Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Israel-Hamas: Kwanini makombora kutoka Yemen yanaweza kuzidisha mzozo Mashariki ya Kati
- Author, Frank Gardner
- Nafasi, BBC
Ni zaidi ya maili 1,000 kutoka pwani ya Yemen hadi Ukanda wa Gaza. Lakini kile kinachoendelea karibu na bahari ya Yemen kinaweza kuathiri vita vya Gaza.
Kwa mujibu wa Kamandi Kuu ya Marekani, kitengo cha Idara ya Ulinzi cha Mashariki ya Kati, waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen walifanya mashambulizi manne dhidi ya meli tatu za kibiashara katika maji ya kimataifa. Mashambulizi hayo yalihusisha ndege zisizo na rubani na makombora.
Jeshi la Wanamaji la Marekani lilitumia ulinzi wa anga kuangamiza makombora na kuangusha ndege tatu zisizo na rubani. Lakini mashambulizi mengine ya Houthi yalifanikiwa kupiga shabaha na kusababisha uharibifu lakini hakuna majeruhi.
"Mashambulizi haya yanaleta kitisho cha moja kwa moja kwa biashara ya kimataifa na usalama wa baharini," imesema Pentagon. Vilevile inaamini mashambulizi kutoka Yemen "yaliwezeshwa na Iran."
Ni eneo la bahari la upana wa maili 20 linalotenganisha Afrika na Rasi ya Arabuni - meli zipatazo 17,000 (10%) ya biashara ya kimataifa hupita kila mwaka.
Meli yoyote inayopita kwenye Mfereji wa Suez na kuelekea kusini kwenye Bahari ya Hindi lazima ipite mkondo huu, karibu na pwani ya Yemen.
Houthi, Israel na Marekani
Sehemu kubwa ya Yemen, ikiwa ni pamoja na pwani yake ya Bahari Nyekundu, ziko chini ya udhibiti wa wanamgambo wa Houthi ambao waliipindua serikali halali, iliyochaguliwa mwishoni mwa 2014.
Wanaungwa mkono na Iran inayodaiwa kuwapa silaha na mafunzo, ikiwa ni pamoja na droni na teknolojia ya makombora, kama ilivyo kwa Hamas huko Gaza na Hezbollah wa Lebanon.
Mapinduzi ya Houthi yalizua janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miaka tisa, na kusababisha maelfu ya vifo na maafa ya kibinadamu.
Wakati Iran inawaunga mkono Wahouthi, Saudi Arabia na UAE ziliingia vitani dhidi yao mwaka 2015, zikisaidiwa na Marekani na Uingereza, katika jitihada zilizoshindwa za kurejesha serikali inayotambulika kimataifa.
Wakati wa vita hivyo Wahouthi walirusha makombora mengi ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani kulenga maeneo ndani ya Saudi Arabia, UAE na ndani ya Yemen - ikiwemo kupiga viwanja vya ndege vya kiraia, miji na miundombinu ya mafuta pamoja na maeneo ya kijeshi.
Kufuatia kuzuka kwa mzozo wa sasa kati ya Israel na Hamas huko Gaza, Wahouthi walitangaza kuunga mkono wale waliowaita, "ndugu zao wa Gaza" na wamerusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea Eilat na maeneo mengine nchini Israel. Ingawa vyote vimenaswa na Jeshi la Wanamaji la Marekani.
Houthi pia wameshambulia meli kadhaa wanazoshuku kuwa na uhusiano na Israel. Novemba, wanamgambo hao waliokuwa katika helikopta walitua kwenye meli ya mizigo, Galaxy Leader na kuiteka.
Wameapa kuzuia meli zozote za Israel kupita katika bahari ya karibu na Yemen na katika taarifa siku ya Jumapili msemaji wao wa kijeshi alisema, meli hizo zilishambuliwa kwa sababu ni za Israel.
Jeshi la Israel lilikanusha uhusiano wowote kati ya serikali yake na meli hizo lakini ripoti za vyombo vya habari zinasema kuna uhusiano wa kibinafsi kati ya meli na wafanyabiashara matajiri wa Israel.
Hatari iliyopo
Washington itasita kuibua mvutano zaidi katika eneo ambalo tayari lina mvutano kutokana na vita huko Gaza.
Lakini iwapo Wahouthi wataendelea kurusha makombora nje ya mipaka yao, Marekani inaweza kuamua kulipiza kisasi kwa kulenga maeneo yao ya kurusha makombora.
Iwapo hilo litatokea kuna hatari Iran, inayounga mkono Houthi, inaweza pia kulipiza kisasi, na kusababisha mzozo wa moja kwa moja kati ya Iran na Marekani. Kwa sasa, hilo ni jambo ambalo pande zote mbili zinatamani kulikwepa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah