CHAN 2024: Tanzania yafuzu robo fainali kibabe na kwa rekodi

Muda wa kusoma: Dakika 1

Timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, imeandika historia mpya baada ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya CHAN 2024 kwa mara ya kwanza.

Mafanikio haya yametokana na ushindi wa 2-1 dhidi ya Madagascar, uliopatikana leo, Jumamosi, Agosti 9, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ushindi huu ni wa tatu mfululizo kwa Taifa Stars. Walianza kwa kuwachapa Burkina Faso 2-0, kisha wakaibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Mauritania, na kumalizia na ushindi huu muhimu dhidi ya Madagascar.

Matokeo haya yanaifanya Stars ifikishe pointi tisa (9), na hivyo kuongoza Kundi B, lenye timu za Madagascar, Burkina Faso, Jamhuri ya Afrika ya Kati, na Mauritania.Pia imekuwa timu ya kwanza kufuzu robo fainali katika mashindano yam waka huu.

Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, alikuwa shujaa wa mchezo, akifunga mabao yote mawili yaliyoipa Stars ushindi. Kwa mabao hayo, Mzize ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa tatu kufunga mabao mawili au zaidi katika mchezo mmoja wa CHAN, akiungana na Given Singuluma (2009) na Chisom Chikatara (2016).

Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Mauritania ilirejesha matumaini yake ya kusonga mbele baada ya kuichapa Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa bao 1-0. Bao la ushindi lilifungwa na Ahmed El Moctar dakika ya 9, na kuiwezesha Mauritania kujipatia pointi zake za kwanza kwenye michuano hii.