marekani nchini Ukraine kama sehemu ya dhamana ya usalama iwapo makubaliano ya amani yatafikiwa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma na Lizzy Masinga

  1. Aliyoyasema Trump baada ya mkutano wake na Rais Zelensky

    Muda mfupi uliopita, Donald Trump alizungumza kwenye Fox News, akitoa maoni yake kwa mara ya kwanza tangu rais wa Marekani na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky kukutana katika Ikulu ya White house Jumatatu, pamoja na washirika wengine wa Ulaya.

    Trump anasema anapanga mkutano kati ya kiongozi wa Urusi Vladimir Putin na Zelensky ambao hautamjumuisha hapo awali.

    "Ikiwa hiyo itafanikiwa, basi nitakwenda na kuufunga," anasema.

    Anasema anatumai Zelensky "ataonesha kubadilika" katika mazungumzo.

    Trump anasisitiza kuwa wanajeshi wa Marekani hawatakuwa Ukraine kama sehemu ya dhamana ya usalama inayotafutwa na Kyiv.

    Mataifa ya Ulaya kwa upande mwingine yanaweza kuwa na wanajeshi nchini Ukraine kama sehemu ya makubaliano, Trump anasema.

    Pia anasema washirika wa Ukraine na Nato wanapaswa kuachana na juhudi za kuifanya Ukraine ijiunge na muungano wa usalama na kurejesha Crimea, ambayo Urusi iliikalia mwaka 2014.

    "Mambo yote mawili hayawezekani," anasema.

    Anasema mazungumzo yake na Putin jana haikufanyika mbele ya washirika wa Ulaya na Nato. "Nilidhani hiyo itakuwa ni dharau kwa Rais Putin," anasema.

  2. Wapatanishi wasubiri majibu ya Israel kuhusu pendekezo jipya la kusitisha mapigano Gaza

    Wapatanishi wa Kiarabu wanasubiri jibu rasmi kutoka kwa Israel baada ya Hamas kusema imekubali pendekezo jipya la kusitishwa kwa mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka.

    Mpango huo uliwasilishwa na Qatar na Misri, ambazo zinajaribu kuepusha mashambulizi mapya ya Israel ya kuikalia Gaza kikamilifu.

    Qatar ilisema "inakaribia kufanana" na pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano kwa siku 60, ambapo karibu nusu ya mateka 50 wanaoshikiliwa Gaza, 20 kati yao wanaaminika kuwa hai, watakabidhiwa na pande hizo mbili zitafanya mazungumzo ya usitishaji vita wa kudumu na kurejea kwa wengine.

    Katika siku za hivi karibuni, serikali ya Israel imesema haitakubali tena makubaliano ya sehemu, makubaliano ya kina tu ambayo yatawafanya mateka wote waachiliwe.

    Vyombo vya habari vya ndani vilimnukuu afisa mkuu wa Israel akisema: "Msimamo wa Israel haujabadilika, kuachiliwa kwa mateka wote na kutimiza masharti mengine yaliyoainishwa ya kumaliza vita."

    Baadaye wiki hii, baraza la mawaziri la Israel linatazamiwa kuidhinisha mpango wa jeshi wa kuukalia kwa mabavu mji wa Gaza, ambapo mashambulizi ya Israel tayari yamewafanya maelfu ya watu kukimbia.

    Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alitangaza nia ya Israel ya kuiteka Gaza yote, ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo wakazi wake wengi milioni 2.1 Wapalestina wametafuta hifadhi, baada ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas juu ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuvunjika mwezi uliopita.

    Unaweza kusoma;

  3. Habari za hivi punde, Trump asema Zelensky anahitaji kuwa tayari kubadilika na tabia ya Putin 'itakua nzuri'

    Akizungumza moja kwa moja kwenye televisheni ya Marekani, Fox News Rais wa Marekani Donald Trump amezungumzia uwezekano wa mkutano wa pande tatu utakaowahusisha Vladimir Putin na Volodymyr Zelensky.

    Anasema alimpigia simu Putin jana na anatumai kuwa tabia ya kiongozi huyo wa Urusi "itakuwa nzuri".

    Ikiwa sivyo, "hali itakuwa mbaya", Trump anaongeza.

    Trump anasema anatumai Zelensky "atafanya kile anachopaswa kufanya", lakini anasisitiza kwamba anahitaji "kubadilika" katika mazungumzo pia.

