Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, nchi za Kiarabu zina mpango gani wa kuijenga Gaza?
- Author, Yasmine Shahine
- Nafasi, BBC News Arabic
- Akiripoti kutoka, Cairo
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Misri na nchi kadhaa za Kiarabu zinafanyia kazi mipango ya kuijenga upya Gaza, kuhakikisha Wapalestina wanasalia katika eneo hilo bila ya kuhama na kuanzisha utawala mpya katika Ukanda huo bila ya kuwashirikisha Hamas.
Mipango hiyo ni kujibu mapendekezo ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kuwahamishia Wagaza na kuwapeleka Misri, Jordan na nchi nyingine, pamoja na kuchukua udhibiti wa Gaza, na kuigeuza kuwa kile alichokiita "eneo la mapumziko la Mashariki ya Kati."
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa mapendekezo manne yameandaliwa kuhusu Gaza, lakini pendekezo la Misri kwa sasa linaonekana kuwa ndio msingi wa juhudi za nchi za Kiarabu ili kutoa njia mbadala kwa mpango wa Trump.
Kulingana na vyanzo vya BBC, Cairo inakaribia kukamilisha mpango huo, unaohusisha kusafisha vifusi, kujenga upya Gaza, kuamua jinsi Wapalestina watakavyo ishi katika kipindi hiki na utaratibu wa utawala baada ya vita. Hata hivyo, mustakabali wa makundi yenye silaha huko Gaza, hususan Hamas na Islamic Jihad, bado unajadiliwa.
Misri inasema mpango huo utaandaliwa kwa ushirikiano na utawala wa Marekani. Vyanzo kutoka Misri pia vimeiambia BBC, Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Ulaya (EU) watashiriki katika mpango huo.
Misri inashauriana na nchi za Kiarabu, zikiwemo Jordan na Saudi Arabia, kuhusu mpango huo kuelekea mkutano wa kikanda mjini Riyadh tarehe 21 Februari, ambao unaweza kujumuisha pia ushiriki wa Mamlaka ya Palestina.
Mkutano huo unatarajiwa kufuatiwa na mkutano wa dharura wa nchi za Kiarabu jijini Cairo, ambao awali ulikuwa umepangwa kufanyika tarehe 27 Februari kabla ya kuahirishwa.
Sura ya mpango wenyewe
Chanzo kutoka Misri kimeiambia BBC, mashauriano ya nchi za Kiarabu tayari yameanza kutayarisha mkutano ujao wa ujenzi wa Gaza na ushiriki mpana wa Ulaya.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa mpango wa Misri unalenga zaidi katika kuijenga upya Gaza na kuugawa Ukanda huo katika maeneo matatu, kila eneo likiwa na kambi kubwa 20 kwa ajili ya wakazi kuishi, na kutoa mahitaji ya kimsingi kama maji na umeme.
Kulingana na mpango huo, maelfu ya nyumba ndogo ndogo na mahema vitapelekwa katika maeneo salama kwa makazi kwa muda wa miezi sita, sambamba na kuondolewa kwa vifusi.
Mpango huo pia utasisitiza ulazima wa kuruhusu mafuta na vifaa vya ujenzi kuingia Gaza.
Kulingana na mpango wa Misri, ujenzi mpya utafadhiliwa na wafadhili wa nchi za Kiarabu na kimataifa, na karibu makampuni 50 ya kimataifa yaliyobobea katika ujenzi yatajenga makazi ndani ya miezi 18 katika maeneo matatu yaliyopendekezwa ya Gaza.
Na ufadhili huo utasimamiwa na kamati inayojumuisha wawakilishi wa nchi za Kiarabu na kimataifa.
Pendekezo hilo pia linajumuisha kuundwa kwa eneo salama na kizuizi cha kuzuia uchimbaji wa mahandaki kwenye mpaka wa Gaza na Misri.
Hata hivyo, siku ya Jumamosi Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza, hataruhusu nyumba ndogo ndogo na vifaa vya ujenzi kuingia katika Ukanda wa Gaza, akitaja wasiwasi wa usalama licha ya kwamba hiki ni kifungu cha makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano.
Mustakabali wa Hamas
Chanzo kutoka Misri kimeiambia BBC kuwa suala muhimu zaidi lililobakia ni mustakabali wa Hamas na makundi mengine yenye silaha katika Ukanda wa Gaza.
Chanzo hicho kinaeleza, pendekezo moja katika mpango wa Cairo linahusisha makundi hayo kupokonywa silaha mara tu taifa la Palestina litakapotangazwa ndani ya mipaka iliyokuwepo kabla ya Vita vya Siku Sita.
Jerusalem Mashariki itakuwa mji mkuu wa taifa hilo na kutakuwa na eneo salama - eneo ambalo bado halijaamuliwa - ili kuihakikishia Israeli kwamba hakuna vitisho vitatoka Gaza.
Pendekezo hilo pia linahusisha kuunda kamati ya Wapalestina itakayosimamia Gaza bila ya ushiriki Hamas. Majeshi ya nchi za Kiarabu na kimataifa yataisaidia kwa muda kamati hiyo katika kusimamia Ukanda wa Gaza.
Hamas hapo awali ilieleza kuwa iko tayari kuachia utawala wa Gaza kwa kamati ya kitaifa lakini ilitaka kuwa na jukumu la kuchagua wanachama wake na haitokubali kutumwa kwa vikosi vyovyote vya ardhini bila ya ridhaa yake.
Chanzo kutoka Misri pia kilisisitiza kuwa, kwa mujibu wa mpango huo, nchi za Kiarabu zitaunga mkono Mamlaka ya Palestina katika kutoa mafunzo kwa maafisa wake kwa ushirikiano na EU.
Vipi kuhusu mpango wa Trump?
Rais wa Marekani amerudia kueleza mpango wake wa kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza, ili kuibadilisha ardhi hiyo kuwa eneo la uwekezaji wa kitalii na kwa manufaa ya Wapalestina wenyewe kwa vile hawataishi tena kwenye vifusi. Trump alitishia kusitisha misaada kwa Misri na Jordan ikiwa hazitawachukua Wapalestina.
Dan Perry, mhariri wa zamani wa Mashariki ya Kati wa Shirika la Habari la Associated Press mjini Cairo, aliandika makala katika gazeti la Jerusalem Post la Israel, mpango wa Trump wa kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza ni kuzishinikiza nchi za Kiarabu na Wapalestina kuiondoa Hamas madarakani. Pia analenga kusitisha msaada wa kifedha kwa Hamas kutoka nchi za Kiarabu, haswa Qatar.
Baada ya mkutano wa hivi karibuni mjini Washington kati ya Trump na Mfalme Abdullah II wa Jordan, msemaji wa rais wa Marekani, Caroline Levitt, alisema Mfalme Abdullah amemweleza wazi Trump kwamba anapendelea Wapalestina wabaki Gaza wakati wa mchakato wa ujenzi. Lakini Trump, bado anapendelea kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza.
Perry anaamini Trump anaweza kukubali Wapalestina kubaki Gaza, kwa kutoa mabilioni ya dola kwa ajili ya ujenzi wa Gaza na kuondolewa kwa Hamas.
Perry pia anaamini serikali ya kiraia inaweza kuundwa huko Gaza, inayohusisha Mamlaka ya Palestina katika Ukingo wa Magharibi, kwa kushirikiana na Misri na nchi za Ghuba.
Ulimwengu wa Kiarabu
Dr. Mubarak Al-Ati, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Saudi Arabia, anaamini ushiriki wowote wa Marekani utazingatia maslahi yake makubwa katika eneo hilo, hasa katika nchi ya Saudi Arabia na Misri.
Ameongeza kuwa mahusiano binafsi kati ya watawala wa Misri, Marekani na Saudi Arabia yatawezesha kupatikana muafaka hasa katika ziara ijayo ya Trump nchini Saudi Arabia ambayo itachagiza uhusiano wa siku za usoni wa nchi za Kiarabu na Marekani.
Dk Hassan Mneimneh, mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Washington, anaamini ikiwa Trump atapunguza misaada ya kijeshi na kiuchumi kwa Misri na Jordan, nchi hizi zinapaswa kujibu pia.
Kwa mfano, Riyadh inapaswa kusitisha uwekezaji wake nchini Marekani na hivyo kufungua mlango wa ushirikiano wa kiuchumi na China, Russia, Umoja wa Ulaya(EU), Afrika na Amerika Kusini.
Ombi la Marekani kwa Saudi Arabia la kurejesha uhusiano na Israel, linatumiwa kama mbinu ya mazungumzo ya Riyadh ili kushinikiza kuanzishwa kwa taifa la Palestina katika mipaka ya 1967.
Chanzo kutoka Misri ambacho hakikutaka kutajwa jina kilibainisha kuwa dokezo la hivi karibuni la Cairo la kufuta mkataba wa amani wa Camp David na Israel, uliotiwa saini mwaka 1979, linaweza pia kuwa na ufanisi dhidi ya Washington ikiwa Trump atakataa mpango wowote wa siku za usoni kutoka nchi za Kiarabu.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi