Maandalizi, Fursa na Changamoto ya AFCON Afrika Mashariki

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili

Baada ya mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika - AFCON yatakayo fanyika Ivory Coast mwaka 2024, yatafuata yatakayo shindaniwa Morocco mwaka 2025 na kisha Kenya, Uganda na Tanzania itakuwa zamu yao kuwa wenyeji 2027.

Nchi za Afrika Mashariki zimeshiriki AFCON mara nyingi, Kenya mara sita, mara yao ya kwanza ni 1972. Uganda mara saba, mara ya mwanzo ni 1962 na Tanzania mara tatu (ikiwemo ya kwenda Ivory Coast). Lakini itakuwa mara ya kwanza kuwa wenyeji wa mashindano hayo makubwa zaidi ya mpira barani Afrika.

Katika tovuti ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), inaeleza mataifa wenyeji wanafuzu moja kwa moja kucheza mashindano ya kombe la Afrika. Kwa muktadha huo nchi zote tatu zitaingia kwenye AFCON ya 2027.

Maandalizi

Ili taifa likidhi vigezo vya kuwa mwenyeji, linapaswa kuwa na angalau viwanja sita; viwili vinavyoweza kuchukua mashabiki 40,000, vingine viwili vya kubeba mashabiki 20,000 na viwili vitakavyo chukua takribani mashabiki 15,000.

Lakini hadi sasa Kenya na Tanzania zina kiwanja kimoja kimoja vinavyokidhi ubora wa kimataifa. Wakati Uganda haina hata kimoja.

Kushindwa kutimiza vigezo ndiko kuliko igharimu Kenya na kupokonywa uenyeji wa AFCON mwaka 1996 na kupewa Afrika Kusini, ikapokonywa tena uenyeji wa mashindano ya CHAN mwaka 2018.

Kwa mujibu wa Waziri wa Michezo wa nchi hiyo Ababu Namwamba ameeleza kwamba ukarabati mkubwa utafanyika wa viwanja vitatu - cha Nyayo, Moi, Kipchoge Keino na kiwanja cha nne kitakuwa kipya kitakacho jengwa.

Mara baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuzipa zabuni ya pamoja Tanzania, Kenya na Uganda haki ya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa agizo:

Agizo kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha usimamizi wa maandalizi ya michuano ya AFCON 2027, ikiwa ni pamoja na kusimamia ujenzi wa viwanja vya michezo katika mikoa ya Dodoma na Arusha.

Ujenzi huo utakwenda sanjari na kufanyiwa maboresho kiwanja cha Amani, Zanzibar na kile cha Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Kwa kuzingatia hilo, ikifika 2027 kutakuwa na jumla ya viwanja vinne nchini Tanzania viko tayari kwa ajili ya timu kupimana nguvu.

Kwa upande wa Uganda rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la nchi hiyo (FUFA), Moses Hassim Magogo, ameweka wazi - kutakuwa na maboresho ya uwanja wa Nelson Mandela huko Namboole katika mji mkuu wa Kampala, kiwanja kingine ni Akii Bua kipo Lira na kuna pendekezo la ujenzi wa kiwanja kipya huko Hoima.

Alipoulizwa na BBC, mchambuzi wa soka kutoka Tanzania, Salama Ngale; Je, matayarisho yanaridhisha kwamba Afrika Mashariki iko tayari sasa kuandaa mashindano makubwa ya soka barani Afrika?

"Kwa mipango ambayo imeelezwa, inaonekana maandalizi yanakwenda vizuri kwa viwanja kujengwa na kuboreshwa. Miundombinu mengine kama usafiri wa ndege kutoka Tanzania kwenda Uganda ama Kenya, ipo na inafanya kazi vizuri."

Lakini Ngale ametahadharisha, "nchi hizi hazitakiwi kubweteka kwa sababu 2027 ni mbali kwa kuhesabu miaka na kwa maneno, ila ni karibu sana kwa kuzingatia maandalizi yanayohitajika."

Fursa

Kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya kimichezo ni gharama kubwa kwa nchi mwenyeji, na hii pengine ndio sababu ya nchi tatu kuamua kuubeba mzigo huu kwa pamoja. Yumkini ni jambo lisilowezekana kwa nchi mojamoja kuandaa mashindano haya kwa kuzingatia hali za nchi hizi.

Ukiweka hesabu za gharama za maandalizi pembeni, pia zipo faida zitakazo onekana wakati mashindano yakiendelea; wadhamini, mashabiki na watalii hawa wote wataleta neema. Pia, kwa biashara ya usafiri, hoteli na mikahawa itanufaika. Vilevile pesa za kigeni zitaongezeka, kutakuwa na mapato kwa makampuni ya ndani na sekta ya utalii.

Faida nyingine zitaendelea kuwepo hata baada ya mashindano kumaliza, wageni kuondoka na timu kufungasha virago vyao - ile miundombinu ya barabara, viwanja vya soka, usafiri - vitaendelea kuwanufaisha raia wa nchi hizo.

"Kuandaa mashindano kutaleta faida kwa nchi kujitangaza na kuonesha vivutio hasa vya utalii, wageni watakuwa na hamu ya kuja tena mara nyingine. Kwa Tanzania visiwani Zanzibar ni eneo zuri kwa utalii, Tanzania bara pia kuna mlima Kilimanjaro na mbuga za wanyama," anasema Ngale.

Mbali na faida za kiuchumi, mchambuzi wa michezo kutoka Kenya, Diamond Oksimba anaamini mashindano haya yatadumisha ule udugu miongoni mwa watu wa Afrika Mashariki.

Changamoto

Uchaguzi mkuu wa Kenya unatazamiwa kufanyika Agosti 2027. Kwa sababu ya historia ya vurugu za kisiasa katika nchi hiyo, Oksimba anaitazama hiyo kama changamoto kwa Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla.

"Kitu kinachonitia wasiwasi ni uchaguzi mkuu 2027. Taifa la Kenya kukiwa na uchaguzi na vurugu pia hutokea. Hivyo ni muhimu kwa wadau wa soka na wanasiasa hasa Kenya wahakikishe kuna amani ili kila kitu kiende sawa."

Mbali ya hilo, ufisadi ni tatizo sugu barani Afrika. Ripoti ya mwezi Januari mwaka huu ya shirika linalofuatilia ufisadi duniani, Transparency International - inaonyesha ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara umepata alama 32 chini ya 100. Huku nchi 44 kati ya 49 zilizo tathminiwa zina alama chini ya 50.

Ufisadi huchelewesha maendeleo. Barabara ya kujengwa kwa miezi sita inaweza kujengwa kwa miaka miwili. Uwanja wa kujengwa miaka miwili utajengwa kwa miaka minne. Hiyo ndio sifa ya ufisadi.

Nchi hizi zina mzigo mkubwa wa kutengeneza miundombinu ndani ya miaka michache kabla AFCON. Zimwi la ufisadi linabaki kuwa changamoto ambayo isipodhibitiwa inaweza kupunguza ufanisi katika uandaaji wa mazingira bora ya mashindano au kupokonywa uenyeji.

Ukiachana na viwanja ambavyo mechi zitachezwa, pia kuna miundombinu mingi ni lazima ijengwe au kuboreshwa kabla ya 2027. Zikiwemo barabara, taa, mawasiliano, upatikanaji wa uhakika wa maji, umeme, usafiri na haya yote yatahitaji fedha nyingi kufanikishwa – fedha ambazo mafisadi nao watazimezea mate.