Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
CHAN 2024: Tanzania yaanza kwa kishindo, yaichapa Burkina Faso 2-0
Timu ya Taifa ya Tanzania, maarufu kama Taifa Stars, imeanza rasmi kampeni yake ya michuano ya TotalEnergies CAF African Nations Championship (CHAN) PAMOJA 2024 kwa ushindi wa nguvu wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso.
Mchezo huo wa kundi B ulipigwa usiku wa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mbele ya umati wa mashabiki waliokuwa wakishangilia kwa sauti kubwa, Taifa Stars walitawala sehemu kubwa ya mchezo huo. Ushindi huu umekuwa wa kihistoria kwa Tanzania, kwani ndio mara ya kwanza kuwahi kushinda mchezo wa ufunguzi wa CHAN, baada ya kupoteza michezo miwili iliyopita katika mashindano mawili yaliyopita.
Bao la kwanza lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Abdul Sopu muda mfupi kabla ya mapumziko. Penalti hiyo ilifuatia baada ya Clement Mzize kufanyiwa madhambi ndani ya boksi. Katika kipindi cha pili, beki Mohamed Hussein alihakikisha ushindi kwa Taifa Stars kwa kufunga bao la kichwa chenye nguvu katika dakika ya 71, na kuwaleta mashabiki katika shamrashamra.
Matokeo haya yanaiweka Tanzania katika nafasi nzuri kwenye kundi gumu linalojumuisha pia Madagascar, Mauritania na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Kwa upande wa Burkina Faso, safari yao ya kutafuta ushindi wa kwanza katika mchezo wa ufunguzi wa CHAN bado inaendelea.
Historia ya pamoja ya Afrika Mashariki
Michuano hii ya CHAN inaweka historia mpya ya soka barani Afrika, kwani ni mara ya kwanza kwa nchi tatu; Kenya, Tanzania na Uganda kuandaa kwa pamoja. Michuano hiyo iliyofunguliwa rasmi Jumamosi, Agosti 2, jijini Dar es Salaam, itashirikisha timu 19 na itaendelea hadi Agosti 30.
Lengo kuu la CHAN ni kutoa jukwaa la kipekee kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani pekee kuonyesha vipaji vyao. Hii inawapa fursa ya kujulikana barani Afrika na kwa wasajili wa kimataifa, huku ikisherehekea msingi wa soka la Afrika.
Ratiba ya Baadhi ya Michezo ya Awali
Jumapili, Agosti 3: Jiji la Nairobi litakuwa na michezo miwili. Kenya wataivaa DR Congo katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi, huku Morocco wakipambana na Angola kwenye Uwanja wa Nyayo. Jioni hiyo, Madagasca watamenyana na Mauritania jijini Dar es Salaam.
Jumatatu, Agosti 4: Michezo itahamia Kampala. Uganda watakutana na Algeria kwenye Uwanja wa Mandela, mchezo utakaotanguliwa na pambano kati ya Niger na Guinea katika uwanja huo huo.
Jumanne, Agosti 5: Mabingwa watetezi Senegal wataanza kampeni yao dhidi ya Nigeria huko Zanzibar.