Kwa nini Simba imepoteza dhidi ya Berkane katika fainali?

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Hatimaye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika 2024/25 (TotalEnergies CAF Confederation Cup), yamefikia tamati baada ya fainali kati ya Simba Sports Club (Simba) kutoka Tanzania, na Renaissance Sportive de Berkane (RS Berkane) kutoka Morocco, kumalizika katika uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Tanzania, Mei 25.

Mechi hiyo ambayo ilikuwa ya marudio ilishuhudia miamba hiyo ya soka barani Afrika, ikitoka 1:1. Mechi ya kwanza iliyochezwa Morocco tarehe 17 Mei, mwaka huu, RS Berkane iliibamiza Simba goli mbili kwa bila. Kwa ujumla RS Berkane 3: Simba 1.

Wakati Simba ikisubiri mashindano mengine ili kutupa tena karata yake. Mjadala umebaki kuhusu yapi yaliifanya timu hiyo ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili katika jedwali la Ligi Kuu Tanzania bara, kushindwa kupindua meza katika uwanja wa nyumbani.

Kuna mambo manne yamekuwa yakitajwa zaidi: Mwamuzi wa mchezo, uwezo wa Berkane, Uwanja na matukio katika mchezo wenyewe, hasa kadi nyekundu dhidi ya mchezaji wa Simba. Katika haya yote, lipi lenye uzito ambalo lilichangia pakubwa Simba kupoteza?

Maamuzi ya Mwamuzi?

Mwamuzi mkuu wa mchezo alikuwa Dahane Beida kutoka Kaskazini-Magharibi mwa Afrika, katika nchi ya Mauritania. Si mashabiki pekee wa Simba waliomwelekezea kidole mwamuzi, pia wachezaji wa Simba wameoneshwa kutoridhishwa na maamuzi yake.

“Kila mtu ameshuhudia kilichotokea katika mchezo wa leo, Mwamuzi ametuumiza sana, kadi nyekundu aliyoitoa imetufanya kuwa nyuma, tulikuwa tayari tume ikamata mechi na tulikuwa na uwezo wa kusawazisha na kupata goli la ushindi,” alisema Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein baada ya mchezo kuisha.

Kutoridhika na maamuzi ya Mwamuzi kulidhihirika pia katika benchi la ufundi la Simba, kocha na wasaidizi wake walionekana mara kwa mara kuinuka kwa ghadhabu na kukosoa maamuzi - yakiwemo yaliyohusisha faulu. Hilo likafanya kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids kupewa kadi ya njano na kocha msaidizi kupewa kadi nyekundu.

Licha ya hayo yote, ikiwa hakuna malalamiko rasmi kutoka Simba kwenda Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) juu ya Mwamuzi, basi kinachoendelea kusemwa kitabaki kuwa ni maoni tu ya wana Simba na maamuzi yote ya Mwamuzi yatabaki kuwa halali.

Ili kuthibitisha Mwamuzi kafanya makosa katika maamuzi yake na yameiathiri Simba kutopata ushindi, hilo linapaswa kuthibitishwa kwa njia rasmi, vinginevyo soga za vijiweni na mtandaoni zitabaki kama zilivyo.

Uwanja umembeba nani?

Kabla ya fainali ya marudio, kulikuwa na vuta nikuvute, kuhusu uwanja upi utatumika. Simba na mashabiki wake, walitaka mchezo huo uchezwe katika uwanja ambao wameuzoea wa Benjamin Mkapa katika jiji la Dar es Salaam.

Uwanja wa Amani una uwezo wa kubeba mashabiki 15500. Huku Mkapa ukiwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000. Simba ina kawaida ya kuwa na matokeo mazuri ichezapo kwa Mkapa. Lakini kwa sababu za kiufundi uwanja huo haukutumika.

Bila shaka mashabiki ni muhimu katika mechi, hasa kwa wenyeji ambao hutegemea kuona sehemu kubwa ya mashabiki wakiwa upande wao. Ingawa mashabiki pekee hawatoi uhakika wa ushindi. Hakuna mtaalamu yoyote wa soka atakaye kuambia, 'kwa sababu una maelfu ya mashabiki, timu yako itashinda.' Hakuna jambo hilo kwenye soka.

Ufundi, ujuzi na mipango na kocha na wachezaji wake, ndio mambo makuu yanayotoka matokeo mazuri au mabaya kwa timu. Mashabiki hubaki kuwa wahamasishaji, na watia moyo, lakini sio wao wanaotikisa nyavu za timu pinzani.

Hata hivyo, Simba walikuwa nyumbani, sehemu kubwa ya mashabiki waliokuwa Aman walikuwa ni upande wa timu hiyo. Mkapa ni pazuri zaidi kupata ushindi, lakini uwanja hauwezi kuwa ndio sababu kuu ya wao kukosa ushindi.

Ubora wa RS Berkane?

Ushindi wa jana, umeifanya RS Berkane kuwa moja ya klabu bora za Afrika kwa upande wa mashindano ya CAF Confederation Cup, ikifikisha mataji matatu ndani ya miaka mitano katika mashindano hayo, baada ya kubeba ubingwa mwaka 2020 na 2022.

Katika mashindano haya RS Berkane wameonesha ubora wa hali ya juu kwa kushinda mechi zote za nyumbani, na wakati mwingine kwa magoli mengi. Hilo linathibitisha kujipanga na uwezo wao katika msimu huu.

Bila shaka hakuna walakini kwamba Simba ni timu kubwa Tanzania na katika Bara la Afrika. Baada ya miaka mingi ya kutofika katika hatua ya fainali katika mashindano makubwa ya vilabu barani Afrika, mchezo huo umeandika upya historia yao.

Kama msemaji wa timu hiyo Ahmed Ally alivyosema baada ya mpira kuisha: "Kuanzia sasa, kiwango cha Simba kitabaki kizuri ili kufika fainali ya mashindano yoyote ya CAF, tumeshinda medali kwa kumaliza nafasi ya pili, na msimu ujao tutavaa medali nyingine, hatutasubiri miaka 60 tufike fainali, Simba sasa ni timu ambayo itafika fainali kila mwaka.”

Kwa hakika Simba si timu changa, lakini rekodi za michuano hii zinaonyesha RS Barkene wamefanya vizuri zaidi kuliko Simba. Wakati wa kujadili kipi kimeifanya Simba kupoteza, yumkini hili la ubora wa RS Barkene katika msimu huu si jambo la kulisahau.

Kadi nyekundu?

Kadi nyekundu dhidi ya kiungo mkabaji wa Simba, Yusuph Kagoma katika dakika ya 53, kwa hakika ndilo jambo hasa la kulitazama. Hakuna usawa mnapocheza wachezaji 11 dhidi ya 10. Hasa ukizingatia kuwa kadi yenyewe ilitoka wakati wa dakika za mwanzo za kipindi cha pili.

Hii ni kadi ambayo ilivuruga mpangilio wa Simba na kuipunguza nguvu timu hiyo. Bila shaka imechangia kwa kiasi kikubwa Simba kushindwa kuongeza bao la pili na wakati huo huo bao lao la kuongoza kurudishwa.

Huku mjadala wa kipi kimeifanya Simba kupoteza ukiendelea, benchi la uongozi wa timu hiyo litakuwa na kazi ya ziada kuendelea kuijenga timu kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu bara, sanjari na kujipanga upya kwa mashindano yajayo ya CAF.

Waswahili wasema, kuvunjika kwa koleo, sio mwisho wa uhunzi. Kwa Simba itakuwa, kupoteza katika fainali sio mwisho wa ushindani wao katika soka la Afrika. Bado kuna muda wa kuzitimiza ndoto zao za muda mrefu.