Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wahouthi wa Yemen waishangaza Marekani kwa kudungua droni zake saba
Waasi wa Houthi nchini Yemen wameangusha ndege saba zisizo na rubani za Marekani aina ya MQ-9 Reaper katika muda wa chini ya wiki sita. Kila ndege isiyo na rubani, iliyotengenezwa na General Atomics, inagharimu takriban dola milioni 30 za Kimarekani, ikimaanisha kuwa Pentagon imepoteza zaidi ya dola za kimarekani milioni 200 ndani ya muda mfupi.
Kulingana na maafisa wa ulinzi, ndege tatu zisizo na rubani zilidunguliwa wiki iliyopita, na kusema kuwa Houthis wamekuwa bora zaidi katika kulenga ndege hizi zisizo na rubani. Droni hizo zilikuwa zikifanya mashambulizi au ujasusi, na zilianguka katika Bahari ya Sham au ardhi ya Yemen, wamesema maafisa hao kwa sharti la kutotajwa majina.
Wameangusha droni ngapi?
Kwa mujibu wa mtandao wa habari wa MSN, Marekani ilipoteza droni zake kuanzia Machi 31, 2025, Aprili 3, Aprili 9, Aprili 13, Aprili 18, Aprili 19, na Aprili 22. Hiki ni kiwango kikubwa cha hasara.
Afisa mmoja alithibitisha kuwa ingawa wanaamini zimedondoshwa, lakini uchunguzi bado unaendelea. Afisa huyo pia alidokeza kuwa, huku Marekani ikiongeza mashambulizi yake ya kila siku tangu Machi 15, misheni za droni hizo zinakabiliwa na hatari zaidi.
Mashambulizi ya Marekani dhidi ya Houthis yalianzishwa na Rais Donald Trump Machi 15. Kwa lengo la kuwazuia Wahouthi waache kufanya mashambulizi dhidi ya meli kwenye moja ya korido muhimu zaidi za baharini - Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden.
Tangu wakati huo, jeshi la Marekani limefanya zaidi ya mashambulizi 750 ya anga yanayolenga maeneo ya Houthi. Licha ya mashambulizi haya, Wahouthi wanaendelea kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kwenye meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani. Kwa bahati nzuri, hadi sasa, hakuna shambulio ambalo limefanikiwa.
Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa sasa limepeleka manowari mbili za kubebea ndege za kivita karibu na Yemen - USS Harry S. Truman na USS Carl Vinson.
Sio kawaida kwa Marekani kupeleka manowari mbili kwa wakati mmoja katika eneo la Mashariki ya Kati. Wakuu wa jeshi la wanamaji kwa kawaida huepuka jambo hilo kwa sababu huharibu ratiba za matengenezo na kuwaweka wanajeshi wa majini mbali na nyumbani kwa muda mrefu kuliko ilivyopangwa.
Vifo vya raia Yemen
Kundi la Maseneta wa Marekani - Chris Van Hollen (Maryland), Elizabeth Warren (Massachusetts), na Tim Kaine (Virginia) - wametoa tahadhari. Walituma barua kwa Waziri wa Ulinzi Hegseth siku ya Alhamisi, wakihoji ikiwa utawala wa Trump unapuuza jukumu la kupunguza madhara kwa raia.
Wasiwasi wao ulikuja baada ya ripoti kwamba huenda shambulio la Marekani katika kituo cha mafuta cha Ras Isa nchini Yemen liliuwa zaidi ya raia 70.
Wameonya kwamba, "vifo vya raia, kwa hakika vinadhoofisha misheni ambayo jeshi limetumwa kuifanya."
Waasi wa Houthi wanadai mashambulizi yao dhidi ya meli ni juhudi za kuishinikiza Israel kukomesha vita vyake dhidi ya Hamas huko Gaza.
Tangu Novemba 2023, wamelenga zaidi ya meli 100 za wafanyabiashara, na kuzamisha meli mbili na kuua mabaharia wanne. Mashambulizi haya yametatiza sana biashara kupitia Bahari ya Shamu, njia ambayo kwa kawaida bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani trilioni 1 zinapitishwa kila mwaka.
Kujibu, Marekani ikaamua kushambulia Houthi. Lakini kupoteza ndege zisizo na rubani saba za Reaper na kutumia mamilioni ya pesa kwenye operesehni ya muda mrefu ya kijeshi ni ishara kwamba operesheni hii sio nyepesi.
Kadiri uwezo wa Wahouthi unavyoboreka na vifo vya raia vinachunguzwa, Marekani inakabiliwa na maamuzi magumu mbeleni – kati ya kuziweka manowari mbili katika eneo hilo na kuzuia vifo visivyo vya lazima vya raia.
Jambo moja liko wazi; mgogoro wa bahari ya Shamu hauna dalili ya kupoa hivi karibuni.