Mzozo wa Israel na Palestina: Je mataifa yenye uwezo mkubwa zaidi duniani yanaegemea upande gani?

Vikosi vya Israel vilianzisha mashambulizi ya kukabiliana katika Ukanda wa Gaza baada ya kundi la wapiganaji wa Palestina Hamas kufanya shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa ndani ya Israel mnamo Oktoba 7 (Jumamosi).

Katika hili, mvutano unaoendelea kati ya maeneo hayo mawili miongo michache iliyopita umegeuka kuwa vita. Ambayo kwa kweli iligawanya ulimwengu katika kambi mbili.

Katika hali hiyo, nchi mbalimbali zimetoa kauli zinazoelezea msimamo wao. Wengine waliegemea moja kwa moja na Israel, huku wengine wakiizungumzia Palestina. Tena, maneno ya 'neutral position' yalijitokeza katika hotuba ya mtu fulani.

Ripoti hii imetolewa kwa msingi wa taarifa zilizopokelewa kutoka kwa serikali au mkuu wa nchi wa nchi tofauti.

Marekani

Rais wa Marekani Joe Biden ameeleza uungaji mkono wake mkubwa na usioyumba kwa Israel.

Mara baada ya shambulio la Jumamosi. Biden alimpigia simu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kueleza kujitolea kwake kwa Israel.

Katika kuunga mkono Israel, shehena ya ndege ya USS Gerald R. Ford na jeti za kivita za makombora na viharibu vinne vya makombora vilitumwa kwenye bahari ya Mediterania karibu na Israel.

Ikulu ya White House imeahidi kutuma msaada zaidi wa silaha kwa Israel katika siku zijazo.

Rais Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris mnamo Jumanne pia waliahidi waziri mkuu wa Israeli silaha mpya kwa mfumo wake wa ulinzi wa makombora wa Iron Dome.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken alitembelea Israel siku ya Alhamisi. Ujumbe wa wazi wa Bw. Blinken ni kwamba Marekani inasimama na Israel leo, kesho, na katika siku zijazo.

Iran

Uongozi wa juu wa Iran umesisitiza uungaji mkono wake kwa kundi la wanamgambo wa Palestina baada ya mashambulizi ya Hamas nchini Israel.

Hata hivyo Iran imekana kuhusika na shambulio hilo.

"Vitendo vya utawala wa Kizayuni wenyewe vinahusika na maafa haya," Kiongozi Mkuu Ali Khamenei alisema kwenye televisheni ya Iran baada ya shambulio la Jumamosi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Reuters, amesema: "Tunabusu mkono wa wale wanaopanga kuushambulia utawala wa Kizayuni."

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alitweet Jumamosi kutoka kwa akaunti yake ya X, akiita ghasia za hivi punde kuwa "jibu linalofaa kwa uhalifu na mauaji ya miaka mingi".

Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni, Rais wa Iran Ibrahim Raisi alitaja tukio hilo kuwa "ushindi kwa jeshi la Palestina na vyama vyote vya Palestina."

Kisha tarehe 11 Mei Bw. Raisi na Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman walijadili 'haja ya kukomesha uhalifu wa kivita dhidi ya Wapalestina' kwa njia ya simu. Vyombo vya habari vya serikali ya Tehran viliripoti habari hii.

Baada ya shambulio hilo, msemaji wa Hamas Ghazi Hamad aliiambia BBC kwamba ilifanya shambulio hilo kwa msaada na usaidizi wa Iran.

China

Inaaminika kuwa China inajaribu kujionyesha kuwa haina upande wowote katika hali hii ya vita kati ya Palestina na Israel. Hata hivyo, nchi hiyo inataja haja ya kuanzisha taifa huru la Palestina.

Nchi haijatoa tamko lolote rasmi kuhusu kuunga mkono moja kwa moja chama chochote. Lakini walizitaka pande zinazohusika kusalia 'tulivu' na kukubaliana kusitisha mapigano mapema.

Mjumbe maalumu wa China katika eneo la Mashariki ya Kati, Zhai Jun tayari amependekeza kwa Misri kuwa China inataka kupatanisha kwa uratibu na Misri ili kutatua mzozo wa Israel na Palestina.

Akisikitishwa na kuzorota kwa hali ya usalama na kibinadamu nchini Palestina amesema "ni muhimu kuanzisha Palestina kama taifa huru na kuhakikisha kuwepo kwa amani kati ya Palestina na Israel," June alisema. Habari hii imechapishwa katika vyombo vya habari kadhaa vya kimataifa ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari vya Marekani CNN.

"China itaendelea kuhimiza usitishaji mapigano na kukomesha ghasia na kusaidia kukabiliana na mzozo wa kibinadamu, kuendeleza kikamilifu mazungumzo ya amani, na kuchukua jukumu la kujenga katika kufikia suluhu kamili, ya haki na ya kudumu ya suala la Palestina," aliongeza.

Wakati huo huo, katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 8 Oktoba, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alizungumza kuhusu suluhu ya mataifa mawili ili kumaliza mzozo kati ya Israel na Palestina.

Kwa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Beijing ilitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutafuta haraka njia ya amani ya kudumu.

Lakini Yuval Walks, afisa mkuu katika ubalozi wa Israel mjini Beijing, alisema nchi yake inatarajia kulaaniwa vikali na Hamas .

"Wakati watu wanauawa, koo zinakatwa mitaani, sio wakati wa kuita suluhisho la serikali mbili," Walks aliwaambia waandishi wa habari Jumapili, kulingana na Reuters.

Kiongozi wa Wengi katika Seneti ya Marekani Chuck Schumer alielezea kusikitishwa kwake na jibu la China wakati wa mkutano na Xi siku ya Jumatatu. Hii inasemwa katika habari za CNN.

"Ninasema kwa heshima kwamba kauli ya China isiyoonesha huruma wala kuunga mkono watu wa Israel wakati huu wa huzuni inakatisha tamaa," Schumer aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kukutana na waziri wa mambo ya nje wa China.

Kumbuka kuwa Chama cha Kikomunisti cha China kina historia ndefu ya uhusiano wa kirafiki na Palestina. Wamekuwa wakitambua mamlaka ya Palestina tangu mwanzo.

Saudi Arabia

Mwanamfalme Mohammed bin Salman, mtawala ambaye hajatangazwa wa Saudi Arabia, ameelezea uungaji mkono wake kamili kwa Palestina.

Katika mazungumzo ya simu na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas, Prince Mohammed alisema nchi yake "itasimama daima na watu wa Palestina kulinda haki yao ya maisha ya kawaida, matarajio yao na kufikia amani ya haki na ya kudumu."

Shirika rasmi la Habari la Saudi liliripoti habari hii Jumanne.

Pia alimwambia Mahmoud Abbas kuwa anafanya kazi na pande za kimataifa na kikanda ili kuzuia "kupanuka" kwa mzozo huo.

Huu ni msimamo tofauti wa Saudi Arabia katika muktadha wa mazungumzo ya pande tatu yanayoendelea kati ya Israel, Saudi Arabia na Marekani ili kurekebisha uhusiano kati ya Riyadh na Tel Aviv.

Kwa hiyo, uungaji mkono wa Saudi Arabia kwa Wapalestina unaonekana kuwa muhimu sana.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi baada ya shambulio la Hamas, Saudi Arabia iliilaumu Israel kwa kukithiri kwa shambulizi hilo.

Saudi Arabia ilisema "imeonya mara kwa mara kwamba hali ya Palestina inaweza kuwa ya kulipuka kutokana na kuendelea kukaliwa kwa mabavu, kunyimwa haki halali za watu wake na mashambulizi yake ya mara kwa mara dhidi ya hisia zao za kidini."

Urusi

Urusi iko katika nafasi karibu sawa na China. Nchi hiyo ilisisitiza utatuzi wa mzozo kati ya Israel na Palestina, pamoja na haja ya kuanzisha taifa huru la Palestina.

Moscow inalaumu kushindwa kwa sera ya Marekani kuwa ndio sababu ya ghasia katika Mashariki ya Kati.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Rais Vladmir Putin wa nchi hiyo jana Jumanne alizungumza na Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia al-Sudani na kusema kuwa, kuzuka machafuko kati ya Israel na Wapalestina ni kielelezo cha kushindwa kwa sera za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Amesema sera ya Marekani haijatilia maanani matakwa ya Wapalestina.

Kulingana naye, Marekani imeshindwa kufikia makubaliano yanayotekelezeka huku ikidumisha udhibiti wake juu ya juhudi za amani kati ya Israel na Palestina.

Msemaji wa Putin, Dmitry Peskov, alisema Kremlin ilikuwa inawasiliana na pande zote mbili zinazopigana na kueleza nia ya kuchukua jukumu la kusuluhisha mzozo huo.' Hatahivyo, Moscow haikuelezea jinsi gani.

Nchi hiyo imekuwa ikifanya kazi na Marekani, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya ili kupatanisha mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati tangu mwaka 2002.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alitoa wito wa kusitishwa mapema mapigano katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian.

"Suluhu "ya kutegemewa zaidi" kwa amani ni kuundwa kwa taifa la Palestina," Lavrov alisema katika mkutano na waandishi wa habari na mkuu wa Umoja wa Kiarabu Ahmed Abul Gheit siku ya Jumatatu.

Uingereza

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak ameelezea uungaji mkono usioyumba wa Uingereza kwa Israel.

Siku moja baada ya shambulio hilo Bwana Sunak, katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, alisema Uingereza "bila shaka" inasimama na Israel na London inajitahidi kuhakikisha ulimwengu unazungumza kwa sauti moja.

Wakati huo huo, akizungumza katika hafla huko Nottinghamshire. Sunak aliita Israeli kama mshirika mkubwa na akasema kwamba angewapa Israeli kila aina ya msaada.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza James Cleverly alizuru nchi hiyo siku ya Jumatano kuonyesha uungaji mkono kwa Israel. Alisema Uingereza itaunga mkono haki ya Israel ya kujilinda.

Jumatatu jioni katika sinagogi la Wayahudi mjini London Bw. "Wale wanaounga mkono Hamas wanahusika kikamilifu na shambulio hili la kutisha," Sunak alisema katika hotuba yake. Wao si wapiganaji, ni magaidi.'

Uturuki

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametaja mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza kuwa ni 'mauaji ya halaiki'.

Bwana Erdoğan alisema kuwa Israel inatumia nguvu kupita kiasi huko Gaza kujibu mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel.

Kabla ya bwana Erdogan kusema kutumwa kwa ndege za kivita za Marekani kuunga mkono Israel kutachochea 'mauaji ya halaiki' huko Gaza.

Wakati huo huo,Uturuki imeonesha nia ya upatanishi ili kutatua mzozo huo. Uturuki imesema itafanya kila juhudi kumaliza mzozo unaoendelea kati ya Israel na Palestina na kutuliza hali haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Anadolu, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema hayo katika mazungumzo ya simu na Rais Mahmoud Abbas siku ya Jumatatu.

Hapo awali, alitoa wito kwa pande zote kujizuia na kusisitiza juu ya suluhisho la serikali mbili. Aidha amesema kuwa nchi yake iko tayari kuwa mpatanishi katika mzozo kati ya Israel na Gaza.

Uturuki ni mojawapo ya nchi zinazosuluhisha mzozo wa Israel na Palestina.

Nyingine

Viongozi wa Uingereza, Marekani, Ufaransa, Italia na Ujerumani walitoa taarifa za kulaani shambulizi la Hamas kwa maneno yasiyo na shaka.

Taarifa ya pamoja ya nchi hizi ilitolewa awali baada ya mazungumzo ya simu kati ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na Rais wa Marekani Joe Biden.

Taarifa hiyo ilisema, " hakuna uhalali wa vitendo vya kigaidi vya Hamas na shambulio hili lazima lilaaniwe kote."

Qatar na Kuwait zinailaumu Israel kwa kuzidisha mzozo na Wapalestina na kwa hali ya vita inayoendelea. Misri ilitoa wito kwa pande zote husika kujizuia, ikionya juu ya matokeo mabaya ya ghasia.