Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Korea Kaskazini yasema mfumo wa ulinzi wa anga wa Marekani unachochea 'vita vya nyuklia vya anga'

Korea Kaskazini inaiona Washington kama adui na mara kwa mara imelaani mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Sheria ya ushuru mpya wa redio kwa madereva yazua ghadhabu Zimbabwe

    Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ametia saini kuwa sheria muswada tata unaowataka madereva wote kununua leseni ya redio kabla ya kupata bima ya gari.

    Kumekuwa na kilio kutoka kwa baadhi ya madereva kwani sasa watalazimika kulipa $92 (£68) kila mwaka ili kusikiliza redio kwenye magari yao.

    Kuanzishwa kwa hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kupanua vyanzo vya mapato kwa shirika la utangazaji la serikali lakini wakosoaji wanasema ada ya leseni ni kubwa mno, hasa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

    Kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa alisema sheria hiyo mpya "ni ya kibabe kupita kiasi, inachukia raia na haina huruma kabisa".

    Akijibu wasiwasi wa madereva kwenye mitandao ya kijamii, Nick Mangwana, afisa mkuu katika wizara ya habari, alisema sheria hiyo mpya ni "lazima" na "ya haki".

    Kuna takribani magari milioni 1.2 yaliyosajiliwa nchini lakini ni 800,000 tu kati yao yanalipa bima, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

    Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC) linalopata hasara linategemea mapato ya ada ya leseni pamoja na ruzuku ya serikali, Pia huzalisha baadhi ya mapato kupitia utangazaji.

    Unaweza kusoma;

  2. Swala adimu walio hatarini kupotea wanaswa katika picha DRC

    Watafiti wa wanyamapori wamenasa na kuchapisha picha ya mmoja wa wanyama wa Kiafrika walio hatarini kutoweka, swala adimu na asiyejulikana kwa kiasi fulani anayeitwa Upemba Lechwe.

    Watafiti walifanya uchunguzi eneo la kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambao waliwaona swala 10 tu, ikionesha idadi yao iko chini ya 100.

    Manuel Weber, ambaye aliongoza utafiti, alielezea spishi kama "ukingoni kutoweka", kulingana na taarifa kutoka Hifadhi ya Kitaifa ya Upemba.

    Upemba Lechwe wanajulikana kwa kukosa mistari meusi kwenye miguu yao tofauti na swala wengine katika eneo hilo, watafiti wanasema.

    Hata hivyo alionya kuwa ni mazingira "ya changamoto kubwa" kuhusiana na uhifadhi. Alisema masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu, uvuvi na uwindaji yanaweka maeneo ya ikolojia "hatarini".

    Kulingana na utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la African Journal of Ecology, hili lilikuwa jaribio la kwanza la kuchunguza viumbe hao katika zaidi ya miaka 50. DR Congo ina historia ya picha za wanyamapori maarufu.

  3. Zaidi ya wafungwa 200 wa Ukraine wamekufa tangu kuanza kwa vita - Associated Press

    Zaidi ya wafungwa 200 wa kivita wa Ukraine wamekufa wakiwa kizuizini tangu kuanza kwa uvamizi nchini Ukraine, kulingana na ripoti ya Associated Press.

    Likiwanukuu wanaharakati wa haki za binadamu, Umoja wa Mataifa, mamlaka za Ukraine na mtaalamu wa uchunguzi wa kimahakama, chapisho hilo linabainisha kuwa kutendewa kikatili katika magereza ya Urusi kunawezekana kuwa sababu ya vifo vingi.

    Mamlaka ya Urusi haikuwa tayari kusema chochote kuhusu hilo.

    Hapo awali waliishutumu Ukraine kwa kuwatendea vibaya wafungwa wa kivita wa Urusi, mashtaka ambayo Umoja wa Mataifa uliyaunga mkono kwa kiasi, lakini kwa tahadhari kwamba dhuluma za Ukraine hazijaenea sana na mbaya zaidi kuliko zile ambazo Urusi inashutumiwa.

    Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya 2024 ilisema 95% ya wafungwa wa Ukraine walioachiliwa waliteswa. Wafungwa walielezea vipigo, shoti za umeme, kukosa hewa, unyanyasaji wa kijinsia, kunyongwa kwa dhihaka na kukosa usingizi.

    Ripoti hiyo pia ilisema kwamba baadhi ya wafungwa wa Urusi walinyanyaswa na vikosi vya Ukraine wakati wa kuwakamata mara ya kwanza, ikiwa ni pamoja na kupigwa, vitisho na shoti za umeme. Hata hivyo, unyanyasaji huo ulikoma mara tu wafungwa wa Urusi walipohamishiwa katika vituo rasmi vya kizuizini vya Ukraine, ripoti hiyo ilisema.

    Unaweza kusoma;

  4. Korea Kaskazini yasema mfumo wa ulinzi wa anga wa Marekani unachochea 'vita vya nyuklia vya anga'

    Korea Kaskazini imekosoa mpango wa Marekani wa ngao iitwayo "Golden Dome", ikisema inaweza "kugeuza anga kuwa uwanja wa vita vya nyuklia".

    Mfumo wa ulinzi, ambao Rais Donald Trump anapanga kuuzindua mwishoni mwa muhula wake, unalenga kukabiliana na vitisho vya angani vya "kizazi kijacho" kwa Marekani, ikiwa ni pamoja na makombora ya balestiki na cruise.

    Wizara ya mambo ya nje ya Pyongyang ilishutumu mpango huo kama "kujihesabia haki na kiburi", vyombo vya habari vya serikali viliripoti.

    Ilishutumu Washington kwa "kudhamiria... kufanya shughuli za kijeshi katika anga za juu" na kuonya kwamba mpango huo unaweza kuibua "mashindano ya kimataifa ya silaha za nyuklia na anga".

    Korea Kaskazini inaiona Washington kama adui na mara kwa mara imelaani mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini.

    Pyongyang pengine inaona ngao hiyo kama tishio ambalo linaweza "kudhoofisha" silaha zake za nyuklia, Hong Min, mchambuzi mkuu katika Taasisi ya Korea ya Umoja wa Kitaifa, ameliambia shirika la habari la AFP.

    "Ikiwa Marekani itakamilisha mpango wake mpya wa ulinzi wa makombora, Kaskazini italazimika kubuni njia mbadala za kukabiliana nayo au kupenya," alisema.

    Mnamo mwaka wa 2022, Kaskazini ilipitisha sheria inayojitangaza kuwa taifa la silaha za nyuklia, na imejaribu aina mbalimbali za makombora ya balestiki na cruise katika miaka ya hivi karibuni.

    Mapema mwaka huu ilidai kuwa ilirusha kombora jipya la masafa ya kati likiwa na kichwa cha kivita ambacho kilisema "kitakuwa na washindani wowote katika eneo la Pasifiki".

    Korea Kaskazini inaungana na China kukosoa mpango wa Marekani.

  5. Kundi linaloungwa mkono na Marekani lasema limeanza usambazaji wa misaada huko Gaza

    Kundi jipya la usambazaji wa misaada lenye utata linaloungwa mkono na Marekani na Israel limeanza kufanya kazi huko Gaza.

    Wakfu wa Misaada ya Kibinadamu wa Gaza (GHF) ulisema shehena ya lori ya chakula imepelekwa kwenye maeneo salama na kwamba imeanza kusambazwa kwa watu.

    Haijaeleza ni wapi na ni kiasi gani cha msaada kilikuwa kimetolewa.

    Kundi hilo, ambalo linatumia wakandarasi wa usalama wa Marekani wenye silaha, linalenga kuukwepa Umoja wa Mataifa kama msambazaji mkuu wa misaada kwa Wapalestina milioni 2.1 huko Gaza, ambapo wataalamu wanaonya juu ya njaa inayokuja baada ya kizuizi cha Israeli kilichochukua wiki 11.

    Umoja wa Mataifa na mashirika mengi ya misaada yamekataa kushirikiana na mipango ya GHF, ambayo wanasema inakinzana na kanuni za kibinadamu na inaonekana "msaada wa silaha".

    Katika taarifa iliyotumwa kwa waandishi wa habari Jumatatu usiku, GHF ilitangaza kwamba "imeanza operesheni huko Gaza" na kuwasilisha "mizigo ya chakula kwenye malori kwenye maeneo Salama ya Usambazaji, ambapo usambazaji kwa watu wa Gaza ulianza".

    "Malori zaidi yakiwa na msaada yatawasilishwa [Jumanne], huku mtiririko wa misaada ukiongezeka kila siku," iliongeza.

    Picha za kitini zilionesha zaidi ya wanaume kumi na wawili wakiwa wamebeba masanduku kutoka eneo ambalo halijabainishwa.

    Unaweza kusoma;

  6. Brazil 'timu bora zaidi duniani' - bosi mpya Ancelotti

    Kocha mpya wa Brazil Carlo Ancelotti amesema anajivuniakuiongoza timu bora zaidi duniani” na analenga kushinda kombe la Dunia la 2026

    Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 alitangazwa kuwa mkufunzi mpya wa Brazil katika mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya shirikisho la soka la Brazil (CBF).

    Raia huyo wa Itali anajiunga na timu ya Brazil kwa jina maarufu Selecao baada ya kuwa meneja wa Real Madrid kwa muda wa miaka minne iliyopita. Ameshinda Ligi ya Mabingwa mara tatu na taji la La Liga mara mbili akiwa kocha wa klabu hiyo.

    Ancelotti pia aliiongoza AC Milan kuwa mabingwa wa Ulaya mara mbili, alishinda Ligi ya Premia na Kombe la FA akiwa na Chelsea pamoja na mataji ya Ufaransa na Ujerumani akiwa na Paris St-Germain na Bayern Munich mtawalia.

    “Nina kazi kubwa mbele yangu,” alisema. “Nimefurahia, changamoto ni kubwa. Nimekuwa na uhusiano maalum na timu hii. Tutafanya kazi ili kuifanya Brazil kuwa bingwa tena.”

    “Ninajivunia kuiongoza timu bora zaidi duniani.”

    Brazil wameshinda Kombe la Dunia mara tano, na ushindi wa hivi karibuni zaidi ulikuwa mwaka 2002, na mchezo wa kwanza wa Ancelotti na wao ni mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Dunia.

    Soma zaidi:

  7. M23 waua, kutesa na kuwashika mateka raia DRC - Amnesty International

    Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema kuwa kundi la waasi wa March 23 Movement (M23) limewaua, kuwatesa na kuwashikilia baadhi ya mateka huku wakiwaweka katika mazingira ya kinyama kwenye maeneo ya kizuizini huko Goma na Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

    "Vitendo hivyo vinakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu na vinaweza kuwa uhalifu wa kivita," Amnesty International ilisema.

    Ripoti iliyotolewa na shirika hilo inasema kati ya Februari na Aprili 2025, ilihoji raia 18 waliokuwa wafungwa - wanaume wote - ambao walishikiliwa kinyume cha sheria katika maeneo ya kizuizini na M23 huko Goma na Bukavu, tisa kati yao waliteswa na wapiganaji wa M23.

    Kulingana na taarifa ya shirika hilo, ngozi iliyojivisha kundi la waasi la M23 ya kuleta amani mashariki mwa DRC, ni njia ya kuficha maovu wanayotenda dhidi ya wale wanaoamini kuwa wanaenda kinyume na matakwa yao.

    Shirika hilo limetoa wito wa kundi hilo kuwaachiliwa wale wanaowashikilia mateka mara moja na kwamba wanastahili kuonyesha ubinadamu kwa kila wanayemzuia na wawaruhusu kuwa na mawakili na familia zao.

    Soma zaidi:

  8. Trump anaweza kuiwekea vikwazo Moscow au kuiondoa Marekani katika mazungumzo na Ukraine - WSJ

    Rais wa Marekani Donald Trump anafikiria kuiwekea Urusi vikwazo wiki hii huku akizidi kuchanganyikiwa na mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine, gazeti la Wall Street Journal linaripoti, likinukuu vyanzo.

    Mmoja wa watu hao alisema vikwazo hivyo vikitekelezwa havitajumuisha vikwazo vipya vya benki, lakini chaguzi nyingine zinajadiliwa ili kumshinikiza kiongozi wa Urusi Vladimir Putin kufanya makubaliano katika meza ya mazungumzo, ikiwa ni pamoja na kukubaliana kusitisha mapigano kwa siku 30, jambo ambalo Urusi imekuwa ikikataa mara kwa mara.

    Trump alisema Jumapili kwamba anazingatia vikwazo baada ya shambulio kubwa nchini Ukraine mwishoni mwa juma. Baadaye tena alimsuta Putin, akisema alidhani "ni mwendawazimu kabisa."

    WSJ inaandika, ikitoa vyanzo vyake, kwamba Trump amechoshwa na majaribio ya suluhu ya amani na anafikiria kuyaacha ikiwa juhudi zake hazitafanikiwa.

    Wakati huo huo, bado haijabainika nini kitatokea iwapo Marekani itajiondoa katika mchakato wa mazungumzo, na iwapo Trump ataendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa Kyiv, gazeti hilo linaandika.

    "Rais Trump ameweka wazi kwamba anataka kuona makubaliano ya amani yaliyojadiliwa," katibu wa habari wa Ikulu ya White House Caroline Leavitt alisema katika taarifa yake kwa WSJ.

    Gazeti la New York Times pia liliandika juu ya uwezekano wa Washington kujiondoa katika mazungumzo hayo, lakini vyanzo vya uchapishaji vilibainisha kuwa Trump aliweka wazi kwa viongozi wa Ulaya kwamba hataki kuongeza shinikizo la vikwazo kwa Moscow.

  9. Rais Yoweri Kaguta Museveni na mkewe waomba radhi kwa makosa yaliyotetokea Uganda

    Rais Yoweri Museveni na mkewe wameomba msamaha katika tukio ambalo ni nadra sana na kukubali kutokea kwa makosa ya hapa na pale katika mkutano uliofanyika uwanja wa Uhuru wa Kololo, viungani mwa jijini kuu la Kampala, Uganda.

    Museveni na mkewe wamezungumza hayo wakiwa katika mkutano wa Injili, ambapo walisimama pamoja na kukiri kuwepo kwa mapungufu katika uongozi, kutokea kwa ufisadi, kujitenga kwa raia.

    "Kama viongozi wakuu wa National Resistance Movement (NRM), tunawajibika kwa makosa yote tuliyofanya sisi wenyewe, mawakala wetu na wawakilishi wetu. Kwa hiyo, tunasimama hapa kutubu na kuomba radhi hasa wananchi wa Buganda na nchi nzima. Tunaomba urejesho na upendeleo.

    Katika hotuba yake Rais Museveni alilipongeza kanisa kwa kile alichoeleza kuwa ni mabadiliko makubwa kutoka kuwa sehemu ya tatizo hadi sasa kuwa msingi wa amani, uwajibikaji na maendeleo ya kiroho nchini Uganda.

    Mungu arejeshe neema ambayo tulikuwa nao mwanzoni na kutuunganisha tena kwa umoja wetu wa kitaifa na kujitolea kwa mabadiliko ya kijamii na uchumi wa nchi yetu pamoja, "viongozi hao wawili walisema katika taarifa yao ya pamoja.

    Mkutano huo ulivutia maelfu ya waumini kutoka nchi nzima kwa sala, ibada, na wito mpya wa mabadiliko ya kitaifa kupitia imani.

    Soma zaidi:

  10. Israel yatangaza kuzuia kombora lililofyatuliwa kutoka Yemen

    Jeshi la Israel limetangaza mapema Jumanne kwamba limenasa kombora lililorushwa kutoka Yemen na kusababisha ving'ora vya mashambulizi ya anga nchini kote.

    Waasi wa Houthi nchini Yemen wanaendelea kurusha roketi dhidi ya Israel, wakidai kuwa hii ni mshikamano na Wapalestina huko Gaza, licha ya kukubali kusitisha mashambulizi dhidi ya meli za Marekani.

    Ikijibu, Israel ilifanya mashambulizi ya anga, ikiwa ni pamoja na la Mei 6 lililoharibu uwanja mkuu wa ndege wa Sanaa na kuua watu kadhaa.

    Haya yanajiri baada ya Marekani kukanusha siku ya Jumatatu kuwa Hamas imekubali pendekezo la kusitisha mapigano Gaza, ambalo linaripotiwa kujumuisha kuachiliwa kwa mateka 10 kwa awamu mbili na mapatano ya siku 70 ya kusitisha vita.

    Soma zaidi:

  11. Walinzi wa pwani wa Ugiriki washtakiwa kwa ajali ya wahamiaji ya 2023

    Mahakama ya wanamaji nchini Ugiriki imewashtaki walinzi 17 wa pwani kutokana na maafa mabaya zaidi ya boti ya wahamiaji katika Bahari ya Mediterania kwa muongo mmoja.

    Hadi watu 650 walihofiwa kufa maji wakati boti ya wavuvi ya Adriana iliyokuwa imejaa watu wengi ilipozama karibu na Pylos, karibu na pwani ya Ugiriki, tarehe 14 Juni 2023.

    Manusura baadaye waliambia BBC kwamba walinzi wa pwani wa Ugiriki walisababisha boti yao kupinduka katika jaribio la kuivuta.

    "Imetuchukua miaka miwili kwa kesi hii, ingawa watu wengi walishuhudia kilichotokea," mmoja wa walionusurika, mwanamume wa Syria tuliyemwita Ahmad, alisema Jumatatu.

    Nahodha wa boti ya walinzi wa pwani ashtakiwa

    Mamlaka za Ugiriki daima zimekanusha madai dhidi yao.

    Naibu Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Wanamaji ya Piraeus amegundua kwamba Walinzi 17 wa Pwani ya Hellenic wanapaswa kushtakiwa kwa uhalifu.

    Miongoni mwao ni nahodha wa boti ya walinzi wa pwani, LS-920, ambaye anashtakiwa kwa "kusababisha ajali ya boti hiyo", na kusababisha vifo vya "watu takriban 82".

    Hii inalingana na idadi ya miili iliyopatikana, ingawa inadhaniwa kuwa zaidi ya watu 500 walikufa maji, wakiwemo wanawake na watoto ambao wote walikuwa chini ya sitaha.

    Maafa hayo yalitokea katika maji ya kimataifa - lakini ndani ya eneo la uokoaji la Ugiriki.

    Meli ya walinzi wa pwani ilikuwa ikiifuatilia boti Adriana kwa saa 15 kabla ya kuzama.

    Ilikuwa imeondoka Libya kuelekea Italia ikiwa na takriban watu 750. Ni 104 tu kati yao wanajulikana kuwa walinusurika.

    Tumekuwa tukifanya uchunguzi tangu siku ya maafa na mfululizo wetu wa matokeo ya utafiti uliofanywa umekuwa na shaka juu ya hatua zilizochukuliwa na Ugiriki.

    Manusura wa Syria wanahisi 'kupata utetezi'

    Mara ya kwanza tulikutana na wakimbizi wa Syria, ambao tuliwaita Ahmad na Musaab ili kulinda utambulisho wao, mwezi mmoja baada ya maafa.

    Walisema kila mmoja alilipa $4,500 (£3,480) kupata nafasi kwenye mashua hiyo.

    Kaka mdogo wa Ahmad pia alikuwemo ndani na hakunusurika.

    Musaab alituelezea wakati ambapo - alidai - walinzi wa pwani wa Ugiriki walisababisha mashua yao kuzama.

    "Waliunganisha kamba kutoka kushoto," alisema. "Kila mtu alihamia upande wa kulia wa boti yetu ili kuifanya isilemee upande mmoja. Boti ya Ugiriki iliondoka haraka na kusababisha boti yetu kupinduka. Waliendelea kuiburuta kwa umbali."

    Pia unaweza kusoma:

  12. Ghana yafunga ubalozi wake nchini Marekani kwa muda kutokana na kashfa ya visa

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana ametangaza kuwa nchi hiyo imefunga kwa muda ubalozi wake katika mji mkuu wa Marekani huku kukiwa na uchunguzi kuhusu madai ya kashfa ya visa.

    Samuel Okudzeto Ablakwa alisema ubalozi huo utafungwa kufuatia "ugunduzi" wa timu ya ukaguzi iliyochunguza madai ya ufisadi katika ubalozi wa Washington.

    Taarifa hiyo iliongeza kuwa ubalozi huwa unafungwa kabisa kwa "siku chache" hadi "urekebishaji upya wa mifumo" utakapokamilika.

    Kulingana na Ablakwa na "washiriki" wa ukaguzi, wahusika katika mpango huo wa "udanganyifu", walichukua pesa kutoka kwa waombaji wa visa na pasipoti.

    Inadaiwa kuwa mpango huo ulijumuisha kuweka kiunganishi ambacho hakijaidhinishwa kwenye tovuti ya ubalozi ili kuwaelekeza waombaji visa na pasipoti kwa kampuni ya kibinafsi ambapo "walitozwa malipo ya ziada kwa huduma nyingi" bila ufahamu wa wizara ya mambo ya nje.

    Ablakwa aliongeza kuwa baada ya hapo "mchakato wote" ulifanywa kwenye akaunti ya kibinafsi, na kwamba mpango huo umekuwa ukiendelea kwa miaka mitano.

    "Tabia hii imeripotiwa kwa mwanasheria mkuu kwa uwezekano wa kufunguliwa mashtaka na kurejesha fedha zilizopatikana kwa njia za udanganyifu," Ablakwa aliongeza.

    Matokeo yake, wafanyikazi wa wizara ya mambo ya nje huko Washington "wamerudishwa nyumbani" na "wafanyakazi wote walioajiriwa ndani ya ubalozi wamesimamishwa kazi," Ablakwa alisema.

    "Serikali ya Rais [John] Mahama itaendelea kuonyesha kutovumilia kabisa rushwa, migogoro ya maslahi na matumizi mabaya ya ofisi."

  13. Urusi yamshtumu Trump kwa 'kuendeshwa na hisia' baada ya kumuita Putin 'mwendawazimu'

    Ikulu ya Urusi imedai kuwa Donald Trump anaonyesha dalili za "kuzidiwa kihisia" baada ya kumuita Vladimir Putin "mwendawazimu" kufuatia shambulio kubwa zaidi la anga la Moscow dhidi ya Ukraine.

    Rais wa Marekani alisema kwenye mtandao wakijamii wa Truth Social kwamba "kuna kitu kimetokea" kwa Putin, baada ya Urusi kuwaua watu 13 nchini Ukraine kwa kutumia droni na makombora 367. "Amekuwa mwendawazimu," Trump alisema. "Inaua watu wengi bila sababu."

    Dmitry Peskov, msemaji wa Putin, alisema maoni hayo "yanajumuisha hisia kali kwa kila anayehusika".

    Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, wakati huo huo alisema kwamba washirika wa Ukraine wameondoa vikwazo vyote vya silaha, huku kukiwa na ripoti kwamba angeipatia Kyiv makombora ya Taurus.

    Soma zaidi:

  14. Hujambo, karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja