Zimbabwe bila Robert Mugabe: Nini kimebadilika?

Hali ya hofu bado imetanda nchini Zimbabwe, miaka mitano baada ya mtawala wa muda mrefu Robert Mugabe kuondolewa madarakani.

Wakati nchi inaadhimisha hatua hii muhimu, watu wachache wako tayari kuzungumza kwa uwazi iwapo serikali iliyochukua mamlaka imetimiza ahadi yake ya mabadiliko, iwe ni katika suala la kuinua viwango vya maisha au kudumisha haki za binadamu.

"Najishughulisha na mambo yangu," mchuuzi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe aliambia BBC. "Watu wanaozungumza mawazo yao - wengine huishia gerezani. Kwa hivyo, mimi hujishughulisha na ya kwangu na kufanya kile ninachopaswa kufanya ili kuishi."

Ni mabadiliko madogo yameshuhudiwa kuhusiana na suala hili tangu kuondoka kwa Rais Mugabe.

Watu wa kawaida na wakosoaji bado wanakamatwa kwa kumtusi rais, wanasema wanasheria wa haki za binadamu.

Tendai (si jina lake halisi) anauza mboga kutoka kwenye buti ya gari lake - sabuni ya kufua, marashi, vitafunwa na mafuta ya kupikia vyote vimepangwa vizuri.

Ijapokuwa amehitimu wa chuo kikuu nani mtaalamuwa masuala ya masoko na usimamizi wa rasilimali watu, anasema kuwa kuuza bidhaa mitaani ndiyo njia pekee ya kujikimu kwa sababu kazi hazipatikani.

"Mambo ni yale yale au mabaya zaidi tangu Robert Mugabe alipoondoka. Lakini bado nina matumaini kuhusu siku zijazo," anaongeza.

Mfumuko wa bei umefikia asilimia 268 - mara nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa wakati Mugabe alipoondoka madarakani, kulingana na data kutoka shirika la takwimu la taifa la Zimbabwe.

Wakati huo huo, idadi ya Wazimbabwe wanaokabiliwa na umaskini imeongezeka karibu mara mbili - kutoka 30% mwaka 2017 hadi 50% wakati wa janga la corona, inasema Benki ya Dunia.

Hii imefanya watu wengi zaidi kukata tamaa.

Harare imejaa wafanyabiashara wasio rasmi, wengi wao watu wengi wa tabaka la kati wanaouza bidhaa kutoka kwa magari yao.

Mwanamke mmoja anauza nyama iliyofungwa kwenye karatasi za plastiki kwa wateja wanaofika kwa miguu au kwa gari ili kupata chakula - wengine wakilipa kama dola 0.50 (£0.42) kwa wakati mmoja.

"Binafsi, sikuwa miongoni mwa watu waliofurahia Mugabe alipojiuzulu. Watu hawakujua kwamba walikuwa wakisherehekea maafa yanayokuja," mchuuzi huyo wa nyama aliambia BBC.

"Walidhani baada ya Mugabe kuondoka watapata mkate na siagi, mayai na maziwa - lakini sivyo ilivyotokea."

Sifa na ahadi

Watu walifurika katika Mitaa ya Harare kusherehekea kujiuzulu kwa Bw Mugabe mnamo 21 Novemba 2017. Wiki moja kabla ya vifaru vilikuwa vimeingia katika mitaa ya mji mkuu huku jeshi lilipokamata shirika la utangazaji la umma na kumweka rais huyo mwenye umri wa miaka 93 chini ya kizuizi cha nyumbani.

Aliyekuwa makamu wa rais wa Mugabe, Emmerson Mnangagwa, aliibuka shujaa aliyesimama dhidi ya mwanasiasa huyo. Aliapa kukomesha siasa mbaya na zenye mgawanyiko wa ndani, kugeuza uchumi na kurekebisha uhusiano uliovunjika na mataifa ya Magharibi.

Hata hivyo, wakosoaji walieleza kuwa amekuwa akifanya kazi kwa karibu na Bw Mugabe kwa miaka mingi na amekuwa akishutumiwa kwa jukumu kubwa katika baadhi ya maovu mabaya zaidi ya enzi ya Mugabe, na kujiuliza iwapo kweli yeye ndiye mtu wa kuleta mabadiliko. Chama cha Bw Mugabe Zanu-PF kilisalia madarakani.

"Niliingia serikalini kwa sababu niliipenda nchi yangu na sio mapinduzi," alisema mwandishi na mwanasheria aliyeshinda tuzo hiyo Petina Gappah, wakati wa majadiliano ya mtandaoni na taasisi ya kisiasa ya SAPES Trust ili kukagua enzi ya baada ya mapinduzi.

Alikuwa ameajiriwa kama mshauri wa ushiriki wa kimataifa katika wizara ya mambo ya nje lakini ilihudumu kwa miezi 18 tu.

Anasema aliondoka kwa huzuni, si kwa hasira na kukata tamaa, si kwa uchungu.

"Viongozi wengine waliiita muujiza, tulihisi kwamba kitu kipya kinakuja - kwa bahati mbaya hakikuja," alisema.

Ziara ya wiki iliyopita ya wajumbe wa Jumuiya ya Madola inayozingatia kurejeshwa kwa Zimbabwe inaashiria kuwa kumekuwa na mabadiliko chanya tangu Rais Mugabe aondoke.

Ziara kama hiyo hapo awali isingewezekana. Zimbabwe ilijiondoa katika Jumuiya hiyo mwaka 2003 ikilaumu kile ilichokiita "muungano usio na heshima wa Anglo-Saxon dhidi ya Zimbabwe".

Mwaka mmoja kabla, Zimbabwe ilikuwa imesimamishwa kazi kwa ukiukaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na unyakuzi wa mashamba yanayomilikiwa na wazungu na mateso dhidi ya wanachama wa upinzani.

Kuingia tena kwa Zimbabwe katika Jumuiya ya Madola kutakuwa ushindi wa kiishara kwa serikali ya Rais Mnangagwa - ishara kwamba ugomvi wake na Uingereza kuhusu ardhi umekwisha, wachambuzi wameiambia Gappah.

Chama kikuu cha upinzani - Citizen's Coalition for Change (CCC) - kinataka masharti ya awali kuwekwa kabla ya Zimbabwe kujiunga tena, ikitoa mfano wa kuendelea kuteswa kwa wanachama wake, waandishi wa habari na wakosoaji wengine wa serikali.

Katika wiki ya ziara ya Jumuiya ya Madola, wanachama 15 wa CCC akiwemo mbunge Godfrey Sithole hatimaye waliachiwa kwa dhamana baada ya kuzuiliwa jela miezi mitano kwa madai ya kuchochea ghasia za umma katika mapigano na wafuasi wa serikali huko Nyatsime, kusini mwa Harare, hatua ambayo wanasema ni ya kisiasa.

Job Sikhala, mbunge mwingine, bado yuko kizuizini kwa tuhuma hizo hizo.

Wakati ujumbe wa Jumuiya ya Madola ukiongozwa na msaidizi wa katibu mkuu Luis Franceschi ulisema Zimbabwe imepata "maendeleo ya kuvutia sana" katika kufikia masharti, nchi wanachama zitapaswa kuzingatia kama mageuzi ya kiuchumi, haki za binadamu na uchaguzi yanatosha kurejeshwa.

Katika hatua hii, serikali ya Zimbabwe inasalia na matumaini.

"Tumefanya kila linalowezekana ili kupokelewa tena - kuna nchi katika Jumuiya ya Madola ambazo zinaweza kulinganishwa na sisi," anasema msemaji wa Zanu-PF Nick Mangwana.

Kujali mahitaji ya bishahara

Lakini biashara zingine zinasema kumekuwa na mabadiliko chanya.

Pato la Taifa limepanda kutoka dola bilioni 17.5 (£14.8bn) mwaka wa 2017, hadi dola bilioni 20.2 mwaka jana.

"Serikali hii inajali zaidi mahitaji ya biashara. Wanaweza kufanya zaidi lakini huwezi kulinganisha na serikali iliyopita," anasema Kurai Matsheza, ambaye ni ŕais wa Shiŕikisho la Viwanda la Zimbabwe.

Anasema ni kampuni chache zilizofungwa ukilinganisha na enzi ya Mugabe, akiongeza, "kuadiliji sera, udhibiti wa bei hauko katika kiwango sawa na ilivyokuwa."

Serikali imeelekeza mamilioni ya dola katika uwekezaji, haswa katika madini.

Kampuni kubwa ya Platinum ya Zimplats itawekeza $1.8bn katika kipindi cha miaka 10 ijayo, kufuatia mazungumzo na serikali.

Wakati huo huo, mchimba madini wa China Zhejiang Huayou Cobalt anatazamiwa kuwekeza dola milioni 300 katika mgodi wake wa lithium.

Mradi wa chuma uliokwama chini ya Mugabe umefufuliwa.

Sekta ya kilimo cha mboga iliyokuwa imeporomoka sasa imeimarishwa kufuatia uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji mashamba maji.

Uzalishaji wa ngano uko katika kiwango cha juu katikai kipindi cha miaka 17.

Barabara na mabwawa yanakarabatiwa na kujengwa.

Licha ya hayo, bado hatua hizi hizijawazuia vijana wa Zimbabwe kufanya kila wawezalo kwenda mahali pengine kutafuta maisha.

Kwa hiyo serikali inafanya nini kuhusu hilo?

"Sasa asilimia 50 ya mapato yanaelekezwa kwenye uwekezaji wa mtaji - ili kuboresha maisha ni lazima uboreshe matokeo hivyo serikali ilibidi ielekeze nguvu yake kwenye miundombinu," anasema msemaji wa serikali Bw Mangwana.

"Word Bank inasema nchi imefikia hadhi ya kipato cha kati, maana yake mapato yameimarika. Hatujafika tunakokwenda, tulichonacho ni kazi inayoendelea," anaongeza.

Lakini Ranga Mberi, mhariri wa tovuti ya habari za biashara Newzwire, anasema juhudi zaidi inahitajika.

"Wakati ni vizuri kuzungumzia ukuaji na uwekezaji katika madini, cha muhimu ni kile kilicho kwenye meza ya chakula na kwenye mifuko ya watu."

"Mfumuko wa bei ni suala kubwa ambalo watu watatumia kumhukumu [Mnangagwa]," anaongeza.

"Ukweli ni kwamba kila kitu kinapaswa kutafsiriwa kwa tumbo lililoshiba. Na huo ndio mtihani mkubwa kwa Bw Mnangagwa kuelekea 2023."