Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
CHAN 2024: Tanzania kutinga robo fainali?
Wenyeji Tanzania wamejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali ya Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024, baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Mauritania, bao lililofungwa dakika za lala salama na beki mkongwe Shomari Kapombe.
Mchezo huo wa Kundi B ulifanyika Jumatano usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo mashabiki walishuhudia dakika 88 za mvutano kabla ya Kapombe kufunga bao hilo muhimu, akimalizia pasi ya kiufundi kutoka kwa Iddy Nado na kumtungua kipa Abderrahmane Sarr, na kuzua shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki wa nyumbani.
Ushindi huo unakuwa wa pili kwa Taifa Stars katika mechi mbili za mwanzo, na sasa wanaongoza Kundi B kwa alama sita bila kuruhusu bao lolote hatua inayowaweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya mtoano. Kwa upande wa Mauritania, hali si shwari kwani bado hawajapata ushindi wowote na sasa wanakabiliwa na kibarua kigumu kusalia kwenye michuano hiyo.
Mudathir Yahya nyota wa mchezo
Katika ushindi huo wa pili mfululizo kwa Tanzania, Yahya Abasi kiungo fundi wa Taifa Stars aliibuka kuwa mhimili wa timu na mchango wake ukamfanya atangazwe kuwa Mchezaji Bora wa Mechi (TotalEnergies Man of the Match). Abasi, ambaye mara nyingi hufananishwa na "moyo wa timu", alikuwa muhimili katika mfumo wa kocha Hemed Suleiman, akiongoza mashambulizi na kuimarisha safu ya ulinzi kwa nidhamu ya hali ya juu.
Akizungumza baada ya mechi, Abasi alisema: "Tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuhakikisha tunafuzu hatua ya mtoano tutachukua kila mechi kwa uzito wake." Kauli yake inaonesha dhamira ya kikosi cha Taifa Stars kutimiza malengo yake hatua kwa hatua.
Akiwa na umri wa miaka 29, Abasi ni mmoja wa wachezaji wakongwe kwenye kikosi cha Tanzania. Alisisitiza umuhimu wa wachezaji wenye uzoefu katika mashindano ya kiwango cha juu kama CHAN: "Uzoefu ni jambo la msingi. Katika mechi ngumu, timu kubwa huhitaji wachezaji waliokomaa. Hawa huwapa moyo vijana na kwa pamoja tunalenga ushindi." Kwa maneno haya, Abasi anaonesha kuwa kiongozi si kwa kucheza pekee, bali pia kwa kuwalea na kuwaongoza wachezaji chipukizi.
Mashabiki waipa nguvu Taifa Stars
Kwa kiwango chake hadi sasa, Yahya Abasi anaonekana kuwa kiongozi mwenye maono, uzoefu na morali ya ushindi mambo yanayoipa Tanzania matumaini makubwa katika CHAN 2024. Tanzania sasa inaongoza Kundi B ikiwa na alama 6 baada ya mechi mbili, bila kuruhusu bao.
Burkina Faso inafuata kwa alama 3, huku Madagascar na Mauritania wakiwa na alama moja kila mmoja. Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) bado haijakusanya pointi lakini ina mechi moja mkononi.
Kwa Tanzania, hali hii inawaruhusu kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wao muhimu katika mchezo ujao dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kabla ya kukamilisha ratiba ya kundi kwa kumenyana na Madagascar.
Kwa Mauritania, hali ni ngumu wanahitaji ushindi wa lazima dhidi ya Burkina Faso na kusubiri matokeo mengine yaende kwa faida yao.