Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maswali gani yalipita akilini mwa Yahya Sinwar kabla ya operesheni dhidi ya Israel? - Magazeti
Katika mgazeti leo, tunazitazama makala tatu - moja, kuhusu kubadilika ya sheria za vita. Makala nyingine ni juu ya kauli zilizotolewa na Marekani na Ulaya za kuionya Israel dhidi ya mauaji ya raia baada ya kumalizika kwa siku saba za mapatano.
Vilevile tutaangalia makala inayojadili operesheni ya Hamas ya Mafuriko ya Al-aqsa ya Oktoba 7, ikiwa ilikuwa ni operesheni ya kujiangamiza au la.
'Sinwar na al-Deif walikuwa wanafikiri nini?'
Tunaanza ziara yetu na kile kilichoandikwa na Ghassan Charbel katika gazeti la Saudi Arabia la Asharq Al-Awsat chini ya anuwani, "Sinwar na Kizibao cha Mabomu."
Mwandishi anasema kilichotokea “tarehe 7, Oktoba - ni cha kuogofya zaidi kuliko kile ambacho Israel imewahi kupitia hapo awali. Kwa maoni yake, ''ni pigo kubwa sana.”
Anaamini shambulizi la Yahya Sinwar lilitikisa makazi na walowezi. Lilitikisa shughuli za kiusalama na za kijeshi na kuwaweka wale wanaodhibiti siasa katika kashfa kubwa isiyokuwa na kifani.
Shambulia hilo limeisukuma Israel kuingia vitani. Kazi kubwa kuliko ile ya kurejesha mateka - ni kazi ya kurejesha heshima na kuhakikisha Sinwar mwingine hatokei mahali pengine.
Pamoja na kuendelea kwa bahari ya damu, majeneza, makundi ya watu wanaofuatana waliohamishwa makazi yao, vichuguu vya vifusi - bado mapambano yanaonekana kuwa mgumu zaidi kuliko vile ulimwengu ulivyofikiria.
Vita ni vigumu kwa pande zote mbili. Kwa Israel kukamilika kwa vita ni kuwaondoa Hamas na Gaza isiwe tishio la usalama wake. Kuiondoa Hamas kutoka eneo hilo inabidi kufanya kazi kubwa, na hilo haliwezekani bila kusababisha janga jipya.
Hamas haiwezi kukubali kuondolewa kirahisi. Haikuanzisha operesheni ya mafuriko ya Al-Aqsa ili baadaye iache kupigana.
Charbel anauliza maswali kuhusu kile Sinwar na Jenerali wa Qassam, Muhammad al-Deif walikuwa wanakiwaza, kabla ya kuanzisha operesheni ya "Mafuriko ya Al-Aqsa."
Je, Sinwar aliona operesheni hiyo ingesababisha wafungwa wa Kipalestina kuachiliwa kutoka kwenye magereza ya Israel kwa kubadilishana na idadi kubwa ya mateka?
Je, alitarajia Israel ijibu operesheni yake kwa uvamizi kama ule wa awali, na kufuatiwa na usitishaji vita na kukamilika kwa mchakato wa kubadilishana mateka na wafungwa - na kufanya msimamo wa Hamas katika Gaza na Ukingo wa Magharibi kuimarika na kuthibitisha kuwa Hamas ndiye mwakilishi pekee halali wa watu wa Palestina?
Je, alizingatia uwezekano wa Marekani kuharakisha meli zake na rais wake kuhakikisha Hamas haitashinda na haitakuwa na uwezo tena wa kutawala Gaza?
Je, Sinwar aliamua kuipiga Israel pigo chungu na kuanzisha vita kwa kiwango kikubwa, bila kujali hesabu na matokeo yake?
Je, alifikiria washirika katika mhimili wa upinzani watazingatia vita hivyo kuwa ni vyao pia na watakimbilia kuiunga mkono Hamas?
Je, Sinwar atakuwa tayari kuivunja Al-Qassam kwa ahadi thabiti ya kimataifa ya kuanzishwa kwa mchakato wa kisiasa utakaoleta suluhisho la serikali mbili?
Charbel anamaliza kwa kuuliza: Je, Sinwar amefanikiwa kubadilisha hali ya mambo au ameivisha Hamas mkanda wa mabomu na kuisukuma katika operesheni ya kishahidi ya kujiangamiza?
'Raia katikati ya mapigano na kuziandika upya sheria za vita'
Tuangalie sasa uchambuzi katika gazeti la The Times ulioandikwa na Richard Spencer chini ya anuwani: "Raia katikati ya mapigano na kuziandika upya sheria za vita."
Mwandishi anasema Israel haonyeshi, “majuto yoyote kwa mashambulizi makali katika vita ambavyo kufikia sasa vimeua watoto wengi zaidi kuliko mgogoro wowote ulimwenguni katika mwaka 2021 na 2022 kwa pamoja,” kulingana na Save the Children.
Spencer anaturudisha nyuma hadi 2002, wakati kombora la Israel lilipomuua kiongozi wa Hamas huko Gaza pamoja na watoto kumi.
Gazeti la Israel wakati huo lilielezea shambulio hilo ni "shambulio la kwanza la kigaidi la Israel." Ariel Sharon, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel wakati huo, alisema, “kama ningelijua matokeo, ningeliahirisha mauaji hayo.”
Mzozo huo umefikia hatua ambapo utawala wa Biden umelazimika hadharani kuitaka Israel ibadilishe mbinu zake baada ya kumalizika kwa usitishaji mapigano wiki iliyopita.
Mwandishi anaamini kuna kitu kimebadilika katika muda wa miongo miwili kuhusu kile, "kinachoitwa uharibifu wa bila kukusudia, yaani, mauaji ya raia ili kufikia lengo la kijeshi.''
Spencer anaeleza IDF imeamua sio tu kukubali kiwango cha juu cha vifo vya raia, lakini pia kutumia nguvu nyingi wakati wa kulenga miundombinu ya kiraia na kiserikali.
Anasema majeshi duniani kote yamekuwa na mwelekeo wa kukubali mauaji na majeruhi ya raia kwa idadi kubwa katika miaka ya hivi karibuni.
Washauri wa kijeshi na wanajeshi wanahalalisha hilo kwa kielelezo cha ukatili uliofanyika katika mashambulizi ya Oktoba 7.
Wakosoaji wanasema Israel imekiuka sheria za kimataifa, sio tu katika suala la kuuwa raia wengi, lakini pia kutofautisha mashambulizi katika maeneo ya kijeshi na ya kiraia.
Spencer anasema majenerali wa Israel hawajijui kuwa wamekuwa wakatili kuliko hapo awali. Akitoa mfano kile kilichosemwa na msemaji wa Jeshi la Israel, Daniel Hagari: "Lengo ni uharibifu zaidi na sio usahihi."
'Wanafiki wa Marekani wanaionya Israel iwe makini'
Tunaendelea na makala nyingine - ambayo pia inawahusu raia, imeandikwa na Odeh Bisharat katika gazeti la Israel la Haaretz chini ya kichwa: "Sasa wanafiki wa Marekani wanaionya Israel kuwa makini."
Mwandishi analaumu wanasiasa nchini Marekani kwa kuchelewa kwao kuionya Israel juu ya kile kinachotokea Gaza, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kutisha, mauaji ya maelfu, uharibifu wa maelfu ya nyumba na mwanzo wa msiba mkubwa wa kibinadamu.
Akinukuu kilichosemwa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin, “katika vita vya mjini, unaweza kushinda tu kwa kuwalinda raia. Ikiwa utawasukuma kwenye mikono ya adui, ushindi kwa mbinu unabadilika na kuwa kushindwa kimkakati."
Mwandishi anauliza: Kama unaweza kusema maneno hayo yenye hekima, ulikuwa wapi wakati wa mauaji ya watu wengi?
Bisharat anauliza, kwanini mlificha lulu hizi za hekima wakati tunazihitaji kwa mara ya kwanza? Baada ya shambulio la umwagaji damu la Hamas na mauaji ya kutisha, wakati damu ya watu wa Israel inachemka, viongozi hawa hawakujaribu kuwatuliza watu.
Mwandishi hawaondolei lawama watu wa Ulaya na Wamarekani kuhusika kwao na damu inayotiririka katika eneo hili, kwani kila tone la damu inayomwagika Gaza na Israel inakuja kwa idhini ya Marekani na Ulaya - kwa msaada usio na masharti kuilipua Gaza na silaha hutiririka kama maji.
Kwa miaka 75 nchi za Magharibi zimekuwa zikirudia "tamko tupu juu ya suluhisho la serikali mbili," huku msaada wake wa kijeshi na kidiplomasia kwa Israel ukiendelea, na kuiwezesha kuendeleza uvamizi. Kana kwamba wanasema: “Tunalaani, lakini kivitendo tunakuunga mkono.”
Mwandishi anamalizia kwa hitimisho, nyinyi si marafiki wa watu wa Israel au Wayahudi wa ulimwenguni. Israel ipo kwa ajili ya kulinda maslahi yenu ya Mashariki ya Kati.
Na muhimu zaidi, yeyote anayejali kuhusu usalama wa watu wa Israel hatowaweka katika kitisho cha usalama milele.
Kwa sababu hii, Israel inazidi kuwa mbaya zaidi na demokrasia inazidi kuporomoka na anachofanya Ben Gvir kimevuka mipaka yote. Haya yote yanafanyika bila nyinyi kufanya lolote.
Mwandishi anaamini Marekani si rafiki wa Israel, wala si rafiki wa watu wa Israel, wala Wayahudi, wala Waarabu. Badala yake hutuma majeshi yake kulinda maslahi yake. Damu ya Israel inamwagika badala ya damu ya Marekani - Ulaya.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi