Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uhusiano wa Trump na Putin mashakani? Je ni hatari kwa usalama wa dunia?
- Author, James Landale
- Nafasi, Diplomatic correspondent
- Author, Phil McCausland
- Nafasi, BBC News, New York
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Mvutano mpya umeibuka kati ya Rais Donald Trump na Vladimir Putin baada ya Trump kusema wazi kuwa amechukizwa na kiongozi huyo wa Urusi.
Trump alisesema kuwa ana "hasira kubwa" na "amechukizwa" na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, baada ya wiki kadhaa za majaribio ya kusitisha mapigano nchini Ukraine.
Katika mahojiano na NBC News, rais huyo wa Marekani alisema anakerwa na Putin kwa kuhoji na kumshambulia Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kuhusu uhalali wake.
Kauli hii imezua maswali kuhusu mustakabali wa uhusiano wao, hasa baada ya miaka mingi ya Trump kuonekana kuwa na msimamo laini kuelekea Urusi. Je, mabadiliko haya yana maana gani kwa siasa za kimataifa na usalama wa dunia?
Historia ya Uhusiano wa Trump na Putin
Kwa muda mrefu, Trump na Putin wamekuwa wakihusiana kwa namna ya kipekee. Wamekuwa maswahiba. Wakisikilizana, na kuaminiana kwenye baadhi ya mambo. Trump aliwahi kusema wakati Joe Biden yuko madarakani kama rais wa Marekani kwamba, Vita vya Ukraine vingekoma siku moja tu angekuwa mamlakani. Alisema hivyo kuashiria namna uswahiba wao ungeweza kurahisisha mapatano ya amani. Na Putin, aliwahi kusema, Trump ana nafasi ya kutafuta suluhu ya mzozo Ukraine.
Wakati wa utawala wa Trump wa awamu ya kwanza na awamu ya pili toka ashike hatamu ya uongozi, alisita kumlaumu Putin moja kwa moja kuhusu masuala nyeti kama uingiliaji wa Urusi kwenye uchaguzi wa Marekani na mgogoro wa Ukraine. Ni kama kuunga mkono baadhi ya sera za Urusi, hasa kuhusu vita vya Ukraine.
Hata baada sasa hali inaanza kuonekana tofauti, haikutarajiwa Trump anaweza kusimama na kuzungumza kukasirishwa na Putin hadharani. Hatujui Putin atasema nini, atajibu nini, kwakuwa bado Ikulu ya Urusi haijatoa maoni kuhusu kauli ya Trump.
Kwa vyovyote vile uhusiano wao wa jana, hauwezi kuwa sawa na wa leo, kwa kauli 'nzito' ya Trump kuhusu Putin. Na kama Putin atarejesha majibu ya 'kuchukiza', huenda uhusiano wao ukadorora zaidi.
Hata Viongozi wa Ulaya walikuwa na wasiwasi kuwa Trump alikuwa karibu sana na Putin wakati mazungumzo ya kusitisha mapigano Ukraine yakiendelea. Wasiwasi huo unajidhihirisha tofauti sasa, Trump akianza kwa maneno na kama anavyofahamika kwenye kusimamia maneno yake.
Nini kimetokea?
Hoja kubwa anayoigusa Trump ni kuhusu Putin anavyochukulia mzozo wa Ukraine na kauli zake kuhusu Zelensky na Ukraine.
Kwa wiki sita zilizopita, Trump amekuwa akimshinikiza Zelensky kwa masharti kadhaa huku akimfurahisha Putin na kukubaliana kwa kiasi kikubwa na matakwa yake.
Lakini hali inaonekana kubadilika. Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kutishia kuiwekea Russia vikwazo kwa kuchelewesha mazungumzo ya amani, jambo linaloipa Moscow mzigo wa kuchukua hatua.
Kwa mujibu wa NBC News, katika mahojiano ya simu ya dakika 10, Trump alisema alikuwa na hasira kubwa wakati Putin alipokejeli hadhi ya Zelensky, ingawa Trump mwenyewe hapo awali alikuwa amemwita Zelensky dikteta na kumshinikiza afanye uchaguzi.
"Unaweza kusema nilikuwa na hasira sana, nimechukizwa, wakati... Putin alipoanza kushambulia uhalali wa Zelensky, kwa sababu hiyo siyo njia sahihi ya kwenda," alisema Trump.
"Uongozi mpya unamaanisha hutakuwa na makubaliano kwa muda mrefu," aliongeza.
Hata hivyo Trump alipoza kidogo makali ya maneno yake kwa kusema Warusi wanajua kuwa amekasirika, lakini akasisitiza kuwa ana "uhusiano mzuri sana" na Putin na kwamba "hasira hupungua haraka... ikiwa atafanya jambo sahihi."
Iwapo Urusi haitakubali kusitisha mapigano, Trump alitishia kuiwekea vikwazo zaidi vya kiuchumi ikiwa atahisi kuwa ni kosa la Putin.
Kutokana na hilo, Trump alisema kutakuwa na ushuru wa 25% kwa mafuta na bidhaa nyingine zinazoingia Marekani kutoka Urusi.
Pia, ushuru wa pili unaweza kufikia hadi 50% kwa bidhaa kutoka kwa nchi zinazonunua mafuta ya Urusi. Wateja wakubwa wa mafuta ya Urusi ni China na India.
Trump alimalizia kwa kusema kuwa atazungumza na Putin baadaye wiki hii.
Je, Dunia itakuwa Salama?
Mabadiliko haya yanaweza kuwa na athari kubwa kwa usalama wa dunia. Ikiwa Trump ataendelea kumshutumu Putin, Urusi inaweza kuchukua hatua mpya za kuimarisha uhusiano wake na mataifa kama China au Iran, hali ambayo inaweza kuongeza mivutano ya kimataifa.
Aidha, ikiwa mgawanyiko huu ni wa muda tu, inaweza kuashiria mchezo wa kisiasa unaolenga kulinda maslahi fulani ya Trump au Urusi.
Bado haijulikani kama kauli ya Trump ni ishara ya mabadiliko halisi katika msimamo wake au ni mkakati mwingine wa kisiasa wa Trump.
Mazungumzo yao ya wiki ijayo huenda yakatoa picha halisi ya msimamo wa Trump na uhusiano wa viongozi hawa.
Pamoja na hatua zozote, hali hii inaonyesha kuwa uhusiano kati ya Marekani na Urusi utaendelea kuwa suala nyeti, lenye athari kubwa kwa siasa za kimataifa na usalama wa dunia.