    Trump anaongeza kuwa hatasema Zelensky na Putin watakuwa "marafiki wa karibu"-

  4. Serikali ya Burkina Faso yamfukuza afisa mkuu wa UN kutokana na ripoti ya haki za watoto

    Utawala wa Burkina Faso umemfukuza afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa katika taifa hilo la Afrika Magharibi kutokana na ripoti kuhusu watoto walionaswa katika mzozo wa wanajihadi.

    Carol Flore-Smereczniak alitangazwa kuwa "mtu asiyekubalika'' kwa sababu ya jukumu lake katika kuandaa ripoti iliyotoka Machi.

    Ukijumuisha kipindi cha miaka miwili, utafiti huo ulieleza kwa kina zaidi ya kesi 2,000 za kuripotiwa kuajiriwa kwa watoto, mauaji, unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji, ukiwalaumu waasi wa Kiislamu, wanajeshi wa serikali na vikosi vya ulinzi vya raia.

    Serikali ya kijeshi, iliyoingia madarakani Septemba 2022 na ikiongozwa na Kapteni Ibrahim Traoré, ilisema haikushauriwa na UN, ikisema ripoti hiyo ina madai yasiyo na msingi.

    Haikutaja nyaraka zozote "au maamuzi ya mahakama kuunga mkono madai ya kesi za ukiukaji wa haki dhidi ya watoto zinazohusishwa na wapiganaji hodari wa Burkinabe", taarifa ya serikali ilisema.

    Tangu mwaka wa 2015, waasi wa kijihadi wenye mafungamano na al-Qaeda na kundi la Islamic State wameendesha uasi ambao umeua maelfu ya watu na kuwalazimisha mamilioni kukimbia makazi yao.

    Imesababisha kukosekana kwa utulivu wa kisiasa, na mapinduzi mawili ya kijeshi mwaka wa 2022.

    Capt Traoré alichukua mamlaka akiahidi kukabiliana na hali mbaya ya usalama ndani ya "miezi miwili hadi mitatu".

  5. Macron asema viongozi wa Ulaya wanataka kuhudhuria mkutano na Urusi

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alielezea mkutano wake na Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumatatu kuwa "mzuri sana" na "unaojenga" na akasema yuko tayari kukutana na Vladimir Putin. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema viongozi wa Urusi na Ukraine wanapaswa kukutana katika nchi "isiyoegamia upande wowote" na kusisitiza kwamba viongozi wa Ulaya wanapaswa pia kuhudhuria mkutano huo.

    Baada ya kukutana na viongozi wa Ulaya, Rais wa Marekani Donald Trump alizungumza kwa njia ya simu na rais wa Urusi na kuzungumzia suala hilo.

    Ikulu ya Urusi ilithibitisha kuwa Trump na Putin walizungumza kwa dakika 40 kwa njia ya simu baada ya mkutano wa rais wa Marekani na viongozi wa Ulaya na kujadiliana (kuendelea mazungumzo ya ana kwa ana) na kuboresha nafasi za wale walio katika timu ya mazungumzo ya Ukraine na Urusi.

    Kufuatia mkutano wa Donald Trump na Rais Zelensky na viongozi wa Ulaya katika Ikulu ya White House hapo jana, sasa mwelekeo umeelekezwa kwenye mazungumzo kati ya viongozi wa Ukraine na Urusi na suala la dhamana ya usalama wa Ukraine.

    Waziri Mkuu wa Uingereza anasema dhamana ya usalama, pamoja na mkutano wa pande tatu kati ya Marekani, Urusi na Ukraine, itakuwa "hatua ya kihistoria mbele."

    Viongozi wa Ulaya wameutaja mkutano wa jana mjini Washington kuwa wenye tija na kupongeza juhudi za rais wa Marekani kumaliza vita nchini Ukraine.

    Wanasema kwamba ingawa wana shaka kuhusu nia ya Putin na Kremlin kwa ujumla, dhamana ya usalama itakuwa muhimu kwa Ukraine.

    Tofauti na mkutano uliopita kati ya Donald Trump na Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House, mkutano huu ulifanyika katika hali ya kirafiki na chanya.

    Soma zaidi:

  6. Tahadhari ya mafuriko mabaya katika Pwani ya Mashariki ya Marekani yatolewa

    Watabiri wameonya kuhusu uwezekano wa mafuriko ya kutishia maisha katika Pwani ya Mashariki ya Marekani kutokana na kuongezeka kwa maji yaliyosababishwa na kimbunga Erin.

    Erin, ambayo kwa sasa ni dhoruba ya Aina ya 3, inatarajiwa kukua kwa ukubwa inapoelekea kaskazini katika Bahari ya Atlantiki ya magharibi.

    Ingawa haijatabiriwa kutua, inatabiriwa kuleta mikondo na mawimbi yanayotishia maisha huko Bahamas, Bermuda, Pwani ya Mashariki ya Marekani na pwani ya Atlantiki ya Canada.

    Onyo la dhoruba ya kitropiki linatumika kwenye visiwa vya Turks na Caicos na kusini mashariki mwa Bahamas na karibu na pwani ya North Carolina, saa ya mawimbi ya dhoruba imetangazwa.

    Kitovu cha dhoruba hiyo kinatabiriwa kupita mashariki mwa Bahamas siku ya Jumanne, kulingana na Kituo cha Kitaifa cha Kimbunga chenye makao yake nchini Marekani.

    Siku ya Jumatano na Alhamisi, inatabiriwa kuelekea kaskazini kati ya Bermuda na Pwani ya Mashariki ya Marekani.

    Unaweza kusoma;

  7. Serikali ya Uingereza yatakiwa kuwazuia watoto kutumia VPN kutazama ponografia

    Serikali inahitaji kuwazuia watoto kutumia mitandao ya binafsi ya (VPNs) ili kukwepa ukaguzi wa umri kwenye tovuti za ponografia, kamishna wa masuala ya watoto nchini Uingereza alisema.

    Dame Rachel de Souza aliiambia BBC Newsnight "ni mwanya kabisa unaohitaji kufungwa" na akataka uthibitisho wa umri kwenye VPN utumike.

    VPN zinaweza kuficha eneo lako mtandaoni, kukuruhusu kutumia intaneti kana kwamba uko katika nchi nyingine.

    Inamaanisha kuwa zinaweza kutumiwa kukwepa hitaji la kisheria ya Usalama Mtandaoni, ambayo iliamuru majukwaa yenye maudhui fulani ya watu wazima kuanza kuangalia umri wa watumiaji.

    Msemaji wa serikali alisema VPN ni zana za kisheria kwa watu wazima na hakuna mipango ya kuzipiga marufuku.

    Pendekezo la kamishna wa watoto limejumuishwa katika ripoti mpya, ambayo iligundua idadi ya watoto wanaosema kuwa wameona ponografia mtandaoni imeongezeka katika miaka miwili iliyopita.

    Mwezi uliopita VPN zilikuwa programu zilizopakuliwa zaidi kwenye Duka la Programu la Apple nchini Uingereza baada ya tovuti kama vile PornHub, Reddit na X kuanza kuhitaji uthibitishaji wa umri.

    Mitandao pepe ya faragha huunganisha watumiaji kwenye tovuti kwa kutumia seva ya mbali na kuficha anwani zao halisi za IP na eneo, kumaanisha kwamba wanaweza kukwepa vizuizi kwenye tovuti au maudhui fulani.

    Dame Rachel aliiambia BBC Newsnight: "Bila shaka, tunahitaji uthibitisho wa umri kwenye VPN, ni mwanya kabisa unaohitaji kufungwa na hilo ni mojawapo ya mapendekezo yangu makuu."

    Anataka mawaziri kuchunguza kuhitaji VPN "kutekeleza uhakikisho wa umri unaofaa sana ili kuwazuia watumiaji wa umri mdogo kupata maudhui ya ponografia."

    Unaweza kusoma;

  8. Mtoto wa binti mfalme wa Norway ashtakiwa kwa ubakaji na unyanyasaji

    Mtoto wa kwanza wa binti wa mfalme wa Norway ameshtakiwa kwa makosa 32, ikiwa ni pamoja na makosa manne ya ubakaji, mwendesha mashtaka anasema.

    Mashtaka dhidi ya Marius Borg Høiby mwenye miaka 28, ni pamoja na unyanyasaji wa mpenzi wa zamani na ukiukaji wa amri za zuio dhidi ya mpenzi mwingine wa zamani.

    Alizaliwa kutokana na uhusiano kabla ya Binti Mfalme Mette-Marit kuolewa na Mwana Mfalme Haakon, ambaye ni mfalme wa baadaye wa Norway.

    Bw Høiby amekanusha mashtaka makubwa zaidi dhidi yake, lakini anapanga kukiri mashtaka machache kesi itakapoanza, wakili wake Petar Sekulic aliliambia shirika la habari la Reuters.

    Anaweza kufungwa jela miaka 10 iwapo atapatikana na hatia ya mashtaka mazito zaidi.

    Pia ameshtakiwa kwa kurekodi sehemu za siri za wanawake kadhaa bila ya wao kujua au ridhaa, mwendesha mashtaka Sturla Henriksbø aliwaambia waandishi wa habari.

    "Hakubaliani na madai kuhusu ubakaji na unyanyasaji wa nyumbani," Bw Sekulic alisema kuhusu mteja wake, kulingana na Reuters.

    Bw Høiby, ambaye hana cheo cha kifalme au majukumu rasmi, alikamatwa mara tatu tofauti mwaka jana, mwezi Agosti, Septemba na Novemba. Alikuwa chini ya uchunguzi tangu kukamatwa kwake Agosti kwa tuhuma za kushambulia.

  9. Baraza la Umoja wa Afrika laomba Sudan Kusini iondolewe vikwazo

    Baraza la Amani na Usalama la Jumuiya ya Afrika limetaka Baraza la Usalama la UN mnamo tarehe 15 Agosti, kuanza taratibu

    kuondoa marufuku ya silaha kwa Sudan Kusini ili kusaidia nchi hiyo kushughulikia changamoto zake za usalama, kituo cha Eye Radio kimesema.

    Baraza hilo lilisema hatua hiyo itawezesha Sudan Kusini "kudumisha umoja na nguvukazi muhimu", kituo hicho kiliripoti.

    "Pia lilitoa wito kwa washirika wa kimataifa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya nchi ili kuwezesha utekelezaji wa haraka wa makubaliano ya msingi ya [amani ya 2018]", Redio hiyo ilisema.

    Baraza hilo pia lilielezea wasiwasi juu ya kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini humo, vurugu kati ya jamii, ukosefu mkubwa wa usalama wa chakula, uhamishaji wa ndani na ufikiaji mdogo wa misaada ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathirika na vita.

    Lilitaka mashirika ya misaada na Sudan Kusini kushughulikia maswala hayo.

    Pia lilionyesha wasiwasi juu ya "kuwekwa kizuizini kwa makamu wa rais wa kwanza Riek Machar na mvutano wa kisiasa uliopo", Eye Radio iliripoti.

    Baraza hilo lilitoa wito Machar kuachiliwa huru mara moja na bila masharti, pamoja na kutatuliwa kwa mgogoro wa kisiasa nchini.

    Soma zaidi:

  10. Uganda yatinga robo fainali ya kwanza katika michuano ya CHAN 2024

    Uganda iliweka historia na kutinga robo fainali ya Mashindano ya Mataifa ya Afrika CHAN 2024, baada ya kutoka sare ya 3-3 na Afrika Kusini kwenye uwanja wa Kitaifa wa Mandela huko Kampala jana usiku.

    Matokeo hayo, pamoja na sare ya Algeria na Niger katika kundi C, yalihakikishia Uganda Cranes ushindi wa kuongoza kundi hilo kwa mara ya kwanza katika historia yao ya Chan.

    Uganda ilihitaji sare tu kuimarisha nafasi yao na ilionekana kuwa tayari kuongoza wakati Jude Ssemugabi alipowaweka mbele katika dakika ya 31, akipiga mkwaju maridadi kabisa baada ya kupata usaidizi kutoka kwa Patrick Kakande.

    Uganda Cranes waliendelea na uongozi wao hadi muda wa mapumziko na wakaonekana kudhibiti mpira, lakini kile kilichofuata baada ya mapumziko kilikuwa ni mashindano ya kufa mtu hadi kipenga cha mwisho kilipopigwa.

    Bafana Bafana iliamka katika kipindi cha pili na kunga’ng’ana hadi dakika za mwisho wakitoka sare ya 3 kwa 3.

    Matokeo hayo yaliiweka Uganda juu ya Kundi C na alama saba, moja mbele ya Algeria kwa sita. Afrika Kusini pia ilimaliza kwa alama sita lakini inatofauti ya magoli, wakati Guinea ikimaliza kwa alama nne na Niger alama mbili zikitoka kwenye mashindano.

  11. Zaidi ya raia 50 wauawa na waasi wa ADF huko DR Congo - MONUSCO

    Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaosaidia Kuleta Utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO) umelaani vikali mashambulizi yaliyofanywa na kikundi cha waasi wa Allies Democratic (ADF) kati ya 9 na 16 Agosti 2025, katika maeneo kadhaa ya Beni na Lubero, katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

    MONUSCO imesema mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu takriban 52 na huenda idadi hiyo ikaongezeka.

    MONUSCO imeongeza kuwa vurugu hizo ziliambatana na matukio ya utekaji nyara, uporaji, uchomaji wa majumba na magari na uharibifu wa mali za raia ambao tayari wanakabiliana na mgogoro wa kibidamanu.

    “Mashambulizi hayo yaliyolenga raia ambayo ni pamoja na mauaji yaliyotekelezwa usiku wa tarehe 26 hadi 27 Julai huko Komanda eneo la Irumu, Ituri, hayakubaliki na ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na haki za binadamu,’’ taarifa ya MONUSCO ilisema.

    Ujumbe huo umetoa wito kwa serikali ya DR Congo kufanya uchunguzi wa kina na kuwajibisha waliohusika na mauaji ya raia.

    MONUSCO imetoa hakikisho la kuendelea kuunga mkono serikali ya Congo na jamii za wenyeji kuzuia ghasia zaidi, kulinda raia pamoja na kuchangia urejeshaji wa utulivu katika maeneo yalioathirika na vita.

    Soma zaidi:

  12. Bobi Wine achukua fomu ya urais kwa chama cha (NUP) Uganda

    Kiongozi wa chama cha National Unity Platform (NUP) Robert Sentamu Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, hapo jana alichukuliwa fomu ya urais ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Januari, 2026 nchini Uganda.

    Kiongozi wa upinzani bungeni Joel Ssenyonyi , Katibu Mkuu wa chama David Rubongoya na Msimamizi wa Hazina ya Kitaifa ya chama Benjamin Katana walichukua fomu kwa niaba ya Kyagulanyi kutoka makao makuu ya Tume ya Uchaguzi.

    Chama cha NUP kilisema kitafanya kampeni zake chini ya kauli mbiu, ‘’Uganda Mpya Sasa’’ na kuongeza kuwa hilo litafikiwa kwa upigaji kura wa kiwango cha juu.

    ‘’Uganda mpya tunayozungumzia ni nchi ambayo watu wote wakuwa wanakwenda kwenye hospitali za umma na kupata matibabu mazuri, barabara zetu ziwe katika hali nzuri, mahali ambapo watoto wetu wanakwenda shule kupata elimu bora,’’ Ssenyonyi aliambia vyombo vya habari.

    Hii itakuwa mara ya pili kwa Robert Kyagulanyi kugombea urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni.

    Mwaka 2021, alimaliza kinyang’anyiro hicho katika nafasi ya pili kwa kupata kura 3,475,398 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Marekani yabatilisha zaidi ya viza 6,000 za wanafunzi

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imebatilisha zaidi ya viza 6,000 za wanafunzi wa kimataifa kwa sababu ya ukiukaji wa sheria za Marekani na kupitisha muda wa kukaa nchini humo, idara hiyo iliambia BBC.

    Wizara hiyo ilisema idadi " kubwa" ya ukiukaji huo ni mashambulizi, kuendesha gari ukiwa umekunywa kileo, wizi na "kuunga mkono ugaidi".

    Hatua hiyo inajiri huku utawala wa Trump ukiendelea na msako mkali dhidi ya wahamiaji na wanafunzi wa kimataifa.

    Ingawa wizara hiyo haikufafanua walichomaanisha na "kuunga mkono ugaidi", utawala wa Trump umewalenga baadhi ya wanafunzi ambao wameandamana kuunga mkono Palestina, wakisema walikuwa wameonyesha tabia ya chuki.

    Soma zaidi:

  14. Kanisa la miaka 113 kuhamishwa hadi katikati ya jiji la Uswidi

    Kanisa la kihistoria ambalo limekuwepo kwa miaka 113 lililo hatarini kuzama kutokana na mtikiso wa chini ya ardhi linakaribia kuhamishwa lote jinsi lilivyo- kwa mwendo wa kilomita 5 (maili 3) kando ya barabara kaskazini mwa Uswidi.

    Kanisa hilo lenye muundo wa mbao nyekundu huko Kiruna tangu 1912 umeinuliwa kwenye majukwaa makubwa kabla ya kuhamishwa katikati mwa jiji.

    Litasafirishwa kwa kasi ya 500m kwa saa, na safari hiyo inatarajiwa kuchukua siku mbili.

    Kijiji cha kale kulipo kanisa hilo, kiko hatarini kutokana na ufa uliojitokeza ardhini baada ya zaidi ya karne ya uchimbaji wa madini ya chuma.

    Hatua ya kuhamisha kanisa hilo ni moja ya matukio ya kuvutia zaidi na kipekee ya uhamishaji wa majengo makubwa huko Kiruna, ambayo iko kilomita 145 kaskazini mwa Mzingo wa Aktiki.

    "Tumefanya matayarisho kabambe," asema mtu anayesimamia uhamishaji huo, meneja wa mradi Stefan Holmblad Johansson.

    "Ni tukio la kihistoria, operesheni kubwa sana na tata na hakuna sababu ya kutokea kwa makosa na kila kitu kiko chini ya udhibiti."

    Kufikia katikati ya miaka ya 2010, majengo mengine huko Kiruna tayari yalikuwa yakihamishwa hadi kwenye ardhi salama.

    Mengi yalikuwa yamebomolewa na kujengwa upya, lakini baadhi ya majengo ya kihistoria yalihamishwa kama yalivyo.

    Pia unaweza kusoma:

  15. Hamas yakubali pendekezo la kusitisha mapigano Gaza – chanzo chasema

    Hamas imekubali pendekezo la hivi karibuni kutoka kwa wapatanishi wa eneo la makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka na Israel, chanzo kimoja katika kundi linalojihami la Palestina kimeiambia BBC.

    Pendekezo hilo kutoka Misri na Qatar linasemekana kuegemea kwenye mfumo uliowekwa na mjumbe wa Marekani Steve Witkoff mwezi Juni.

    Linajumuisha Hamas kuwaachilia huru karibu nusu ya mateka 50 waliosalia wa Israel - 20 kati yao wanaaminika kuwa hai - katika makundi mawili wakati wa usitishaji mapigano wa siku 60 wa awali. Pia kutakuwa na mazungumzo ya kusitisha mapigano ya kudumu.

    Haijulikani jibu la Israel litakuwa nini kwani ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ilisema wiki iliyopita kwamba itakubali tu makubaliano ikiwa "mateka wote wataachiliwa kwa wakati mmoja".

    Katika video iliyotolewa baada ya ripoti za idhini ya Hamas kuibuka, Netanyahu hakutoa maoni moja kwa moja lakini alisema kwamba "kutoka kwao unaweza kupata hisia moja - Hamas iko chini ya shinikizo kubwa."

    Mkuu wa majeshi ya Israel, Lt Jenerali Eyal Zamir, wakati huo huo alisema ilikuwa katika hatua ya mabadiliko katika vita vilivyodumu kwa miezi 22, "ikilenga kuimarisha mashambulizi dhidi ya Hamas katika mji wa Gaza".

    Soma zaidi:

  16. Zelensky asema yuko tayari kwa mazungumzo ya Putin huku Ulaya ikifurahishwa na hakikisho la usalama wa Trump

    Rais Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kwa mazungumzo ya Putin huku Ulaya ikifurahishwa na hakikisho la usalama wa Trump.

    Zelensky amesema kuwa hakuna tarehe iliyothibitishwa kwa mazungumzo yoyote yajayo kati yake na Putin na kuwa "wamethibitisha tu baada ya mkutano huu wenye tija na rais," kwamba mazungumzo yataendelea kati ya Ukraine na Urusi.

    Zelensky alisema "imethibitishwa kwamba wako tayari kwa mkutano wa pande tatu," lakini akaongeza kuwa "ikiwa Urusi ilipendekeza kwa rais wa Marekani mkutano wa kidiplomasia kati ya pande zinazowakilisha nchi mbili, pia tutaona matokeo yake".

    "Ukraine haitakuwa kikwazo cha kufikia amani," alisema.

    Hayo yanajiri baada ya Trump kumpigia simu Putin wakati wa mkutano wa White House ukiendelea.

    "Wakati wa kuhitimisha mikutano hiyo, nilimpigia simu Rais Putin, na kuanza maandalizi ya mkutano katika eneo litakaloamuliwa kati ya marais Putin na Zelenskyy," aliandika.

    "Baada ya mkutano huo kufanyika, tutakuwa na mkutano wa pande tatu, ambao utakuwa Marais wawili, pamoja na mimi mwenyewe."

    Trump pia alisema dhamana ya usalama kwa Ukraine ilijadiliwa wakati wa mazungumzo ya leo, ambayo alisema "itatolewa na Nchi mbalimbali za Ulaya, kwa uratibu na Marekani".

    Soma zaidi:

  17. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni taraehe 19/08/2025