Fahamu vita vikubwa vinavyoendelea duniani kwa sasa, na kwanini vingine havivutii hisia kubwa

Ulimwengu unazidi kushuhudia ghasia na vurugu kuliko mwanzoni mwa karne hii, na kufikia mwisho wa 2023 kutakuwa na vita vikuu nane, pamoja na mapigano kadhaa yanayohusisha silaha katika kutafuta maeneo au serikali, watafiti wanaonya.

Kando na vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza, ambavyo vimesababisha maelfu ya vifo tangu Oktoba 7, na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, ambao utakuwa unatimiza miaka miwili mwezi Februari 2024, migogoro inayohusisha silaha na mashambulizi makubwa inaendelea hivi sasa nchini Burkina Faso, Somalia, Sudan, Yemen, Burma, Nigeria na Syria.

Kuvutia nadhari au kutovutia

Mambo mengi yanaweza kuelezea hili, kutoka kuongezeka kwa mvutano wa kiuchumi na kijamii karibu na mataifa dhaifu hadi kuongezeka kwa mvutano kati ya mataifa makubwa na hata athari za awali za mabadiliko ya hali ya hewa.

Hata hivyo, nyingi ya vita hivi na migogoro haivutii nadhari ya dunia, hata kwa viwango vya juu vya vifo na uharibifu. Kwa nini iwe hivi?

Sababu nyingi huathiri mwonekano wa kimataifa wa vita, wanaelezea maprofesa waliohojiwa katika ripoti hiyo.

Vita vinavyoendelea

Mwaka jana ulionekana kuwa mbaya zaidi kwa sababu ya vita tangu mauaji ya halaiki ya Rwanda ya 1994, na jumla ya vifo 237,000, kulingana na habari kutoka kwa Jarida la Utafiti wa Amani, lililochapishwa huko Oslo, Norway.

Ongezeko kubwa la mwaka 2022 linatokana hasa na vita viwili vikali: Urusi na Ukraine na vita vya Ethiopia dhidi ya TPLF (Tigray People's Liberation Front), ambapo zaidi ya watu 81,500 na 101,000 mtawalia walifariki kufikia mwishoni mwa 2022.

Fahamu kuhusu vita vikuu vinavyoendelea duniani kote.

1. Burkina Faso

Burkina Faso ndio sehemu yenye vurugu zaidi ya mzozo mkubwa wa silaha katika eneo la Sahel, ambayo iko Afrika Kaskazini na inajumuisha sehemu za nchi 10: Mauritania, Senegal, Mali, Burkina Faso, Niger, Nigeria, Chad, Sudan, Eritrea na Ethiopia.

Tangu mwaka wa 2016, Burkina Faso imekuwa eneo la mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na makundi yenye itikadi kali kama vile Ansarul Islam lenye uhusiano na Al-Qaeda na Islamic State katika eneo la Sahel (ISS).

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linakadiria kuwa takriban maeneo 46 nchini Burkina Faso yalikuwa yakizingirwa na makundi yenye silaha kufikia Julai 2023.

Mnamo 2022, mwaka mbaya zaidi tangu takwimu zilipoanza kurekodiwa kuanza, raia 1,418 waliuawa, kulingana na Hifadhidata ya Matukio ya Migogoro ya Kivita (ACLED).

2. Somalia

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia viliongezeka katika muongo wa kwanza wa miaka ya 2000 baada ya kuibuka kwa kundi la Al Shabaab, mshirika wa Al-Qaeda, wakipambana na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na Umoja wa Afrika.

Al Shabaab inajaribu kupindua serikali ya mitaa, inayoungwa mkono na nchi za Magharibi, ili kuanzisha serikali yake kwa kuzingatia tafsiri kali ya sheria za Kiislamu.

Kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Human Rights Watch, "kundi la wapiganaji la Al Shabaab linatekeleza mashambulizi ya kiholela na yanayolenga raia na kuwasajili watoto kwa nguvu."

Kiwango cha vurugu kiliongezeka mnamo 2022, na kufikia idadi kubwa zaidi ya vifo tangu miaka ya mapema ya 1990, kulingana na Uppsala Conflict Data Program (UCDP).

3. Sudan

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi linasema mgogoro wa kibinadamu "usiofikirika" unaendelea nchini Sudan.

Takriban watu milioni sita wamelazimika kuyahama makazi yao tangu vita hivyo kuanza mwezi Aprili mwaka huu.

Katika muda wa miezi sita, vita kati ya jeshi la Sudan na kundi la wanamgambo linalojaribu kuchukua madaraka vimesababisha vifo vya hadi watu 9,000, kulingana na Umoja wa Mataifa, na kuunda "moja ya jinamizi mbaya zaidi la kibinadamu katika historia ya hivi karibuni" .

Mapigano hayo yamesababisha watu milioni 25, zaidi ya nusu ya watu wote kutegemea misaada ya kibinadamu, kulingana na shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa.

4. Burma

Kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi mwaka 2021 na kusababisha ukandamizaji dhidi ya waandamanaji waliopinga serikali mpya uilikuwa mwanzo wa kuongezeka kwa ghasia katika nchi hiyo ya Kusini Mashariki mwa Asia.

Kulingana na watafiti huru waliotajwa na Umoja wa Mataifa, zaidi ya watoto 13,000 wamefariki nchini humo na watu milioni 1.3 wamelazimika kuyahama makazi yao.

Makundi kadhaa ya waasi yamekuwa yakiendesha shughuli zake nchini humo tangu miaka ya 1950. Wengi wao wana silaha na wamebadili misimamo yao katika jaribio la kunyakua mamlaka na kuuangusha utawala mpya wa kijeshi.

5. Uruis-Ukraine

Mnamo Februari 2022, Urusi ilizindua uvamizi kamili wa Ukraine, na kusababisha wimbi jipya la mamilioni ya wakimbizi na makumi ya maelfu ya vifo vya kiraia na kijeshi.

Umoja wa Mataifa ulithibitisha rasmi vifo vya raia 9,900, lakini ukasema "idadi halisi hakika ni kubwa."

Mgogoro huo ulianza mwaka wa 2014, wakati Urusi ilipotwaa eneo la Ukraine la Crimea, katika hatua isiyotambulika kimataifa.

Tangu wakati huo, utawala wa Vladimir Putin umekuwa ukiwaunga mkono waasi wanaopigana na jeshi la Ukraine katika eneo la Donbass, kwenye mpaka kati ya nchi hizo mbili.

Mapema Novemba 2023, Ukraine iliripoti kuwa karibu maeneo 120 yalishambuliwa kwa mabomu katika saa 24 zilizopita, na kuashiria shambulio kubwa zaidi tangu kuanza kwa mwaka huu. Kwa sasa Urusi inadhibiti takriban asilimia 17.5 ya eneo linalotambulika kimataifa la Ukraine.

6. Israel-Gaza

Kundi la Wapalestina la Hamas linalodhibiti Ukanda wa Gaza lilifanya shambulizi la kushtukiza dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba na kuua zaidi ya watu 1,400 na kuwateka mateka zaidi ya watu 200.

Israel ilijibu kwa mashambulizi makali ya kijeshi yaliyoua zaidi ya watu 10,000, asilimia 40 kati yao wakiwa watoto, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.

Umoja wa Mataifa unaishutumu Israel kwa kufanya "uhalifu wa kivita" kwa kutumia "adhabu za pamoja" kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza.

Israel inadai kuwa na haki ya kujilinda na inataka kuliangamiza kundi la Wapalestina la Hamas.

Pia alidai kuwa Hamas ilifanya uhalifu wa kivita kwa kuishambulia Israel na kuwachukua mateka raia.

7. Nigeria na Syria

Migogoro mbalimbali ya ndani katika nchi hizi mbili iko kwenye hatihati ya kufikia kiwango cha vifo 1,000, ambacho kinaziainisha kama vita, kulingana na data ya awali kutoka kwa Mpango wa Takwimu za Migogoro wa Uppsala (UCDP).

"(Nchi zote mbili) hadi sasa ziko chini ya kiwango hiki katika data ya awali na kuna uwezekano mkubwa zaidi zitajumuishwa katika orodha ya mwisho ya vita," mratibu wa programu Therese Petterson aliiambia BBC News Brasil.

"Pia kuna (migogoro) mingine ambayo inaweza kuishia kuainishwa kama vita kulingana na kile kitakachotokea katika miezi ijayo, kama huko Pakistan."

Nigeria imekuwa ikishuhudia ghasia za makundi yaliyopangwa tangu uhuru wake mwaka 1960. Mtazamo wa sasa ni katika mapigano kati ya majeshi ya serikali na makundi ya Kiislamu yenye itikadi kali katika mataifa tofauti yanayotaka kudhibiti maeneo.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, vilivyoanza wakati wa maandamano dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad mwezi Machi 2011, vinahusisha makundi ya waasi na mataifa makubwa ya kigeni kama vile Urusi, Uturuki, Qatar, Saudi Arabia na Marekani.

8. Yemen

Jumatano ya tarehe (08/11), serikali ya Marekani ilisema kuwa moja ya ndege zake zisizo na rubani ilidunguliwa katika pwani ya Yemen na waasi wa kundi la Houthi.

Kundi hili linaungwa mkono na Iran na linafuata mkondo wa Uislamu wa Kishia unaojulikana kwa jina la ‘Zaidism’.

Kutunguliwa kwa ndege hiyo isiyo na rubani ya Marekani kumekumbusha mzozo ambao umepamba moto nchini Yemen tangu mwaka 2014 - na ambao unawakutanisha Wahouthi na serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia, mpinzani mwingine wa Iran, na vile vile Marekani na Israel.

Mnamo Septemba mwaka huo, Houthi waliteka mji mkuu, Sanaa, na kuiondoa serikali rasmi. Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia na kuungwa mkono na Uingereza na Marekani ulijibu, lakini miaka minane baadaye pamoja na maelfu ya mashambulizi ya angani, waasi bado wanadhibiti mji mkuu.

Imefasiriwa na Asha Juma

Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi